KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 1, 2017

NAPE: NITAHAKIKISHA TIMU ZA DODOMA ZINACHEZA LIGI KUUWaziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye amewahakikishia wapenzi wa mpira mjini Dodoma, kuwa timu za mpira mkoani humo zitashiriki Ligi Kuu ili kuwapa raha ya ligi hiyo mashabiki wa mpira na michezo kwa ujumla.

Amezungumza hayo mara baada ya kukutana na kufanya mazoezi na vijana kutoka Jogging Club mbalimbali mjini Dodoma, ikiwa ni ishara rasmi ya wizara yake kuhamia katika makao makuu ya nchi.

Nape amesema kuwa haitawezekana serikali ikahamia Dodoma na kusiwe na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hivyo yeye kama waziri anayehusika na michezo kwa kushirikiana na wadau wa michezo atahakikisha timu zinafanya vizuri na kushiriki Ligi hiyo.

“Haiwezekani Rais akawa hapa na Makamu wa Rais na mawaziri tukakosa ladha na furaha ya Ligi kuu hapa Dodoma. Nitahakikisha timu za hapa zinashiriki Ligi kuu,” alisisitiza Nnauye.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kazi Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amewapongeza vijana wa Jogging Club na wakazi wa Dodoma kwa kushiriki michezo na kuhimiza kujituma zaidi
kwa timu za michezo hasa mpira wa miguu ili kushiriki Ligi kuu Tanzania Bara.

Katibu Mkuu Wizara wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel amewaomba wakazi wa Dodoma kufanya michezo kuwa ni Utamaduni wao wa kila siku ili kujenga Taifa la wapenda michezo kwa nia ya kuimarisha afya na kuendeleza michezo nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Omary Singo amewahakikishia wakazi na wapenzi wa michezo, ushirikiano katika kuendeleza na kukuza michezo hasa katika makao makuu ya nchi Dodoma.

No comments:

Post a Comment