KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 14, 2013

KIEMBA: NIMEFUNGA MJADALA



MSHAMBULIAJI Amri Kiemba amesema kwa sasa ameamua kufunga mjadala kuhusu mustakabali wake kisoka baada ya kutia saini mkataba mpya wa kuichezea Simba kwa miaka miwili.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Kiemba alisema si kweli kwamba alikuwa katika harakati za kurejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga.

"Unajua mimi si muongeaji sana. Wakati magazeti yanaandika mimi nimesaini mkataba na Yanga, nilikuwa nashangaa sana, lakini sikutaka kujibu. Sasa ukweli ni huu, nimeingia mkataba na Simba kwa miaka miwili zaidi,"alisema.

Kiemba alisema kwa sasa anaelekeza nguvu zake katika timu ya Taifa, Taifa Stars, ambayo inajiandaa kumenyana na Ivory Coast katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.

"Naamini mjadala wa Kiemba umekwisha salama, sasa ni zamu ya wengine,"alisema.

Kiemba alimwaga wino Simba juzi mbele ya Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are, maarufu kwa jina la Mzee Kinesi.

Kiungo huyo alimwaga wino Simba siku moja baada ya kurejea kutoka Morocco, ambako alikwenda kuichezea Taifa Stars katika mechi dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.

Kiemba alikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Morocco kutokana na kuifungia Taifa Stars bao la kujifariji kwa shuti kali la umbali wa mita zipatazo 25. Katika mechi hiyo, Taifa Stars ilichapwa mabao 2-1.

Baada ya mchezo huo, mashabiki wa soka wa Morocco walianza kumfuatafuata Kiemba wakiomba kupiga naye picha na walimtambua kwa urahisi kutokana na rasta zake.

LIGI YA MABINGWA YA MIKOA KUANZA KESHO


MECHI za kwanza za hatua ya tatu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao, zinatarajiwa kuchezwa keshokutwa.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, mechi za marudiano zinatarajiwa kuchezwa Juni 19 mwaka huu.

Wambura alisema Kamati ya Mashindano ya TFF ilikutana juzi mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kupitia ripoti za michezo iliyopita na kufanya uamuzi mbalimbali, ikiwemo mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars na Machava FC, ambayo haikuchezwa.

Ofisa huyo wa TFF alisema, Machava FC, ambayo ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Moshi kwa mabao 2-0, inaendelea katika hatua ya tatu kwa vile haikuhusika katika kukwamisha mchezo wa marudiano uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Wambura alisema Chama cha Soka cha Dodoma (DOREFA) kiliuhamishia mchezo huo kwenye Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa kinyume na maelekezo ya Kamati ya Mashindano ya TFF.

"Kamati katika kikao chake cha awali iliekeleza kuwa mechi zote za RCL zitachezwa makao makuu ya mikoa, isipokuwa kwa Morogoro ambapo timu ya Techfort FC iliruhusiwa kutumia Uwanja wa CCM Mkamba mjini Ifakara,"alisema.

Wambura alizitaja timu nane zilizofuzu kucheza raundi hiyo kuwa ni Friends Rangers ya Dar es Salaam, Kariakoo ya Lindi, Katavi Warriors ya Katavi, Kimondo SC ya Mbeya, Machava ya Kilimanjaro, Njombe Mji ya Njombe, Polisi Jamii ya Mara na Stand United FC ya Shinyanga.

Wakati timu nyingine zimefuzu kwa kushinda mechi zao za raundi ya pili, Njombe Mji imeingia hatua hiyo kwa kuwa timu yenye uwiano mdogo wa kufungwa (best looser) katika hatua ya pili.

Kwa mujibu wa ratiba, katika mechi za hatua hiyo, Kariakoo itamenyana na Friends Rangers, Machava FC na Stand United FC, Polisi Jamii na Katavi Warriors, Kimondo SC na Njombe Mji. Timu zilizoanza kutajwa ndizo zinazoanzia nyumbani.

Wambura alisema kamati ya mashindano imeagiza kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars na Machava FC, Mwijage Rugakingira wa Tanga, ambaye alikwenda uwanja wa Mgambo badala ya Uwanja wa Jamhuri kinyume na maelekezo ya TFF, aondolewe kwenye orodha ya makamishna.

Aliongeza kuwa, waamuzi wa mechi hiyo ambao nao walikwenda Mpwapwa badala ya Dodoma Mjini, wamepelekwa mbele ya Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kutokana na tukio hilo.

"Kamati ya Mashindano imekumbusha kuwa RCL ni mashindano yanayosimamiwa na TFF, hivyo maelekezo yoyote kuhusiana na mashindano hayo, yatatoka TFF na si mahali pengine popote. Msimamizi wa kituo hana mamlaka ya kubadili uwanja,"alisema.

Wambura alisema hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

AZAM YAMTOSA KASEJA



UONGOZI wa klabu ya Azam umesema hauna mpango wa kumsajili kipa namba moja wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Juma Kaseja.

Meneja Msaidizi wa Azam, Jemedari Saidi alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, kikosi chao kwa sasa kimekamilika katika idara zote.

Jemedari alisema kikosi cha Azam kinao makipa watatu walio kwenye kiwango cha juu kisoka, akiwemo kipa namba moja Mwadini Ally na Aishi Manula.

"Tumekuwa tukisia taarifa kupitia kwenye vyombo vya habari kwamba Azam ina mpango wa kumsajili Kaseja kwa ajili ya msimu ujao, lakini msimamo wetu ni kwamba hatutasajili mchezaji yeyote kutoka klabu za ligi kuu,"alisema.

"Uamuzi uliofikiwa na benchi la ufundi ni kwamba, tutawapandisha vijana wetu kutoka kikosi cha pili na tayari tumeshafanya hivyo. Pia hatuna mpango wa kusajili wachezaji wapya kutoka nje ya nchi,"aliongeza.

Kumekuwa na taarifa zenye utata kuhusu hatma ya Kaseja kwenye kikosi cha Simba baada ya mkataba wake kumalizika mwezi uliopita.

Viongozi wa klabu hiyo kongwe nchini wamekuwa wakivutana kuhusu kipa huyo, baadhi yao wakitaka aongezwe mkataba mpya na wengine wakitaka aachwe.

Alipoulizwa kuhusu hatma ya mchezaji huyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are alisema jana kuwa, itajulikana hivi karibuni.

"Kwa sasa sina la kusema, lakini wakati utakapofika, kila kitu kitakuwa wazi,"alisema.

Thursday, June 13, 2013

IVORY COAST KUTUA DAR LEO USIKU



SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA) limewateua waamuzi kutoka Algeria kuchezesha mechi kati ya timu ya Taifa, Taifa Stars na Ivory Coast.

Timu hizo mbili zinatarajiwa kumenyana Jumapili katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 204 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, waamuzi walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo ya kundi C wataongozwa na Charef Mehdi Abid atakayekuwa mwamuzi wa kati.

Aliwataja waamuzi wengine kuwa ni Hamza Hammou na Bouabdallah Omari wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Sofiane Bousseter.

Wambura alisema Abdi na wezake wanatarajiwa kutua nchini kesho saa 12 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri (EgyptAir).

Aliongeza kuwa mtathmini wa waamuzi wa mechi hiyo atakuwa Athanase Nkubito kutoka Rwanda, ambaye naye atatua nchini kesho saa 12 jioni kwa ndege ya RwandAir.

