KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 15, 2017

AMINA KUAGWA KIPUNGUNI KESHO, KUZIKWA KESHOKUTWA TANGA


MWILI wa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), inayochapisha magazeti ya Uhuru, Uhuru Wikiendi, Burudani na Mzalendo, Amina Athumani (30), unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo asubuhi kwa boti kutoka Zanzibar.

Msemaji wa familia ya marehemu, Athumani Kazukamwe, alisema mjini Dar es Salaam, jana jioni kuwa, mwili wa Amina utasafirishwa kwa boti kutoka Zanzibar saa moja asubuhi na unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kati ya saa tatu na saa nne asubuhi.

Kazukamwe, ambaye ni baba mkubwa wa mume wa marehemu, alisema mazishi ya Amina, yamepangwa kufanyika kesho katika makaburi ya Soni, nje kidogo ya mji wa Tanga.

Alisema awali, upande wa mume wa marehemu ulitaka mazishi hayo yafanyike leo Dar es Salaam, lakini baada ya majadiliano na familia ya marehemu, walikubaliana mazishi yafanyike Tanga.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia ya marehemu, taratibu za kuuaga mwili wa Amina zitafanyika papo hapo bandarini na mara baada ya kumalizika, utasafirishwa kwa basi maalumu la kukodi kupelekwa Tanga.

Amina, mwandishi wa habari za michezo katika magazeti hayo, alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, alikokuwa amelazwa.

Alilazwa kwenye hospitali hiyo baada ya kuzidiwa kutokana na kushikwa uchungu, ambapo alijifungua mtoto wa kiume, lakini kwa bahati mbaya alifariki.

Baada ya mtoto kufariki, Amina aliendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomkuta jana asubuhi.

Marehemu Amina alikwenda Zanzibar kikazi kwa ajili ya kuripoti mashindano ya Kombe la Mapinduzi, yaliyomalizika Ijumaa iliyopita na ilikuwa arejee Dar es Salaam jana.

Akizungumzia kifo hicho cha Amina, Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL, Ramadhani Mkoma, alithibitisha mazishi ya marehemu Amina kufanyika kesho Tanga.

Ramadhani alisema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu hawakutarajia iwapo Amina angetangulia mbele ya haki katika umri mdogo.

Alisema Amina ameacha pengo kubwa kwa sababu alikuwa mmoja wa wanahabari wa UPL waliokuwa wakifanyakazi kwa kujituma, aliipenda kazi yake na ilikuwa mwiko kwake kusukumwa kutimiza wajibu wake.

Alisema kazi aliyoifanya wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo alitumwa kuandika habari zake akiwa Unguja, ni uthibitisha wa wazi wa utendaji mzuri aliokuwa nao.

Alisema hawana la kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu kwa kuwa kila alipangalo, hakuna anayeweza kulipangua. Amewataka wafanyakazi wa UPL kumuenzi Amina kwa kuiga utendaji wake wa kazi.

Baadhi ya wafanyakazi wa UPL, wamekielezea kifo hicho cha Amina kuwa ni pengo kubwa, kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kuandika habari na makala zinazohusu michezo.

No comments:

Post a Comment