KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 11, 2012

Wachezaji Yanga wapasua ya moyoni



BAADHI ya wachezaji wa timu ya soka ya Yanga wamekanusha madai kuwa, walicheza chini ya kiwango katika mechi yao dhidi ya Simba kwa lengo la kuwahujumu viongozi.
Wachezaji hao wamesema kipigo cha mabao 5-0 walichokipata kutoka kwa Simba mwishoni mwa wiki iliyopita kilitokana na kuzidiwa kimchezo na pia baadhi yao kukosa ari.
Wakizungumza na Burudani wiki hii kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema viongozi wa Yanga wameshindwa kuwalipa madeni wanayodai kwa miezi kadhaa.
Mmoja wa wachezaji hao alisema, uongozi uliahidi kuwalipa madeni hayo mara baada ya mechi kati yao na Simba, lakini hadi sasa wapo kimya.
Akifafanua kuhusu madeni hayo, mchezaji huyo alisema wanadai mishahara ya miezi mitatu na posho za mechi 15.
Alisema wakati timu ilipokwenda kambini Bagamoyo, uongozi uliwapatia sh. 100,000 kila mchezaji kwa ajili ya kuacha nyumbani.
Mchezaji huyo alisema pia kuwa, kabla ya mechi yao dhidi ya Simba, uongozi uliamua kuwalipa wachezaji sh. 300,000 kila mmoja baada ya kugoma kwenda uwanjani.
Nyota mwingine wa timu hiyo alisema, wamesikitishwa na kitendo cha viongozi wao kuwatekeleza baada ya pambano hilo kumalizika.
‘Hali ni mbaya kwa wachezaji na mapenzi ya kuichezea Yanga msimu ujao kwa baadhi yetu yameanza kupungua,’ alisema.
Mchezaji huyo alisema anahisi uongozi huenda ukashindwa kuwalipa madai yao kutokana na kipigo walichokipata kutoka kwa Simba.
Pambano kati ya Simba na Yanga lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, liliingiza sh. milioni 260 na kila timu ilipata mgawo wa sh. milioni 62.

CHAMBUA: Moto wa Simba si mchezo


KIPIGO cha mabao 5-0 ilichokipata Yanga kutoka kwa Simba kimepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa soka nchini. Wapo wanaowalaumu wachezaji kwa uzembe na wengine wamewatupia lawama viongozi kwa kutoihudumia timu ipasavyo. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars, Sekilojo Chambua amekielezea kipigo hicho kuwa ni aibu kubwa katika historia ya Yanga katika miaka ya hivi karibuni. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, mchezaji huyo anaelezea alivyokipokea kipigo hicho.
SWALI: Wiki iliyopita, timu yako ya zamani ya Yanga ilicheza na Simba na kupokea kipigo cha mabao 5-0. Umekipokeaje kipigo hicho na unadhani nini chanzo cha maafa hayo?
JIBU: Kusema ule ukweli, kipigo hicho kimenisikitisha sana kwa sababu haijawahi kutokea kwa miaka mingi Simba kuifunga Yanga idadi hiyo ya mabao. Wakati mimi nachezea Yanga, hatukuwahi kupatwa na aibu hii. Hii ni aibu ya mwaka na siwezi kukisahau kipigo hicho katika maisha yangu.
Naweza kusema kwamba kipigo hicho kimetokana na matatizo mengi, yakiwemo ya uongozi kushindwa kufuata ushauri au programu za kocha wa timu hiyo, ambaye amemaliza mkataba wake hivi karibuni, Kostadin Papic. Aliporejea nchini mwaka jana, Papic alikuja na vitu vingi vizuri, lakini utekelezaji wake ulikuwa sifuri.
Kwa mfano, kuna wakati alitaka timu ikaweke kambi Mwanza kwa ajili ya kujiandaa na ligi kuu, lakini viongozi walikataa. Lengo lake kubwa lilikuwa kutaka kupata nafasi ya kuwaona wachezaji wapya ambao, walisajiliwa na Kocha Sam Timbe kutoka Uganda.
Sababu zingine zilizoifanya Yanga ifanye vibaya katika ligi ni kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wachezaji, ambao hawana uwezo wa kuichezea timu hiyo. Kitimu, Simba walikuwa na timu nzuri zaidi msimu huu kuliko Yanga.Tatizo lingine lililokuwepo Yanga ni baadhi ya viongozi wa klabu
kutotaka kusikiliza ushauri. Awali waliwahi kupewa taarifa ya kutomchezesha Nadir Haroub 'Cannavaro' katika mechi yao dhidi ya Coastal Union kule Tanga, lakini walipuuza na kujikuta wakipoteza pointi tatu.
Kwa upande wa Simba, napenda kukiri wazi kwamba, timu yao ipo vizuri na imekamilika kila idara na ilikuwa na uwezo mkubwa wa kushinda mchezo huo kutokana na kuwa fiti kwa asilimia 100 kuliko Yanga, ambayo maandalizi yake kwa ajili ya mchezo huo yalikuwa ya zima moto kuliko wapinzani wetu, ambao msimu huu wapo makini kila kukicha.
SWALI: Kwa maana hiyo, ulichokigundua ni kwamba wapo baadhi ya wachezaji, ambao ni wabovu ndani ya kikosi cha Yanga?
JIBU: Ukweli huo upo dhahiri na ulianza kuonekana tangu Yanga ilipocheza na Zamalek ya Misri katika mechi ya michuano ya klabu bingwa Afrika. Inasikitisha kuona kuwa, wachezaji wanaolipwa mamilioni ya pesa, hasa wale wanaotoka nje, wameshindwa kutoa msaada wowote kwa timu yao na kukosa mabao mengi ya wazi na kusababisha tutolewe mapema. Binafsi naamini wakati umefika kwa viongozi wa benchi la ufundi la Yanga na timu nyingine za soka hapa nchini, kuwa makini na wachezaji, ambao zinataka kuwasajili kwa kupima kwanza uwezo wao kabla ya kufikia uamuzi huo.
Tatizo lingine la Yanga lilikuwa ni wachezaji wake kuonyesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu, hasa katika mchezo wao dhidi ya Azam, ambapo walimpiga mwamuzi Israel Nkongo. Katika mechi hiyo, wachezaji wa Yanga hawakuandaliwa kisaikolojia.
Wengi waliingia ndani ya mchezo huo wakiwa na mawazo ya kukosa pesa zao, matokeo yake ni kujazba, ambayo ilichangia timu kufungwa kwa kufanya madhambi, ambayo walikuwa na uwezo wa kuyaepuka badala ya kusababisha penaliti tatu. Nadhani pia kuwa, kocha Fred Felix Minziro alipaswa kubadili mfumo wa uchezaji, hasa katika kipindi cha pili. Yanga haikupaswa kuiga aina ya uchezaji ya Simba. Ilitakiwa kutumia staili tofauti.
Pengine kikubwa zaidi ni kwamba, mgogoro uliopo Yanga baina ya viongozi na wanachama ulichangia kuwaathiri wachezaji. Nadhani ni vyema ufike wakati viongozi wasajili wachezaji wenye mapenzi na klabu badala ya kuokoteza wachezaji holela.
SWALI: Wewe ni mchezaji wa zamani, unafikiri mgogoro kati ya wazee na viongozi ulichangia Yanga kupokea kipigo hicho? Na unadhani ni sahihi kwa viongozi waliopo madarakani kujiuzulu?
JIBU: Nadhani yapo matatizo ndani ya uongozi wa Yanga, lakini bado ninajiuliza kwa nini wachezaji nao waingie kwenye mgogoro huo, wakati wao ni waajiriwa na tayari wameshaisababishia klabu aibu.
Ni kweli yapo matatizo ya wazi na kila mtu anajua kwamba hali ndani ya klabu hiyo kongwe ya soka nchini sio nzuri, hivyo umefika wakati kwa uongozi kujitazama upya ili kuepusha kutokea matatizo makubwa zaidi.
Balaa, ambalo naliona linaweza kutokea ni Yanga kupoteza wachezaji wengi wazuri msimu ujao na pengine amani kutoweka klabuni. Hivyo nawashauri viongozi wa Yanga kulifikiria kwa makini jambo hili.
SWALI: Wewe ni mmoja kati ya wachezaji wa zamani wa Taifa Stars, una maoni gani kuhusu kujitoa kwa mshambuliaji Jonh Bocco wa Azam kwenye timu hiyo baada ya kuzomewa na mashabiki na kisha TFF kumuomba afute mawazo hayo?
JIBU: Binafsi nimekerwa sana na tabia ya baadhi ya mashabiki wa soka kuwazomea wachezaji, hasa wanapofanya vibaya ndani ya kikosi cha Taifa Stars. Tabia hiyo inawavuruga sana wachezaji ndani ya dimba na pengine kuwatoa kabisa kwenye mchezo.
Unajua mchezo wa soka ipo siku unamkubali mchezaji, lakini wakati mwingine unakataa na hata kusababisha kocha amgundue mapema na kumtoa kwenye timu. Lakini napenda kusema kwamba, Bocco bado ni mdogo na ni muhimu kuendelea kuwepo katika kikosi hicho.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaonya wadogo zangu (wachezaji wa sasa) kujichunga na kulinda vipaji vyao kwa vile huo ndio mtaji wa kuanzisha biashara katika maisha yao ya siku zijazo.
Wapo wachezaji wazuri, ambao wameanza kupoteza mwelekeo kama ilivyo kwa Jerryson Tegete, ambaye nina imani kwamba inabidi afanye kazi ya ziada ili kurejesha kiwango chake cha zamani. Pamoja na kufungiwa, bado naamini Tegete amepotea kidogo katika soka.
SWALI: Uliwahi kuwa kocha wa timu ya Polisi Dodoma miaka michache iliyopita. Unadhani ni kipi kilichosababisha timu hiyo ifanye vibaya katika ligi msimu huu na kushuka daraja?
JIBU: Kushuka daraja kwa Polisi Dodoma kumetokana na hali mbaya ya kuchumi. Uwezo wa jeshi hilo kuihudumia Polisi ulipungua. Tatizo hili linanikumbusha umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuangalia uwezekano wa kuzitafutia wadhamini timu zote za ligi kuu badala ya kutegemea udhamini wa Vodacom pekee.
Zamani kulikuwepo na timu kama vile Sigara, ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na idadi kubwa ya wachezaji wao walikuwa waajiriwa wa kampuni hiyo.
Pia zilikuwepo timu kama vile Pamba, iliyokuwa inamilikiwa na Mamlaka ya Pamba Tanzania, RTC Kagera, Ushirikia ya Moshi, Ndovu na Pilsner, ambazo zote zilikuwa zikimilikiwa na kampuni mbalimbali na ziliweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya soka, lakini zote hizo hazipo hivi sasa.
Yaliyoikuta Polisi ni sawa na yale yaliyozikuta Moro United na Villa Squad, ambazo nazo zimeshuka daraja. Ni matatizo ya pesa. Nadhani wakati umefika kwa timu za aina hii kuanza kusaidiwa kwa udhamini

Tuesday, May 8, 2012

Taifa Queens yaanza kwa kishindo kuwania ubingwa wa Afrika


TIMU ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, leo imeanza vema mashindano ya Afrika baada ya kuichapa timu ya Lesotho kwa magoli 57-13, katika mechi ya ufunguzi iliyorindima kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Taifa Queens ikiongozwa na wafungaji wake, Mwanaidi Hassan ‘Pereirra’ (GS) na Irene Elias (GA), ambao walikuwa wakiunganishwa vema na kiungo, Faraja Malaki (C), Evodia Kazinja (WA), na Restuta Boniface (WD), hadi robo ya kwanza inamalizika, walikuwa mbele kwa magoli 13-3.

Robo ya pili, Taifa Queens ilizidi kuchanua mbele ya mgeni rasmi, Mke wa Rais Kikwete, Mama Salma, ambapo hadi inamalizika walitoka na magoli 23-9 huku robo tatu wakimaliza kwa 40-13.

