KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 15, 2017

MALINZI AMPONGEZA MKURUGENZI MPYA IDARA YA MICHEZO


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Malinzi amempongeza Bw. Yusuph Singo Omari kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Tanzania.

Mapema wiki hii, Yusuph Singo Omari, aliteuliwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye kushika wadhifa huo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Leonard Thadeo aliyehamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Kabla ya uteuzi huo uliofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 kifungu namba 6, kifungu (1) (b) kikisomwa pamoja na kifungu namba 8 cha sheria hiyo, Bw. Yusuph Singo Omari alikuwa Mkufunzi Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Ardhi katika masuala ya Michezo.

Katika pongezi zake, Rais Malinzi amepokea wito wa Waziri Nape Nnauye kumpa ushirikiano wa kutosha kwa Yusuph Singo Omari atakapokuwa anatekeleza majukumu yake.

“Sisi wa TFF tunakupongeza kwa nafasi hiyo, tunachukua nafasi hii kukuahidi kukupa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yako mapya. Hii ni kuitikia wito wa Waziri Nape ambaye aliomba wanafamilia yote ya michezo kukupa ushirikiano,” alisema Malinzi alipozungumza na mtandao wa www.tff.or.tz.

Rais Malinzi alisema kwamba program za TFF kwa sasa kwa timu zake zote za taifa, hazina budi kuungwa mkono na Serikali ili kufanikisha na kiungo mkubwa katika eneo hilo ni Bw. Yusuph Singo Omari ambaye ndiye mkuu wa Idara ya Maendeleo ya michezo – mpira wa miguu ukiwa ni miongoni mwa michezo hiyo.

No comments:

Post a Comment