'
Thursday, May 23, 2013
JAYDEE: NITASAMBAZA ALBAMU YANGU KWA KUTUMIA MAX MALIPO
MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura 'JayDee' amesema anatarajia kuuza albamu yake mpya ya Nothing but the Truth kwa kutumia wakala wa Max Malipo.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, JayDee alisema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kudhibiti wizi wa kazi za sanaa na pia kuboresha soko la kazi zake.
JayDee alisema Max Malipo itaitumia Kampuni ya Posta yenye ofisi zake kote nchini kwa ajili ya kusambaza albamu hiyo.
"Naamini kwa kutumia wakala wa Max Malipo, albamu yangu itaweza kupatikana kote nchini na kwa muda mfupi,"alisema msanii huyo aliyewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki nchini.
"Nataka nijaribu na kujifunza, nikifanya hivi itakuwaje au nifanyeje ili kuboresha soko la muziki wangu,"aliongeza.
Kwa mujibu wa msanii huyo, onyesho la uzinduzi wa albamu yake hiyo mpya limepangwa kufanyika Mei 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge.
JayDee alisema katika onyesho hilo, atamshirikisha msanii Juma Kassim 'Nature', mwanamuziki mkongwe nchini, Hamza Kalala, Grace Matata na Joseph Haule 'Profesa Jay', ambaye ameshirikiana naye kuimba kibao cha Joto la hasira.
Msanii huyo anayemiliki bendi ya Machozi alisema, ameamua kuandaa onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 13 katika fani ya muziki.
Alisema katika kipindi hicho, ameweza kujifunza mambo mengi kuhusu muziki ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu mkubwa wa fani hiyo.
Mwanadada huyo alisema alisimama kwa muda mrefu kutoa nyimbo mpya kutokana na kuelekeza nguvu zake zaidi katika bendi yake ya Machozi.
"Unajua usipotoa nyimbo kwa muda mrefu, si rahisi kupata maonyesho. Lakini kwa upande mwingine, bendi ina manufaa makubwa zaidi katika muziki,"alisema.
JayDee alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya kwa sasa umekuwa na mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira nyingi kwa vijana na kuwabadilisha kimaisha.
Hata hivyo, alisema soko la muziki huo lilikuwa zuri miaka ya nyuma kutokana na kuwepo kwa wasanii wachache, tofauti na sasa, ambapo idadi ya wasanii wa muziki huo imekuwa kubwa na hivyo kusababisha mauzo yapungue.
Aliitaja changamoto nyingine inayowakabili wasanii wa muziki huo kuwa ni kukithiri wa wizi wa kazi za sanaa, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiendelea kudurufu nyimbo za wasanii na kutengeneza albamu bila ridhaa yao huku wengine wakifanya biashara ya kuingiza nyimbo za wasanii kwenye simu za mkononi bila kuwalipa chochote.
"Ninachowaomba watanzania ni kuendelea kuwaunga mkono wasanii wa muziki huu ili kuongeza ajira kwa vijana,"alisema msanii huyo mkongwe wa muziki wa kizazi kipya.
Pamoja na kupatikana kwa mafanikio hayo, JayDee alisema bado maonyesho yanayofanywa na wasani wa Tanzania katika baadhi ya nchi za Ulaya ni ya kiwango cha chini.
Alisema mara nyingi maonyesho hayo yamekuwa yakihudhuriwa na watanzania wachache wanaoishi katika nchi hizo za Ulaya, ama raia wengine kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda na zile zinazozungumza lugha ya kiswahili.
"Ninachoweza kusema ni kwamba, faida pekee wanayoipata wasanii wa Tanzania wanapokwenda Ulaya ni kusafiri, kujifunza mambo tofauti na kukutana na watu wengi,"alisema.
JayDee alisema binafsi amekuwa akitembelea baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili ya shughuli zake binafsi na ni mara chache amewahi kualikwa kufanya maonyesho.
Msanii huyo alisema amefurahi kukamilisha ndoto yake ya kurekodi wimbo na mwanamuziki mkongwe wa Zimbabwe, Oliver Mutukuzi na kwamba kwa sasa, ndoto nyingine aliyonayo ni kurekodi na mwanamuziki Dr. Dre wa Marekani.
Msanii huyo alisema pia kuwa, ndoto nyingine aliyonayo katika maisha yake ni kuanzisha kituo cha redio, ambacho kitakuwa kikifanyakazi kwa ajili ya watanzania wote.
Aliongeza kuwa, yupo tayari kutoa mchango wa mawazo kwa wasanii wanaochipukia wa muziki huo kuhusu nini la kufanya kwa lengo la kuendeleza vipaji vyao, lakini si kuwapa pesa kwa vile hana uwezo huo kwa sasa.
WASIFU WA JAYDEE
ALIZALIWA: Juni 15, 1979
KAZI: Mwanamuziki
NDOA: Ameolewa na mtangazaji wa redio, Gardner Habbash
TUZO ALIZOSHINDA: Msanii bora wa kike wa R&B (2002)
Albamu bora ya R&B (2004)
Video bora ya msanii wa kike nchini Afrika Kusini
(2005)
Wimbo bora wa mwaka wa Tanzania (2008)
Mwimbaji bora wa kike (2010)
Mwimbaji bora wa kike (2012)/
Mwimbaji bora wa kike anayechipukia Afrika Mashariki (2003, 2004 na 2005).
Tuesday, May 21, 2013
NGASA ATUA YANGA KWA MIL 30/-
HATIMAYE mshambuliaji Mrisho Ngasa wa klabu ya Simba ametia saini
mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu yake ya zamani ya Yanga
kwa ajili ya michuano ya ligi kuu na kimataifa.
Japokuwa viongozi wa Yanga hawakuwa tayari kutaja kiwango cha pesa
walichomlipa mchezaji huyo, kuna habari kuwa, Ngasa amechota zaidi
ya sh. milioni 30 na atakuwa akilipwa mshahara wa sh. milioni tatu
kwa mwezi.
Mara baada ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari jana makao
makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam,
Ngasa alisema amefurahi kurudi nyumbani.
Ngasa alisema amekubali kutia saini mkataba na Yanga kwa sababu ana
mapenzi na klabu hiyo, aliyokuwa akiichezea kabla ya kujiunga na
Azam.