Alisema kamishna wa mechi hiyo ni Bernard Mfubusa kutoka Burundi, ambaye anatarajiwa kuwasili nchini kesho saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.

Kwa mujibu wa Wambura, maofisa wote watakaosimamia mechi hiyo wanatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu kurejea kwao.

Wakati huo huo, msafara wa timu ya Taifa ya Ivory Coast (The Elephants) utakaokuwa na watu 80, wakiwemo wachezaji 27, unatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ndege maalumu.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa, kikosi hicho kitawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam saa 2.50 usiku na kitafikia hoteli ya Bahari Beach iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Wambura, nahodha wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba ameachwa kwenye msafara huo.

Aliwataja Wachezaji watakaokuwemo kwenye kikosi hicho kuwa ni Abdoul Razak, Akpa Akpro Jean-Daniel Dave Lewis, Angoua Brou Benjamin, Arouna Kone, Aurier Serge Alain Stephane, Bamba Souleman, Barry Boubacar, Boka Etienne Arthur, Bolly Mathis Gazoa Kippersund, Bony Wilfried Guemiand, Cisse Abdoul Karim, Diarrassou Ousmane Viera na Dja Djedje Brice Florentin.

Wengine ni Doumbia Seydou, Gbohouo Guelassiognon Sylvain, Gosso Gosso Jean-Jacques, Kalou Salomon Armand Magloire, N’dri Koffi Christian Romaric, Sangare Badra, Serey Die Gnonzaroua Geoffroy, Sio Giovanni, Tiote Cheik Ismael, Toure Yaya Gnegneri, Traore Lacina, Ya Konan Didier, Yao Kouassi Gervais na Zokora Deguy Alain Didier.

Katika hatua nyingine, kiingilio cha chini katika mechi kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.

Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, ambavyo viko 17,045, kiingilio kitakuwa sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.

Viingilio vya daraja la juu ni sh. 15,000 kwa VIP C,sh. 20,000 kwa VIP B na sh. 30,000 kwa VIP A.

DIAMOND, WEMA WAKUTANISHWA KWENYE FILAMU


Waandaaji wavunja benki kuwalipa washiriki
Diamond akiri itakuwa kazi ngumu kuliko muziki

LICHA ya kuvunjika kwa uhusiano wao wa kimapenzi, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' na msanii nyota wa filamu, Wema Sepetu watakutanishwa katika filamu.

Wapenzi hao wawili, ambao wamekuwa wakirudiana na kuachana mara kwa mara, wanatarajiwa kucheza filamu mpya itakayoanza kurekodiwa hivi karibuni.

Akihojiwa katika kipindi cha Take One Action kilichorushwa hewani hivi karibuni na kituo cha televisheni cha Clouds, Diamond alisema amelipwa pesa nyingi kwa ajili ya kucheza filamu hiyo.

Diamond alisema hakuna msanii wa filamu aliyewahi kulipwa kiwango hicho cha pesa na kwamba hata yeye hajawahi kulipwa pesa kama hizo katika kazi yake ya muziki.

Hata hivyo, Diamond hakuwa tayari kutaja kiwango hicho cha pesa kwa madai kuwa, taarifa zaidi zitatolewa na waandaaji wa filamu hiyo hivi karibuni.

"Taarifa kuhusu filamu hiyo inahusu nini, lini tutaanza kufanya 'shooting', washiriki wamelipwa kiasi gani cha pesa na picha zake zitachukuliwa maeneo gani, itatolewa na waandaaji,"alisema

Msanii huyo nguli wa muziki wa kizazi kipya alisema anaamini filamu hiyo itakuwa babu kubwa kutokana na maelezo aliyopewa na waandaaji wake.

 "Haitakuwa kama hizi filamu zilizozoeleka,"alisema msanii huyo, ambaye amewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki za Kilimanjaro.

Diamond alisema amewahi kuombwa na watu mbalimbali kucheza filamu zao, lakini amekuwa akiwatolea nje kutokana na kutoridhishwa na maudhui yake na mazingira ya uandaaji wake.

Alisema lengo lake ni kuifanya filamu hiyo atakayoicheza kwa kushirikiana na Wema, iwe katika kiwango cha juu ili aweze kuuza jina lake kimataifa.

Licha ya kukubali kucheza filamu hiyo, Diamond alisema anahisi kutatokea matukio mengi ya ajabu wakati wa kupiga picha za filamu hiyo katika maeneo husika.

"Nina hakika baadhi ya wakati mpenzi wangu atakuwa akija kwenye maeneo ya kupiga picha za filamu hiyo kila atakapopata nafasi, hivyo kutakuwa na vijembe na maneno ya hapa na pale,"alisema.

"Hii kazi nahisi itakuwa ngumu kuliko hata ya muziki, lakini namuomba Mungu anisaidie ili niweze kuimaliza salama,"aliongeza msanii huyo.

Japokuwa hakutaka kuweka wazi kuhusu wasiwasi alionao wa kutokea matukio ya ajabu wakati wa upigaji wa picha za filamu hiyo, kauli yake hiyo inamuhusisha Wema na mpenzi wake wa sasa, Penny.

Diamond ana wasiwasi kuwa, iwapo Penny atakuwa akimtembelea katika maeneo watakayokuwa wakipiga picha za filamu hiyo, huenda akakwaruzana na Wema na kurushiana vijembe.

"Si unajua kila mtu analinda chake. Nina hakika yataripotiwa mambo mengi wakati wa kupiga picha za filamu hiyo,"alisema.

Alipoulizwa ni msanii yupi wa filamu wa kike anayevutiwa naye, Diamond hakusita kumtaja Wema.

"Napenda sana uigizaji wa Wema, si kwa sababu alikuwa mpenzi wangu. Waswahili wanasema palipo na ukweli, hakuna haja ya kuficha mambo. Wema anaigiza vizuri sana,"alisema.

Kwa upande wa wacheza filamu wa kiume, Diamond alimtaja msanii anayemvutia kuwa ni Jacob Steven, maarufu kwa jina la JB.

Diamond amewataka watanzania kujenga tabia ya kuwasamehe wasanii pale wanapoteleza na kufanya matendo mabaya mbele ya jamii. Alisema inasikitisha kuona kuwa, matendo mabaya yanavuma zaidi kuliko mazuri.

"Mimi kama Diamond nimekuwa nikifanya mambo mengi mazuri, lakini hayaonekani. Lakini inapotokea nimefanya kitu kidogo chenye mwonekano mbaya, kinakuzwa sana,"alisema.

Sunday, June 9, 2013

TAIFA STARS YACHAPWA 2-1 NA MOROCCO



Taifa Stars imepoteza mechi ya ugenini baada ya kufungwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya kundi C ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Morocco imechezwa leo (Juni 8 mwaka huu) usiku kwenye uga wa Grand Stade de Marrakech, jijini Marrakech.

Licha ya kufungwa, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumjaribu kipa wa Morocco, Nadir Lamyaghri aliyeokoa shuti la mpira wa adhabu la Aggrey Morris katika sekunde ya 40 tu tangu refa Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika Kusini apulize filimbi ya kuanzisha pambano hilo.

Refa alitoa faulo hiyo baada ya mshambuliaji Thomas Ulimwengu kukwatuliwa na Ahmed Kantari baada ya kumtambuka beki mwingine wa Simba hao wa milima ya Atlas.

Stars walicheza pungufu kwa dakika 58 baada ya Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumkwatua ndani ya eneo la hatari Abdelaziz Barrada huku akiwa amebaki yeye na mshambuliaji huyo. Adhabu hiyo iliandamana na penati ambayo Morocco waliitumia kupata bao la kuongoza dakika ya 37 mfungaji akiwa Abderazzak Hamed Allah.

