KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 26, 2017

TAIFA STARS YAWAPA RAHA WATANZANIA, YAWATUNGUA BOTSWANA MABAO 2-0, SAMATTA ATUPIA ZOTE MBILI

MABAO mawili yaliyofungwa na nahodha Mbwana Samatta, jana yaliiwezesha timu ya Taifa, Taifa Stars kuibwaga Botswana mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbwana alifunga bao la kwanza dakika ya pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shiza Kichuya na kumtoka beki Kaone Vanderwesthuizem kabla ya kupiga shuti lililompita kipa Kabelo Dambe wa Botswana.

Mshambuliaji huyo anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, aliongeza bao la pili dakika ya 87 kwa shuti la mpira wa adhabu lililotinga moja kwa moja wavuni.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Taifa Stars mwaka huu na pia ya kwanza kwa kocha mpya, Salum Mayanga, aliyerithi mikoba ya Charles Boniface, aliyejiuzulu mapema mwaka huu.

Katika mechi hiyo, Mayanga aliwachezesha wachezaji wengi chipukizi, wakiwemo aliowaita kwa mara ya kwanza, ambao walionyesha kiwango kizuri cha soka na kuwapa raha mashabiki.

Iwapo mshambuliaji Simon Msuva angekuwa makini, Taifa Stars ingeweza kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao, lakini alipoteza umakini kwa kupiga mashuti nje ya lango.

No comments:

Post a Comment