KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 4, 2017

SIMBA YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI


SIMBA jana ilikuwa timu ya kwanza kupata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa KVZ bao 1-0.

Katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Simba ilijipatia bao hilo la pekee kipindi cha kwanza kupitia kwa Muzamil Yassin.

Muzamil alifunga bao hilo dakika ya 43 baada ya washambuliaji wa Simba kufanikiwa kutegua mtego  wa kuotea uliotegwa na mabeki wa KVZ.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa inazo pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikiwa inaongoza kundi hilo.

Pambano hilo lilitawaliwa na ufundi mkubwa huku KVZ ikifanikiwa kuwabana washambuliaji wa Simba kwa kutumia mtego wa kuotea.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Simba. Katika mechi yake ya kwanza, iliichapa Taifa Jang'ombe mabao 2-1.

Katika mechi ya awali ya kundi hilo iliyochezwa jioni, Jang'ombe Boys iliwalaza mabingwa watetezi URA ya Uganda mabao 2-1.
 
Michuano hiyo inaendelea tena leo kwa mechi za Kundi B, kati ya Zimamoto na Yanga kuanzia saa 10:00 jioni na Jamhuri dhidi ya Azam kuanzia saa 2:30 usiku.

No comments:

Post a Comment