"Nimefurahi kurejea katika klabu, ambayo naipenda. Nilicheza Simba
kwa ajili ya kazi tu na nilicheza kwa nguvu zangu zote ili kupata
ushindi, lakini hawakuwa na imani na mimi,"alisema.
Ngasa aliwasili makao makuu ya Yanga akiwa amefutana na Mwenyekiti
wa Yanga, Yussuf Manji, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Abdalla
Bin Kleb, mjumbe wa kamati ya usajili, Seif Ahmed 'Magari' na
mjumbe wa baraza la wadhamini, Francis Kifukwe.
Bin Kleb alisema ujio wa mchezaji huyo utaiongezea nguvu Yanga na
kwamba walimsaka mchezaji huyo kwa miezi sita kabla ya kufanikiwa
kumshawishi arejee nyumbani.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema Ngasa ni
mchezaji mahiri nchini hivyo kurejea kwake Yanga ni faraja kubwa
kwa klabu hiyo.
Ngasa alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza 2006 akitokea Kagera
Sugar, ambayo ilimsajili kutoka Toto Africans. Mshambuliaji huyo
alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu
ya West Ham, 2009 kabla ya kwenda kujaribiwa Seattle Sounders ya
Marekani.
Sunday, May 19, 2013
SIMBA, YANGA ZAINGIZA MIL 500/-
MECHI ya watani wa jadi Simba na Yanga la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyochezwa jana (Mei 18 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa mabingwa wapya Yanga kushinda mabao 2-0 imeingiza sh. 500,390,000.
Mechi hiyo namba 180 ambayo ilikuwa kati ya saba la kuhitimisha ligi hiyo msimu wa 2012/2013 ilishuhudiwa na watazamaji 57,406 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,970,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,330,677.97.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 19,039 na kuingiza sh. 95,195,000 wakati kile cha sh. 7,000 kiliingiza watazamaji 17,647 na kupatikana sh. 123,515,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 63,036,064.81, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 37,821,638.88, Kamati ya Ligi sh. 37,821,638.88, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,910,819.44 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,708,415.12.
YANGA NG'ARING'ARI
TIMU ya soka ya Yanga jana iliichapa Simba mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wauaji wa Simba katika mechi hiyo walikuwa washambuliaji Didie Kavumbagu na Hamisi Kiiza, bao moja katika kila kipindi.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kumaliza ligi hiyo ikiwa na pointi 60 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 55 na Simba yenye poinri 45.
Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tano ya mchezo baada ya kuuwahi mpira wa juu, kufuatia kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima.
Simba ilipata nafasi ya kusawazisha dakika ya 27 baada ya Mrisho Ngassa kuangushwa kwenye eneo la hatari na mabeki Nadir Cannavaro na Kevin Yondan, lakini mkwaju wa Mussa Mudde ulipanguliwa na Ally Mustafa ‘Barthez’ kabla ya kipa huyo kuuchupia na kuudaka.
Kiiza aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 62 baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti la kinyumenyume mpira wa krosi uliopigwa na Simon Msuva kutoka pembeni ya uwanja.
Mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro alijikuta akijeruhiwa dakika ya 87 wakati akiwa anaamua ugomvi kati ya beki Masoud Nassor Chollo wa Simba na mshambuliaji Didier Kavumbagu wa Yanga na kutibiwa kwa dakika mbili.
Thursday, May 16, 2013
KIEMBA, CHOLO, KAZIMOTO WATEMWA TAIFA STARS
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' Kim Poulsen, amewaacha wachezaji watano katika kikosi chake kitakachoingia kambini kujiwinda na mchezo dhidi ya Morocco.
Wachezaji hao na timu wanazotoka ni Issa Rashid na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Nassor Masoud ‘Chollo’, Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba (Simba).
Katika timu hiyo, Poulsen amemuita kipa wa Yanga Ally Mustafa 'Bartez' na Zahor Pazi wa JKT Ruvu ambao walikuwa nje ya timu hiyo kwa muda.
Poulsen alisema wachezaji hao wataingia kambini Mei 20 kujiwinda na mchezo dhidi ya Morocco huku pia wakijiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Sudan.
Kocha huyo alisema timu yake itacheza na Sudai Juni 2 mwaka huu kabla ya kwenda Morocco na kusema mchezo huo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake.
Alisema tayari programu ya kambi ya timu hiyo imekwishaandaliwa na ni matarajio yake kuwa timu itajiandaa vyema na kufanikisha malengo yake.
Stars iliyopo kundi C na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba.
Kikosi kamili cha timu hiyo kinaundwa na makipa Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga), Juma Kaseja wa (Simba), Mwadini Ally na Aishi Manula (Azam).
Mabeki ni Erasto Nyoni, Aggrey Morris (Azam), Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Shomary Kapombe (Simba), na Yahya Mudathir (Azam).
Viungo ni Haroun Chanongo na Mrisho Ngassa (Simba), Simon Msuva, Frank Domayo na Athumani Iddi ‘Chuji’ (Yanga), Salum Abubakar, Vicent Barnabas, Khamis Mcha ‘Vialli’ (Azam) wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), John Bocco(Azam FC), Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Zahor Pazi (JKT Ruvu).
SHOMARI KAPOMBE: SINA MPANGO NA YANGA
JINA la Shomari Kapombe kwa sasa limetawala katika vinywa vya mashabiki wengi wa soka nchini. Ni kutokana na umahiri wake wa kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani na pia uwezo wake wa kupanda mbele kusaidia mashambulizi. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, beki huyo anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka.
SWALI: Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa kwamba uko mbioni kuondoka katika kikosi cha Simba na kujiunga na mojawapo kati ya timu za Yanga na Azam FC. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Kusema ule ukweli, kwa sasa sina mpango wowote wa kuondoka Simba na kujiunga na Yanga au Azam. Ninachokifikiria kwa sasa ni kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi. Tayari kuna klabu mbili, moja ya Uholanzi na nyingine ya England zimeshaonyesha nia ya kunifanyia majaribio. Hicho ndicho ninachokifikiria kwa sasa.
Lengo langu ni kuwa na maisha mazuri zaidi kutokana na kucheza soka. Nataka kutumia kipaji na uwezo wangu kunufaika kisoka. Naushukuru sana uongozi wa Simba kwa kunilea vizuri na kunifikisha hapa nilipo hadi nikapewa unahodha msaidizi wa Simba.
Na kwa kuweka mambo wazi, sijawahi kufanya mazungumzo yoyote na viongozi wa Yanga au Azam kuhusu kujiunga nazo. Nawahakikishia viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kwamba nitaendelea kuwa mchezaji wao hadi mipango yangu ya kwenda nje itakapofanikiwa.Nawaomba watu wanaovumisha habari hizo waache mara moja.
SWALI: Ni klabu zipi ambazo zimekuomba ukafanye majaribio ya kucheza soka ya kulipwa?
JIBU: Ofa ya kwanza inatoka kwa klabu ya Sunderland ya England na nyingine imetoka Uholanzi, lakini sina hakika na jina la timu. Na nitakwenda huko baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu na kwa baraka za uongozi wa Simba.
SWALI: Kwa sasa wewe na wachezaji wenzako wa Simba mnajiandaa kucheza na Yanga katika mechi ya mwisho ya ligi kuu itakayochezwa Mei 18 mwaka huu huku baadhi ya wachezaji wenu nyota wakiwa wamesimamishwa. Unadhani wewe na wachezaji wenzako chipukizi wanaopewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza hivi sasa mtaweza kuhimili mechi hiyo?
JIBU: Kuwepo kwa wachezaji wengi chipukizi kwenye kikosi chetu kumeleta changamoto kubwa na pia kuongeza ushindani wa namba kwa vile kila mchezaji anacheza kwa kujituma. Lengo la kila mmoja ni kuendelea kuwemo kwenye kikosi cha Simba msimu ujao.
Hata mimi nimeshaanza kupata wasiwasi kuhusu namba yangu kwa sababu hawa vijana wameanza kunitisha na kunilazimisha nifanye mazoezi kwa bidii zaidi ili kujihakikishia namba. Ni vijana wazuri na wenye mwelekeo mzuri si kwa Simba tu, bali hata Taifa Stars.
Kuhusu mechi yetu na Yanga, sina wasiwasi nayo kwa sababu naamini tunacho kikosi kizuri. Ninachowaomba mashabiki wetu ni kujenga imani kwa timu yao na kuamini inao uwezo wa kufanya vizuri.
Kwa upande wa wachezaji waliosimamishwa, hilo siwezi kulizungumzia
kwa sababu ni masuala ya kiuongozi na kiutawala, mimi ni mwajiriwa tu kama wachezaji wengine. Isipokuwa napenda kuwahakikishia mashabiki wetu kwamba wasiwe na wasiwasi.
SWALI: Kwa maana hiyo unataka kusema kwamba, kikosi chenu kinachoundwa na chipukizi wengi kinao uwezo wa kuifunga Yanga?
JIBU: Uwezo huo upo ndio sababu umeweza kuona katika mechi zetu za hivi karibuni tumekuwa tukiibuka na ushindi. Hao wanaotamba kuwa Yanga itaifunga Simba idadi kubwa ya mabao, wanakosea kwa sababu mchezo wa soka hauko hivyo. Mchezo wa soka unaweza kutoa matokeo tofauti na inavyotabiriwa.
SWALI: Una maoni gani kuhusu uamuzi wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kuunda kikosi cha pili cha timu hiyo?
JIBU: Binafsi nimefarijika sana kutokana na uamuzi wake huo kwa sababu utaongeza ushindani wa namba na kuwafanya wachezaji walioko Taifa Stars kuwa na bidii zaidi ili wasipokonywe namba na wale walioko kikosi cha pili.
SWALI: Unapenda kuwaeleza nini mashabiki wa soka nchini?
JIBU: Nawaomba waendelee kuiunga mkono timu yao ya Taifa (Taifa Stars) ili hatimaye iweze kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na zile za dunia.
Wednesday, May 15, 2013
SIMBA YAANDAA MPANGO MKAKATI
Simba Sports Club inapenda kuwataarifu wanachama na mashabiki wake kwamba imeingia makubaliano na Open University Consultancy Bureau (Hapa itafahamika kama “OCB”) kwa ajili ya kuandaa mpango mkakati wa klabu (Strategic Plan).
Mchakato huo unaanza mara moja na OCB wameshaandaa timu yao inayoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Prof. Tolly Mbwette ambapo ili kufanikisha hilo imebidi kuunda kamati ya marejeo ya Simba SC (Referral committee) ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kuiongoza OCB :-
1. Kuhusu makundi/watu/maeneo yatakayotumiwa kufanya utafiti.
2. Kunyambulisha kitaalamu nguvu, mianya na maeneo ya maboresho ya mfumo mzima wa Simba SC (SWOT analysis)
3. Kupitia mpango mkakati ukishaandaliwa baada ya kukusanya maoni ya wanachama, wadau na mashabiki wa klabu kabla ya kuupeleka katika kamati ya utendaji kwa kupitishwa ili ukapitishwe na mkutano mkuu wa wanachama.
Katika kikao cha kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kilichofanyika tarehe 8/5/2013 Referal Committee ya Simba Sports Club iliyochaguliwa ni:-
1. Joseph Itang’are
2. Swedy Mkwabi
3. Francis Waya
4. Ramesh Patel
5. Evance Aveva
6. Mulamu Ng’hambi
7. Salim Mhene
8. Mtemi Ramadhani
9. Moses Basena
10. Henry Tandau
11. Omary Gumbo
12. Michael Wambura
13. Glory Ngahyoma
14. Crensencius Magori
15. Honest Njau
16. Ruge Mutahaba
17. Evodius Mtawala
18. Dr Mwafyenga
Kikao cha kwanza kati ya OCB na Kamati husika kitakuwa siku ya tarehe 25/5/2013.
Uongozi wa Simba Sports Club unawataarifu wanachama na wadau kwamba, mpango mkakati huu ndio mwanzo wa mabadiliko ya klabu kuelekea katika kujiendesha kiweledi (professionalism) kwani utabainisha malengo ya klabu kwa kipindi maalumu yakiwemo masuala muhimu kama ujenzi wa uwanja, academy set up, miundo mbinu ya klabu, masuala ya biashara za klabu yakilenga kukuza taswira (brand) ili kufanikisha mauzo ya bidhaa zenye nembo ya klabu, malengo ya mafanikio ya ndani ya uwanja, kujiwekea kiwango/kipimo cha utendaji wa klabu na wanachama (brand goodwill) ili kuvutia wawekezaji.
Mpango mkakati huo pamoja na hayo pia utaweka mipango hiyo katika uhalisia wa utekelezaji na muda wa kutekeleza masuala hayo, jambo litakalofanikisha kuleta kipimo cha utendaji wa uongozi na watendaji wa klabu katika uwajibikaji kwa wadau na wanachama wa klabu.
Mpango mkakati huo utakuwa tayari kwa ajili ya kuingizwa katika mkutano mkuu wa klabu wa mwaka 2013/2014.
Imetolewa na
Evodius Mtawala
Katibu Mkuu,
Simba Sports Club.
Mchakato huo unaanza mara moja na OCB wameshaandaa timu yao inayoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Prof. Tolly Mbwette ambapo ili kufanikisha hilo imebidi kuunda kamati ya marejeo ya Simba SC (Referral committee) ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kuiongoza OCB :-
1. Kuhusu makundi/watu/maeneo yatakayotumiwa kufanya utafiti.
2. Kunyambulisha kitaalamu nguvu, mianya na maeneo ya maboresho ya mfumo mzima wa Simba SC (SWOT analysis)
3. Kupitia mpango mkakati ukishaandaliwa baada ya kukusanya maoni ya wanachama, wadau na mashabiki wa klabu kabla ya kuupeleka katika kamati ya utendaji kwa kupitishwa ili ukapitishwe na mkutano mkuu wa wanachama.
Katika kikao cha kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kilichofanyika tarehe 8/5/2013 Referal Committee ya Simba Sports Club iliyochaguliwa ni:-
1. Joseph Itang’are
2. Swedy Mkwabi
3. Francis Waya
4. Ramesh Patel
5. Evance Aveva
6. Mulamu Ng’hambi
7. Salim Mhene
8. Mtemi Ramadhani
9. Moses Basena
10. Henry Tandau
11. Omary Gumbo
12. Michael Wambura
13. Glory Ngahyoma
14. Crensencius Magori
15. Honest Njau
16. Ruge Mutahaba
17. Evodius Mtawala
18. Dr Mwafyenga
Kikao cha kwanza kati ya OCB na Kamati husika kitakuwa siku ya tarehe 25/5/2013.
Uongozi wa Simba Sports Club unawataarifu wanachama na wadau kwamba, mpango mkakati huu ndio mwanzo wa mabadiliko ya klabu kuelekea katika kujiendesha kiweledi (professionalism) kwani utabainisha malengo ya klabu kwa kipindi maalumu yakiwemo masuala muhimu kama ujenzi wa uwanja, academy set up, miundo mbinu ya klabu, masuala ya biashara za klabu yakilenga kukuza taswira (brand) ili kufanikisha mauzo ya bidhaa zenye nembo ya klabu, malengo ya mafanikio ya ndani ya uwanja, kujiwekea kiwango/kipimo cha utendaji wa klabu na wanachama (brand goodwill) ili kuvutia wawekezaji.
Mpango mkakati huo pamoja na hayo pia utaweka mipango hiyo katika uhalisia wa utekelezaji na muda wa kutekeleza masuala hayo, jambo litakalofanikisha kuleta kipimo cha utendaji wa uongozi na watendaji wa klabu katika uwajibikaji kwa wadau na wanachama wa klabu.
Mpango mkakati huo utakuwa tayari kwa ajili ya kuingizwa katika mkutano mkuu wa klabu wa mwaka 2013/2014.
Imetolewa na
Evodius Mtawala
Katibu Mkuu,
Simba Sports Club.
UFAFANUZI KUHUSU LIGI YA MABINGWA WA MIKOA
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilianza tarehe 12 Mei 2013 ikishirikisha klabu bingwa za mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa mikoa ya Pwani na Manyara ambayo kutokana na sababu tofauti ilishindwa kuwasilisha majina ya klabu zake hadi siku ya mwisho iliyowekwa na Kamati ya Mashindano, yaani tarehe 10 Mei 2013.
Suala la kukosekana kwa wawakilishi wa mikoa hiyo miwili limezua maswali mengi kiasi kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linalazimika kutoa ufafanuzi kwa faida ya wadau wote wa mpira wa miguu.
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, ambayo ni mpya baada ya TFF kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu, ilipangwa kuanza tarehe 5 Mei 2013, lakini hadi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, yaani tarehe 2 Mei 2013 mikoa michache ndiyo iliyokuwa imemaliza ligi zao na kupata mabingwa.
Kuchelewa huko kwa mikoa kumaliza ligi zao kuliilazimisha Kamati ya Mashindano ya TFF kuongeza muda wa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi hao hadi tarehe 10 Mei 2013 na hivyo siku ya kuanza kwa Ligi kusogezwa mbele hadi tarehe 12 Mei 2013.
Hadi kufikia tarehe hiyo mpya ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, ni mikoa sita tu iliyofaidika na kuongezwa huko kwa muda na kupata wawakilishi wake. Mikoa hiyo ni Iringa, ambayo pamoja na kuongezwa kwa muda, iliandika barua ya kuihakikishia Kamati ya Mashindano kuwa itapata bingwa kabla ya kuisha kwa siku ya tarehe 10 Mei 2013.
Mikoa mingine ni Lindi, Mtwara, Geita, Tabora na Dodoma.
Mkoa wa Manyara haukuweza kumaliza ligi yake hadi mwisho wa siku ya tarehe 10 Mei 2013 na hivyo Kamati ya Mashindano iliyosubiri majina hadi saa 12:00 jioni siku hiyo kuamua kuwaondoa wawakilishi wa Manyara kwenye ratiba.
Awali, Kamati ya Mashindano iliamua kuwa ratiba ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ipangwe tarehe 7 Mei 2013, ikishirikisha mikoa ambayo ilishapata mabingwa wake, lakini baada ya kuona baadhi ya mikoa ilikuwa haijakamilisha ligi zake, Kamati iliamua kuwa ratiba ipangwe kwa kutumia majina ya mikoa kwa matumaini kuwa hadi kufikia tarehe 10 Mei 2013, mikoa itakuwa imeshapata wawakilishi wake na kwa kuwa ratiba inahusu mikoa jirani, ingekuwa rahisi kwa timu kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Lakini Mkoa wa Manyara haukuweza kufanya hivyo na Kamati kulazimika kuuondoa kwenye ratiba kutokana na kushindwa kukidhi utashi huo.
Mkoa mwingine ambao uliondolewa kwenye ratiba ni Pwani ambayo pamoja na kutuma jina la mwakilishi wake, Kamati ilipokea malalamiko kutoka klabu zilizoshiriki Ligi ya Mkoa, zikidai kuwa jina la bingwa wa Pwani lililowasilishwa TFF lilikuwa batili kwa kuwa klabu ya Kiluvia United haikustahili kushiriki Ligi ya Mkoa kutokana na ukweli kuwa haijasajiliwa mkoani Pwani na wala haikushiriki ligi ya mkoa msimu uliopita. Kamati ya Mashindano iliiondoa Pwani kwenye ratiba na kulirudisha suala hilo mkoani.
Ingawa Katibu wa Pwani alijaribu kuishawishi Sekretarieti ya TFF iliangalie suala hilo kwa undani zaidi, Sekretarieti ilimjibu kuwa lilishafanyiwa uamuzi na Kamati, hivyo uamuzi huo usingeweza kutenguliwa na kumshauri katibu huyo arejee mkoani kwake kuwasiliana na viongozi wenzake kuona ni jinsi gani mkoa unaweza kunusuru hali hiyo kwa kufanya uamuzi ambao ungeuwezesha mkoa kupata mwakilishi.
Kwa mantiki hiyo, masuala ya Manyara na Pwani yalikuwa ndani ya uongozi wa mikoa husika na si Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kuwa Kamati ilitaka ipatiwe jina la bingwa ambaye alipatikana kwa mujibu wa mfumo mpya wa Ligi ya Mikoa.
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na hivyo timu zilizokutana tarehe 12 Mei 2013, zitarudiana mwishoni mwa wiki hii na kupatikana timu zitakazosonga mbele kwenye raundi nyingine hadi timu tatu bora zitakazopanda daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakapopatikana.
Ligi za Mikoa, kwa mujibu wa kanuni mpya, zinatakiwa ziwe na timu kati ya 16 na 20 na zinatakiwa zicheze mechi mbili za nyumbani na ugenini, hata kama zitakuwa zinatumia uwanja mmoja.
Uamuzi wa kubadilisha mfumo huo ulifanywa ili kuhakikisha kuwa mikoa inakuwa na na mashindano kwa mwaka mzima na hivyo kuiwezesha mikoa kujikita katika kutafuta mbinu za kupata fedha na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwenye mikoa yao.
Uamuzi huo pia unasaidia kupunguza mtindo wa wachezaji kuzunguka klabu tofauti katika msimu mmoja kwa kuwa wanalazimika kutulia kwenye klabu moja hadi muda wa usajili unapofika.
Pamoja na wachezaji kutulia sehemu moja kwa muda mrefu, pia walimu wanapata fursa ya kujikita vizuri kwenye programu zao kwa kuwa wanakuwa na uwezo wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji wao.
Pamoja na hayo yote, mfumo huo utasaidia kurudisha msisimko kwenye mikoa na hivyo kutoa fursa kwa vijana wengi wenye vipaji kuonekana na kuendelezwa.
TFF inatoa wito kwa viongozi wa mikoa kuanza kubuni sasa mikakati ya kuendesha ligi hizo msimu unaokuja kwa kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya kuongeza muda kwa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao.
KUZIONA SIMBA, YANGA BUKU TANO
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 18 mwaka huu) kitakuwa sh. 5,000. Kiingilio hicho kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.
Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.
Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Martin Saanya kutoka Morogoro ambapo atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha, na Jesse Erasmo kutoka Morogoro. Mwamuzi wa akiba ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Leslie Liunda
DRFA KUENDESHA KOZI ZA MAKOCHA, WAAMUZI
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kinatarajia kuendesha kozi ya makocha pamoja na waamuzi ili kusaidia kuinua kiwango cha mchezo huo.
Katika kikao cha Kamati ya Ufundi, kilichoketi Mei 11 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Harbours Club, chini ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Kanakamfumu, alisema kozi ya ualimu wa mpira wa miguu ngazi ya cheti (Inter-Mediate), ambayo imekuwa kwenye mahitaji makubwa, itaanza Juni 3 hadi 28 mwaka huu.
Kozi itakuwa kwa siku 10, tunatarajia kupata washiriki watakaofikia 60, iwapo idadi hiyo itafikia na kuzidi, kutakuwa na awamu mbili za wanafunzi ambao kisheria darasa linatakiwa kuwa na wanafunzi 35 hadi 40.
Watu wataanza kujiandikisha kuanzia Mei 15 hadi 26 na awamu ya kwanza ya kozi itaanza Juni 3 hadi 14 na ya pili itaanza Juni 17 hadi 28.
Ada ya ushiriki itakuwa Sh 50,000 na itahusisha gharama ya kuchukulia fomu 5,000 na zilizobaki ni gharama ya cheti, kitambulisho pamoja na chakula cha mchana.
Kwa upande wa kozi ya waamuzi itaanza Septemba 3 hadi 9 mwaka huu na ada itakuwa Sh 25, 000.
Fomu zitapatikana katika ofisi za Mikoa ya kisoka, TEFA, IDFA,KIFA na DRFA na kozi zote zitafanyika kwenye ukumbi huo wa Harbours Club.
Kamati hiyo imepanga kukutana Mei 19 kwenye Ukumbi huo wa Harbours Club saa tatu asubuhi na viongozi wote wa timu za wanawake kutathimini michango yao kwa ukuzaji wa soka la Wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam.
Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya DRFA, Kennedy Mwaisabula, Jovin Ndimbo (Mwenyekiti Kamati ya Waamuzi), Benny Kisaka (Mwenyekiti Kamati ya Soka la Wanawake), Abdallah Mitole (Mjumbe kamati ya waamuzi), Sijali Juma (Mjumbe kamati ya waamuzi), Richard Mbuya (Mjumbe kamati ya Soka la Wanawake) na Dk. Maneno Tamba (Mjumbe Kamati ya Soka la Wanawake).
Imetolewa na Mohamed Mharizo
Ofisa Habari wa DRFA
Friday, May 10, 2013
SIMBA, YANGA KUKUTANA DARFUR
TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya kuwa, maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo yanakwenda vizuri.
Musonye alisema Yanga itashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa mtetezi wakati Simba itashiriki ikiwa bingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Yanga imetwaa kombe hilo mara mbili mfululizo, mwaka jana na mwaka juzi wakati mashindano hayo yalipofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Musonye amezihakikishia nchi wanachama wa baraza hilo kuwepo kwa usalama wa kutosha katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.
Musonye alisema jana kuwa, alifanya ziara katika jimbo hilo hivi karibuni na kuridhishwa na hali ya usalama.
CECAFA imepanga michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame ifanyike katika jimbo hilo kwa lengo kulisaidia kimaendeleo na pia kuimarisha amani.
"Tumechukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa, wakati wote wa mashindano hayo kutakuwa na usalama wa kutosha kwa ajili ya timu zote,"alisema Musonye.
"Tumekutana na viongozi wa jimbo hilo na viongozi wa serikali ya Sudan na wote wametuhakikishia kuwa, maandalizi yanakwenda vizuri na usalama upo wa kutosha,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Musonye, baraza lake linatarajia kutangaza majina ya timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo baada ya kuwasiliana na vyama vya soka vya nchi wanachama.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya kuwa, maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo yanakwenda vizuri.
Musonye alisema Yanga itashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa mtetezi wakati Simba itashiriki ikiwa bingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Yanga imetwaa kombe hilo mara mbili mfululizo, mwaka jana na mwaka juzi wakati mashindano hayo yalipofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Musonye amezihakikishia nchi wanachama wa baraza hilo kuwepo kwa usalama wa kutosha katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.
Musonye alisema jana kuwa, alifanya ziara katika jimbo hilo hivi karibuni na kuridhishwa na hali ya usalama.
CECAFA imepanga michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame ifanyike katika jimbo hilo kwa lengo kulisaidia kimaendeleo na pia kuimarisha amani.
"Tumechukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa, wakati wote wa mashindano hayo kutakuwa na usalama wa kutosha kwa ajili ya timu zote,"alisema Musonye.
"Tumekutana na viongozi wa jimbo hilo na viongozi wa serikali ya Sudan na wote wametuhakikishia kuwa, maandalizi yanakwenda vizuri na usalama upo wa kutosha,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Musonye, baraza lake linatarajia kutangaza majina ya timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo baada ya kuwasiliana na vyama vya soka vya nchi wanachama.
MSIBA MZITO MAN UNITED
LONDON, England
KLABU ya Manchester United ya England imethibitisha kuwa, Kocha wake mkuu, Sir Alex Ferguson atastaafu mwishoni mwa msimu huu.
Fergie mwenye umri wa miaka 71, anaondoka Old Trafford akiwa na rekodi ya kutwaa mataji 13 ya ligi kuu ya England.
Kocha huyo raia wa Scotland alisema jana kuwa, uamuzi wake wa kustaafu ni kati ya mambo aliyokuwa akiyafikiria na haikuwa rahisi.
“Ilikuwa muhimu kwangu kuiacha taasisi ipo imara na muonekano mzuri na naamini nimefanya hivyo,"alisema kocha huyo kipenzi cha mashabiki wa Manchester United.
"Ubora wa kikosi kilichotwaa ubingwa wa ligi hii na uwiano wa umri uliopo, wapo fiti kuendeleza mafanikio katika kiwango cha juu na kuzingatia mpango wa muda mrefu wa kukuza vijana," aliongeza kocha huyo na kusisitiza kuwa, klabu itazidi kuendelea kung'ara.
“Vifaa vyetu vya mazoezi ni kati ya vilivyo bora katika ulimwengu wa michezo na nyumbani kwetu Old Trafford panapendeza na kuchukuliwa kati ya viwanja bora duniani.
“Kwa upande mwingine, nina furaha kupewa majukumu yote ya mkurugenzi na balozi wa klabu. Kwa shughuli hizi, pamoja na manufaa yangu mengine mengi, natazama mbele kwa baadaye," alisema.
Ferguson alisema anaishukuru familia yake kwa upendo wao kwake na kumuunga mkono kwa kipindi chote alichokuwa akiitumikia Manchester United akiwa kocha.
"Mke wangu Cathy amekuwa ufunguo muhimu katika kazi yangu kwa uvumilivu na kunipa moyo. Maneno hayatoshi kuelezea hii ina maana gani kwangu,"alisema kocha huyo anayependa kutafuna 'bazoka' muda wote wa mchezo.
“ Kwa wachezaji wangu na wafanyakazi, waliopita na waliopo, napenda kuwashukuru wote kwa kucheza katika kiwango cha juu na juhudi zilizosaidia kutwaa mataji mengi ya kukumbukwa. Bila ya mchango wao, historia ya klabu hii isingefika ilipo,"alisema.
“Katika miaka yangu ya mwanzo, nikisaidiwa na bodi na hasa Sir Bobby Charlton, walinifanya nijiamini na kupata muda wa kuijenga klabu ya soka, kuliko kuwa timu ya mpira.
“Zaidi ya muongo mmoja uliopita, familia ya Glazer ilinipa ofa za kuweza kuiongoza Manchester United kwa uwezo wangu bora na nilibahatika kufanya kazi na mtendaji mkuu mwenye kipaji na kuaminika, David Gill. Ukweli wote wamenifurahisha.
“Nawashukuru mashabiki kwa kutuunga mkono kwa miaka mingi, kumekuwa na msisimko wa kina. Imekuwa heshima kubwa kupata bahati ya kuongoza klabu yenu na kuwa kipenzi cha Manchester United.”
Mbali ya kutwaa mataji 13 ya ligi, Sir Ferguson pia aliiongoza Manchester United kutwaa vikombe viwili vya Ulaya, mataji matano ya FA na vikombe vinne vya Kombe la Ligi.
Mechi ya mwisho kuwaongoza Mashetani Wekundu itakuwa dhidi ya West Bromwich itakayochezwa Mei 19 mwaka huu, siku ambayo msimu wa ligi kuu England utafungwa.
Kustaafu kwa kocha huyo kunatoa nafasi kubwa kwa mikoba yake kurithiwa na aidha Davis Moye wa Everton au Jose Mourinho wa Real Madrid ya Hispania.
Makocha hao wawili ndio chaguo namba moja la Ferguson kuwaachia mikoba ya kuinoa Manchester United, ambayo ina mashabiki lukuki kote duniani.
Tayari Moyes ameshakaririwa na baadhi ya vyombo vya habari vya England akiwaaga mashabiki wa klabu hiyo huku kukiwa na tetesi kubwa Mourinho anataka kurudi katika klabu yake ya zamani ya Chelsea.
UCHAGUZI MKUU WA TFF SASA SEPT 29
HATIMAYE uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
umepangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.
Uchaguzi huo utafanyika baada ya mkutano wa dharula wa marekebisho
ya katiba uliopangwa kufanyika Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga
alisema tarehe hizo zimepangwa na kikao cha dharula cha kamati ya
utendaji ya shirikisho hilo kilichofanyika mjini Dar es Salaam
jana.
Tenga alisema kamati hiyo imepokea maagizo ya Shirikisho la Soka la
Dunia (FIFA) na kupanga utekelezaji wake unaoelekeza cha kufanya na
siyo TFF au mtu mwingine anayeweza kuongeza jambo lingine.
Rais huyo alisema FIFA iliagiza kuundwa kwa kamati ya maadili,
kamati ya rufani ya maadili na kufanya marekebisho ya katiba kabla
ya kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi na wagombea waliokuwepo na
wengine wapya waruhusiwe kugombea.
"Tumejitahidi kuhakikisha uchaguzi uwe kabla ya Oktoba 30 mwaka huu
kama FIFA walivyotuagiza, tumefanya kikao cha dharula na kupanga
tarehe za mkutano mkuu wa uchaguzi,"alisema Tenga.
Aliongeza kuwa, kazi kubwa itakuwa ni kutayarisha kanuni hizo kwa
kuwa kamati za maadili lazima ziwe na kanuni zake na kuhakikisha
hakuna mgongano kati ya kanuni za nidhamu na kanuni za maadili.
Alisema kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, rasimu ya mwanzo ya
kanuni hizo inatakiwa iwe imetoka kufikia Mei 30 na Juni 15 mwaka
huu.
Tenga alisema kamati ya utendaji ya TFF itakutana kwa ajili ya
kupokea mapendekezo hayo na baada ya kuyapitisha, itayapeleka FIFA.
Alisema yaatifa ya mkutano mkuu wa dharula, ambayo kikatiba ni siku
30, itatolewa Juni 12 au 13 na baada ya mkutano mkuu wa dharula wa
marekebisho ya katiba, kamati ya utendaji itakutana kati ya Julai
14 a 15 mwaka huu kuunda kamati ya maadili na kamati ya rufani ya
maadili ili kuruhusu mchakato wa uchaguzi uanze.
Uchaguzi huo umetokana na FIFA kuagiza mchakato wake uanze upya
baada ya kuibuka kwa mgogoro mkubwa kutokana na baadhi ya wagombea
kuenguliwa. Uchaguzi wa awali ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka
huu.
SERIKALI YAINGILIA KATI SAKATA LA JAYDEE NA RUGE
SERIKALI imeamua kuingilia kati sakata la mwanamuziki nyota nchini, Judith Wambura 'LadyJaydee' na uongozi wa kituo cha redio cha Clouds FM cha mjini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alisema jana kuwa, wanatarajia kuzikutanisha pande hizo mbili ili kupata suluhu na mgogoro uliojitokeza kati yao.
Makalla alisema lengo la kuzikutanisha pande hizo mbili ni kutaka kupata ukweli wa nini kilichotokea na kusababisha kuzuka kwa mgogoro huo.
Naibu Waziri alisema malumbano yanayoendelea kati ya JayDee na viongozi waandamizi wa Clouds FM, hayana tija na yanaweza kuukuza zaidi mgogoro huo na kusababisha chuki na visasi.
Makalla alisema yuko tayari kukutana na JayDee na uongozi wa Clouds FM wakati wowote ili kumaliza tofauti zilizojitokeza kati yao.
"Nawasihi sana ndugu zangu hawa, jambo hili halipendezi kwa jamii, hivyo tunapaswa kukaa na kulimaliza kwa njia ya mazungumzo,"alisema Makalla.
Alisema anaamini mzozo uliozuka kati ya pande hizo utamalizika kwa kuwa serikali haifurahii kuona wasanii na viongozi wa wasanii wakilumbana hadharani.
Sakata kati ya JayDee na uongozi wa Clouds FM lilizuka Mei Mosi mwaka huu baada ya JayDee kuandika kwenye mtandao wake akimtaka Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wa Clouds FM wasihudhurie mazishi yake.
Katika taarifa yake hiyo, JayDee aliwataja viongozi hao wawili kuwa wamekuwa mstari wa mbele kutaka kummaliza kimuziki, ikiwa ni pamoja na kuidhoofisha bendi yake ya Machozi kwa kuwalaghai wanamuziki wake.
Siku chache baadaye, Ruge alijibu tuhuma hizo za JayDee kwa madai kuwa, zinaonyesha wazi jinsi mwanamuziki huyo anavyotapatapa.
Thursday, May 9, 2013
KAVUMBAGU KUFUNGASHIWA VIRAGO YANGA, BAHANUZI AKALIA KUTI KAVU
KLABU ya Yanga imepanga kuwaacha wachezaji wake kadhaa nyota kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kutokana na kushuka kwa viwango vyao vya soka.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, mpango wa kuwaacha nyota hao pia utawahusu baadhi ya wachezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa nyota wa kigeni watakaoachwa msimu ujao ni pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu kutoka Burundi.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, tayari benchi la ufundi la Yanga limeshaanza kuandaa ripoti ya ushiriki wa kila mchezaji katika msimu huu kabla ya kuikabidhi kwa uongozi.
Tayari baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga wameshaanza kupatwa na hofu baada ya kuwepo kwa tetesi kuhusu kuachwa kwao.
Kavumbagu alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Vital'O ya Burundi na alikuwa mmoja wa washambuliaji wa kutegemewa kabla ya kiwango chake kuonekana kushuka katika mzunguko wa pili.