Robo ya nne, ukuta wa Taifa Queens uliokuwa chini ya Lilian Sylidion (GD), na Doritha Mbunda (GK), uliwabana vilivyo wafungaji wa Lesotho na hadi mchezo unamalizika, waliibuka kidedea kwa ushindi huo wa magoli 57-13.

Michuano hiyo inayoshirikisha nchi nane, inaendelea tena leo kwa mechi kati ya Botswana na Zambia, Malawi na Zimbabwe, huku wenyeji Tanzania wakitupa karata tena kwa Zambia.

Monday, May 7, 2012

Umri wa Lulu waanza kuzua utata mahakamani


UTATA kuhusu umri wa mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ leo umeanza kutoa matokeo, kwenye ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, huku kesi yake ikipigwa tena kalenda hadi Mei 21, mwaka huu.
Lulu anayekabiliwa na kesi ya kumuua mwigizaji mwenzake, Steven Charles Kanumba, kwa sasa anasema ana miaka 17, lakini katika mahojiano kwenye kipindi cha TV cha Mikasi, kabla ya kifo cha The Great aliwahi kusema ana umri wa miaka 18.
Wakili wa mwigizaji huyo aliyekulia kwenye sanaa hiyo kuanzia akiwa kinda katika kundi la Kaole Sanaa la Magomeni pamoja na marehemu Kanumba, Kenned Fungamtama leo aliwasilisha ombi katika Mahakama hiyo, akiitaka iitupilie mbali kesi hiyo ili ikafunguliwe upya katika Mahakama ya Watoto, akidai Lulu ana umri chini ya miaka 18.
Lakini Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda alipinga akisema suala hilo, inabidi kwanza lifanyiwe uchunguzi na vyombo vya dola ili kugundua ukweli kuhusu umri wa Lulu.
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili Kaganda alisema mbali na umri wa Lulu kuwa na utata, lakini hata jina lake halisi nalo ni tatizo, pia kwani wakati wengi wanamfahamu kama Elizabeth Michael, lakini cheti chake cha kuzaliwa kinasomeka Diana Elizabeth.
Katika ufafanuzi wake, Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alisema analitupilia mbali ombi la upande wa utetezi, kwa sababu mtuhumiwa anakabiliwa na kesi ya mauji na imefunguliwa chini ya Kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alisema kwa mujibu wa kesi hiyo, Mahakama yake haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo, zaidi ya Mahakama Kuu.
Hakimu Mmbando ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 21, mwaka huu.Tayari msisimko wa kesi hiyo unaonekana kuanza kupungua taratibu, kwani leo Lulu aliwasilishwa katika ulinzi wa kawaida na mahakamani hapo hakukuwa na idadi kubwa ya watu, kama ilivyokuwa alipofikishwa mahakamani mara ya pili, mwezi uliopita.

Azam yafanya mambo mazito


MKURUGENZI wa Michezo wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo amesema
kwamba wachezaji wa Tanzania wanacheza tu soka bila ya kuwa ndoto, jambo ambalo limewafanya
wasifike mbali
Akizungumza katika hafla maalum ya kuwapongeza wachezaji wa Azam FC kwa kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Thadeo ambaye ni beki wa zamani wa Yanga,
amesema kwamba kutokuwa na ndoto kwa wachezaji wa Tanzania ni tatizo kubwa.
Akizungumza katika
hafla hiyo iliyoandaliwa na Azam FC kwenye hoteli ya JB Belmonte katikati ya Jiji la Dar es Salaam,
Thadeo aliwataka viongozi kuchangia ndoto zao za kuwa timu tishio Tanzania na wachezaji
wao.
Alisema iwapo Azam itakuwa na ndoto ya kufika mbali bila ya wachezaji wao na ndoto hiyo
itakuwa ni sawa na kuchukua sukari na kumwaga baharini.“Lazima wachezaji wa Azam wawe na ndoto
ya kufika mbali, ndipo ndoto za Azam FC zitatimia kwa urahisi,”alisema Thadeo.
Aidha, Thadeo
aliwataka Azam wasiogope mkwara wa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage ambaye mapema
akizungumza kwenye hafla hiyo, alisema Azam wacheze ligi wakigombea nafasi ya pili tu, wakithubutu
kuchukua ubingwa timu yao itakufa.“Katika historia, timu zote zilizochukua ubingwa msimu uliofuata
zilishuka na kufa kabisa kasoro Mtibwa Sugar tu, hivyo nawaomba Azam wacheze ligi wakigombea
nafasi ya pili tu kila mwaka,”alisema Rage.
Akimjibu Rage, Thadeo alisema; “Madai kwamba mkichukua ubingwa timu yenu itakufa, ilikuwa wakati
huo, siyo sasa, hizo timu zilizokufa zilikuwa hazina misingi bora, hazikuwa na academy, hawakuwekeza,
ila Azam iko imara.
Nawapongeza sana na nawaomba endeleeni na juhudi zenu hivyo hivyo.Pamoja na
madai ya Rage, timu zikichukua ubingwa zinakufa, lakini msimu huu mbali na Mtibwa Sugar,
mabingwa mara mbili mfululizo 1999 na 2000, msimu huu wa ligi ukiacha Simba na Yanga, ulishirikisha
bingwa mwingine wa zamani wa ligi hiyo, Coastal Union ya Tanga waliochukua taji hilo mwaka
1988.
Timu zilizowahi kuchukua ubingwa na sasa hazipo kwenye ramani ya soka ni Mseto mwaka 1975
na Tukuyu Stars mwaka 1986, Pan African imeshuka tu daraja na inapigania kurejea Ligi Kuu, ingawa
haina makali ya awali na hiyo ni kama alivyoseam Thadeo hawajawekeza.
Naye Mwenyekiti wa Azam FC, Abubakar Bakhresa alilaani hila na njama ilizokuwa ikifanyiwa timu yake masimu huu ili kuwadhoofisha, ikiwemo kuwapiga marefa wa mechi zao.
Abubakar alisema kwamba pamoja na hila hizo hawakukata tamaa, walipigana hadi dakika ya mwisho na kufanikiwa kupata nafasi ya pili kwenye ligi, ambayo itawawezesha kushiriki Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani.“Soka Tanzania sasa inainuka na imekuwa ajira nzuri na wachezaji wengi sasa wanavutiwa kucheza Tanzania. Mchezaji anaona bora kuja kucheza Azam, kuliko kwenda kuhangaika sehemu nyingine.Wachezaji wa Azam wanalipwa vizuri, wanaishi vizuri na wanafurahia maisha na ajira yao nzuri,”alisema.Alisema wakati wanashiriki Ligi Kuu msimu wa kwanza, ndoto zao zilikuwa kucheza ili kubaki kwenye ligi, lakini msimu wao wa nne, wanashika nafasi ya pili na hayo wanayachukulia kama mafanikio makubwa.Alisema mafanikio haya ni mwendelezo wa mafanikio yaliyoanzia kwenye kutwaa Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu visiwani Zanzibar mbele ya vigogo wa soka Tanzania, Simba na Yanga.Abubakar alisema dhamira ya Azam msimu ujao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho.
Akimalizia hotuba yake, Abubakar aliwataka wachezaji wa Azam kutumia vizuri kipindi chao cha likizo
kwa kujitunza, ili warejee msimu ujao wakiwa vizuri. Akaagana kabisa na wachezaji ambao
hawatasajiliwa tena timu hiyo, akisema anawatakia maisha mema popote waendako.
HABARI HII KWA HISANI YA BLOGU YA MAMA PIPIRO

Simba, Yanga zaingiza mil 269/-


Watazamaji 41,733 walikata tiketi kushuhudia mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga iliyochezwa jana (Mei 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya
rangi ya chungwa, sh. 20,000 VIP C, sh. 30,000 VIP B na sh. 40,000 VIP A. Watazamaji 36,980
walinunua tiketi za sh. 5,000 wakati 203 walikata za sh. 40,000.
Mechi hiyo ambayo ni moja kati ya saba zilizochezwa siku hiyo kufunga msimu wa 2011/2012 iliingiza
sh. 260,910,000. Kila klabu ilipata sh. 62,646,395.85. Asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
ni sh. 39,799,830.51 wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilipata sh. 19,908,361.95.
Gharama za mechi kabla ya mgawo ni nauli ya ndani ya waamuzi na kamishna sh. 20,000, posho ya
kujikimu kwa kamishna sh. 40,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, gharama za tiketi sh. 8,539,950,
maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, ulinzi na usafi wa uwanja
sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Mgawo wa uwanja ni sh. 19,908,361.95, gharama za mechi sh. 19,908,361.95, Mfuko wa Maendeleo
ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 9,954,180.97, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 1,990,836.19 na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 10,467,324.78.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Maandalizi tuzo za TASWA yaanza


CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeanza mchakato wa Tuzo kwa
Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011.
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba kama
ilivyokuwa mwaka uliopita Kamati ya Utendaji ya TASWA imeamua suala la mchakato wa kuwapata
wanamichezo hao lifanywe na kamati maalum nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA lengo ikiwa ni
kupanua wigo na kuwashirikisha wadau wengi zaidi katika jambo hili nyeti.Kutokana na hali hiyo Kamati
ya Utendaji ya TASWA imeshateua kamati maalum ya kusimamia tuzo hiyo, ambapo kamati hiyo
ambayo tayari imeshaanza vikao vyake jijini Dar es Salaam ipo chini ya Mhariri Mkuu wa gazeti la Spoti
Starehe, Masoud Sanani, ambaye pia aliiongoza kamati hiyo mwaka uliopita.Kamati hiyo ya Tuzo
ilikutana mara ya mwisho hivi karibuni kwa ajili ya kupanga namna ya kuendesha tuzo hizo kwa mwaka
huu ili iwe bora zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana.Pamoja na mambo mengine kamati ilikubaliana vyama
vya michezo vishirikishwe kwa kuviandikia barua ili vitume majina ya wanamichezo wao waliofanya
vizuri kwa mwaka 2011.Kutokana na hali hiyo kila chama cha michezo kitawasilisha  kwa kamati majina
matatu ya wanamichezo wake waliofanya vizuri mwaka jana kwa wanaume matatu na wanawake
matatu, ambao mmojawao atakuwa ndiye mshindi wa mchezo husika kwa mwaka jana.Pia kila mshindi
miongoni mwa wanamichezo hao atashiriki kuwania tuzo ya Mwanamichezo wa Bora wa Mwaka 2011.
Tarehe na mahali ambapo tuzo itafanyika itatangazwa wiki hii baada ya kumalizika vikao muhimu,
ambapo pia mdhamini wa tuzo atatajwa, ingawa TASWA inafungua mlango kwa kampuni zaidi
zijitokeze kudhamini kwa vile tuzo ya mwaka huu itakuwa ya aina yake.Kwa hiyo wafuatao ndio
wanaunda Kamati ya TASWA ya Kusimamia Upatikanaji wa Wanamichezo Bora wa Tanzania kwa
mwaka 2011, wengi wakiwa ni wale waliokuwepo mwaka uliopita..Mwenyekiti wa Kamati atakuwa
Sanan, ambaye ni Mhariri wa gazeti la Spotistarehe, Katibu wa kamati atakuwa Amir Mhando ambaye
ni Katibu Mkuu wa TASWA,  Mshauri wa Kamati atakuwa Juliana Yassoda ambaye ni Naibu Mkurugenzi
wa Idara ya Maendeleo ya Michezo. Pia Kamati itaomba Ofisa mmoja wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT) naye kuwa mshauri wa kamati.
Orodha kamili ya wajumbe ni
1.Amour Hassan-Mhariri Nipashe
2. Rashid Zahoro-Mhariri gazeti la Burudani
3. Alex Luambano-Clouds FM
4. Tulo Chambo-Mhariri Tanzania Daima
5. Mbonile Burton-HabariLeo
6. Chacha Maginga-TBC1
7.Frank Sanga-Mhariri Mwanaspoti
8. Michael Maurus-Super Star
9. James Range-Star TV
10.Editha Mayemba-Radio Tumaini
11. Said Kilumanga-Chanel Ten/Magic Radio
12.Rehule Nyaulawa-Mkurugenzi Times FM
13. Angel Akilimali-Meneja Vipindi Radio Uhuru
14. Masoud Sanan-Mhariri Spotistarehe
15. Amir Mhando-Katibu Mkuu TASWA
16. George John –Katibu Msiadizi TASWA
17.Patrick Nyembela-EATV
18: Juliana Yassoda-Naibu Mkurugenzi Idara ya Michezo
19. Luqman Maloto-Championi
20. Deo Rweyunga-Radio One
21. Andrew Kingamkono-Mhariri Mwananchi
22. Dominick Isiji-The African
23. Ofisa kutoka BMT
HABARI HII KWA HISANI YA BLOGU YA BIN ZUBEIRY NA MAMA PIPIRO

TUNAKUKUMBUKA



SLEYUM MOHAMED ZAHOR (1922-2003)

HATIMAYE leo umetimiza miaka tisa tangu ulipofariki dunia mwaka 2003 baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa katika makaburi ya Kigilagila, Kiwalani, Dar es Salaam.
Kifo chako kimetuachia pengo na upweke mkubwa. Tunazikosa simulizi zako, maono yako, ucheshi wako, busara zako na hekima zako.
Unakumbukwa sana na mke, Bibi Fatuma Rashid na watoto wako, Rashid, Pili, Amisa, Shani, Asha, Saumu, Nuru na Hilali pamoja na wajukuu zako wote.
Hakika sisi zote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake lazima tutarejea. Tunaamini maandiko ya kwamba kila chenye roho, lazima kitaonja mauti.
Mungu ailaze roho yako mahali pema, peponi. Amin

Sunday, May 6, 2012

SIMBA NOMA!


