KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 16, 2015

SIMBA YAWAPA RAHA MASHABIKI WAKE, YAITUNGUA URA 2-1



Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM

BAO la dakika ya 82 la beki wa kimataifa wa Uganda, Juuko Murushid limeipa Simba SC ushindi wa 2-1 dhidi ya URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Beki huyo ‘mbishi’ alifunga bao hilo kwa guu lake la kushoto baada ya kuuwahi mpira ulioparazwa na kipa Brian Bwete kufuatia kona maridadi iliyochongwa na kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Refa Israel Mujuni wa Dar es Salaam, Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Kelvin Ndayisenga dakika ya nne aliyemalizia krosi ya Mrundi mwenzake, Emery Nimubona.

Juuko Murushid (kulia) akishangilia mbele ya mashabiki wa Yanga na Ibrahim Hajib baada ya kuifungia Simba SC bao la ushindi

Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani URA walisawazisha dakika ya 20 kupitia kwa Frank Kalanda, aliyefumua shuti la juu lililompita kiulaini kipa, Peter Manyika.

Kipindi cha pili, timu zote zilifanya mabadiliko na mchezo ukazidi kuwa mtamu kutokana na mashambulizi na kosakosa za pande zote mbili.

Wachezaji Peter Mwalyanzi wa Simba SC na Jimmy Kulaba wa URA waligongana wakati wakigombea mpira wa juu na wote kushindwa kuendelea na mchezo, wakipelekwa katika zahanati ndoto ya uwanjani hapo kupatiwa huduma ya kwanza.

URA walimuingiza Deo Otieno baada ya kutoka Jimmy Kulaba wakati Simba SC ilimalizia mchezo pungufu kutokana na kuwa imemaliza wachezaji wa kubadili.

Huo unakuwa mchezo wa saba mfululizo wa kirafiki, Simba SC inashinda chini ya kocha wake mpya,
Muingereza Dylan Kerr, baada ya awali kuzifunga 2-1 Kombaini ya Zanzibar, 4-0 Black Sailor, 2-0 Polisi, 3-0 Jang’ombe Boys, 3-2 KMKM zote za Zanzibar na 1-0 SC Villa ya Uganda.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Emery Nimubona/Hassan Kessy dk46, Samih Haji Nuhu/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk46, Juuko Murudhid, Said Issa/Hassan Isihaka dk46, Abdul Banda/Justuce Majabvi dk46, Simon Sserunkuma/Peter Mwalyanzi dk46/, Awadh Juma/Said Ndemla dk46, Kevin Ndayisenga/ Ibrahim Hajib dk67, Danny Lyanga/Mussa Mgosi dk68 na Issa Abdallah/Mwinyi Kazimoto dk46.

URA: Bwete Brian, Massa Simon, Sekito Sam, Samuel Senkoom, Kasozi Bob, Agaba Oscar, Kagimi Sadiq/ El Kanah Mkugwa dk67, Kyeyune Said, Oniamucha Villa, Kalanda Frank/Ronald Kigonyo dk72 na Lutimba Yayo/Jimmy Kulaba dk51/Deo Otieno dk72.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment