KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 16, 2017

UPELELEZI KESI YA WEMA SEPETU HAUJAKAMILIKA
UPANDE wa Jamhuri  katika kesi ya kukutwa bangi na misokoto, inayomkabili msanii Wema Sepetu na wenzake, umeieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo uko hatua za mwisho kukamilika.

Kutokana na hilo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ameutaka upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi huo mapema.

Wakili wa Serikali, Constatine Kakula, alidai jana mbele ya Hakimu Simba, kuwa upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Baada ya kueleza hilo, Hakimu Simba aliutaka upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi mapema.

Wakili Kakula aliieleza mahakama kuwa, upelelezi huo uko hatua za mwisho kukamilika.

Kabla ya kuingia katika chumba cha mahakama, Wema aliyekuwa amevalia gauni refu, alielekezwa na askari kutafuta ushungi wa kufunika kifua chake, ambacho sehemu kubwa kilikuwa wazi.

Kutokana na hilo, mmoja wa wanawake waliokuwa wameongozana na Wema, alilazimika kutoa mtandio wake mweusi na kumpatia msanii huyo ambaye alijifunika sehemu iliyokuwa inaonekana.

Mbali na Wema, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Angelina Msigwa  na Matrida Abas.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na msokoto mmoja wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi, vyenye uzito wa gramu 1.08.

Washitakiwa hao wanadaiwa walikutwa na bangi na msokoto huo, Februari 4, mwaka huu, nyumbani kwao Kunduchi Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Wema na wenzake wako nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment