KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 5, 2013

RATIBA RCL KUPANGWA J'NNE, LIGI KUANZA MEI 12



Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.

Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka RCL isogezwe mbele.

Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.

Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa msimu mpya.

Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).

Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).

Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.

Mikoa iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.

DRFA YAZIPONGEZA RED CROSS, ABAJALO NA FRIENDS RANGERS


CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimezipongeza timu zake tatu zilizofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa, baada ya kumalizika kwa Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora Aprili 27 mwaka huu.

Timu hizo ni Red Coast, Abajalo na Friends Rangers, zitakazoungana na timu za mikoa mingine kucheza Ligi ya Mabingwa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya Usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema ligi hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu na kuzitaka timu zilizofuzu hatua hiyo kujipanga vizuri ili kuuwakilisha vyema mkoa na hatimaye kucheza Ligi Daraja la Kwanza.

“Kwa niaba ya DRFA napenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza timu hizo kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuuwakilisha mkoa wa Dar es Salaam katika kutafuta kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao wa 2013/2014.

“Tunaamini watajiandaa vyema na kutuwakilisha vizuri katika ligi hiyo, kufanya kwao vizuri ndio itakuwa fahari yetu DRFA na wadau wa mpira wa miguu mkoa wa Dar es Salaam, tunawatakia kila la kheri na tupo pamoja katika kushirikiana nao.

Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora mkoa wa Dar es Salaam ilianza Aprili 15 mwaka huu ambapo ameziomba timu za Sharif Stars, Day Break na Boom FC zilizoshiriki ligi hiyo kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo.

BOCCO, MWANTIKA WAIPONZA AZAM



AZAM jana ilitolewa kiume katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa mabao 2-1 na FAR Rabat ya Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.

Kipigo hicho kimeifanya Azam itolewe kwa ushindi wa jumla wa idadi hiyo ya mabao, kufuatia timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam itabidi ijilaumu kutokana na mshambuliaji wake, John Bocco kukosa adhabu ya penalti dakika ya 85, ambayo ingeiwezesha kupata sare na kusonga mbele katika michuano hiyo.Shuti la Bocco liligonga mwamba wa juu wa goli.

Mbali na kukosa penalti, Azam ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake, David Mwantika kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya mchezaji wa FAR Rabat.

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita lililofungwa na Bocco kwa mpira wa adhabu baada ya beki mmoja wa FAR Rabat kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Wamorocco walisawazisha bao hilo dakika sita baadaye kupitia kwa Abdelrahim Achchakir kwa mkwaju wa penalti baada ya Mwantika kumchezea rafu mbaya mchezaji mmoja wa FAR Rabat.

FAR Rabat nayo ilipata pigo dakika ya 35 baada ya beki wake, Achchakir kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Brian Umony.

Bao la pili la FAR Rabat lilifungwa na Mustafa Allaoui dakika ya 42 kwa shuti la mpira wa adhabu la umbali wa mita 25 na kumpita kipa Mwadini Ally.

Waziri Salum wa Azam naye alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kumchezea rafu Kaddioiu Yuossef.

Friday, May 3, 2013

KIKOSI CHA PILI CHA TAIFA STARS CHAANZA KAMBI



Wachezaji 25 kati ya 30 walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha pili cha Taifa Stars (Young Taifa Stars) wameripoti kambini ambapo mazoezi yalianza tangu jana jioni (Mei 2 mwaka huu).

Kocha Kim amewaitaka wachezaji katika kambi hiyo ya siku tano ili kuangalia uwezo wao katika maeneo kadhaa kwa lengo la kupata baadhi ambao anaweza kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars siku za usoni.

Wachezaji watano walioshindwa kujiunga katika kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam ni Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, Samih Nuhu na Seif Abdallah ambao wako Morocco na timu yao ya Azam.

LALA SALAMA VPL KUENDELEA JUMAPILI

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.

Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.

African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.

KAMATI YA UTENDAJI TFF KUKUTANA MEI 9



Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Mei 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu uchaguzi wa shirikisho.

Kikao hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.

FIFA katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.

KILA LA KHERI AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam katika mechi yake ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayochezwa Morocco kesho (Mei 4 mwaka huu).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa jijini Rabat kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Morocco. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Azam iko nchini Morocco kwa karibu wiki nzima sasa ikijiandaa kwa mechi hiyo chini ya Kocha wake Stewart John Hall. Msafara wa Azam nchini humo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.