Mshambuliaji huyo mrefu na mwenye umbo lililojaa, alimudu kumweka benchi Jerry Tegete katika mzunguko wa kwanza kabla ya kibao kugeuka mwishoni mwa mzunguko wa pili.
Hivi karibuni, Kavumbagu alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akilalamika kuwa, baadhi ya wachezaji wenzake wamempiga 'juju' kwa lengo la kushusha kiwango chake.
"Uongozi unataka timu iwe na washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao katika michuano ya Kombe la Kagame na klabu bingwa Afrika,"kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga.
Wachezaji wengine wanaotajwa kukalia kuti kavu ni pamoja na mshambuliaji Saidi Bahanuzi, ambaye alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar.
Bahanuzi alionekana kuwakera mashabiki wa Yanga wakati timu hiyo ilipomenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na kukosa mabao mengi.
Monday, May 6, 2013
SIMBA YAVUTA KASI
SIMBA jana ilizinduka katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba kuchupa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 26 na hivyo kuiondoa kwenye nafasi hiyo, Kagera Sugar.
Mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 14 baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Felix Sunzu, aliyemtoka beki, Ernest wa Ruvu Shooting.
Ruvu Shooting nusura isawazishe dakika ya 26 wakati Saidi Madega alipoingia na mpira ndani ya 18 na kufumua shuti lililowababatiza mabeki wa Simba.
Abdalla Seseme nusura aifungie Simba bao dakika ya 36 baada ya kupewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari la Ruvu Shooting, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.
Ruvu Shooting ilisawazisha dakika ya 52 kwa bao lililofungwa na Abdulrahman Mussa kwa shuti lililomshinda kipa Abel Dhaira wa Simba.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Christopher Alex baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Ruvu Shooting kabla ya Ismail Mkoko kuongeza la tatu dakika ya 89.
Sunday, May 5, 2013
TAIFA STARS KUANZA COSAFA JULAI 6
Taifa Stars imepangwa kundi A la michuano ya Kombe la COSAFA ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Julai 6 mwaka huu jijini Lusaka, Zambia dhidi ya Shelisheli.
Upangaji ratiba (draw) wa mashindano hayo ulifanyika juzi (Mei 3 mwaka huu) jijini Lusaka ambapo timu nyingine zilizo na Taifa Stars katika kundi hilo ni Namibia na Mauritius. Kundi la Taifa Stars litachezea mechi zake jijini Lusaka.
Mechi ya pili ya Taifa Stars katika hatua ya makundi itakuwa Julai 8 mwaka huu dhidi ya Mauritius. Mechi ya mwisho katika hatua hiyo itakuwa Julai 10 mwaka huu dhidi ya Namibia.
Kundi B lina timu za Kenya (Harambee Stars), Botswana (Zebras), Lesotho na Swaziland. Hatua itakayofuata baada ya hapo ni ya mtoano (knockout) na kila kundi litatoa timu moja tu.
Iwapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itafuzu kwa hatua itakayofuata itacheza Julai 13 mwaka huu na Afrika Kusini (Bafana Bafana) ambayo pamoja na timu nyingine tano zimekwenda moja kwa moja katika hatua ya mtoano.
Nyingine zilizokwenda moja kwa moja hatua ya mtoano ni wenyeji Zambia, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Malawi ambazo kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ziko juu ya zile zilizoanzia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA itafanyika Julai 20 mwaka huu.
RATIBA RCL KUPANGWA J'NNE, LIGI KUANZA MEI 12
Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
DRFA YAZIPONGEZA RED CROSS, ABAJALO NA FRIENDS RANGERS
CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimezipongeza timu zake tatu zilizofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa, baada ya kumalizika kwa Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora Aprili 27 mwaka huu.
Timu hizo ni Red Coast, Abajalo na Friends Rangers, zitakazoungana na timu za mikoa mingine kucheza Ligi ya Mabingwa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya Usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema ligi hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu na kuzitaka timu zilizofuzu hatua hiyo kujipanga vizuri ili kuuwakilisha vyema mkoa na hatimaye kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
“Kwa niaba ya DRFA napenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza timu hizo kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuuwakilisha mkoa wa Dar es Salaam katika kutafuta kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao wa 2013/2014.
“Tunaamini watajiandaa vyema na kutuwakilisha vizuri katika ligi hiyo, kufanya kwao vizuri ndio itakuwa fahari yetu DRFA na wadau wa mpira wa miguu mkoa wa Dar es Salaam, tunawatakia kila la kheri na tupo pamoja katika kushirikiana nao.
Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora mkoa wa Dar es Salaam ilianza Aprili 15 mwaka huu ambapo ameziomba timu za Sharif Stars, Day Break na Boom FC zilizoshiriki ligi hiyo kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo.
BOCCO, MWANTIKA WAIPONZA AZAM
AZAM jana ilitolewa kiume katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa mabao 2-1 na FAR Rabat ya Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.
Kipigo hicho kimeifanya Azam itolewe kwa ushindi wa jumla wa idadi hiyo ya mabao, kufuatia timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam itabidi ijilaumu kutokana na mshambuliaji wake, John Bocco kukosa adhabu ya penalti dakika ya 85, ambayo ingeiwezesha kupata sare na kusonga mbele katika michuano hiyo.Shuti la Bocco liligonga mwamba wa juu wa goli.
Mbali na kukosa penalti, Azam ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake, David Mwantika kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya mchezaji wa FAR Rabat.
Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita lililofungwa na Bocco kwa mpira wa adhabu baada ya beki mmoja wa FAR Rabat kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Wamorocco walisawazisha bao hilo dakika sita baadaye kupitia kwa Abdelrahim Achchakir kwa mkwaju wa penalti baada ya Mwantika kumchezea rafu mbaya mchezaji mmoja wa FAR Rabat.
FAR Rabat nayo ilipata pigo dakika ya 35 baada ya beki wake, Achchakir kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Brian Umony.
Bao la pili la FAR Rabat lilifungwa na Mustafa Allaoui dakika ya 42 kwa shuti la mpira wa adhabu la umbali wa mita 25 na kumpita kipa Mwadini Ally.
Waziri Salum wa Azam naye alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kumchezea rafu Kaddioiu Yuossef.
Subscribe to:
Posts (Atom)