Kabla, Stars wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager walitengeneza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 25 baada ya Ulimwengu kufanikiwa kuwatoka mabeki wawili wa Morocco na kuingia eneo la hatari lakini shuti lake hafifu lilidakwa na kipa Lamyaghri.

Morocco waliongeza bao lingine dakika ya 50 na Youssef El Arabi baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kudhibiti pasi ya mwisho ya wachezaji wa timu hiyo, na mshambuliaji huyo kumfunga kirahisi kipa Juma Kaseja.

Kiungo mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Stars bao maridadi dakika ya 61 kwa mkwaju wa mbali uliomshinda kipa Lamyaghri. Kabla ya kuachia shuti hilo, Kiemba aliwatoka wachezaji wa timu ya Morocco ambayo ndiyo imepeta ushindi wake wa kwanza katika mechi hizo za mchujo za Kombe la Dunia.

Dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho Mbwana Samata angeweza kuisawazishia Stars, lakini licha ya kuwatoka mabeki wawili wa Morocco baada ya kupokea pasi ya John Bocco mpira aliopiga ulitoka nje.

Stars ambayo bado inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita inaondoka hapa kesho (Juni 9 mwaka huu) mchana kwa ndege ya EgyptAir kupitia Cairo, Misri na itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 alifajiri (Juni 10 mwaka huu).

Katika mechi hiyo Stars iliwakilishwa na; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa/Nadir Haroub, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha/John Bocco, Amri Kiemba na Mbwana Samata.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Marrakech, Morocco
+212 610120619

TENGA: USHIRIKI KOMBE LA KAGAME MIKONONI MWA SERIKALI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.

Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.

“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.

“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.

“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”

Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.

Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.

“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.

“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.

Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.

“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.

“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”

Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.

“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.

“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”

Friday, June 7, 2013

M 2 THE P AZURU KABURI LA MANGWEA

Hili ndilo kaburi la msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, marehemu Albert Mangwea aliyezikwa jana nyumbani kwao, Kihonda mkoani Morogoro.

Swahiba mkubwa wa marehemu Mangwea, msanii M 2 THE P akiuaga mwili wa mwenzake kabla ya kuzikwa jana. M 2 THE P alisafiri na Mangwea kwenda Afrika Kusini na alikuwa pamoja na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake.

Wednesday, June 5, 2013

TUNAMLILIA MANGWEA BAADA YA KUFA!


NA STEPHEN BALIGEYA

KAMA kuna kitu ambacho kimenipa kichefuchefu, kunitia kinyaa na kunijengea dhambi ya chuki juu ya baadhi ya watu wanaojinasibisha wema mbele za uso wa dunia na Watanzania, basi ni kifo cha msanii Albert Mangwea.

Niliwasikiliza kwa umakini na wamenifanya nitakafakari na kunipa fursa ya kuchambua kwa umakini kiasi cha kuandika pia kwa umakini juu ya namna Watanzania walivyomlilia msanii huyo.

Ngwea, ‘Mzee wa mikasi’ kama nilivyopenda kumwita, ametutoka, amechoka kuishi kwa fitina, majungu, unafiki na uzandiki wa hapa duniani. Kwangu mimi naona amefanya uamuzi sahihi na makini wa kuamua kwenda kupumzika katika nyumba ya milele.

Nasema kachoka kuishi kwa unafiki, fitina, majungu na uzandiki kwa sababu, kinachozungumzwa na kufanywa juu yake leo, kama kingekuwa kinafanywa wakati yuko hai, inawezekana Mangwea asingechukua uamuzi wa haraka namna hii.

Si kwamba nasema Mangwea kajiua, hapana. Nasema Mangwea angeondoka kwa furaha zaidi kuliko huzuni aliyoondoka nayo. Ameondoka na huzuni huku manyang’au, wanafiki, wafitini na wazandiki wakibaki wakifaidi furaha yake.

Kwa nini baada ya Mangwea kuaga dunia ndipo kila kituo cha redio kinapiga nyimbo zake kwa wingi na kumsifia kuwa alikuwa akiimba nyimbo bora kabisa? Kwa nini wakati akiwa hai, nyimbo hizo zilikuwa hazisikiki katika baadhi ya vituo vya redio nchini?

Nimetafakari kwa kina jambo hili, ambalo limenitia kichefuchefu na kinyaa kisichomithilika. Kwa sababu wasanii wanategemea nyimbo zao kupigwa mara kwa mara katika vituo vya redio na televisheni ili waweze kujitangaza.

Nyimbo zao zinapigwa bure na vituo hivyo, lakini hawalipwi chochote. Hata katika kupigwa huko, bado nyimbo za baadhi ya wasanii akiwemo Mangwea zilikuwa nadra kupigwa.

Kimsingi, nyimbo za wasanii zinapokuwa zinapigwa kwenye redio na televisheni, husaidia vyombo hivyo vya habari kupata wasikilizaji na watazamaji wengi, ambao ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza biashara zao.

Bila wasikilizaji na watazamaji, hakuna redio wala televisheni inayoweza kuwa na ubavu wa kushawishi watangazaji kufanya nayo kazi. Watatangaza vipi na redio na televisheni isiyokuwa na wasikilizaji wala watazamaji wa matangazo yao?.

Ndiyo maana leo kuna vipindi vya muziki, kila redio na televisheni inaweka mbinu za kuwa na wasanii ili iweze kusikilizwa na kuangaliwa na watu wengi ili wafanyabiashara nao wafurahie kuwapa matangazo.

Lakini wakati redio na televisheni zinapata mabilioni ya fedha kupitia wasanii, wahusika hawaingizi kitu. Kibaya zaidi wanaombwa hata fedha ili nyimbo zao ziweze kupigwa katika redio na televisheni.

Kinachokera zaidi ni kwamba bado kuna makupe wanaotumia fursa walizonazo kwenye redio kuwakandamiza wasanii. Wapo wanaokataa kupiga nyimbo za wasanii wanaokataa kunyonywa.

Msanii akikataa kuingia mikataba ya kunyonywa na makupe hao, adhabu yake ni nyimbo zake kutopigwa redioni wala kwenye televisheni wanazoziongoza. Msanii akigoma kwenda kwenye tamasha la makupe hao kwa kudai maslahi mazuri, tishio lake ni kutopigwa nyimbo zake au kutoalikwa kwenye matamasha mengine.

Mangwea alikuwa mmoja wa waathirika. Waliomfanya aishi maisha ya shida na tabu wakati akiwa msanii mkubwa, ndio hao walioubeba msiba wake na kujifanya walimpenda sana.

Wanamsifu kwa nyimbo na mapambio, wanamtukuza mtu aliyekufa, lakini walishindwa kumtukuza na kumsifu akiwa hai. Makupe hawa, ambao wamekuwa na tabia ya kunyonya wasanii, wamejifanya mama na baba wa Mangwea wakati wa mauti.

Walikataa kupiga nyimbo zake kama njia ya kumtangaza na kumfanya apate fursa nyingi za kimuziki. Walikataa kumwalika kwenye matamasha, ambayo wamekuwa wakiyaandaa kama njia ya kumpatia kipato, leo wanajigamba kuwa kijana huyu alikuwa mpole na hakuwa na ugomvi na watu.