KAMATI YA MASHINDANO KUPITIA MAANDALIZI RCL



Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.

Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).

Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.

Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.

YANGA, COASTAL UNION ZAINGIZA MIL 66/-



Mechi namba 172 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa juzi (Mei 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 imeingiza sh. 66,022,000.

Watazamaji 11,478 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,378,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,071,152.54.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 10,230 na kuingiza sh. 51,150,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 69 na kuingiza sh. 1,380,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,819,793.62, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 4,691,876.17, Kamati ya Ligi sh. 4,691,876.17, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,345,938.09 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,824,618.51.

Thursday, May 2, 2013

FIFA YAIAMURU TFF KUANZA UPYA MCHAKATO WA UCHAGUZI



Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa uchaguzi baada ya kubaini kasoro iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.


FIFA ambayo ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF, ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa, suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya FIFA kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa juzi kwa barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke.

Baada ya kupokea barua hiyo, Rais wa TFF alifunga safari kwenda Dodoma jana kukutana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

“Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake tumepokea maagizo hayo. Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka.” alisema Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.

“Lengo letu ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale mambo yanayoweza kufanyika kwa pamoja, yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA,.”alisema.

Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyika tarehe 23 na 24 Februari 2013 na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini baadhi ya wagombea walienguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na ndipo walipo andika barua FIFA kuomba iingilie kati.

Rais Tenga alisema kuwa ujumbe wa FIFA ulikutana na pande zote zilizoathiriwa na mchakato wa uchaguzi na kwamba baada ya kukusanya taarifa hizo, maagizo hayo ya FIFA sasa yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya muda mrefu katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

Katika barua hiyo, FIFA imeiagizaTFF:

1. Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;

2. Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;

3. Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:

4. Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.

Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji.

Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibara ya 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja.

Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.

“Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapogombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema barua hiyo ya FIFA.

Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.

LADY JAYDEE 'JIDE' ATOA WOSIA MZITO, AWASHUKIA RUGE NA KUSAGA

Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja.  Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi na bado naendelea ku experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa.
Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha , ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari.

Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki.

Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliyopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa.

Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anayeweza ku survive bila wao.

Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria.

Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu.

Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia.

Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa.

Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao.

Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu.

Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige mawe, enyi mtakaokuwa hai baada yangu.

Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu.

Sina haja wanipende pia kwa kuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.

Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa, lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge.

Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha, lakini naona moto ndio unazidi kuwaka.

Na hii ni kwa sababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha. Hamuwezi kumiliki dunia.

Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani? Kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba, basi beba jiwe liimbe liwe star.

Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie?

Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto, wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu.

Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili.

Mnadhani nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi? Nyimbo hazitakuwa nzuri.

Basi sawa, ngoja tuone MUNGU ni nani, binadamu nani??
Kwa hiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi??

Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili.

Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu.

Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma?? Roho gani hiyo??

Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu

JIDE



YANGA KWA RAHA ZAO


YANGA jana ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pamoja na kulazimishwa sare hiyo, Yanga bado inaongoza ligi hiyo huku ikiwa imeshatwaa ubingwa, ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 26. Yanga imesaliwa na mechi moja dhidi ya Simba itakayochezwa Mei 18 mwaka huu.

Coastal Union ililianza pambano hilo kwa kasi na kulishambulia lango la Yanga mara kwa mara. Kutokana na mashambulizi hayo, kipa Saidi Mohamed wa Yanga alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 10 kupangua shuti la Pius Kisambale.

Dakika mbili baadaye, Yanga ilijibu shambulizi hilo kupitia kwa Jerry Tegete, ambaye alifunga bao la kwanza kwa shuti kali. Tegete alifunga bao hilo kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Nizar Khalfan.

Coastal nusura isawazishe wakati Selemani Kassim Selembe alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilipaa sentimita chache kwenye lango la Yanga.

Abdi Banda aliisawazishia Coastal Union dakika ya 15 kwa mpira wa adhabu baada ya beki mmoja wa Yanga kucheza rafu karibu na eneo la hatari.