L YAIBUGIZA YANGA 5-0
L OKWI AMWAIBISGA NCHUNGA

Simba leo ilisherehekea ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa staili ya aina yake baada ya kuibugiza Yanga mabao 5-0 katika moja ya mechi za mwisho za ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba ndiye  aliyeibuka shujaa wa Msimbazi baada ya kufunga bao moja na kusababisha mabao mengine matatu.
Okwi alifunga bao la kwanza baada za mapema baada ya kuingia na mpira ndani ya 18 na kupiga shuti lililompima vyema kipa Yaw Berko na mpira kutinga wavuni.
Goli la pili la Simba likafungwa na mchezaji Felix Sunzu kwa njia ya penati na dakika chache baadae Emmanuel Okwi akaongeza goli la tatu. Juma Kaseja akaongeza goli la nne kwa penati wakati pia Patrick Mafisango akafunga hesabu kwa kufunga  goli la tano baada ya wachezaji wa Yanga kufanya makosa katika eneo la hatari
Waziri wa Habazri, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mkangara alimkabidhi kombe nahodha wa timu ya Simba Juma K. Juma baada ya timu ya Simba kuifunga Yanga magoli 5-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar salaam katika mchezo uliokuwa wa  kumaliza michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom uliomalizika jioni hii  kwenye uwanja wa Taifa, huku ikiwa tayari ni mabingwa wapya wa ligi hiyo.


Thursday, May 3, 2012

Simba, Yanga sasa kucheza J'pili, Azam kurudiana na Mtibwa leo


UNAWEZA kuiita vita. Na hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati Simba na Azam zitakaposhuka dimbani kwenye viwanja viwili tofauti kumenyana na Yanga na Kagera Sugar katika mechi za mwisho za ligi kuu ya Tanzania.
Awali, mechi hizo ilikuwa zichezwe kesho, lakini kufuatia uamuzi wa kamati ya nidhamu na usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mechi hizo sasa zitachezwa Jumapili badala ya Jumamosi.
Kamati hiyo, inayoongozwa na Kamanda Mstaafu wa Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, ilifikia uamuzi huo kufuatia rufani iliyokatwa na African Lyon.
Katika rufani hiyo, Lyon ilipinga uamuzi wa kamati ya ligi ya TFF kuipa Azam ushindi wa pointi tatu na mabao mawili katika mechi yake dhidi ya Mtibwa Sugar, badala yake ilitaka Mtibwa Sugar ishushwe daraja kwa kususia mechi hiyo.
Pambano kati ya Mtibwa na Azam lilivunjika dakika ya 89 baada ya wachezaji wa Mtibwa Sugar kugomea penalti iliyotolewa kwa Azam na mwamuzi Rashid Msangi kwa madai kuwa, haikuwa halali. Hadi pambano hilo lilipovunjika, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.
Kufuatia Mtibwa kugomea penalti hiyo, kamati ya ligi iliamua kuipa Azam ushindi wa pointi tatu na mabao mawili, lakini ilimfungia mwamuzi Msangi kwa madai kuwa, ripoti yake haikueleza iwapo alivunja pambano hilo baada ya kusubiri kwa dakika 15.
Katika uamuzi wake, kamati ya rufani imesema, kamati ya ligi haikuwa sahihi kuiadhibu Mtibwa kwa sababu si kweli kwamba waligomea pambano hilo, bali wachezaji wake walikuwa ndani ya uwanja hadi mwamuzi alipoamua kulivunja.
Kutokana na uamuzi huo wa kamati ya nidhamu, pambano la Mtibwa na Azam sasa litarudiwa leo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na mechi za mwisho za ligi sasa zitachezwa Jumapili.
Katika mechi hizo, Simba itavaana na watani wao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Azam itamenyana na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi.
Mechi hizo mbili zinatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka kwa kuwa ndizo zitakazotoa bingwa wa ligi hiyo msimu huu baada ya mchuano mkali uliodumu kwa miezi kadhaa.
Simba na Azam ndizo pekee zenye nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, kutokana na kutofautiana kwa pointi tatu. Lakini Simba ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi kwa vile inahitaji sare tu kwa Yanga.
Hadi sasa, Simba inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25 wakati Azam ni ya pili kwa kuwa na pointi 56. Timu hizo mbili zinatofautiana kwa mabao mawili ya kufunga huku kila moja ikiwa imefungwa mabao 12.
Iwapo Simba itaifunga Yanga ama kutoka nayo sare ya aina yoyote, itatawazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu. Lakini iwapo Simba itafungwa na Yanga na wakati huo huo Azam kuishinda Kagera Sugar kwa zaidi ya mabao matatu, ubingwa huenda ukatua kwa wanalambalamba.
Habari zaidi zimeeleza kuwa, viongozi wa Simba na Azam wamekuwa wakihaha huku na kule kwa ajili ya kuweka mambo sawa ili kushinda mechi zao za keshokutwa.
Kuna habari kuwa, viongozi wa Azam wamekuwa wakiwasiliana na wachezaji wa Yanga ili kuwashawishi wacheze kufa na kupona na kuibuka na pambano lao dhidi ya Simba.
Mbali na mkakati huo, kuna habari pia Azam imeshajitengenezea mazingira mazuri kwa Kagera Sugar ili iweze kupata ushindi mnono wa mabao.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa, Azam imeigharamia Kagera Sugar gharama za malazi na chakula kwenye hoteli moja iliyopo Manzese, Dar es Salaam na pia imewalipa posho wachezaji wake.
Baada ya kushtukia dili hiyo, uongozi wa Simba umeamua kuwachimbia mkwara wachezaji wao na kuwaonya kuwa, yeyote atakayeihujumu katika mechi dhidi ya Yanga, atashughulikiwa.

Swahiba wa Kanumba aacha uigizaji filamu


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Ramsey Nouah amesema anatarajia kuacha uigizaji hivi karibuni baada ya kuwepo kwenye tasnia hiyo kwa miaka kadhaa.
Ramsey, ambaye ni swahiba mkubwa wa aliyekuwa mwigizaji nyota wa Tanzania, marehemu Steven Kanumba alisema wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kuona inatosha.
Nyota huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, ameona ni bora kuachia ngazi akiwa bado kwenye kiwango cha juu badala ya kusubiri fani hiyo imtupe mkono.
“Kwa mashabiki wangi na wengine, naelewa siku zote wanataka kuniona kwenye luninga, lakini kama waswahili wanavyosema, ni bora kuondoka wakati bado upo juu,”alisema.
Ramsey alisema anaamini ameacha kumbukumbu kubwa katika uigizaji na kuongeza kuwa ni vigumu kuzungumzia Nollywood bila kutaja jina lake.
Alisema kwa kipindi kirefu sasa hajacheza filamu yoyote kwa sababu hataki kuonekana kwenye luninga. Alisema anachotaka ni kucheza filamu za kiwango cha juu na zitakazoiweka fani hiyo nchini Nigeria kwenye hatua za juu zaidi.
Alisema baada ya kustaafu kazi hiyo, anatarajia kuwa mwongozaji wa filamu. Alisema asingependa kuwaona watoto wake wakijihusisha na fani hiyo, lakini hawezi kuwalazimisha.

Zawadi Kombe la Ester zaongezwa


MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) mkoa wa Mara, Ester Bulaya ameamua kuongeza zawadi kwa ajili ya washindi watatu wa kwanza wa mashindano ya Kombe la Ester.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Ester alisema bingwa wa kwanza mwaka huu atazawadiwa kitita cha sh. 500,000 na kikombe.
Ester alisema mshindi wa pili atapata sh. 250,000 na kikombe, mshindi wa tatu atapata sh. 150,000, mfungaji bora na mchezaji bora watapata sh. 50,000 kila mmoja wakati timu yenye nidhamu itapata sh. 100,000.
Kwa mujibu wa Ester, mashindano hayo yalizinduliwa rasmi juzi na yatafanyika katika jimbo la Bunda mkoani Mara. Hii ni mara ya pili kwa Ester kuandaa mashindano hayo.
Mashindano hayo yalianzishwa mwaka jana, yakizishirikisha timu 15 za soka kutoka katika kata zote za Jimbo la Bunda. Bingwa wa mwaka jana ilikuwa timu ya Bunda Store.
Ester alisema kutokana na hamasa ya mashindano hayo, idadi ya timu mwaka huu imeongezeka. Alisema mashindano ya mwaka huu yatazishirikisha timu 21 za jimbo hilo.
Mbunge huyo alisema mashindano ya mwaka huu yatagharimu sh. milioni 6.5, zikiwemo fedha za zawadi, vifaa vya michezo na matumizi ya uendeshaji wa ligi hiyo kama vile malipo ya waamuzi, huduma ya kwanza na viwanja. Alisema kila timu itapatiwa seti moja ya jezi na mpira.
Wakati huo huo, Ester amesema ataendelea na utaratibu wake wa kugawa vifaa vya michezo kwa kila kata za mkoa wa Mara kwa lengo la kuendeleza michezo.
Ester alisema jana kuwa, safari hii atatoa vifaa hivyo katika wilaya za Musoma Mjini yenye kata 13. Alisema kila kata itapata seti ya jezi na mipira miwili, ambavyo thamani yake ni sh. milioni 4.2.
"Kama, ambavyo nilieleza mwaka jana wakati nazindua mashindano ya Ester Cup, pamoja na mradi wa kugawa vifaa vya michezo, lengo kuu ni kukuza vipaji vya vijana kwenye Jimbo la Bunda na mkoa mzima wa Mara,"alisema.
"Tunatambua kuwa michezo ni ajira, afya, vilevile inakuza umoja naushirikiano, kwa hiyo nataka kuhakikisha naliweka hai soko la ajirakwa vijana, kupitia michezo, kadhalika kudumisha ushirikiano na afya zao," aliongeza.

Hakimu Simba na Yanga huyu hapa


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limempanga mwamuzi Hashim Abdalla wa Dar es Salaam kuchezesha pambano la marudiano la ligi kuu ya Bara kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga.
Hashim ni mwamuzi wa daraja la kwanza na ni mara yake ya kwanza kuchezesha mechi kati ya timu hizo kongwe nchini, ambayo kwa kawaida huvuta hisia za mashabiki wengi.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Hashim atasaidiwa na Iddi Maganga na Omary Kambangwa. Mwamuzi wa akiba atakuwa Hamisi Chang’walu wote wa Dar es Salaam.
Pambano kati ya Simba na Yanga linatarajiwa kupigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi ya awali iliyochezwa mwishoni mwa mwaka jana kwenye uwanja huo, Yanga iliichapa Simba bao 1-0.
Wakati huo huo, klabu ya Simba imeamua kuwapatia wachezaji wake sh. milioni 35 kutokana na kuichapa Al-Ahly Shandy ya Sudan katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirisho.

Ngorongoro watua Sudan salama

Ngorongoro Heroes imewasili salama hapa Khartoum jana saa 4 usiku kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa Jumamosi kuanzia saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ni wa nyasi bandia, na hakutakuwa na kiingilio kwa watazamaji.

Awali Ngorongoro Heroes ilitarajiwa kuwasili saa 2.10 usiku, lakini ndege iliyokuwa ipande Nairobi kuja hapa ilichelewa kuondoka kwa saa moja na nusu kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Mara baada ya kuwasili Taka Hotel ambapo imefikia, Ngorongoro Heroes ilifanya mazoezi ya saa moja kuanzia saa 4.30 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi dhidi ya Sudan. Ngorongoro Heroes ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hoteli ya Taka ndipo pia timu ya El Merreikh ya hapa Sudan imeweka kambi yake kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). El Merreikh ililala mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Lubumbashi.
Kwa mujibu wa kocha Kim Poulsen, wachezaji wote wako katika hali nzuri na kikosi kitakachoanza kwenye mechi hiyo kitajulikana kesho (Ijumaa) baada ya mazoezi ya mwisho yatakayofanyika saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum.
Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Aishi Manula, Ramadhan Singano, Hassan Dilunga, Frank Damayo, Frank Sekule, Issa Rashid, Hassan Ramadhan, Saleh Malande, Said Zege, Emily Mugeta, Jerome Lambele, Samir Ruhava, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Atupele Green, Dizana Yarouk, Jamal Mroki na nahodha Omega Seme.
Mwamuzi Aden Abdi Djamal wa Djibouti ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Djamal atasaidiwa na Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah. Waamuzi hao watawasili kesho (Ijumaa) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakati Kamishna wa mechi hiyo Patrick Naggi kutoka Kenya atawasili leo (Alhamisi) saa 2.10 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza mechi ya raundi ya pili dhidi ya Nigeria. Mechi ya kwanza itchezwa Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa kati ya Agosti 10 na 12 mwaka huu.
Ikifanikiwa kuitoa Nigeria, Ngorongoro Heroes itacheza mechi ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Afrika Kusini na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya Septemba 21 na 23 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.
Boniface Wambura,
Khartoum, Sudan
Mei 3, 2012

TIMU ZA MAJESHI ZAONGEZEKA LIGI KUU


MICHUANO ya soka ya fainali za ligi daraja la kwanza Tanzania Bara, ilimalizika hivi karibuni mjini Tanga kwa timu tatu za kwanza kupata tiketi ya kucheza ligi kuu msimu ujao.
Polisi Morogoro ilimaliza ligi hiyo ikiwa ya kwanza baada ya kupata pointi 20, ikifuatiwa na Mgambo Shooting ya Tanga iliyopata pointi 15 na Prisons ya Mbeya iliyopata pointi 14.
Timu zingine zilizoshiriki katika ligi hiyo, pointi zao kwenye mabano ni Polisi Dar es Salaam (13), Mbeya City Council (11), Rhino Rangers ya Tabora (8), Mlale JKT ya Ruvuma (8), Polisi Tabora (6) na Transit Camp ya Dar es Salaam (2).
Timu hizo tatu zitachukuwa nafasi ya Polisi Dodoma na Moro United, ambazo tayari zimeshashuka daraja kutoka ligi kuu baada ya kushika nafasi mbili za mwisho. Timu ya tatu itajulikana baada ya mechi za mwisho za ligi hiyo, inayotarajiwa kumalizika keshokutwa.
Kwa mujibu wa msimamo wa ligi kuu, timu zilizopo hatarini kuungana na Moro United na Polisi Dodoma kushuka daraja ni Villa Squad, African Lyon na Toto African.
Villa Squad inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani, ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 24 wakati juu yake zipo African Lyon yenye pointi 24 na Toto African yenye pointi 26.
Katika mechi za mwisho, Toto African itacheza na Coastal Union mjini Tanga, African Lyon na JKT Ruvu, Villa Squad na Ruvu Shooting.
Kupanda daraja kwa timu za Polisi Moro, Mgambo Shooting na Prisons kumeongeza idadi ya timu zinazomilikiwa na majeshi ya ulinzi na usalama katika ligi hiyo.
Katika msimu huu wa ligi, idadi ya timu za majeshi zilikuwa nne, lakini baada ya kupanda kwa timu hizo tatu, idadi hiyo itaongezeka na kuwa sita.
Timu za majeshi, ambazo tayari zipo ligi kuu na zimeshajihakikishia kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao ni JKT Oljoro, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambazo zinamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Prisons, inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, siyo timu ngeni katika ligi hiyo. Iliwahi kushiriki kwa kipindi kirefu miaka ya nyuma kabla ya kushuka daraja misimu mitatu iliyopita.
Timu hiyo imewahi kutoa nyota wengi waliowahi kuzichezea Simba na Yanga na hata kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars. Baadhi ya nyota hao ni kipa Ivo Mapunda, aliyewahi kuichezea Yanga na ambaye kwa sasa anacheza soka ya kulipwa katika klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
Nyota wengine waliotokea Prisons ni Primus Kasonzo, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Yona Ndabila na Henry Morris, ambao wamewahi kutamba kwa nyakati tofauti katika timu hizo kongwe.
Nsajigwa na Mwasika bado wamo kwenye kikosi cha Yanga. Lakini kuna habari kuwa, Nsajigwa huenda akastaafu kucheza soka baada ya msimu huu kumalizika.
Polisi Moro imewahi kucheza ligi kuu kwa miaka kadhaa kabla ya kuvurunda misimu miwili iliyopita na kushuka daraja. Timu hiyo yenye maskani yake mjini Morogoro imerejea tena kwenye ligi kuu, ikichukua nafasi ya maafande wenzao wa Polisi Dodoma.
Kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, upo uwezekano mkubwa kwa wachezaji walikuwemo kwenye kikosi cha Polisi Dodoma kuhamishiwa Polisi Moro kwa ajili ya kuiongezea nguvu.
Mgambo Shooting ni timu nyingine inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa na ni mara yake ya kwanza kufuzu kucheza ligi kuu. Uwepo wake kwenye ligi hiyo kumeongeza idadi ya timu za jeshi hilo kwenye ligi kuu kuwa nne msimu ujao.
Timu pekee za uraiani, ambazo zitaendelea kuwepo kwenye ligi hiyo msimu ujao ni Simba, Yanga, Coastal Union na Toto African wakati majaliwa ya Villa Squad na African Lyon bado hayajajulikana. Timu
zinazomilikiwa na kampuni ni Azam, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.
Hata katika mechi za fainali ya ligi daraja la kwanza, idadi kubwa ya timu zilizoshiriki na kubaki kwenye ligi hiyo zilikuwa za majeshi. Timu hizo ni Polisi Dar es Salaam, Rhino Rangers ya Tabora na Transit Camp ya Dar es Salaam, zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), JKT Mlale ya Ruvuma na Polisi Tabora.
Iwapo vyama vya soka vya mikoa havitafanya jitihada za makusudi za kufufua timu za mitaani kama vile Milambo, Majimaji, AFC, Lipuli, Katavi Rangers, African Sports upo uwezekano mkubwa katika miaka michache ijayo, ligi hiyo kutawaliwa zaidi na timu za majeshi.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba uwepo wa timu nyingi za majeshi katika ligi kuu umetokana na huduma nzuri zinazopata muda wote wa mashindano. Pia timu hizo za majeshi zimekuwa zikitoa ajira kwa vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka na hivyo kuachana na maisha ya mitaani.
Timu zilizokuwa zikitamba miaka ya nyuma, zilizokuwa zikimilikiwa na bodi za mazao, mashirika na kampuni kama vile Pamba, RTC, Ushirika, CDA, Reli, Waziri Mkuu, Pilsner, Ndovu sasa hazipo tena na uwezekano wa kuzifufua haupo.
Ni vyema viongozi wa vyama vya soka vya mikoa wafanye jitihada za kuzifufua baadhi ya timu hizo ili kuongeza ushindani zaidi wa kisoka kwa timu za mikoa. Hii pia itasaidia kuibua vipaji vingi vya vijana na kuwaendeleza kisoka ili hatimaye waje kuwa hazina kubwa ya taifa katika miaka ijayo.

Okwi, Niyonzima watikisa ligi kuu


LIGI kuu ya soka ya Tanzania Bara inatarajiwa kufikia ukingoni Jumamosi wiki hii huku kitendawili cha timu ipi itakayotwaa ubingwa kikiwa bado hakijateguliwa.
Kwa mujibu wa ratiba, timu zote 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo msimu huu, zinatarajiwa kushuka dimbani siku hiyo huku mechi kati ya Simba na Yanga na ile kati ya Azam na Kagera Sugar zikitarajiwa kutoa bingwa.
Hadi sasa, Simba inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 56 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi. Yanga inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 49.
Kimahesabu, Simba inahitaji sare katika pambano kati yake na Yanga ili iweze kuwa bingwa kwa vile itafikisha pointi 60, ambazo Azam haitaweza kuzifikia. Azam ina uwezo wa kufikisha pointi 59.
Lakini iwapo Simba itafungwa na Yanga na Azam kuibuka na ushindi katika mechi kati yake na Kagera Sugar, kwa mara ya kwanza huenda taji hilo likaenda kwa Wanarambaramba, lakini kwa kutegemea uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa.
Simba hadi sasa imefunga mabao 42 na kufungwa mabao 12 wakati Azam imefunga mabao 40 na kufungwa mabao 12.
Wakati ligi hiyo ikiwa inaelekea ukingoni, tayari timu za Polisi Dodoma na Moro United zimeshateremka daraja baada ya kushika nafasi mbili za mwisho. Timu ya tatu huenda ikawa Villa Squad, African Lyon na Toto African.
Katika ligi ya msimu huu, timu saba kati ya 14 ziliweka maskani yake mjini Dar es Salaam na kucheza mechi zake kwenye Uwanja wa Taifa na Chamazi. Timu hizo ni Simba, Yanga, Azam, African Lyon, Moro United, Villa Squad, JKT Ruvu na Ruvu Shooting. Timu zilizoshiriki kutoka mikoani ni Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Toto African, Polisi Dodoma, JKT Oljoro na Coastal Union.
Timu za Simba, Yanga na Azam, ambazo zinafundishwa na makocha wa kigeni, ndizo pekee zilizofanya vizuri na kushika nafasi tatu za kwanza. Simba inanolewa na Milovan Cirkovic kutoka Serbia kama ilivyo kwa Yanga, inayonolewa na Kostadin Papic. Azam inanolewa na Stewart Hall kutoka Uingereza.
Kadhalika, timu zilizokuwa na wachezaji wengi wa kigeni ndizo zilizofanya vizuri katika ligi hiyo msimu huu. Simba iliwatumia Emmanuel Okwi kutoka Uganda, Felix Sunzu kutoka Zambia na Gervas Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wachezaji wa kigeni walioichezea Yanga msimu huu ni kipa Yaw Berko na Kenneth Asamoah kutoka Ghana, Davis Mwape kutoka Zambia, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Hamisi Kiiza kutoka Uganda.
Wageni wengine waliocheza ligi ya msimu huu ni Gideon Ssekamwa kutoka Uganda, Chika Chimaobi Chukwu na Enyinna Darlinton Ariwood walioichezea Toto African na Mosse William Musoke,
Michael Katende na Hannington Kalyeswebula walioichezea Kagera Sugar.
Wengine ni Ibrahim Shikanda kutoka Uganda, Tchetche Hermann na Brice Kipre kutoka Ivory Coast, Awudu Nafiu na Wahab Yahya kutoka Ghana na kipa Obren Curkovic kutoka Serbia walioichezea Azam. Lyon ilimsajili Hood Mayanja kutoka Uganda.
Nyota wengine wa kigeni waliokuja kusakata kabumbu katika ligi hiyo ni Abubakar Shamshudin Hussein, Ben Mwalala na Edwin Mukenya kutoka Kenya, Samuel Tonnyson Temi na Felix Amechi Stanley kutoka Nigeria, ambao waliichezea Coastal Union.
Pamoja na kuwepo kwa wanasoka wengi wa kigeni, ni wachache walioweza kuziletea mafanikio timu zao. Hao ni Okwi, Sunzu na Mafisango wa Simba, Niyonzima na Kiiza wa Yanga na Kipre Tcheche wa Azam.
Okwi, Mafisango na Sunzu walikuwa na mchango mkubwa kwa Simba katika mechi za ligi na michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo waliifungia mabao mengi muhimu.
Ushirikiano wa nyota hao watatu pamoja na wanasoka wazalendo kama vile Haruna Moshi, Mwinyi Kazimoto, Uhuru Selemani na Machaku Salum, umeifanya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iwe tishio na kuzifunga timu ngumu za Kiyovu ya Rwanda, ES Setif ya Algeria na Al-Ahly Shandy ya Sudan katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kadhalika Niyonzima na Kiiza wamekuwa na msaada mkubwa kwa Yanga kutokana na kuonyesha soka ya kiwango cha juu. Niyonzima ni muunganishaji mzuri wa mipira wakati Kiiza ameifungia Yanga mabao kadhaa muhimu.
Lakini baadhi ya wachezaji wa kigeni kama vile Kago wa Simba, Asamoah na Mwape wa Yanga, ambao walisajiliwa kwa pesa nyingi na klabu hizo, walionekana kuwa mzigo na upo uwezekano mkubwa wa kutemwa msimu ujao.
Asamoah na Mwape wamekuwa wakilalamikiwa kwa muda mrefu na mashabiki wa Yanga kwa kushindwa kuifungia mabao katika mechi muhimu, likiwepo pambano lao la awali la michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri. Yanga ilitolewa kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Kipa Berko wa Yanga naye ameshindwa kuonyesha cheche zake, hasa katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Nyota wa kigeni waliosajiliwa na Toto African, Kagera Sugar na Coastal Union nao wameshindwa kuonyesha cheche zao, badala yake walionekana mzigo mkubwa kwa klabu hizo.
Kipa Curkovic wa Azam pamoja na beki Nafiu na mshambuliaji Wahab wa Azam nao walishindwa kudhihirisha makali yao. Wachezaji hao watatu walitemwa baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Beki wa zamani wa Yanga na Simba, Mukenya aliamua kuitosa Coastal Union kabla ya ligi kumalizika, lakini Mwalala na Mnigeria, Felix walikuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo na kuinusuru kushuka daraja.