Wanamsifu kwa upole wake, kwani wanajua kuwa upole huo ndio walioutumia kumfanya aishi kinyonge mpaka mauti yanamkuta. Walimfanya mbuzi wa kafara, ambaye nina imani kifo chake kitakuwa chachu katika kuleta mabadiliko katika fikra katika vichwa vya wasanii wengine.

Haiwezekani mtu afe ndipo nyimbo zake zinapigwa siku nzima, lakini wakati akiwa hai, nyimbo hizo hizo, ambazo zinasifiwa, zilikuwa hazisikiki wala kuzungumzwa kama zenye ubora. Ubora huo unakuja baada ya kufa kwake.

Unafiki, ujinga na upuuzi huu, ambao unazidi kuwa kasumba ya makupe kuwasifu waliokufa, unazidi kuwafanya watu waliokufa kwa sababu ya mateso yaliyojengwa na wazandiki hawa kumea.

Hebu fikiria, kama nyimbo hizo za Mangwea zingepigwa kama zinavyopigwa leo, angekuwa tajiri kiasi gani? Sifa anazopewa leo, angepewa miaka ya nyuma, angeshiriki matamasha mangapi, ambayo yangempatia fedha?

Leo kila mtoto anamfahamu Mangwea. Wanamfahamu kwa sababu kafariki dunia, lakini kabla ya hapo, waliomfahamu walikuwa wale waliofuatilia kazi zake tangu zamani. Ghafla Mangwea kawa maarufu kama enzi zake, kwa sababu tu amefariki dunia.

Nimesikiliza baadhi ya watangazaji walioko katika redio zilizoshiriki kuua majina ya wasanii wakimsifu Mangwea kwa namna, ambayo mpaka inakera. Wanajulikana namna walivyomfanya Mangwea awe mtumwa na ajutie kuwa msanii.

Nafsi zao zinajua namna walivyoshiriki kumuua Mangwea kiusanii na pengine hata kiroho, lakini leo wanajifanya ndio wasemaji wa Mangwea, ndugu wa Mangwea na familia ya Mangwea. Wanajaribu kuwaaminisha Watanzania kwamba ni watu wema na makini katika kazi zao.

Kwa jumla watu hawa wanatia kichefuchfeu kwani kama wasanii wetu wangekuwa wanatukuzwa namna hii wanapokuwa hai, wangekuwa matajiri kuliko kuwaua na kisha kujifanya tunawalilia siku ya msiba.

Maoni na ushauri 0752646938.

Rooney ampasua kichwa Wenger



LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England, Wayne Rooney amewaweka roho juu mashabiki wa klabu ya Manchester United baada ya kukiri hadharani kwamba, anaweza kuondoka Old Trafford msimu huu.

Kauli hiyo ya Rooney imemfanya Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger awe tayari kuvunja benki na kuweka rekodi ya kumsajili nyota huyo kwa bei mbaya.

Wenger alisema wiki hii kuwa, hawezi kupoteza nafasi adhimu ya kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye anaonekana kutofurahia uwepo wake Old Trafford.

Rooney (27) aling'ara mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni pamoja na kuifungia bao England ilipomenyana na Brazil na kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja wa Maracana.

Mwezi uliopita, gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti kuwa, Arsenal imepata uhakika mkubwa wa kumsajili Rooney baada ya mchezaji huyo kusema kuwa, anataka kuondoka Old Trafford.

Tayari Wenger ameshaweka wazi kuwa, yuko tayari kuvunja rekodi ya kumsajili nyota huyo wa zamani wa klabu ya Everton.

"Rooney ni mchezaji, ambaye anamvutia kila mtu duniani, nani anayeweza kukataa kumsajili," Wenger alikieleza kituo cha televisheni cha Al Jazeera wiki hii.

Wakati Wenger akihaha kumsajili nyota huyo, Kocha Mkuu mpya wa Manchester United, David Moyes anakabiliwa na kazi nzito ya kumshawishi Rooney abaki Old Trafford.

Moyes alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, angependa kumuona Rooney akiendelea kuitumikia Manchester United chini yake kwa vile ni miongoni mwa wachezaji muhimu.

Rooney amekuwa hana uhakika wa namba Manchester United tangu ilipomsaili Robin van Persie. Mholanzi huyo amekuwa akicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, ambayo Rooney alikuwa akiicheza kabla ya ujio wake.

Mapema 2010, Rooney alitishia kuihama Manchester United kabla ya Sir Ferguson kufanikiwa kumtuliza na kumuongezea mkataba mpya.

Msimu huu, Ferguson alimweka benchi Rooney wakati Manchester United iliporudiana na Real Madrid ya Hispania katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya. Badala yake, Ferguson aliwachezesha Van Persie na Danny Welbeck katika nafasi ya ushambuliaji.

Mbali na kumwania Rooney, Wenger pia amepania kumrejesha kiungo wake wa zamani, Cesc Fabregas, ambaye alihama Emirates msimu uliopita na kujiunga na Barcelona ya Hispania.

Wenger anaamini kuwa, mpango wake wa kumrejesha Fabregas hautakuwa mgumu kutokana na mchezaji huyo kutokuwa na uhakika wa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa wakati Fabregas alipojiunga na Barcelona 2011, Arsenal inaweza kumrejesha mchezaji huyo kwa malipo kidogo ya pauni milioni 20.

"Nafikiri kwa sasa amepoteza uhakika wa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona,"alisema Wenger alipokuwa akimuelezea mchezaji huyo.

Wenger alimwelezea Fabregas kuwa ni mchezaji mwenye utulivu na kiwango cha juu cha soka, hivyo anaumia moyoni kwa kutopata nafasi ya kuichezea timu hiyo.

Hata hivyo, Wenger anaweza kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa Manchester City, Manchester United na Chelsea katika kinyang'anyiro cha kumsajili nyota huyo wa England.

Kuna habari kuwa, klabu hizo tatu nazo zimekuwa zikimuwinda kwa udi na uvumba Fabregas kwa lengo la kuziongezea nguvu katika msimu ujao wa ligi.

Fabregas anatarajiwa kukutana na Kocha Mkuu wa Barcelona, Tito Vilanova wiki hii kwa ajili ya kuzungumzia mustakabali wake.

Marafiki wa karibu wa Fabregas wanaamini kuwa, kiungo huyo anaweza kuamua kubaki Barcelona iwapo atahakikishiwa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa upande wake, Moyes amemtaja Fabregas kuwa ni mmoja wa wachezaji, ambao amepanga kuwasajili kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi chake.

Moyes, ambaye amerithi mikoba ya kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, anatarajiwa kuanza rasmi kibarua cha kuinoa timu hiyo Juni 16 mwaka huu.

NASEEB ABDUL 'DIAMOND' : NATAKA KUWA MSANII WA KIMATAIFA



MSANII nyota wa muziki wa kizazi nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amesema kiwango chake cha chini cha malipo kwa kila onyesho analofanya nje ya nchi ni dola 10,000 za Marekani (sh. milioni 16).

Akihojiwa katika kipindi cha Take One Action kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds wiki hii, Diamond alisema katika baadhi ya nchi, kiwango chake cha malipo kwa kila onyesho ni kati ya dola 15,000 (sh. milioni 24) na 25,000 (sh. milioni 42)

"Sifanyi shoo nje ya nchi chini ya dola 10,000. Katika nchi kama Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), kiwango changu ni dola 25,000. Wakati mwingine nalipwa hadi dola 30,000,"alisema msanii huyo.

Diamond alisema katika nchi kama vile Comoro, ambako anatarajia kwenda kufanya onyesho mwishoni mwa mwezi huu, malipo yake kwa onyesho ni dola 25,000.

Hata hivyo, Diamond alisema wakati mwingine amekuwa akilipwa pesa nyingi kuliko alivyotarajia na alitoa mfano wa Rwanda, ambako promota aliyemwalika huko alimlipa sh. milioni 180,000.

"Mimi nina msimamo na ninapoalikwa nje ni lazima nifuatane na wacheza shoo wangu. Wapo wasanii wengine wa Tanzania wanaomba waende Ulaya wakafanye shoo bure kwa sababu tu hawajakwenda huko siku nyingi,"alisema.

Diamond alisema lengo kubwa alilonalo kwa sasa ni kuwa msanii wa kimataifa na amefikia uamuzi huo kutokana na funzo kubwa alilolipata wakati wa ziara yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Ili kutimiza azma yake hiyo, Diamond alisema ameanza kuandika mashairi yenye mvuto, kurekodi nyimbo zake kwenye studio za kisasa na pia kutengeneza video zenye ubora wa kiwango cha juu.

"Nimeshaanza pia kujifunza elimu ya biashara na kuboresha lugha ya Kiingereza kwa sababu nimekuwa nikikutana na mapromota wengi wa kimataifa,"alisema.

Diamond alisema anatarajia kuingia mkataba na Kampuni ya Fuse ya Uingereza, ambayo imewahi kufanyakazi na wasanii wengi maarufu wa Afrika Magharibi na Fally Ipupa wa DRC.

"Unajua muziki mzuri pekee hautoshi kukufanya uwe mwanamuziki wa kimataia. Lazima uwe na sura na mtazamo wa kimataifa,"alisema msanii huyo aliyewahi kunyakua tuzo kadhaa za muziki za Kilimanjaro.

Diamond alisema haamini iwapo imani za ushirikina zinaweza kumsaidia msanii kupata mafanikio. Alisema anawafahamu watoto wengi wa waganga wa kienyeji, lakini hakuna hata mmoja aliyepata mafanikio makubwa kimaisha.

Alisema mafanikio katika maisha yanapatikana kutokana na mipango ya Mungu na kuongeza kuwa, aliyeandikiwa kupata, hakuna anayeweza kuzuia riziki yake.

"Sijawahi kwenda kwa mganga wa kienyeji hata siku moja katika maisha yangu. Utaratibu wangu ni kuamka usiku na kufanya ibada, nikimuomba Mungu anisaidie. Namuomba sana Mungu,"alisema.

Diamond alisema katika uendeshaji wake wa kazi za muziki, amekuwa akisaidiwa na watu 12, kila mmoja akiwa na kazi yake. Alisema miongoni mwa watu hao, wamo madansa wanne, mtaalamu wa mavazi, wapiga picha wawili, mlinzi na msaidizi wake wa karibu.

Alisema hawezi kukaa na mtu, ambaye hawezi kumsaidia kimuziki na kuongeza kuwa, wapo ndugu zake, ambao wamekuwa wakipenda kusafiri naye, lakini anawakatalia kwa sababu hawawezi kuwa na manufaa kwake.

Diamond alisema miongoni mwa mambo anayotarajia kuyafanya ili kuhakikisha maisha yake hayatetereki ni pamoja na kuwekeza katika ardhi.

"Mimi ni mwoga wa maisha. Nimepitia katika mazingira magumu. Hata niwe na pesa kiasi gani, siwezi kusahau maisha niliyopitia. Wakati mwingine huwa napenda kwenda hoteli ya Slipway, nakaa baharini na kukumbuka nilikotoka, huwa nalia sana,"alisema.

"Ndio sababu nimeamua kuwekeza katika ardhi. Ninamiliki nyumba nyingi. Si sahihi kuwa na fedha nyingi benki, lakini hazizalishi. Nimeshindwa kufanya biashara kubwa kutokana na kukosa wasimamizi,"aliongeza.

Diamond alisema kamwe hapendi kutumia pesa zake kuwahonga wanawake. Alisema amekuwa akifanya hivyo kwa sababu maalumu na kwa jambo la msingi.

Msanii huyo alisema thamani ya mali alizonazo kwa sasa, ni zaidi ya shilingi bilioni moja na ushehe na kutamba kuwa, tangu 2011, haijawahi kutokea akaunti yake kupungua sh. milioni 100.

Licha ya kutunga nyimbo nyingi, Diamond alisema anavutiwa zaidi na 'Binadamu', 'Ukimuona', 'Nenda kamwambie', 'Nitarejea' na 'Lala salama'.

Alisema wimbo wa 'Ukimuona' aliutuinga maalumu kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani, Wema Sepetu wakati wimbo wa Mawazo aliutunga kwa ajili ya mpenzi wake mwingine wa zamani, Jacqueline Wolper.

Alimtaja mwanamke mwingine aliyewahi kumtungia nyimbo kuwa ni mpenzi wake wa kwanza, anayejulikana kwa jina la Sara. Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Mbagala na Nenda kamwambie.

"Sara ndiye mwanamke wangu wa kwanza. Alinipenda japokuwa sikuwa na kitu. Lakini huko mbele alinieleza wazi kwamba, hawezi kuwa na mwanaume asiyekuwa na maslahi kwake. Nilipatwa na uchungu sana,"alisema.

Diamond alisema anapenda kutunga nyimbo zake kwa kufuata mashairi ya muziki wa taarab, ikiwa ni pamoja na kutumia maneno ya kiswahili yenye mvuto.

Je, ni kwa nini Diamond aligoma kupokea fedha alizotuzwa na Wema wakati wa onyesho lake lililofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City?

"Wakati ule nilikuwa bado nina hasira sana baada ya kugombana na Wema. Alinilaghai kimapenzi. Nilikuwa na hasira sana. Nilijifanya kama simuoni,"alisema.

Hata hivyo, Diamond alikiri kuwa hajawahi kutokea kumpenda mwanamke kama ilivyokuwa kwa Wema. Alisema hata mama yake na rafiki zake wanautambua ukweli huo.

Aliitaja skendo iliyowahi kuripotiwa na vyombo vya habari na kuumiza moyo wake kuwa ni ile iliyomuhusisha mama yake na meneja wake, Papaa Misifa kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.

"Habari hiyo iliniumiza sana. Ni bora mtu acheze na kitu chochote kuhusu mimi,lakini siyo mama yangu. Naweza kufanya lolote,"alisema.

"Ni bora tucheze ulingoni wenyewe kwa wenyewe, usimchezee mama yangu. Baada ya Mungu na yeye siogopi kitu kingine chochote na ninaweza kufanya lolote baya. Sintaogopa kwenda jela iwapo itatokea mtu anamuhusisha mama yangu na mambo mabaya,"aliongeza.

BRANDTS AMCHIMBIA MKWARA NGASA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amebariki kuondoka kwa mshambuliaji Hamisi Kiiza kutoka Uganda, lakini amemchimbia mkwara mshambuliaji mpya, Mrisho Ngasa.

Brandts amesema hana tatizo kuhusu uamuzi wa Kiiza kuondoka Yanga baada ya kushindwa kuelewana na uongozi kuhusu mkataba mpya kwa vile lengo lake lilikuwa ni kutaka kuongezewa pesa.

Kocha huyo alisema hayo juzi usiku baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam akitokea Ubelgiji alikokwenda kwa mapumziko.

"Acha aende, kama anataka fedha nyingi kuliko wenzake, aendetu. Viongozi watafute mchezaji mwingine,"alisema kocha huyo aliyepokewa na Meneja wa Yanga, Hafidh.

Akimzungumzia Ngasa, kocha huyo alisema ni mchezaji mzuri na anaufahamu vyema uwezo wake, lakini amemtahadharisha kwa kusema kuwa, kupangwa kwake kutazingatia uwezo wake mazoezini.

“Inabidi anihakikishie uwezo wake kuanzia mazoezini ili nimpange, vinginevyo nitakuwa nakaa naye benchi,”alisema.

Brandts alisisitiza kuwa, sera yake ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji mazoezini na hatampanga mtu kwa sababu ya jina lake.

Mbelgiji huyo alisema lengo lake ni kuiona Yanga ikicheza kwa kasi zaidi msimu ujao, lakini alikiri kuwa, tatizo kubwa linalowakabili kwa sasa ni kukosa uwanja mzuri wa mazoezi.

Kocha huyo alieleza kusikitishwa kwake na mahudhurio hafifu ya wachezaji katika mazoezi yaliyoanza wiki iliyopita kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.

Alisema iwapo hali hiyo itaendelea, mashabiki wa Yanga wasitarajie timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 18 mwaka huu nchini Sudan.

“Nimeambiwa wachezaji saba tu wa kikosi cha kwanza ndio wanafika mazoezini, wengine wote ni wa kikosi cha pili. Sasa hii si nzuri, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia sana hili, hadi nitakapokutana na uongozi. Nahitaji nidhamu katika timu ili kutimiza malengo na kuwafurahisha mashabiki wetu,”alisema.

Brandts alisema wakati anaondoka nchini, aliuagiza uongozi kusajili wachezaji wapya wazuri katika kila idara ili kuongeza ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza.

HANSPOPE AMPANDIA NDEGE KASEJA

BAADHI ya viongozi wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba wanatarajiwa kuondoka nchini kati ya leo na kesho kwenda Morocco ili kumalizana na kipa Juma Kaseja.

Kaseja yuko nchini Morocco akiwa na kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kinachotarajiwa kurudiana na timu ya taifa ya nchi hiyo keshokutwa katika mechi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope anatarajiwa kwenda Morocco akitokea Libya, ambako alikwenda kukamilisha usajili wa mchezaji wa kimataifa wa Uganda, Moses Oloya.

Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, Hanspope alimalizana na mchezaji huyo wa Uganda mara baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo kuchapwa mabao 3-0 na Libya mjini Tripoli.

Kwa mujibu wa habari hizo, lengo la vigogo hao wa Simba kwenda Morocco ni kumbembeleza Kaseja ili aongeze mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo.

Mkataba wa Kaseja kuichezea Simba ulimalizika mwishoni mwa msimu huu na kuna habari kuwa, amekuwa akiwaniwa na klabu ya Azam.

Awali, kamati ya usajili ya Simba ilikuwa imegawanyika kuhusu usajili wa mchezaji huyo, lakini baadaye imeona kuna umuhimu wa kumuongezea mkataba.

TBL YAZIMWAGIA VIFAA SIMBA NA YANGA



MENEJA wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (kushoto) akiwa na viongozi wa klabu ya Yanga baada ya kuwakabidhi vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, wa pili kulia ni Msaidizi wa Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Geoffrey Makau akifuatiwa na Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kaziguto. (Na mpiga picha wetu).

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), imekabidhi vifaa vya michezo kwa klabu za Simba na Yanga kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame.

Akikabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema jana kuwa, vifaa hivyo vimelenga kuzisaidia klabu hizo mbili kushiriki vyema katika michuano hiyo.

Michuano ya Kombe la Kagame imepangwa kuanza Juni 18 mwaka huu, ikizishirikisha klabu bingwa kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

"Bila ubishi Simba na Yanga ndizo klabu kubwa za mpira wa miguu Tanzania na zote zimefika katika fainali za michuano ya Kombe la Kagame kwa mara ya 19 sasa, haya ni mafanikio makubwa kwa hizi timu,"alisema Kavishe.

"Sisi kama wadhamini wakuu wa timu hizi, Kilimanjaro Premium Lager inaziunga mkono Simba na Yanga katika harakati zao za kucheza tena fainali za michuano hii ya kusisimua na ya kihistoria,"aliongeza.

Kavishe alisema Kombe la Kagame ni mashindano makubwa Afrika Mashariki na Kati na ni jukwaa bora kwa wachezaji wa Tanzania kuonyesha vipaji vyao dhidi ya wachezaji wa viwango vya juu katika ukanda huu.

Meneja huyo wa bia ya Kilimanjaro alisema mafanikio ya ushirikiano uliopo kati ya kampuni yake na klabu hizo kongwe nchini kuzishuhudia zikitoa mara kwa mara zikitoa wachezaji wengi katika timu ya Taifa, Taifa Stars.

Alizitaka klabu hizo kongwe nchini kuhakikisha zinaiwakilisha vyema Tanzania Bara katika michuano hiyo, inayodhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

INAUMA SANA


MAMIA ya wananchi jana walijitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Albert Mangwea kwenye viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam.

Miongoni mwa waliojitokeza kuuaga mwili wa msanii huyo ni pamoja na wasanii kadhaa maarufu wa muziki wa kizazi kipya na wasanii wa filamu nchini.

Baadhi ya wasanii hao ni pamoja na Naseeb Abdul 'Diamond', Khaleed Mohammed 'TID', Ommy Dimpoz, Ally Ahmed 'Madee', Khadija Shaaban 'Keysher', Akili The Brain, P Funky, Saidi Fela, Daf Assey, Bico Hoza, Dagmar Iddi, Mchizi Mox, Mez B, Mully B na Edward Muhoza.

Kwa upande wa wasanii wa filamu, walikuwepo Jacob Steven 'JB', Natasha, Yvonne Cherry 'Monalisa', Steve Nyerere, Mzee Magari, Raymond Kigosi 'Ray' na Mainda.

Ndugu wa marehemu walioshiriki katika shughuli ya kuuaga mwili wa Mangwea ni pamoja na dada yake, Consolata Mangwea, baba yake mdogo, David Mangwea na mama yake mdogo, Ellah Mangwea.

Shughuli za kuuaga mwili wa msanii huyo, aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Afrika Kusini, zilianza saa tatu asubuhi baada ya kuwasili kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam na kumalizika saa saba mchana chini ya usimamizi mkali wa jeshi la polisi.

Akisoma risala kwa niaba ya wasanii wenzake, msanii Mez B alisema kifo chake kimeacha pengo kubwa katika kundi lake la Chamber Squad.

Alisema walishirikina vyema na marehemu Mangwea kwa hali na mali huku wakitumia muda mwingi kujipanga kwa ajili ya kazi zao na maisha yao.

"Sijui niseme nini, lakini najua kila mtu anajua jinsi msiba huu ulivyotuchanganya kwani umetokea katika kipindi ambacho hatujatarajia licha ya kuwa kifo hutokea bila kujua saa wala dakika," alisema Mez B.

Gari lililobeba mwili wa marehemu na magari mengine yasiyopungua 30 likiwemo gari la doria na gari la kubeba wagonjwa, yaliondoka katika viwanja hivyo saa saba mchana na kuanza safari ya kwenda Morogoro.

IDD AZAN
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan alisema aliposikia kifo cha msanii huyo na mazingira yake, alisikitika na kuamua kuacha shughuli za Bunge na kurudi Dar es Salaam kujumuika na waombolezaji wengine.