Joseph Mahundi nusura aiongezee Coastal bao la pili dakika ya 43 baada ya kufyatua kiki kali kwenye lango la Yanga, lakini kipa Saidi aliiona na kuipangua.

Katika kipindi cha pili, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.

Wednesday, May 1, 2013

YANGA KUIENDEA SIMBA PEMBA



UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kuipeleka timu hiyo kambini kisiwani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya mwisho ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, Yanga itakwenda Pemba baada ya mchezo wao mwingine wa ligi hiyo dhidi ya Coastal Union uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Yanga na Simba limepangwa kuchezwa Mei 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tayari Yanga imeshatwaa taji hilo kutokana na kuwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 24, ambazo hakuna timu nyingine inayoweza kuzifikia.

Simba imeshapoteza matumaini ya kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo na sasa inawania nafasi ya nne, ikichuana vikali na Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa habari hizo, Yanga itakwenda Pemba kutokana na kupokea maombi mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wanaoishi visiwani humo.

"Wanachama wetu walioko Pemba na Zanzibar kwa ujumla wametuomba tukaweke kambi huko kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Simba na sisi tumewakubalia. Timu itakwenda huko baada ya mchezo wetu dhidi ya Coastal Union," kilisema chanzo hicho cha habari.

Uamuzi wa Yanga kuweka kambi Pemba pia umetokana na ombi la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts kutaka timu ikaweke kambi nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

MTANZANIA AOMBEWA ITC NORWAY



SHIRIKISHO la Soka la Norway (NFF) limetuma maombi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kupatiwa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) mchezaji Godfrey Mlowoka wa Tanzania.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, NFF inamuombea hati hiyo Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL ya nchini humo akiwa mchezaji wa ridhaa, ambapo klabu yake ya zamani imetajwa kuwa ni Sadani.

Wambura alisema TFF inayafanyia kazi maombi hayo na baada ya taratibu zote kukamilika, hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini Norway.

Wakati huo huo, Wambura amesema mikoa 18 kati ya 27 ya kimpira imeshapata mabingwa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa TFF.

Wambura alisema jana kuwa, timu tatu za juu katika Ligi hiyo ya mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).

Alisema ligi ya FDL inazo jumla ya timu 24, ambapo tatu katika ligi hiyo ni zile zilizoshuka daraja msimu huu. Timu hizo ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya Rukwa na Morani FC ya Manyara.

Aliwataja mabingwa waliopatikana hadi sasa, mikoa yao kwenye mabano kuwa ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).

Wengine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).

Wambura alisema kila klabu inatakiwa kulipa ada ya ushiriki, ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika ligi ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho.

"TFF inapenda kusisitiza kuwa, hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo,"alisema Wambura.

KOCHA MOROKO ALIPUA BOMU



KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Coastal Union ya Tanga, Hemed Moroko amewataka wachezaji wa timu hiyo kujitambua na kucheza soka kwa malengo.

Akizungumza na Burudani mjini hapa mwanzoni mwa wiki hii, Moroko alisema wachezaji wanapaswa kutambua kuwa, kucheza soka ni ajira kwao, hivyo wajiepushe na vishawishi vya kuihujumu timu yao.

Moroko alisema inashangaza kuona kuwa, baadhi ya wachezaji wamekuwa wakikubali kucheza chini ya kiwango katika baadhi ya mechi kutokana na kushawishiwa kufanya hivyo na viongozi wa timu pinzani.

"Hili ni kosa kubwa kwa mchezaji kwa sababu hilo siyo lengo lake katika kucheza soka,"alisema kocha huyo, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Zanzibar.

"Mchezaji anaposajiliwa, anakuwa na kiwango bora kinachomshawishi kocha kumpa namba kwenye kikosi cha kwanza, lakini unapofika wakati wa ligi, anakubali kununuliwa na timu pinzani," alilalamika kocha huyo.

Moroko alisema kufanya vibaya kwa timu katika ligi husababisha makocha kubebeshwa lawama wakati wanaosababisha hali hiyo ni baadhi ya wachezaji.

Kocha huyo alisema wachezaji wengi wanaojihusisha na vitendo hivyo ni wale walioachwa na klabu kubwa na ndio chanzo cha kuporomoka kwa timu wanazozichezea.

“Mtatuhukumu makocha kila mara, lakini tatizo kubwa katika klabu za Tanzania ni kwamba, wanaoharibu mchezo ni wachezaji wanaokubali kuzihujumu timu zao,"alisisitiza.

Moroko alisema mdudu anayezitafuna klabu za mikoani, ni wachezaji wanaokubali kuhongwa na timu pinzani kwa maslahi yao binafsi.

YANGA YAPANIA REKODI DARFUR



KLABU ya Yanga imetamba kuweka rekodi nyingine ya kutwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Kagame ugenini.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, tayari Kocha Ernest Brands ameshaandaa programu kwa ajili ya michuano hiyo.

"Tumepania kuweka rekodi ya kutwaa kombe la Kagame ugenini kwa mara ya tatu ndio sababu tunataka kuanza maandalizi mapema,"alisema Bin Kleb.

Aliongeza kuwa, kikosi cha Yanga kina uwezo mkubwa wa kuweka rekodi hiyo kutokana na kufanya vizuri katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

"Tunafanya mambo yetu kwa umakini mkubwa ili tuweze kuendelea kutisha na hilo halina mjadala. Baada ya ligi kuu kumalizika tu, tutakwenda kuweka kambi mahali kwa ajili ya kujiandaa kwa Kombe la Kagame,"alisema.

Mabingwa hao wa ligi kuu msimu huu, wameweka rekodi ya kutwaa taji hilo kabla haijamalizika kutokana na kuwa na idadi kubwa ya pointi, ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Yanga ilitwaa kombe la Kagame ugenini kwa mara ya kwanza 1993 nchini Uganda kabla ya kulitwaa tena 1999 nchini humo. Pia ilitwaa kombe hilo mara mbili mfululizo 2011 na 2012.

Michuano ya kombe hilo imepangwa kufanyika Juni mwaka huu katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeamua kupeleka michuano hiyo katika Jimbo la Darfur kwa lengo la kulisaidia kupata maendeleo.

CECAFA inaamini kuwa, kwa kuendesha michuano hiyo na kufanikiwa, utakuwa uthibitisho wa kurejea kwa amani katika jimbo hilo, ambalo lilikuwa likikabiliwa na vita vya mara kwa mara.

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alitembelea jimbo hilo wiki iliyopita kwa ajili ya kukagua maandalizi ya michuano hiyo, ikiwa ni pamoja na kukagua viwanja na hoteli.

Michuano hiyo imepangwa kufanyika Darfur Kaskazini na Kordofan Kusini na itadhaminiwa na Gavana wa Darfur Kaskazini, Osman Mohamed Yousef.

KASSIM DEWJI: NIPO TAYARI KUREJEA SIMBA




MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage wiki iliyopita alikaririwa akisema kuwa, anatarajia kuisuka upya kamati ya usajili kwa kuwarejesha kundini baadhi ya wanachama waliotoa mchango mkubwa kwa klabu hiyo. Miongoni mwa wanachama wanaotajwa kurejeshwa Simba ni katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Kassim Dewji. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kiongozi huyo wa zamani wa Simba anaelezea msimamo wake kuhusu taarifa hizo.

SWALI: Kwa muda mrefu sasa umekuwa kimya kuhusu masuala ya soka, hasa katika klabu yako ya Simba. Unaweza kueleza ni kwa sababu gani umejiweka pembeni na Simba?

JIBU: Ni kweli nipo kimya kuhusu Simba, lakini sababu kubwa ni kwamba sina nafasi yoyote katika uongozi. Nimebaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Simba nikiangalia mambo yanavyokwenda.

SWALI: Je, umebaini kuwepo kwa kasoro yoyote ndani ya Simba iliyosababisha timu ifanye vibaya katika msimu huu wa ligi?

JIBU: Sio siri kwamba kikosi chetu msimu huu hakikusajiliwa vizuri. Kinapaswa kufumuliwa na kusukwa upya ili kiweze kutoa ushindani na kufanya vizuri msimu ujao. Tusipokuwa makini katika hili, hatuwezi kufika mbali katika ligi.

SWALI: Mbali na usajili kutokuwa mzuri, unadhani ni sababu zipi zingine zilizosababisha timu ivurunde msimu huu?

JIBU: Baadhi ya wachezaji, uwezo wao ni mdogo na wengine wamejenga kiburi kwa viongozi na benchi la ufundi. Wanapopewa maelekezo na kocha, wanakuwa wabishi kutekeleza na kujiona mastaa. Wachezaji wa aina hii hawapaswi kuendelea kuwemo ndani ya Simba.

Tatizo lingine lililoigharimu Simba ni wachezaji kushindwa kucheza kwa kujituma uwanjani, hasa inapotokea malipo yao ya mishahara yamechelewa. Hili ni tatizo sugu. Sidhani kama yupo kiongozi anayependa kuchelewesha mishahara ya wachezaji kwa makusudi. Kila kiongozi anapenda kuona mchezaji anapata haki zake anazostahili.

SWALI: Hivi karibuni ulitokea mvurugano ndani ya Simba na kudaiwa kwamba, baadhi ya viongozi wa zamani, ukiwemo wewe wamekuwa wakihujumu timu. Je, kuna ukweli wowote kuhusu tuhuma hizi?

JIBU: Kwa watu wanaonifahamu vyema, hakuna anayeweza kupinga kwamba mimi ni Simba damu. Naipenda Simba kwa moyo wangu wote. Kamwe siwezi kuihujumu kwa njia yoyote. Nimepata umaarufu kwa sababu ya Simba.

Nimeshawahi kuiongoza Simba miaka ya nyuma na kuiletea mafanikio makubwa, hivyo kuisaliti ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa kwangu. Kama ni kugombea uongozi, ninao uwezo wa kufanya hivyo na wanachama ndio watakaoamua.

Hao wanaodai kwamba nimekuwa nikiihujumu Simba, nadhani wamekosa la kuzungumza na wanataka kuficha udhaifu wao. Lengo lao ni kunichafua. Kamwe siwezi kuwa na mawazo ya kuihujumu Simba ili ifungwe. Pia sina mawazo ya kutaka uongozi kwa sasa kwa vile tunao viongozi waliochaguliwa kikatiba.

Nawaomba watu wanaonihusisha na vitendo hivyo waache mara moja kwa sababu huko ni kurudisha nyuma maendeleo ya klabu yetu, ambayo ina historia kubwa barani Afrika.

SWALI: Uliupokeaje uamuzi wa makamu mwenyekiti wa zamani, Geofrey Nyange 'Kaburu' na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope kujiuzulu?

JIBU: Siwezi kusema lolote kwa sasa kuhusu uamuzi wao huo zaidi ya kuwataka wanachama wa Simba kuwa watulivu. Wanapaswa kuivumilia timu yao, ambayo inaundwa na vijana wengi wachanga. Nina hakika vijana hawa wakikaa pamoja kwa miaka miwili, Simba itakuwa na timu tishio sana katika ligi.

Nina hakika baada ya ligi ya msimu huu kumalizika, uongozi utachukua hatua za kukiimarisha zaidi kikosi hicho na kukifanya kitishe msimu ujao. Ni suala la kukipa muda tu.

SWALI: Hivi karibuni, Rage alikaririwa akisema kuwa, anafikiria kuunda upya kamati ya usajili na upo uwezekano mkubwa wa wewe kurejeshwa kwenye kamati hiyo. Unasemaje kuhusu taarifa hizi?

JIBU: Sijapata taarifa zozote kuhusu jambo hilo, lakini nipo tayari kuitumikia Simba wakati wowote. Na iwapo itakuwa hivyo, naahidi kwamba nitafanyakazi hiyo kwa moyo wangu wote kwa lengo la kuhakikisha kuwa, Simba inarejesha hadhi yake na kupata mafanikio makubwa zaidi.

SWALI: Ungependa kutoa ushauri gani kwa wanachama wa Simba, ambao wamekuwa wakitaka uongozi wa sasa uondoke madarakani?

JIBU: Nawaomba wawe na subira na uvumilivu. Wasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa na uongozi katika kurekebisha matatizo yaliyojitokeza msimu huu.

Kama wana mawazo, maoni ama ushauri kwa uongozi, wasubiri mkutano ulioitishwa Julai mwaka huu. Hakuna sababu ya kushinikiza kufanyika mambo, ambayo hayawezekani.

SWALI: Ligi kuu inatarajiwa kumalizika Mei 18 kwa mechi saba, ikiwemo ya Simba na Yanga. Nini mtazamo wako kuhusu mechi hii?

JIBU: Kama tutaendelea kuwa watulivu na wenye umoja kama ilivyo sasa, sioni kipi kinachoweza kutukwamisha kuifunga Yanga. Ni lazima tulinde heshima yetu kwa Yanga.

JAYDEE KUZINDUA ALBAMU MPYA MEI 31

MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Judith Wambura 'Lady JayDee' anatarajia kuzindua albamu yake mpya katika onyesho litakalofanyika Mei 31 mwaka huu.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Lady JayDee alisema albamu yake hiyo yenye nyimbo 10, ambayo ni ya sita, itajulikana kwa jina la Nothing but the truth.

JayDee alisema onyesho hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge uliopo Msasani, Dar es Salaam.

Alisema uzinduzi wa albamu hiyo utakwenda sambamba na sherehe za kutimiza kwake miaka 13 tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki.

"Nawashukuru sana mashabiki wangu kwa kuendelea kuniunga mkono na kunipa nguvu. Pia navidhukuru vyombo vya habari kwa kukuza na kuilinda sanaa ya Tanzania bila kujali maslahi binafsi,"alisema msanii huyo, ambaye anamiliki bendi ya Machozi.

Kwa mujibu wa JayDee, katika onyesho hilo, atapiga nyimbo zake zote zilizowahi kutamba, ikiwa ni pamoja na zile alizowashirikisha wasanii mbalimbali nchini.

Alisema onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo litadhaminiwa na kituo cha televisheni cha East Africa

NAKAAYA AKIRI KUWA MJA MZITO



MSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nakaaya Sumari amekiri kuwa na uja uzito na kusema kuwa, anatarajia kujifungua wakati wowote.

Hata hivyo, Nakaaya hakuwa tayari kutaja umri wa uja uzito alionao na baba wa mtoto, anayetarajia kujifungua.

"Uja uzito nilionao ni wa mtu mtakatifu, siyo mtu anayejulikana," alisema Nakaaya alipozungumza na kituo kimoja cha redio mjini Dar es Salaam wiki hii.

Wakati huo huo, Nakaaya amerekodi wimbo wake mpya unaojulikana kwa jina la Utu uzima dawa.

Nakaaya alisema amerekodi wimbo huo katika studio za Fish Crub chini ya usimamizi wa Prodyuza Dunga.

Alisema tayari kibao hicho kimeshaanza kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini na kupokewa vizuri na mashabiki wa muziki.

Nakaaya alianza kujipatia umaarufu mkubwa baada ya kuibuka na kibao chake kinachokwenda kwa jina la Mr. Politician. Alirekodi kibao hicho miaka mitatu iliyopita.

Baada ya kupata mafanikio makubwa kutokana na kibao hicho, Nakaaya aliamua kujitosa kwenye ulingo wa siasa kwa kujiunga na CHADEMA kabla ya kurejea CCM.

KOLABO ZAMIMINIKA KWA VANESSA


MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Vanessa Mdee amesema amekuwa akipokea maombi mengi kutoka kwa wasanii mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya nao kolabo.

Vanessa alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, maombi aliyoyapata hadi sasa ni zaidi ya 10 na yamemfanya ajione msanii aliyepata mafanikio katika kipindi kifupi.

Binti huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, amepokea maombi hayo baada ya kufanya vizuri katika wimbo wake mpya wa Closer.

"Unajua watu wanapenda vitu vipya na vitu tofauti, hivyo namshukuru Mungu nimepata ofa za kutosha na kwangu hayo ni mafanikio makubwa,"alisema.

"Mtu anapotaka kukuweka kwenye korasi ya wimbo wake, ujue amekukubali na anaamini utaufanya wimbo wake uwe na mvuto zaidi, hivyo kwangu hilo ni jambo zuri na la kuvutia,"aliongeza.

Vanessa alisema binafsi amepata mafanikio makubwa kupitia wimbo wake wa Closer kutokana na kusaidiwa na Ommy Dimpoz na Ambwene Yesaya (AY) katika viitikio.

Alisema anamshukuru Mungu kuona kwamba watu wameanza kukitambua kipaji chake na kumkubali kama msanii chipuziki anayekuja juu kimuziki.

REHEMA TAJIRI ALIA NA MAMA MKWE

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanamuziki Rehema Tajiri ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Msikilize mama.