Milovan, Stewart wawafunika makocha wazalendo



SAFARI ndefu ya kusaka ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2012/2013, inatarajiwa kufikia tamati keshokutwa huku timu za Simba na Azam zikiwa na nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo.
Katika mechi za mwisho zitakazochezwa keshokutwa, Simba itamenyana na watani wao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa wakati Azam itavaana na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Simba na Azam zitashuka dimbani zikiwa zimetofautiana kwa pointi tatu. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 59 wakati Azam ni ya pili kwa kuwa na pointi 56.
Iwapo Simba itaifunga Yanga ama kutoka nayo sare, itatwaa taji hilo, lakini iwapo itateleza kwa kufungwa na wakati huo huo Azam kuifunga Kagera Sugar, taji hilo linaweza kubaki Chamazi.
Itakachotakiwa kufanya Azam ni kuifunga Kagera Sugara mabao zaidi ya mawili kwa vile timu hiyo inatofautiana na Simba kwa mabao mawili ya kufunga. Simba imefunga mabao 42 wakati Azam imefunga mabao 40. Kila moja imefungwa mabao 12.
Wakati ligi inatarajiwa kufikia tamati keshokutwa, baadhi ya makocha wa kigeni wameonekana kuzipa mafanikio timu zao huku makocha wazalendo wakishindwa kuonyesha makali yao.
MILOVAN CIRKOVIC
Ni kocha aliyeipa Simba mafanikio makubwa, si tu katika ligi, bali hata michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo timu hiyo imefuzu kucheza hatua ya 16 bora.
Kocha huyo kutoka Serbia pia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibadili Simba kimchezo, ambapo sasa inacheza soka ya kuvutia zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa ikicheza katika mzunguko wa kwanza.
Awali, wachezaji wa Simba walikuwa wakichoka haraka hasa katika kipindi cha pili. Haikuwa na uwezo wa kucheza kwa kasi katika dakika zote 90. Lakini hivi sasa, kadri dakika zinavyosonga mbele, kasi ya Simba imekuwa ikizidi kuongezeka.
Cirkovic pia aliiongoza vyema Simba kuzitoa Kiyovu ya Rwanda katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho kabla ya kuitupa nje ES Setif ya Algeria katika raundi ya pili.
Kocha huyo pia ameiweka Simba kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kuiongoza vyema kuichapa Al-Ahly Shandy ya Sudan mabao 3-0 katika mechi ya awali ya raundi ya tatu iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana wiki mbili zijazo nchini Sudan.
Iwapo Simba itatwaa ubingwa wa ligi kuu, ni wazi kuwa Cirkovic naye atatwaa tuzo ya kocha bora kwa kuiwezesha timu hiyo kuibuka mabingwa.
Mafanikio mengine ya Simba katika ligi hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na umahiri wa kipa Juma Kaseja, ambaye ameweka rekodi ya kucheza mechi zote na kufungwa mabao 12.
STEWART HALL
Ni kocha mwingine wa kigeni, aliyeleta changamoto kubwa katika ligi hiyo msimu huu na kutoa ushindani mkali kwa timu kongwe za Simba na Yanga.
Azam ndiyo timu pekee iliyoweka rekodi ya kuzishinda Simba na Yanga katika ligi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutwaa kombe la Mapinduzi katika michuano iliyofanyika Zanzibar mapema mwaka huu.
Kocha huyo ndiye aliyeziweka Simba na Yanga roho juu katika mbio za kuwania ubingwa na nafasi ya pili kwa kuzitenganisha timu hizo kongwe kutoka nafasi ya kwanza na ya tatu.
Azam sasa ina uhakika mkubwa wa kushika nafasi ya pili na hata kutwaa ubingwa iwapo Simba itateleza na hivyo kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Mafanikio ya Azam katika ligi hiyo msimu huu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kusajiliwa kwa nyota kadhaa wa kigeni kutoka Ivory Coast, akiwemo mshambuliaji machachari Kipre Tchetche.
Azam ni miongoni mwa timu zinazoundwa na wachezaji wengi wazuri na kwa sasa hakuna shabiki anayeweza kushangaa iwapo timu hiyo itazifunga Simba au Yanga kwenye ligi ama michuano mingine yoyote.
Mabao 16 aliyofunga Boko ni heshima kubwa kwa Azam na kocha wake, Hall na bila shaka tuzo ya mfungaji bora itatua tena kwa mshambuliaji huyo mrefu na tegemeo kubwa la Taifa Stars.
Azam ni timu pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na kituo cha michezo chenye ubora wa hali ya juu cha Chamazi huku uwekezaji wake ukiendelea kufanyika kwa awamu na inategemewa na wengi kutikisa kwenye soka la Afrika kama ilivyo kwa TP Mazembe.
Tayari bodi ya wakurugenzi ya Azam FC imeweka wazi kuwa, dhamira ya kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kuondoa dhana kuwa watanzania hawawezi na stahili yao ni jina la ‘kichwa cha mwenda wazimu’.
Uongozi wa Azam umedhamiria kugeuza hali hii na kuifanya Tanzania iwe nchi ya kuogopwa na kuheshimika kwenye soka la Afrika. Lakini ili kufikia malengo hayo, inahitaji muda na pia kuungwa mkono na wadau.
KOSTADIN PAPIC
Ni kocha aliyerejeshwa Yanga kimizengwe baada ya kutimuliwa kocha wa zamani wa timu hiyo, Sam Timbe kutoka Uganda, ambaye aliiwezesha kutwaa taji la ligi kuu msimu uliopita na Kombe la Kagame.
Awali, Papic aliletwa Yanga kwa ajili ya kuziba pengo la Dusan Kondic msimu wa 2010/2011, lakini alilazimika kufungasha virago mapema baada ya kushindwa kuelewana na viongozi.
Kurejeshwa kwake Yanga kulisababisha mashabiki wa klabu hiyo wagawanyike, baadhi wakiunga mkono na wengine wakipinga kwa madai kuwa, hakuwa na jipya.
Hata hivyo, Papic ameshindwa kukidhi kiu ya mashabiki wa Yanga kutokana na kutoiletea mafanikio makubwa. Mbaya zaidi, kocha huyo kutoka Serbia amekuwa akitoa kauli za mara kwa mara za kuwashutumu viongozi kwa kushindwa kuihudumia timu vizuri.
Hivi karibuni kocha huyo alikaririwa na vyombo vya habari akilalamikia kutolipwa mishahara yake ya miezi miwili, lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na uongozi, ambao ulidai kuwa alishachukua malipo ya awali.
Pengine kilichotibua mipango ya Papic ni kitendo cha wachezaji watano wa Yanga kufungiwa kucheza mechi kadhaa kwa kosa la kumpa kipigo mwamuzi Israel Nkongo na pia kupokwa pointi ilizopata kwa kuifunga Coastal Union baada ya kumchezesha beki Nadir Haroub Cannavaro aliyekuwa na kadi nyekundu.
Tayari kocha huyo ameshamaliza mkataba wake wa kuinoa Yanga na upo uwezekano mkubwa kwa timu hiyo kuwa chini ya kocha mwingine msimu ujao.
TOM OLABA
Unaweza kumwita kocha kijana wa kigeni, aliyemudu kutoa upinzani mkali katika ligi kuu ya msimu huu licha ya kushindwa kutimiza malengo aliyokusudia ya kutwaa ubingwa.
Olaba ameweza kuhimili purukushani za ligi hiyo hadi timu yake kushika nafasi ya tatu. Lakini ni wazi kuwa, makali ya Mtibwa Sugar yameanza kupungua kwa kiasi kikubwa, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa, Mtibwa imeshinda mechi 10,
imetoka sare sita na kupoteza tisa. Imefunga mabao 32, imefungwa mabao 29 na imeambulia pointi 37.
Ni wazi kuwa, iwapo Olaba anataka kuwa na kikosi imara, anapaswa kusajili wachezaji wazuri zaidi msimu ujao, hasa vijana kwa vile wachezaji wengi waliopo sasa wameanza kuzeeka.
JAMHURI KIHWELU ‘JULIO’
Ni kocha aliyekabidhiwa jukumu la kuifundisha Coastal Union baada ya kuondoka kwa Hafidh Badru, ambaye alishindwa kuhimili mikiki mikiki ya ligi kuu.
Julio alileta mageuzi makubwa ndani ya Coastal Union kiasi kwamba timu hiyo ilianza kucheza kwa kujiamini na hatimaye kujinasua katika janga la kuteremka daraja.
Licha ya kuikimbia timu hiyo na kutimkia Arabuni baada ya raundi ya kwanza kumalizika, Julio alirejea nchini na kufufua tena matumaini ya timu hiyo kubaki ligi kuu baada ya kuiwezesha kufanya vizuri katika mechi kadhaa za mzunguko wa pili.
Hadi sasa, Coastal Union inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 25. Imeshinda mechi 11, imetoka sare mechi tatu na kupoteza 11. Imefunga mabao 28 na kufungwa 29.
SALUM MAYANGA
Alianza kuinoa Kagera Sugar msimu huu akitokea Mtibwa Sugar. Ni kocha aliyerithi mikoba ya George Ssemogerere kutoka Uganda, ambaye aliamua kufungasha virago msimu uliopita.
Kocha huyo ameonyesha uwezo mzuri wa kuiongoza timu hiyo na huenda akapewa tena jukumu hilo msimu ujao. Lakini changamoto kubwa inayomkabili ni kusajili wachezaji wengine wapya.
Kagera Sugar ya sasa siyo ile iliyokuwa ikitamba miaka ya nyuma na kutoa upinzani mkali kwa vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga. Makali ya Kagera Sugar yamepungua.
Licha ya kuilazimisha Simba kutoka nayo sare katika mzunguko wa pili na kuichapa Yanga bao 1-0 mjini Bukoba, bado Kagera Sugar inahitaji kusukwa upya ili kuongeza ushindani katika ligi.
Hadi sasa, Mayanga ameiwezesha Kagera Sugar kushika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 25.
CHARLES KILINDA
Msimu huu Kocha Charles Kilinda ameendelea kuihakikishia timu hiyo kubaki ligi kuu msimu ujao baada ya kuwa katika nafasi saba za juu.
Katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa, imeshinda mechi saba, imetoka sare 11 na kufungwa mechi saba ikiwa imeambulia pointi 32.
Hata hivyo, sifa na heshima ya JKT Ruvu imeporomoka katika msimu huu, kufuatia kubebeshwa mabao mengi katika mechi walizopoteza. Kabla ya mechi za keshokutwa, tayari JKT Ruvu imeshafungwa mabao 32 na kufunga mabao 27.
Ladha ya soka ya maafande hao waliocheza vyema msimu wa 2008/2009 chini ya Kilinda, msimu huu haikuonekana kabisa. Huenda tatizo la majeruhi linaweza kuwa kikwazo kwa kocha huyo, aliyewahi kucheza katika timu ya Yanga miaka ya nyuma.
Katika baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza, Kilinda alisema majeruhi waliharibu malengo yake na katika mzunguko wa pili walikuwa nyanya zaidi kwa kupoteza mechi nyingi.
Huenda mazoea ya kukaa miaka mingi na wachezaji bila ya kuwaondoa au kuongeza damu changa, imechangia kikosi hicho kuyumba katika ligi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Kilinda hajafanya vibaya sana kiasi cha kutajwa hafai, isipokuwa anatakiwa kufanya mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa nia ya kuleta nguvu mpya.
CHARLES BONIFACE MKWASA
Amefanya kazi nzuri ya kuinusuru Ruvu Shooting isishuke daraja, licha ya kukabiliwa na jukumu lingine la kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Hadi sasa Ruvu Shooting ipo kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa inashika nafasi ya nane. Inazo pointi 31 baada ya kucheza mechi 25 na haipo kwenye janga la kushuka daraja.
Katika mechi ilizocheza hadi sasa, Ruvu Shooting imeshinda mechi saba, imetoka sare 10 na kupoteza nane, imefunga mabao 22 na kufungwa mabao 21.
Mkwasa alikiri hivi karibuni kuwa, licha ya kutokuwa kwenye nafasi nzuri, kikosi chake kimekuwa kikicheza soka ya kuvutia na ndiyo sababu kimejihakikishia kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
ALI KIDI
Ni kocha aliyejijengea jina kubwa katika mechi za mzunguko wa kwanza baada ya timu yake kutwaa uongozi wa ligi mara kadhaa kabla ya kupokonywa usukani.
Kidi aliiongoza JKT Oljoro kushinda mechi nyingi za mzunguko huo na kuonekana tishio kwa vigogo, lakini makali hayo yalipungua mzunguko wa pili na timu hiyo kuanza kupoteza mechi nyingi.
Hadi sasa, JKT Oljoro inashika nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 24. Imeshinda mechi saba, imetoka sare nane na kupoteza tisa. Imefunga mabao 17 na kufungwa 24.
ATHUMANI BILALI
Ni kocha aliyerithi mikoba ya Choki Abeid, ambaye naye alirithi mikoba ya John Tegete.
Sifa kubwa aliyonayo Bilali hadi sasa ni kuiongoza Toto African kutoka sare na Simba katika mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa mjini Dar es Salaam kabla ya kuibamiza Yanga mabao 3-2 mjini Mwanza.
Mechi hizo mbili zilifufua matumaini ya Toto African kubaki ligi kuu msimu ujao, lakini kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata kutoka kwa Azam, kimeiweka tena kwenye janga la kushuka daraja.
Majaliwa ya Toto African sasa yatategemea matokeo ya mechi yake ya mwisho dhidi ya Coastal Union itakayochezwa mjini Tanga. Sare ya aina yoyote itainusuru timu hiyo kushuka daraja.
Hadi sasa, Toto African inashika nafasi ya 10, ikiwa na pointi 26 baada ya kucheza mechi 25. Imeshinda mechi tano, imetoka sare 11 na kupoteza tisa. Imefunga mabao 24 na kufungwa 30.
JUMANNE CHALE, HABIBU KONDO, HASSAN BANYAI, RASHID CHAMA
Chale ni kocha wa African Lyon, ambayo mwaka jana iliponea kushuka daraja baada ya kufanya vizuri katika mechi za mwisho. Lakini safari hii, Lyon ipo tena mtegoni na iwapo itavurunda mechi yake ya mwisho, huenda ikarejea tena ligi daraja la kwanza.
Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Habibu Kondo, ambaye ni miujiza pekee, inayoweza kuinusuru timu yake ya Villa Squad kuepuka kushuka daraja iwapo itafungwa ama kutoka sare katika mechi yake ya mwisho.
Mambo ni mabaya zaidi kwa Hassan Banyai wa Moro United na Rashid Chama wa Polisi Dodoma, ambao timu zao zimeshateremka daraja na mwakani zitacheza ligi daraja la kwanza.

Wachezaji Simba wapigwa mkwara


PG 3
UONGOZI wa klabu ya Simba umewaonya wachezaji wa timu hiyo kuepuka vishawishi vyovyote vinavyoweza kuwafanya wahujumu pambano lao dhidi ya Yanga kwa kucheza chini ya kiwango.
Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alipokuwa akizungumza na Burudani jana kuhusu maandalizi ya pambano hilo, litakalochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Rage alisema pambano hilo ni muhimu kwa Simba kushinda ili iweze kutawazwa kuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Alisema iwapo Simba itafungwa, upo uwezekano mkubwa kwa taji hilo kunyakuliwa na Azam, iwapo itashinda pambano lake dhidi ya Kagera Sugar kwa idadi kubwa ya mabao.
Mbali na kuwepo kwa hofu ya kuhujumiwa, Rage alisema wamewaelekeza wachezaji wao kucheza kwa tahadhari kubwa kwa hofu ya kuumizwa.
Simba inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 56. Iwapo Simba itafungwa na Yanga, Azam inaweza kutwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Simba.
“Ni lazima tuwashinde ndugu zetu wa Yanga ili tuwe na uhakika mkubwa wa ubingwa, hivyo tumewatahadharisha wachezaji wetu wasikubali kulaghaiwa kwa njia yoyote kwa sababu wataifedhehesha Simba,”alisema.
Tahadhari hiyo ya Rage imekuja huku kukiwepo na taarifa kwamba, uongozi wa Azam umekuwa ukihaha kuweka mambo sawa ili timu yao iweze kuipiku Simba na kutwaa ubingwa.
Akizungumzia hofu ya wachezaji wao kuumizwa, Rage alisema upo uwezekano mkubwa wa kutokea jambo hilo kwa lengo la kuwaharibia ushiriki wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Simba inajiandaa kurudiana na Al-Ahly Shandy ya Sudan wiki mbili zijazo baada ya kushinda pambano lao la awali lililochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa mabao 3-0.
Rage alisema wamewaelekeza wachezaji wao kutokaa na mpira kwa muda mrefu na hilo litawasaidia kuepuka kuumizwa na wachezaji wa timu pinzani.
Hata hivyo, Rage alikiri kuwa Yanga ni timu nzuri na wanaiheshimu kutokana na kuundwa na wachezaji wengi nyota, hivyo lolote linaweza kutokea.
“Ninachoweza kusema ni kwamba mchezo utakuwa mzuri kwa vile kila timu itakuwa na malengo ya kulinda heshima yake huku sisi tukitaka ubingwa,”alisema.
Wakati huo huo, Rage amesema kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu kwenda Sudan kwa ajili ya pambano lao la marudiano dhidi ya Al-Ahly Shandy.
Rage alisema wameamua kwenda Sudan mapema kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya huko ili isiweze kuwaathiri wachezaji katika pambano hilo.
Alisema Simba itakwenda huko ikiwa na msafara mkubwa wa viongozi na wadau wa timu hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanakabiliana vyema na hujuma zozote.