Azzan alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kwa wasanii wa muziki nchini na hata wale waliokuwa wakifanya naye kazi katika kundi la Chamber Squad.

Alisema kifo cha masanii huyo kinatoa funzo kubwa kwa wasanii la kuwataka kuimarisha upendo na ushirikiano kwao bila kujali wanatoka katika makundi gani.

Alisema uhusiano baina ya wasanii utazidi kuwajenga na kuwafanya wawe kitu kimoja na kusaidiana katika shida na raha kama walivyofanya kwa Mangwea.

WASANII WA FILAMU
Jacob Steven 'JB' alisema kifo cha msanii huyo kinazidi kuwaumiza wasanii nchini kwani kimetokea wakati bado wasanii wakiwa na kumbukumbu ya kifo cha Steven Kanumba.

Hata hivyo, JB alisema yote hiyo ni mipango ya Mungu na kuongeza kuwa, hakuna kiumbe kitakachobaki hai.

Raymond Kigosi 'Ray' alisema ameshukuru kuona ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa baina ya wasanii wa filamu na muziki katika kufanikisha shughuli za maandalizi ya msiba huo.

Alisema wasanii wamejitoa na kuhakikisha mwenzao anakwenda kupumzika katika nyumba yake ya milele kwa kupata heshima zote alizostahili katika jamii.

WASANII WA MUZIKI
Khaleed Mohamed 'TID' alisema haamini kama kweli Mangwea na rafiki yake wa karibu amefariki, lakini tukio la kuaga limemfanya kuamini na kukubali matokeo.

"Nakubali kilichotokea na ninajua ni mapenzi ya Mungu na hakuna mtu yeyote katika dunia hii atakayeepuka kifo," alisema TID.

TID alisema anasikia uchungu kuona jinsi mama wa marehemu atakavyopata tabu na uchungu kwa kumpoteza mtoto wake, lakini anaomba awe mvumilivu na kumshukuru Mungu.

Alisema akiwa rafiki wa karibu wa marehemu, atahakikisha anakuwa bega kwa bega na mama wa marehemu katika kipindi hiki kigumu na kutoa msaada wa hali na mali.

MAZIKO
Marehemu Mangwea anatarajia kuzikwa leo mjini Morogoro nyumbani kwa mama yake mzazi.

Mangwea alifariki Mei 28 nchini Afrika Kusini na kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kuwasili Juni 4 mwaka huu kabla ya kuagwa jana na kusafirishwa kwenda Morogoro.

Wakati huo huo, Shirikisho la Wanamuziki Tanzania limesema limepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha msanii Albert Mangwea kilichotokea nchini Afrika Kusini.

Rais wa shirikisho hilo, Addo Mwasongwe alisema jana kuwa, kifo hicho ni pigo kubwa kwa tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini kutokana na umahiri aliokuwa nao katika fani hiyo.

"Marehemu tutamkumbuka kwa mengi, hasa msimamo aliouonyesha katika mambo aliyoyaamini. Alikuwa ni mtu mwenye jitihada kwani hadi mauti yalipomfika, alikuwa katika jitihada za kujitafutia riziki,"alisema.

Addo alisema shirikisho lake limeshirikiana vyema na kamati ya mazishi katika kuhakikisha shughuli ya kuuaga mwili wa msanii huyo inafanyika kwa mafanikio.

Aliwashukuru Watanzania kwa heshima waliyompa Mangwea katika safari yake ya mwisho na kuongeza kuwa, kitendo hicho kimewafariji.

Addo pia aliishukuru serikali, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Zitto Kabwe (mbunge) na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia, January Makamba kwa jitihada walizozifanya kuhakikisha mwili wa Mangwea unarejeshwa nchini.

Rais huyo wa shirikisho la muziki alivilaumu vyombo vya habari nchini kwa kuripoti taarifa kuhusu kifo cha msanii huyo kabla ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.

"Maadam kuna ripoti ya daktari kuhusu uchunguzi wa kifo hicho, ingekuwa busara kuisubiri familia yake iitoe hadharani iwapo itapenda kufanya hivyo,"alisema Addo.

Tuesday, June 4, 2013

SAMATTA, ULIMWENGU WATUA MOROCCO



Taifa Stars imewasili hapa Marrakech, Morocco leo- Juni 3 mwaka huu tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itakayochezwa Jumamosi- Juni 8 mwaka huu.


Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia hoteli ya Pullman ambayo pia Ivory Coast ilifikia ilipokuja kucheza hapa dhidi ya Morocco. Stars imetua na wachezaji 21 huku Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu waliokuwa Maputo, Msumbiji kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho na timu yao ya TP Mazembe watawasili kesho- Juni 4 mwaka huu saa 8 mchana.

Mechi kati ya Stars na Morocco itachezwa kuanzia saa 3 usiku kwa saa za hapa wakati nyumbani itakuwa ni saa 5 usiku.

Wakati huo huo, washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamejiunga na kikosi cha Taifa Stars kilichoko nchini Morocco.

Samatta na Ulimwengu waliwasili Morocco juzi mchana wakitokea Maputo, Msumbiji ambako walikwenda kuichezea timu yao ya TP Mazembe katika mechi ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+212610120619
Marrakech, Morocco

MWILI WA MANGWEA WATUA DAR


Mamia ya watu jana walijitokeza kuupokea mwili wa aliyekuwa msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Albert Mangwea.

Vilio na simanzi vilitawala kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam wakati mwili wa msanii huyo ulipowasili saa 8.00 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

Mwili wa marehemu Mangwea unatarajiwa kuagwa leo kuanzia saa 2.00 asubuhi kwenye viwanja vha Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya mazishi.

Monday, June 3, 2013

NSSF ALL STARS YAVUNJA MWIKO WA BUNGE SC


Meneja wa timu ya NSSF All Stars, Rashid Zahor (wa pili kulia) akiwa ameshikilia kombe la ubingwa baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Wabunge katika mechi iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Wachezaji wa timu za soka na netiboli za NSSF All Stars wakiwa katika picha ya pamoja na vikombe walivyoshinda.
Wachezaji wa timu za soka za NSSF All Stars na Bunge SC wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mechi kati yao iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kikosi cha timu ya soka ya NSSF All Stars kabla ya kucheza mechi yake ya kirafiki dhidi ya Bunge SC.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TIMU ya soka ya kombaini ya vyombo vya habari, iliyoundwa kutokana na mashindano ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), NSSF All Stars juzi iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wabunge katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ushindi huo uliiwezesha NSSF Media Stars kuvunja mwiko wa timu ya soka ya wabunge wa kutofungwa katika mechi za kirafiki inazocheza kwenye uwanja huo dhidi ya timu za taasisi mbalimbali.

Wakati NSSF All Stars iliibuka na ushindi katika soka, dada zao walipigwa mweleka wa mabao 38-11 na Wabunge. Mechi zote mbili zilionyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star TV.

Kutokana na ushindi huo katika soka, NSSF All Stars ilikabidhiwa kombe la ubingwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai. Kombe hilo lilipokelewa na nahodha wa NSSF All Stars na nahodha wa timu hiyo, Majuto Omary.

Kwa upande wa Wabunge, kombe la ushindi wa pili lilipokelewa na nahodha wake,Ahmed Ngwali.

Katika netiboli,kombe la ubingwa lilipokelewa na nahodha wake, ....wakati kombe la ushindi wa pili kwa NSSF All Stars lilipokelewa na nahodha Lulu Habibu.

Mara baada ya kupokea vikombe vyao, wachezaji wa timu zote mbili za NSSF All Stars walivikabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk. Ramadhani Dau na kisha kupiga naye picha ya pamoja.

Timu ya soka ya NSSF All Media Stars ilionyesha dhamira ya ushindi tangu mwanzo wa mchezo kutokana na kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la wabunge lililokuwa chini ya Iddi Azzan.

Majuto nusura aifungie bao NSSF All Stars dakika ya 15 wakati alipofumua shuti la mpira wa adhabu wa umbali wa mita 25, lakini liligonga mwamba wa pembeni wa goli na kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa na mabeki wa Wabunge.

Dakika 10 baadaye, Julius Kihampa aliiandikia NSSF All Stars bao pekee na la ushindi baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi maridhawa kutoka kwa Majuto.

Zikiwa zimesalia dakika 10 kabla ya mapumziko, kipa Azzan wa wabunge alilazimika kufanyakazi ya ziada kupangua shuti la Majuto, ambapo mpira ulimtoka mikononi kabla ya kuudaka tena. Timu hizo zilikwenda mapumziko NSSF All Stars ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Katika kipindi cha pili, timu zote mbili zilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji. Wabunge waliwatoa Faki Haji Makame, Adam Malima, Athumani Mfutakamba na Ahmed Ngwali na kuwaingiza Mussa Elisha, Michael Kadebe, Onesmo Laulau na Suleiman Jafu.

Kwa upande wa NSSF All Stars, iliwapumzisha Linus Bwegego, Maulid Kitenge, Julius Kihampa na Edward Mbaga na kuwaingiza Mohamed Mharizo, Nassoro Nassoro, Ridhiwani Ramadhani na Salum Mkandemba.

Katika kipindi hicho, Wabunge walichachamaa na kulishambulia lango la NSSF All Stars mara kadhaa, lakini uimara wa mabeki Mbozi Katala, Heri Mselemu na kipa Saidi Ambua uliikosesha mabao.

George Balibojani alipata nafasi nzuri ya kuifungua bao Bunge dakika ya 65 alipoingia na mpira ndani ya 20, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.

Kipa Ambua wa NSSF alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 79 baada ya kuokoa shuti la Michael Kadebe aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kuifungia bao Bunge.

Akizungumza baada ya pambano hilo, Kocha wa NSSF All Stars, Sanifu Lazaro aliwapongeza vijana wake kwa kucheza vyema na kufuata vyema maelekezo yake na hatimaye kuibuka na ushindi.

"Vijana wamecheza vizuri sana. Tulifanya mazoezi kwa siku tatu tu kabla ya kuja Dodoma, lakini wameweza kucheza kwa kufuata maelekezo niliyowapa,"alisema.

Kocha wa Bunge, Patrick Amri alisema hawakuwa na bahati kwa vile walipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini walishindwa kuzitumia vyema. Pia alisema bao walilofungwa lilitokana na mabeki wake kutokuwa makini.   Nkumba, Jenista, Lusinde waonyesha vibweka uwanjani
MBUNGE wa Jimbo la (Sikonge), Saidi Nkumba juzi alikuwa kivutio cha aina yake kwa mashabiki baada ya kuingia uwanjani akiwa amevaa shuka nyeupe na nyekundu na kuvaa baraghashia huku akiwa ameshika usinga na kujifunga kitambaa kichwani.

Tukio hilo lilitokea wakati wa mapumziko ya pambano la soka la kirafiki kati ya Bunge na kombaini ya vyombo vya habari 'NSSF All Stars' lililofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Nkumba aliyeingia uwanjani kwa gari lake, alipokewa kwa mbwembwe nyingi na mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde.

Akiongozana na wabunge hao wawili, Nkumba alikwenda nao katikati ya uwanja huku akipunga usinga hewani na baadaye kutoka nje, ambako alisalimiana na wachezaji wa Bunge kwa kuwashika vichwa.

Tukio hilo lilishangiliwa kwa mayowe mengi na wabunge waliokuwa wamefurika kwenye uwanja huo kabla ya wachezaji wa timu ya netiboli ya NSSF All Stars kujibu mapigo kwa kuingia uwanjani na kwenda kwenye eneo la mzunguko, ambako walilizunguka wakiigiza kufanya kafara.

Wakati kipindi cha pili cha pambano hilo kikiendelea, Nkumba alikwenda kusini mwa uwanja karibu na kibendera, ambako alisimama kwa muda wote wa mchezo akipiga simu na kupunga usinga wake hewani.

Akizungumza kabla ya washindi kukabidhiwa zawadi, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau alisema waliamua kuandaa pambano hilo kwa lengo la kusherehekea miaka 10 ya mashindano ya Kombe la NSSF.

Alisema mashindano hayo, ambayo yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi mkubwa, yamelenga kuwakutanisha wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kufahamiana na kuiweka miili yao katika afya nzuri.

Dk. Dau alisema lengo la shirika lake ni kuhakikisha kuwa, mashindano hayo yanaendelea kufanyika kila mwaka na kwa ufanisi mkubwa na kwamba wamepanga kuzidi kuyaboresha kwa zawadi na kiuendeshaji.

Kwa upaande wake, mgeni rasmi katika pambano hilo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai aliipongeza NSSF kwa kuandaa mechi hizo mbili na kuwataka wabunge na wana habari kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri uliopo kati yao.

Meneja wa NSSF All Stars, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Kombe la NSSF, Rashid Zahor alisema vijana wake wameifurahia safari hiyo na pia kupata nafasi ya kucheza na wabunge.

Zahor alisema ziara hiyo pia imewawezesha vijana wake kujifunza mengi, ikiwa ni pamoja na kukutana na baadhi ya wabunge, ambao hawakuwa wakiwafahamu.

Timu za NSSF All Stars ziliwasili Dodoma, Mei 31 mwaka huu kwa mabasi mawili ya kukodisha na kurejea Dar es Salaam jana. Msafara wa timu hizo uliongozwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu.

TAIFA STARS YATOKA SARE NA SUDAN



Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imetoka sare ya bila kufungana na Sudan (Nile Crodcodile) katika mechi ya kujipima nguvu iliyochezwa leo (Juni 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Addis Ababa nchini Ethiopia.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Bamlak Tessema wa Ethiopia ilikuwa sehemu ya maandalizi kwa timu zote ambazo wikiendi ijayo zinacheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia. Wakati Stars itakuwa ugenini nchini Morocco, Sudan itacheza nyumbani dhidi ya Ghana.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilicheza vizuri mechi hiyo, hasa kipindi cha pili ambapo ilifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini ama washambuliaji walipiga nje au mipira yao kuokolewa na kipa Ehab Abdelfatahh wa Sudan.

Washambualiji wa Stars akina Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba wakiongozwa na John Bocco walilitia msukosuko mara kwa mara lango la Sudan ambalo lilikuwa chini ya beki wa kati Nadir Eltayeb ambaye alifanya kazi ya ziada dakika ya 72 kuokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni.

Stars katika mechi hiyo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nadir Haroub/Vicent Barnabas, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba/Khamis Mcha na Simon Msuva/Athuman Idd.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.

Timu inaondoka kesho alfajiri kwenda Morocco kwa kupitia Cairo, Misri ambapo inatarajia kuwasili Casablanca saa 8 mchana.

BALOZI BISWARO AIPA CHANGAMOTO TAIFA STARS



Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.

Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.

Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.

Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.

Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.

Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.