Rehema amerekodi kibao hicho kwa kutumia miondoko ya zouk, akimshirikisha msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Dogo Sama.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Rehema alisema amerekodi kibao hicho katika studio za Suresh zilizopo Temeke, Dar es Salaam.

Rehema alisema katika kibao hicho, amezungumzia masuala ya mapenzi kati yake na mpenzi wake, lakini kikwazo kikubwa kipo kwa mkwe wake.

"Nimesimulia jinsi mimi na mpenzi wangu tunavyopendana, lakini mkwe wangu (mama wa mpenzi wake) hanipendi, anataka niachane na mwanawe,"alisema.

Kwa mujibu wa Rehema, tayari wimbo huo umeshaanza kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini na kuwavutia mashabiki wengi.

Hata hivyo, kutokana na ushauri alioupata kutoka kwa baadhi ya wataalam wa muziki, Rehema alisema anatarajia kuufanyia marekebisho kidogo wimbo huo.

"Baadhi ya wataalamu waliousikia wimbo huo, wamenishauri niurekodi upya kwa kutumia vyombo vya muziki badala ya kutumia ala za studio. Wanasema kwa hadhi yangu, sipaswi kurekodi muziki wa kompyuta,"alisema.

Rehema amewataka mashabiki wake wakae mkao wa kula kwa vile amejipanga upya kuhakikisha anateka tena soko la muziki nchini.

Alisema ukimya wake wa muda mrefu ulitokana na kutingwa na matatizo ya kifamilia na pia kujipanga upya.

MR. NICE AVUNJA UKIMYA, AJA NA CHARLIE WA KIBERA



WASWAHILI wanasema, ukimuona kobe yuko kimya, ujue anatunga sheria na kwamba kimya kingi kina mshindo mkuu.

Hivyo ndivyo anavyotaka kudhihirisha msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nice Lucas Nkenda, maarufu kwa jina la Mr. Nice.

Msanii huyo, ambaye kwa sasa ameamua kuhamishia maskani yake nchini Kenya, anatarajia kuzindua albamu yake mpya ya Charlie wa Kibera hivi karibuni nchini humo.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha East Africa wiki hii, Mr. Nice alisema uzinduzi wa albamu hiyo unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

Mr. Nice alisema ameamua kuibuka na albamu hiyo kwa lengo la kuwadhihirishia mashabiki wake kwamba hajafulia ama kufilisika kama watu wengi wanavyompakazia.

Kwa mujibu wa Mr. Nice, asilimia 20 ya mapato yatakayopatikana katika onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo, atayatoa kwa serikali ya Kenya ili yawasaidie watoto yatima na wenye matatizo nchini humo.

Msanii huyo aliyewahi kutamba katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati miaka ya mwanzoni mwa 2000, alisema si kweli kwamba amefilisika kimuziki.

Alisema madai hayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya maadui zake kwa lengo la kumdhoofisha kimuziki na kumkatisha tamaa.

"Wanaotoa madai hayo wamekuwa wakitumiwa na adui zangu. Ni vichaa. Kichaa anapokuibia nguo zake na wewe ukaamua kumkimbiza, wewe ndiye utakayeonekana kichaa,"alisema.

"Pesa kazi yake ni matumizi. Nafanyakazi kutafuta pesa, natoka jasho, nakata viuno stejini kwa ajili ya kutafuta pesa. Na hata kama nimeishiwa, sijawahi kumgongea mtu mlango kumuomba pesa," aliongeza.

Mr. Nice alisema maadui zake hao wanashindwa kumchafua kimuziki kwa sababu wanafahamu wazi kwamba muziki upo kwenye damu yake na ni kipaji alichobarikiwa na Mungu.

Msanii huyo pia alikanusha madai kwamba, amekuwa akijihusisha na uvutaji bangi na dawa za kulevya. Alisema katika maisha yake yote, hajawahi kutumia vitu hivyo au sigara.

Mr. Nice alijizolea umaarufu mkubwa alipoibuka na vibao vyake vilivyotamba kama vile ‘Kidali po’, ‘Kila mtu na demu wake’, ‘Kikulacho’, ‘Fagilia’, ‘Mbona umeniacha’, ‘Rafiki’ na ‘First Lady’.