Yanga, Polisi na utovu wa nidhamu

ILIKUWA Machi 10 mwaka huu wakati Yanga ilipomenyana na Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ni pambano lililovuta hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, si tu kutokana na ushindani wa kisoka uliopo kati ya timu hizo, bali pia kila moja ilipania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika dakika za mwanzo, pambano hilo lilionekana kuwa zuri kutokana na kila timu kuonyesha soka ya kiwango cha juu huku mashabiki wakilipuka mayowe ya kuzishangilia. Ndani ya dakika 20 za mwanzo, Azam ikahesabu bao la kuongoza.
Mambo yalianza kubadilika baada ya wachezaji wa timu zote mbili kuanza kuonyeshana ubabe na hatimaye mwamuzi Israel Nkongo kumwonyesha kadi nyekundu kiungo Haruna Niyonzima baada ya kumpa kadi ya pili ya njano.
Ni kuanzia wakati huo, pambano hilo liligeuka uwanja wa vurugu. Wachezaji wa Yanga walimvamia Nkongo na kuanza kumpa kipigo huku nahodha wao Shadrack Nsajigwa akijitahidi kuwatuliza, lakini ilikuwa vigumu.
Kutokana na vurugu hizo, Nkongo aliamua kumtoa nje kwa kadi nyekundu beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kosa la kutaka kumpiga. Yanga ikalazimika kucheza ikiwa na wachezaji tisa na hadi pambano lilipomalizika, ilichapwa mabao 3-1.
Kufuatia vurugu hizo, Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliwafungia wachezaji watano wa Yanga na kuitoza klabu hiyo faini ya jumla ya sh. milioni moja. Wachezaji waliofungiwa ni Cannavaro, Nurdin Bakari, Omega Seme, Jerry Tegete na Stephano Mwasika.
Mbali ya kuwafungia wachezaji hao, kamati hiyo pia iliwatoza faini
ya sh. 500,000 kila mmoja. Adhabu zote hizo zilitolewa kwa mujibu wa kanuni za ligi.
Hata hivyo, Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF iliamua kupunguza adhabu hizo baada ya Yanga kukata rufani, lakini iliongeza adhabu ya faini kwa wachezaji wote watano.
Vurugu zilizofanywa na wachezaji wa Yanga si tu kwamba ziliwashtua mashabiki wa soka nchini, bali pia ziliitia doa ligi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa, matukio ya aina hiyo yalishasahaulika katika mchezo wa soka.
TFF ilikemea vikali vurugu hizo na kuwataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji wao. Pia uongozi wa Yanga uliomba radhi kwa mashabiki wa soka kutokana na vurugu hizo na kuahidi kuwa, kosa hilo halitajitokeza tena.
Mchezaji Mwasika, ambaye picha za video zilimwonyesha dhahiri akimtandika ngumi Nkongo, naye alimuomba radhi mwamuzi huyo pamoja na mashabiki wa soka nchini na kuahidi kutorudia kosa hilo. Mwasika alifungiwa kucheza mechi zote zilizosalia msimu huu baada ya kamati ya nidhamu kutengua adhabu yake ya kufungiwa kwa mwaka mmoja.
Tukio lingine lililoitia doa kubwa ligi hiyo msimu huu ni lile la wachezaji wa Polisi Dodoma kumpa kipigo mwamuzi Martin Saanya baada ya mchezo kati yao na Azam uliochezwa Aprili 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kufuatia vurugu hizo, Kamati ya Ligi ya TFF iliwafungia kucheza mechi tatu kila mmoja wachezaji tisa wa Polisi na pia kuwatoza faini ya sh. milioni moja kila mmoja.
Wachezaji wa Polisi waliofungiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25(g)(iii) ni Noel Msekwa, Frank Sindato, Abdallah Matila, Bantu Admin, Salmin Kisi, Madope Mwingira, Sihaba Mkude, Kaliyasa Mashaka na Ibrahim Massawe. Iwapo wachezaji hao watahama Polisi na kujiunga na timu nyingine, watahama na adhabu zao.
Dosari nyingine iliyojitokeza katika ligi hiyo msimu huu ni Yanga kupokonywa pointi tatu katika mechi yake dhidi ya Coastal Union kwa kosa la kumchezesha beki Cannavaro wakati alikuwa na kadi nyekundu kwa kosa la kupigana.
Kitendo cha Yanga kumchezesha Cannavaro katika mechi hiyo kiliwashangaza wadau wengi wa soka kwa vile kanuni za ligi zipo wazi kwa mchezaji mwenye kadi nyekundu kwa kosa la kufanya vurugu uwanjani.
Wapo wadau waliowatupia lawama viongozi na benchi la ufundi la Yanga kwa kosa hilo huku wengine wakiilaumu kamati ya nidhamu na usuluhishi ya TFF, ambayo ilimpungumzia adhabu Cannavaro na wachezaji wengine wa klabu hiyo.
Kasoro nyingine ilijitokeza katika pambano kati ya Azam na Mtibwa Sugar lililochezwa Aprili 23 mwaka huu kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Pambano hilo lilishindwa kumalizika baada ya Mtibwa Sugar kugomea adhabu ya penalti iliyotolewa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma katika dakika ya 88. Mwamuzi akaamua kuvunja pambano hilo.
Kinachoshangaza, ripoti ya mwamuzi na kamisaa zilitofautiana kuhusu sababu za kuvunjika kwa pambano hilo. Mwamuzi hakusema alisubiri kwa muda gani kabla ya kulivunja wakati kamisaa alisema pambano lilivunjika kabla ya dakika 15 za kusubiri.
Kutokana na utata huo, kamati ya ligi iliamua kumuondoa Msangi na wasaidizi wake, Samuel Mpenzu na Abdalla Uhako kwenye orodha ya waamuzi wa ligi hiyo na kuipa Azam ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Uamuzi wa kamati hiyo ulizua malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka. Wapo walioilalamikia kamati kwa kushindwa kuiadhibu Mtibwa Sugar kulingana na kanuni, ambapo timu inayogomea mchezo, hutakiwa kushuka daraja.
Lakini wadau wengine wameilalamikia kamati kwa kuipa ushindi Azam wakati kosa lilifanywa na mwamuzi, ambaye aliamua kuvunja pambano huku wachezaji wa Mtibwa wakiwa bado wapo uwanjani.
Kamati ya ligi pia iliwaadhibu baadhi ya makamisaa kwa kushindwa kufika kwenye mechi walizopangiwa kusimamia bila kutoa taarifa na wengine walipewa onyo kali kutokana na ripoti za mechi walizosimamia kuwa na mapungufu.
Kutokana na kasoro hizo, ni vyema TFF ijipange vizuri zaidi ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali wachezaji watakaoendelea kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kupiga waamuzi uwanjani.
TFF pia inapaswa kuwa makini na makamisaa wanaoshindwa kutimiza wajibu wao. Pengine ni vyema TFF iwe na makamisaa wachache wanaofahamu na kutimiza wajibu wao kuliko kuwa na utitiri wa makamisaa, lakini wasiotambua vyema majukumu yao.

ISHA MASHAUZI: Sijawahi kuhusiana kimapenzi na Thabiti Abdul au Mzee Yusuph


 Asema kwa sasa hana mpango wa kuolewa tena
 Awashangaa na kuwaonea huruma mashoga
 Akana kuvuta bangi, hajawahi kukuza matiti yake
MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Isha Ramadhani amesema hafikirii kuolewa kwa sasa kwa sababu lengo lake kubwa ni kukiimarisha kikundi chake cha Mashauzi Classic. Isha alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipohojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five. Makala hii ya ana kwa ana inaeleza mengi zaidi kuhusu mahojiano hayo kama yalivyonukuliwa na mwandishi wetu.
SWALI: Kwa nini wanawake wengi wanashindwa kudumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu?
JIBU: Si kweli kwamba wanaoshindwa ndoa, wanaume ndio wanaokuwa wakorofi.
Wakati mwingine ni wanawake wenyewe. Kila mmoja anakuwa na mtazamo wake.
Mi mwenyewe napenda kuolewa, lakini kwa sasa kutokana na kazi yangu, nimeona ni bora niimarishe bendi ndipo baadaye nifikirie suala la kuolewa, maana ndoa ni suala la majaliwa, unaweza kufikiria utaolewa, lakini kumbe usiolewe. Kwa hiyo baadaye naweza kufikiria kuolewa, lakini kwa sasa napumzika kidogo.
SWALI: Inawezekana hayo yote yametokea kwa sababu uliolewa mapema sana?
JIBU: Naweza kusema sikuolewa mapema sana kwa sababu sina ndoa moja. Nina ndoa mbili.
SWALI: Kwa maana hiyo inawezekana wewe ndiye unayetafuta bucha?
JIBU: Unajua kumpata mpenzi wa kweli ni sawa na kuingia kwenye pori kumsaka mnyama mkali, ambaye binadamu tunaogopa. Inategemea, unaweza ukabahatisha, lakini pia unaweza ukakosa. Lakini yote mawili yanawezekana, ni sawa na bahati nasibu. Ni sawa na kupapasa kizani, utakachoibuka nacho ndicho hicho hicho.
SWALI: Wanawake wengi maarufu huwa wameolewa, wakaachika ama wanakuwa na wachumba wengi sana. Hili likoje kwako?
JIBU: Mimi kwa upande wangu, naweza kusema wakati nilipoolewa kwa mara ya kwanza, nilikuwa sijulikani. Waliokuwa wananijua ni familia yangu na marafiki zangu na ndugu zangu. Nilipokuja kuolewa mara ya pili, nilikuwa najulikana, lakini kutokana na hitilafu zangu mimi na yeye, hatukuweza kudumu kwa muda mrefu.
Si kwamba niliachika kwa sababu ya umaarufu, la hasha au ukiwa maarufu unakuwa na wapenzi wengi, hapana. Naweza kukwambia kwa sasa nina mpenzi mmoja, huwezi kuamini, lakini ni ukweli kutoka moyoni mwangu. Nampenda ananipenda, namjali ananijali.
Wapo wanaosumbua kwa sababu wapo wanaokuja kwa nia nzuri, anaomba namba yako ya simu, anasema oooh, nitakuhitaji, lakini mwisho wa siku anakusumbua, oooh nakupenda, ooh kila ninapokuona kwenye TV, napenda kukuona vile kama unavyocheza, lakini tuwe wawili tu.
Lakini hayo yote yanategemea na wewe mwenyewe, ukiwa na tamaa, ukiona ana chapaa, unajikuta unakwenda, lakini kwa mtu kama mimi sidhani kama ninayo tamaa ya pesa kwa sababu mimi mwenyewe najua kutafuta.
SWALI: Kuna mtazamo kwamba mwanamke anapomiliki bendi, lazima kunakuwa na mwanaume nyuma yake, ambaye ndiye anayemuunga mkono. Kuna ukweli wowote kuhusu msemo huu?
JIBU: Hicho kitu sikikatai, inawezekana kabisa kipo kwa sababu haiwezekani mtu kuja kuwekeza kwako bila sababu maalumu, inawezekana kabisa mtu akaja kuwekeza kwako kwa sababu maalumu, akijua kuna kitu ambacho atakipata.
SWALI: Hivi asili yako hasa ni wapi kwa sababu ulivyo, unaonekana kuwa ni mtanzania, lakini umechanganya marashi fulani. Hebu tueleze kwenu hasa ni wapi?
JIBU: Mimi na taarabu ni vitu viwili tofauti, lakini yote haya ni kwa sababu ya kutafuta maisha. Mimi hasa chimbuko langu kwa wazazi wangu, hasa upande wa baba, wametokea Burundi. Kwa hiyo mimi jina langu halisi, ambalo linatambulika katika ukoo, naitwa Mlundi.
Kwa hiyo baada ya wazazi wetu kutoka kule Burundi, wakawa wanaishi Tanzania. Ndio sababu najiita mkuria wa kwanza kuimba taarabu. Kwa hiyo Musoma ndiko hasa nilikokulia, lakini kiasili hasa, mimi siyo mtu wa Musoma, asili ya wazazi wangu ni Burundi.
Baada ya hapo, wazazi wangu wakaamua kuhamishia maisha yao Dar es Salaam. Ni kuanzia hapo, nilisoma Dar es Salaam na kukulia Dar es Salaam. Kwa hiyo hata kuolewa, niliolewa Dar na walionilea, baadhi yao ni watu wa Pemba.
Mama yangu alikuwa msanii, kwa hiyo kila alipokuwa akitoka, tuseme saa mbili usiku, alikuwa akiniacha kwa majirani zetu, ambao wengi walikuwa Wapemba, ndio sababu na mimi nilikuwa naitwa Mpemba kwa sababu hata lafudhi yangu ilikuwa kama ya kwao, lakini mimi si mpemba hata kidogo, sihusiki nao kwa lolote.
SWALI: Kwa hiyo ile stori kwamba wewe na Mzee Yusuph ni ndugu haina ukweli wowote?
JIBU: Hapana, mimi na Mzee Yusuph hatuna undugu wowote.
SWALI: Kwa nini muziki wa taarab unaitwa mipasho?
JIBU: Ni kwa sababu tunaimba vitu, ambavyo ni vya kweli, ndio maana wakaita mipasho, ingawaje mtu akisikia wimbo ukiimbwa, anadhani kaambiwa yeye, ndio sababu wanasema anayejishuku, hajiamini.
SWALI: Kwa nini unaitwa Mashauzi? Una dharau sana?
JIBU: Mimi nasema anayenizungumzia, mara nyingi anakuwa hanitambui. Mimi ni mtu ambaye napenda sana kucheka na watu, napenda kutaniana na watu, naweza nikafika sehemu, watu wasiponiona, labda siku mbili au tatu, wanaweza kunipigia simu wakaniuliza, inakuwaje mbona hatukuona? Isha tumekumiss sana, hebu njoo mahali fulani. Kwa hiyo mtu anayenizungumzia kwa mwelekeo huo, hanijui kiundani.
SWALI: Hivi wewe huwa unaandika maishairi ya muziki?
JIBU: Unajua unaweza kukaa na mtu mahali, lakini huwezi ukajua hisia zake zikoje. Wewe unaweza kuzungumza kitu, lakini hujui kwamba hicho kitu mimi kimenigusa. Kwa hiyo ninapoona hivyo, namtumia ujumbe mkurugenzi wangu, ambaye ni Thabiti Abdul na kumweleza kwamba kuna mtu amezungumza kitu hiki na kile kimenigusa sana, naomba unitungie mashairi na yeye atafanya hivyo.
Kwa mfano, kuna wakati tulipokuwa tumekaa pale nje, kuna mtu alisema neno kuhusu mimi, nikamwambia kama nimekukera, hama mji. Inapokuwa hivyo, namweleza mkurugenzi wangu kwamba kuna hiki na kile na yeye anaandika, anaweka muziki na sauti, nyimbo inakuwa imekamilika. Baadaye ananifuata na kuniambia wimbo umekamilika kwa hiyo kazi yangu inakuwa ni kuweka vikorombwezo vya chini. Mara nyingi hivyo huwa vinatoka kichwani.
SWALI: Taarabu ina mashabiki wengi sana, lakini mara nyingi wanakuwa wale, ambao mwonekano wao ni tofauti na wengine na kwa wanawake, inakuwa ni wale, ambao wameshindikana katika familia zao. Kwa nini inakuwa hivyo?
JIBU: Hakuna uhusiano isipokuwa vile vitu vinavyoimbwa, wao ndio wanakuwa wanapenda. Wanakuwa wanapenda kupashana, kuchambana, labda niseme hivyo.
Lakini nikirudi kwenye swali la awali, si watu wote wanaopenda taarabu wanakuwa ni watu walioshindikana. Sasa hivi naweza kusema kwamba taarabu inapendwa hata na akina baba, ambao ni marijali, wanapenda watoto, wanapenda wasichana, utakuta mtu anakwenda klabu huku akiwa anamjua mwimbaji taarabu.
Zamani wanaume walikuwa wanahisi kwamba mwanamke akipenda taarabu, huenda ni shangingi na vivyo hivyo mwanaume akipenda taarabu, alikuwa akionekana namna gani vipi.
SWALI: Hivi inakuwake mwanaume, ambaye namna gani vipi anaweza kuwachukua shoga zake wa kike wanne au hata watano, akajiweka katikati yao na kucheza kama vile naye ni mwanamke ama shughuli ni ya kwake. Inakuwaje kitu kama hicho kinatokea?
JIBU: Niseme tu kwamba, awali ya yote namshukuru Mungu kwamba sisi wanawake bado tunaendelea kuzaa. Lakini huwa nasikia uchungu sana ninapoona kitu kama kile, lakini huwezi kusikia uchungu, ukamfuata mtu na kumweleza acha maana jibu atakalokupa, ukirudi nyumbani unaweza kutafuta maji ili ushushie.
Wale ni watu ambao wanakuwa wameshaamua kuishi maisha ya aina fulani. Kuna wengine ukionyeshwa na kuambiwa huyu ni dizaini fulani, unaweza kukataa.
SWALI: Mara ya mwisho kulia ilikuwa lini?
JIBU: Siku kama nne hivi zilizopita.
SWALI: Nini hasa kilitokea?
JIBU: Naweza kusema ni sababu ya mapenzi.
SWALI: Unataka kusema ni maumivu? Ulilizwa?
JIBU: Hapana hapana, unajua wakati mwingine furaha nayo inaweza kuleta kilio. Lakini sikulia kwa kuumizwa, nililia kwa kujiumiza kwa maana kwamba nilipatwa na kitu kama wivu fulani hivi.
SWALI: Kuna wasanii fulani wa kundi la taarab la Five Stars walipata ajali ya barabarani kule Morogoro mwaka jana. Ulijisikiaje baada ya kupata taarifa hizo?
JIBU: Ukweli ni kwamba kila chenye roho lazima kitaonja mauti, lakini mauti yanapomfika mtu wa karibu yako, huwa yanaumiza sana, na hasa ukikumbuka ajali yenyewe jinsi ilivyotokea, ni kitu ambacho tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Binafsi siwezi kusema kwamba nilishuhudia, lakini nilikuwa mmoja kati ya watu wa mwanzo kupata taarifa za ajali ile kuliko watu wengine. Ah, inasikitisha sana.
SWALI: Kuna taarifa kwamba matiti yako yametengenezwa na wachina na wewe ulikuwa mtu wa mwanzo kuyatengeneza. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizo?
JIBU: Asante sana kwa swali lako. Naweza kusema kwamba, huyo mchina mwenyewe mimi huwa nakutana naye barabarani. Mimi nilivyo ndivyo jinsi nilivyoumbwa na Mungu. Kama nimejaaliwa au vinginevyo, siwezi kujua. Lakini sijawahi kwenda mahali popote kuomba ama kutaka umbo langu liboreshwe.
Sijui huyo aliyeandika kwenye gazeti kwamba aliniona au vipi au aliamua tu kufanya hivyo ili auze gazeti lake, lakini sijawahi kufanya kitu kama hicho kwa sababu mimi ni mtoto wa kiislamu na dini yetu inazuia kufanya kitu kama hicho.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu masuala ya dini na muziki? Unadhani dini yako inaruhusu wewe kujishughulisha na muziki?
JIBU: Kazi ya muziki ni kazi kama zilivyo kazi zingine, lakini si mbaya mtu kama mimi nikipata muda wakati mwingine kujihusisha na muziki kwa sababu siku zote, kabla sijapanda jukwaani, huwa namuomba Mungu kwa maana hiyo, ukimkumkuka Mungu, siku sote ndivyo atakavyozidi kukujalia na kukuwezesha kufanikiwa katika mambo yako.
SWALI: Hivi jina la Mashauzi limetokea wapi?
JIBU: Jina hilo limetokana na mashabiki. Zamani nilikuwa najulikana zaidi kwa jina la Mama Afrika kwa sababu nilikuwa napenda sana kuvaa kiafrika. Nilipokuwa nikienda kwenye kitchen part, nilikuwa najulikana zaidi kwa jina hilo kwa sababu wakati huo nilikuwa nafanyakazi kama MC.
SWALI: Kwa maana hiyo, kabla hujaanza kuimba ulikuwa MC?
JIBU: Ni kweli kabisa kwamba kabla ya kuanza kuimba taarabu nilikuwa MC. Ilikuwa miaka hiyo kabla sijaanza kuganga njaa.
SWALI: Kila mtu anajijua thamani yake, wewe binafsi unaijua thamani yako?
JIBU: Ni kweli, kwa sasa naijua thamani yangu kwa sababu nilivyokuwa huko nyuma sio sawa na nilivyo hivi sasa.
SWALI: Kwa hiyo thamani yako huwa unaiona?
JIBU: Thamani naiona kwa sababu bila ya wewe mwenyewe kuiona thamani yako, hakuna mtu mwingine anayeweza kuiona.
SWALI: Bangi vipi? Nasikia ndio zako hizo (kuvuta)?
JIBU: Hicho kitu mimi situmii kabisa. Katika vitu ambavyo sijawahi kukifanya ni kuvuta bangi. Muziki mimi upo kwenye damu kwa hiyo siwezi kuunogesha kwa kitu chochote zaidi ya kusema naanza kwa kutaja jina la Mwenyezi Mungu na sasa nakwenda kazini.
SWALI: Gari lako la kwanza kumiliki lilikuwa la aina gani?
JIBU: Gari langu la kwanza lilikuwa Lexas. Ukweli hiyo ni ndoto kubwa niliyokuwa nayo kwa sababu mimi huwa sipendi kitu cha kununuliwa kwa sababu mtu anaweza kukufanyia hivyo, baadaye akaja na kukueleza kitu kingine.
Sasa ikitokea mtaani watu wameshazoea kukuona na kitu fulani, halafu baadaye hicho kitu huna, utakuwa huna mahali pa kuuweka uso wako.Nilikaa na gari hiyo kwa muda wa kama mwaka mmoja na miezi mitatu hivi.
SWALI: Ni kweli kwamba wasanii wa taarab, hasa wa kike wana tabia ya kutembea na waume za watu?
JIBU: Unajua mapenzi ni kitu, ambacho hakiingiliwi. Na mapenzi ni siri, ingawaje sasa hivi imekuwa dhahiri na ndio sababu baadhi yetu tumekuwa tukishutumiwa kwamba unatembea na mume wa mtu, lakini kama tungekuwa tunafanya siri, sidhani kama kuna mtu angekuja kugundua hicho kitu. Kila mtu anataka ajionyeshe kwamba mimi nilikuwa natembea na fulani.
SWALI: Kuna kipindi ulishutumiwa kwa kutimua wasanii wote wa kike kwenye kikundi chako na stori iliyozagaa mjini ni kwamba ulikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Thabiti Abdul. Hebu tueleze mahusiano yako na Thabiti, kuna ukweli wowote kuhusu hilo?
JIBU: Usinione nacheka, nafanya hivyo kwa sababu umeniambia nifunguke. Mimi Thabiti sina mahusiano naye yoyote zaidi ya kazi. Nimemtambua Thabiti miaka mingi iliyopita. Alianza kazi ya sanaa siku nyingi, tangu mimi nikiwa mdogo. Mimi ni mdogo sana kwa Thabiti. Nilikuwa nikimuona akifanyakazi na mama yangu na sehemu nyingine.
Mwaka 2009 wakati nikiwa Jahazi, baada ya kuona mambo yanakwenda longo longo ama mrama, nikaamua kutengeneza albamu yangu mimi kama mimi. Nilianza kushirikiana na watu kama akina Ally J, Fikirini pamoja na Mussa, lakini baadaye nikasema hata, wacha nimshirikishe na huyu mtu ili niweze kupata kitu kizuri zaidi. Ndipo hapo nilipoanza mahusiano ya kikazi na Thabiti Abdul.
Ikaenda hivyo kwa muda mrefu, lakini waswahili wanasema kila mtu na mtuwe ama kila shetani na mbuyu wake. Jinsi tulivyokuwa tumeshibana kikazi, ndivyo watu walivyoanza kututafsiri kivingine. Unajuwa hakuna kitu kizuri kama unapomuelekeza mtu kitu, akaweza kukifanya vile unavyotaka ama kufundisha mtu, lakini akawa haelewi. Kila alichokuwa akikifanya, mimi nilikuwa naelewa. Vile vitu vikamfanya anielewe ndipo tukashikana mpaka kumaliza albamu yangu ya kwanza.
Kamwe hatujawahi kuunganisha viungo vyetu vya uzazi kwa sababu kila mmoja anaye wa kuunganisha naye. Lakini ndio hivyo tena, stori zimeshaenea mjini, lakini nilishawahi kusema kwamba, hakuna kitu chochote kinachoendelea kati yangu mimi na Thabiti.
SWALI: Huko nyuma ulikuwa katika kikundi cha Jahazi kinachoongozwa na Mzee Yusuph, lakini baada ya kutokea purukushani, ukaamua kuanzisha bendi yako na sasa upo na Thabiti, mnafanya kazi kama wakurugenzi. Kitu gani kilitokea kati yako na Mzee Yusuph?
JIBU: Hakuna kitu chochote kibaya kilichotokea kati yangu na Mzee Yusuph. Wakati naanza kufanya zing zong, nilimwambia nahitaji kufanya kitu fulani kutokana na majukumu yaliyonibana na akaniambia sawa. Nikaanza kutengeneza albamu zangu.
Nilipoanza kutengeneza albamu ya pili, ndipo nilipoanza kuona utamu wa vimeo. Ilikuwa kila nikipita huku na kule, naulizwa wewe ndiye Isha Ramadhani, tunakuomba siku fulani tuna kitchen party, uje kutumbuiza. Tunataka ile mama nipe radhi, na nikienda huko naulizwa tukupe shilingi ngapi, wakati mwingine nilipotaka kiasi kidogo cha pesa, waliniongeza, oooh tutakupa shilingi laki mbili.
Kwa hiyo ikafika kipindi nikasema hebu wacha nijaribu, lakini nikaona kwa nini nijaribu, bora nithubutu, kwa kweli nikaweza na sasa nasonga mbele.
SWALI: Kwa hiyo wewe na Mzee Yusuph hamna uhusiano wowote wa kimapenzi?
JIBU: Kusema ule ukweli, Mzee Yusuph ni kama baba yangu, ingawaje kuna watu huwa wanapenda kutuona tukigombana, lakini mimi siwezi kuwa mjinga kiasi hicho. Namshukuru hata yeye mwenyewe ananielewa mimi ni nani na ninataka kufanya nini.
SWALI: Kitu gani kinachokufurahisha katika maisha yako? Dhahabu, maisha mazuri, matiti yako kusimama vizuri kifuani au nywele? Ni kipi kinachokufanya uwe na furaha?
JIBU: Kitu kinachonifurahisha katika maisha yangu ni kuwa na furaha na yule ninayempenda na pia niwe na furaha na familia yangu, nisiwaudhi wazazi wangu wote wawili, bila wao mimi nisingekuwepo, wangeweza kuninyonga miaka mingi iliyopita. Napenda sana kuwa na furaha kila wakati ndio maana huwa sipendi kujiudhi.