KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 3, 2015

AZAM BINGWA KOMBE LA KAGAME


MABAO mawili yaliyofungwa na John Bocco na Kipre Tchetche, moja katika kila kipindi, jana yaliiwezesha Azam kuandika historia mpya katika soka ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuizabua Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame.

Azam imekuwa timu ya tatu kutoka Tanzania Bara kushinda kombe hilo baada ya Simba na Yanga. Simba inaongoza kwa kulitwaa mara tano ikifuatiwa na Yanga iliyolitwaa mara nne.

Ushindi huo umeiwezesha Azam kutwaa kitita cha Dola za Marekani 30,000 wakati Gor Mahia imezawadiwa Dola 20,000 kwa kushika nafasi ya pili. KCCA ya Uganda imetwaa kitita cha Dola 10,000 kwa kushika nafasi ya tatu.

Fedha hizo zimetolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye ni mdhamini mkuu wa mashindano hayo. Rais Kagame hutoa Dola 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi za washindi watatu wa kwanza,

Iliwachukua Azam dakika 16 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Bocco na kudumu hadi mapumziko. Bao la pili lilifungwa na Tchetche dakika ya 63.

Azam ilitinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuichapa KCCA bao 1-0 wakati Gor Mahia iliilaza Al Khartoum ya Sudan mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment