KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 30, 2017

YANGA YAIENGUA SIMBA KILELENI MWA LIGI KUU


KIUNGO wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa jana aliipa furaha Yanga baada ya kuifungia mabao mawili, ilipoilaza Mwadui mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, Chirwa aliyekuwa ameingia kipindi cha pili, alifunga mabao hayo dakika ya 69 na 82 na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wa Yanga.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuiengua Simba kileleni mwa ligi kuu, ikiwa sasa inaongoza kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 45.

Chirwa, ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima, alifunga bao la kwanza kwa shuti kali baada ya kuuwani mpira uliopanguliwa vibaya na kipa Shaaban Kado wa Mwadui.

Mzambia huyo aliongeza furaha mashabiki wa Yanga kwa kufunga bao la pili kwa shuti lingine kali, kufuatia kupewa pasi ya kichwa na kiungo Thabani Kamusoko.

Sunday, January 29, 2017

AZAM YAITAMBIA TENA SIMBA




BAO lililofungwa na mshambuliaji John Bocco, jana liliiwezesha Azam kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Azam dhidi ya Simba katika siku za hivi karibuni. Azam pia iliichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, iliyochezwa mapema mwezi huu kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Bocco, ambaye pia ni nahodha wa Azam, alifunga bao hilo la pekee dakika ya 70 baada ya kumtoka beki Method Mwanjali wa Simba ndani ya eneo la hatari.

Kipigo hicho kimepunguza matumaini ya Simba kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwani huenda ikapokonywa uongozi na Yanga, iwapo mabingwa hao watetezi wataifunga Mwadui leo.

TFF YAMSHUKURU RAIS DK. MAGUFULI KURUHUSU UWANJA WA TAIFA UTUMIKE KWA MECHI ZA LIGI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kufunguliwa tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kadhalika, TFF inamshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kwa juhudi zake na kwamba namna aliyoonesha ushirikiano kufanikisha suala la kufunguliwa uwanja huo uliofungiwa matumizi yake na Serikali, Oktoba mwaka uliopita.

TFF inachukua nafasi hii kuahidi kuwa itasimamia matumizi mazuri ya uwanja huo kwa kutoa elimu kwa wadau ili kuutumia uwanja huo vema ikitambua kuwa ni hazina ambayo imetokana na nguvu na gharama kubwa za Serikali kuujenga uwanja huo.

TFF inatahadharisha mashabiki wa mpira wa miguu kwamba uwanja huo umejengwa kwa gharama kubwa hivyo ni jukumu letu kuutuza na kuutumia vema kwa sababu ni hazina kubwa tuliyonayo na ni miongoni mwa urithi bora kwa vizazi vijavyo.

Kwa sasa tumetuma maombi yetu Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuomba kuutumia uwanja huo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi Januari 28, mwaka huu kati Simba na Azam utapigwa kwenye uwanja huo wa Taifa, Dar es Salaam kadhalika keshokutwa katika mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Mwadui ya Shinyanga.

Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inaonesha kuwa ligi hiyo huko Mbeya kutakuwa na ‘derby’ kwa maana ya mchezo wa upinzani baina ya timu zinazotoka mkoa mmoja wa Mbeya ambazo ni Tanzania Prisons na Mbeya City utakaochezwa na Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Keshokutwa Jumapili Januari 29, mwaka huu kutakuwa na mchezo mwingine ambao Young Africans itacheza na Mwadui jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Majimaji ya Songea itasafiri hadi Mtwara kucheza na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Jumatatu Januari 30, 2017 kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Thursday, January 26, 2017

RUFANI YA POLISI DAR DHIDI YA SIMBA YATUPILIWA MBALI



KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekataa kuisikiliza Rufaa ya klabu ya Polisi Dar es Salaam dhidi ya Simba SC, kwa sababu taratibu hazikufuatwa.
Polisi Dar iliikatia rufaa Simba SC kwa kumtumia beki wake, Novaty Lufunga katika mchezo wa kombe la TFF, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) hatua ya 32 Bora Jumapili, Uwanja wa Uhuru, Dar rs Salaam.
Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda 2-0, mabao ya Pastory Athanas kipindi cha kwanza na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kipindi cha pili, Lufunga alikuwa benchi kama mchezaji wa akiba muda wote mchezo.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kwamba Rufaa ya Polisi haikusikilizwa kabisa kwa sababu timu hiyo haikukamilisha taratibu.
“Polisi walifanikiwa kukata rufaa yao ndani ya muda, lakini bahati mbaya kitu kimoja tu, hawakulipa ada, hivyo rufaa yao haikusikilizwa kwa kuwa ilikuwa ipo kinyume cha utaratibu,”alisema Lucas.
Pamoja na hayo, Msemaji huyo wa TFF akasema kwamba hata kama rufaa hiyo ingesikilizwa Polisi Dar wasingeshinda kwa sababu kanuni za Kombe la ASFC hazikuwazuia Simba kumtumia mchezaji huyo.
Akifafanua, Lucas alisema kwamba adhabu zote za michuano hiyo hufanya kazi katika msimu husika pekee na kwamba kila msimu mpya mambo huanza upya.

Wednesday, January 25, 2017

MECHI ZINGINE ZA KOMBE LA SHIRIKISHO KUPIGWA TENA LEO


Mechi za raundi ya tano ya mechi za Kombe la Shirikisho la Azam 2016/17 (Azam Sports Federation Cup – ASFC), zitaendelea kesho Jamatano Januari 25, 2017 kwa timu za Singida United na Kagera Sugar kucheza kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Mchezo mwingine utakaozikutanisha timu za The Mighty Elephant ya Songea na Mashujaa ya Kigoma katika mchezo utakaofanyika Uwanja Majimaji mjini Songea.

Katika mchezo huo ambao uliahirishwa Jumatano iliyopita, mshindi wa kesho ndiye atacheza na Majimaji katika tarehe mpya itakayotangazwa hapo baadaye kama ilivyo kwa mechi kati ya African Lyon na Mshikamano.



LIGI YA WANAWAKE KUENDELEA LEO



Ligi ya wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano Januari 25, mwaka huu kwa michezo sita – mitatu kwa kila kundi.

Kundi A, linatarajiwa kuna na mchezo kati ya JKT Queens Dar es Salaam na Mburahati Queens pia ya jijini utakaofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Ilala.

Kadhalika Viva Queens ya Mtwara itakuwa mwenyeji wa Evergreen ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wakati Mlandizi ya mkoani Pwani itakuwa mgeni wa Fair Play katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Kwa upande Kundi B, Sisterz ya Kigoma itaikaribisha na Baobab ya Dodoma kwenye mfululizo wa ligi hiyo. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Lake Tanganyika.

Mchezo mwingine utachezwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa kati ya Panama na Majengo Women ya Singida ilihali Victoria Queens ya Kagera na Marsh Academy zitapambana hiyo kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Kagera.

TFF YAUFUNGIA UWANJA WA JAMHURI



SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limeufungia uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuchezwa mechi za ligi kuu na daraja la kwanza hadi utakapofanyiwa marekebisho.

Uwanja huo unamilikiwa na Chama cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro umekosa vigezo vya kutumika kwenye ligi kutokana na miundo mbinu yake hasa sehemu ya kuchezea kutofaa hivyo kuanzia leo hautatumika hadi utakapofanyiwa marekebisho.

Uwanja huo hutumika kwa mechi mbili tu za ligi zinazohusisha timu za Simba na Yanga zinapocheza na Mtibwa Sugar kutokana na uwezo wake wakuingiza watu wengi kwakua miamba hiyo ya soka nchini ina mashabiki lukuki.

Mechi namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika mashabiki waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv upande wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.

Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas alisema katika mchezo kati ya Mtibwa na Simba uliofanyika uwanjani hapo wiki mbili zilizopita ulikosa mvuto na kuzifanya timu hizo kushindwa kuonyesha kandanda safi kutokana na ubovu wa dimba hilo.

TFF imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi.

Vilevile sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Hivyo, Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. Kama marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Tuesday, January 24, 2017

YANGA YATOZWA FAINI SHILINGI MILIONI MOJA



TIMU ya Yanga imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa makosa mawili ikiwemo na timu yao kutoingia vyumba vya kubadilishia nguo pamoja na kutumia mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Halikadhalika mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi aliyechezesha mchezo huyo namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Young Africans ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF limemwondoa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.

Mwamuzi Ngole Mwangole: Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya amepewa barua ya onyo kali na kumtaka aongeze umakini wakati akichezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kubainika kukataa bao lililoonekana kutokuwa na mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Licha ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa Bw. Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu uliopita (2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya uamuzi uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.

Mechi namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar, Godfrey Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi baada ya mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la ufundi la timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti kadhia hiyo.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Mechi namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Pia mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa mapumziko. Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi na Msimamizi wa Kituo.

Mechi namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United, Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000 kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba moja.

Mechi namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.

Lakini pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.

Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao..

Adhabu hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza.

Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.

Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.

Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.

Mechi namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili kupoteza muda.

Mechi namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi; Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

Mechi namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

LIGI DARAJA LA PILI

Mechi namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Mechi namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3).

Mechi namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.

Mechi namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi Daraja la Pili.

Malalamiko ya klabu za Mwadui FC na Polisi Morogoro kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji wa Stand United, Kheri Mohamed Khalifa na wachezaji wawili wa Njombe Mji kucheza mechi bila leseni yamepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Pia maombi ya klabu ya Singida United kuhusu kubadilishiwa Mwamuzi kwenye mechi yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi, wakati maombi ya Alliance Schools, Friends Rangers FC, The Mighty Elephant na Kariakoo FC yanayohusu uendeshaji yanashughulikiwa na Sekretarieti ya TPLB.

Kuhusu JKT Ruvu, Kamati ilipitia maombi ya timu ya JKT Ruvu Stars FC kubadilisha uwanja wake wa nyumbani kutoka Mabatini mkoani Pwani hadi Mkwakwani mkoani Tanga kutokana na wachezaji wake 12 wa kikosi cha kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi mkoani Tanga. Ombi hilo limekubaliwa. Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(6) ya Ligi Kuu, TFF/TPLB zina mamlaka ya mwisho kuhamisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona zinafaa na kwa wakati husika.


Kuhusu Mchezaji Venance Ludovic, Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajiwa kukaa wiki ijayo kusikiliza malalamiko dhidi ya usajili wa wachezaji mbalimbali akiwemo mchezaji Venance Joseph Ludovic.

SIMBA, YANGA SASA KUVAANA FEBRUARI 25



MCHEZO wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya mahasimu, Simba na Yanga umesogezwa mbele hadi Februari 25, kutoka Februari 18, mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba sababu ya kusogezwa mbele kwa mchezo huo ni muingiliano na Ratiba ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika.
Februari 10, mwaka huu, Yanga watakuwa wageni wa Ngaya FC katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Mde mjini Mde nchini Comoro, kabla ya kurudiana Februari 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa sababu hiyo, mchezo wa Simba na Yanga usingeweza kufanyika tena Februari 18 na busara za TFF zimeupeleka hadi Februari 25.

AZAM YAZIFUATA SIMBA NA YANGA HATUA YA MTOANO KOMBE LA SHIRIKISHO



AZAM FC imeungana na Simba na Yanga kusonga mbele katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho, baada ya kuichapa Cosmopolitan mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kutokana na ushindi huo wa mechi hiyo ya raundi ya tano, Azam sasa itaungana na Simba na Yanga kwenye hatua ya 16 ya mtoano.

Yanga ilisonga mbele wiki iliyopita baada ya kuitandika Ashanti mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Simba iliichapa Polisi Dar mabao 2-0 kwenye uwanja huo huo.

Nahodha John Bocco alifungua biashara kwa Azam dakika ya 69 baada ya kuifungia bao lake la kwanza kabla ya chipukizi Shabani Iddi kuongeza la pili dakika ya 76.

Cosmopolitan, moja ya timu kongwe za soka nchini, ilipata bao la kujifariji dakika ya 78 kupitia kwa Fidelis Kyanga kabla ya Azam kuongeza la tatu dakika ya 80 kupitia kwa Joseph Mahundi.

MWANJALI WA SIMBA MCHEZAJI BORA MWEZI DESEMBA, 2016


BEKI wa Simba, Method Mwanjali amechaguliwa kuwa mchezaji bora Desemba wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2016/2017.
Beki huyo wa kati, aliwashinda kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na beki Yakubu Mohamed wa Azam FC. Mwezi Desemba ulichezwa raundi tatu za Ligi hiyo, huku Simba ikicheza mechi mbili ugenini na moja nyumbani. Raundi hizo ni ya 16, 17 na 18.
Mwanjali aliiongoza Simba kushinda mechi zote tatu, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kunyakua pointi zote tisa, na kubaki katika nafasi yao ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi, nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya 16.
Pia katika raundi hizo tatu ambapo Simba haikufungwa bao hata moja, Mwanjali alicheza dakika zote 270, na bila kuonyeshwa kadi yoyote. Alichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya timu yake huku akiongoza safu ya ulinzi.
Kwa kushinda tuzo hiyo ya mchezaji bora, Mwanjali atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wakuu wa Ligi hiyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.
Wachezaji wengine walioshinda tuzo za mchezaji bora kwa msimu wa 2016/2017 hadi sasa ni John Raphael Bocco wa Azam (Agosti), Shiza Ramadhan Kichuya wa Simba (Septemba), Simon Happygod Msuva wa Yanga (Oktoba), na Rifati Hamisi wa Ndanda (Novemba).

Tuesday, January 17, 2017

YANGA YAIKARIBIA SIMBA, YAITUNGUA MAJIMAJI BAO 1-0


MABINGWA watetezi Yanga, leo wameichapa Majimaji bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga iwe nyuma ya vinara Simba kwa tofauti ya pointi moja. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 44, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 43.

Kiungo Deus Kaseke ndiye aliyeiwezesha Yanga kutoka uwanjani na pointi zote tatu, baada ya kuifungia bao hilo la pekee dakika ya 14, baada ya kipa Agathon Athony kupangua vibaya krosi iliyopigwa na Haruna Niyonzima.

Ligi Kuu itaendelea tena kesho kwa michezo miwili, Simba wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Azam FC wakiwa wenyeji wa Mbeya City, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Sunday, January 15, 2017

AMINA KUAGWA KIPUNGUNI KESHO, KUZIKWA KESHOKUTWA TANGA


MWILI wa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL), inayochapisha magazeti ya Uhuru, Uhuru Wikiendi, Burudani na Mzalendo, Amina Athumani (30), unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo asubuhi kwa boti kutoka Zanzibar.

Msemaji wa familia ya marehemu, Athumani Kazukamwe, alisema mjini Dar es Salaam, jana jioni kuwa, mwili wa Amina utasafirishwa kwa boti kutoka Zanzibar saa moja asubuhi na unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kati ya saa tatu na saa nne asubuhi.

Kazukamwe, ambaye ni baba mkubwa wa mume wa marehemu, alisema mazishi ya Amina, yamepangwa kufanyika kesho katika makaburi ya Soni, nje kidogo ya mji wa Tanga.

Alisema awali, upande wa mume wa marehemu ulitaka mazishi hayo yafanyike leo Dar es Salaam, lakini baada ya majadiliano na familia ya marehemu, walikubaliana mazishi yafanyike Tanga.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa familia ya marehemu, taratibu za kuuaga mwili wa Amina zitafanyika papo hapo bandarini na mara baada ya kumalizika, utasafirishwa kwa basi maalumu la kukodi kupelekwa Tanga.

Amina, mwandishi wa habari za michezo katika magazeti hayo, alifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, alikokuwa amelazwa.

Alilazwa kwenye hospitali hiyo baada ya kuzidiwa kutokana na kushikwa uchungu, ambapo alijifungua mtoto wa kiume, lakini kwa bahati mbaya alifariki.

Baada ya mtoto kufariki, Amina aliendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomkuta jana asubuhi.

Marehemu Amina alikwenda Zanzibar kikazi kwa ajili ya kuripoti mashindano ya Kombe la Mapinduzi, yaliyomalizika Ijumaa iliyopita na ilikuwa arejee Dar es Salaam jana.

Akizungumzia kifo hicho cha Amina, Kaimu Mhariri Mtendaji wa UPL, Ramadhani Mkoma, alithibitisha mazishi ya marehemu Amina kufanyika kesho Tanga.

Ramadhani alisema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwa sababu hawakutarajia iwapo Amina angetangulia mbele ya haki katika umri mdogo.

Alisema Amina ameacha pengo kubwa kwa sababu alikuwa mmoja wa wanahabari wa UPL waliokuwa wakifanyakazi kwa kujituma, aliipenda kazi yake na ilikuwa mwiko kwake kusukumwa kutimiza wajibu wake.

Alisema kazi aliyoifanya wakati wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo alitumwa kuandika habari zake akiwa Unguja, ni uthibitisha wa wazi wa utendaji mzuri aliokuwa nao.

Alisema hawana la kufanya isipokuwa kumshukuru Mungu kwa kuwa kila alipangalo, hakuna anayeweza kulipangua. Amewataka wafanyakazi wa UPL kumuenzi Amina kwa kuiga utendaji wake wa kazi.

Baadhi ya wafanyakazi wa UPL, wamekielezea kifo hicho cha Amina kuwa ni pengo kubwa, kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kuandika habari na makala zinazohusu michezo.

HATMA YA SERENGETI BOYS KUCHEZA FAINALI ZA AFRIKA KUJULIKANA NDANI YA SIKU 10, TENGA ATEULIWA KUWANIA UJUMBE FIFA



Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), limetoa nafasi ya mwisho kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT) kumpeleka mchezaji Langa Lesse Bercy jijini Libreville, Gabon kwa ajili ya kipimo kipya cha MRI ili kutambua umri wake.

CAF limetaka FECOFOOT kumpeleka mchezaji huyo huko Libreville, Gabon ndani ya siku 10 zijazo kuanzia jana Januari 12, 2017.

CAF limepata kumwita mchezaji huyo mara mbili mwaka jana, na FECOFOOT imeshindwa kumpeleka kwa sababu mbalimbali wanazozijua FECOFOOT.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, vijana waliohitajika kucheza ni wale wenye umri wa chini ya miaka 17.

Langa Lesse Bercy, amelalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwamba amezidi umri hivyo kuhitajika kumpeleka kwani hakustahili kucheza hatua ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.

Fainali za vijana zinatarajiwa kufanyika katika nchi nyingine itakayotangazwa hapo baadaye baada ya Madagascar kuondolewa kuandaa fainali hizo baada ya kubainika kutokamilisha baadhi ya taratibu.

Hii inatokana na ripoti ambayo CAF wameipata kutoka kwa wakaguzi wa maandalizi ya fainali hizo. CAF imefungua kandarasi ya kwa nchi wanachama wengine kuandaa fainali hizo. Mwisho wa kupokea maombi ni Januari 30, mwaka huu.

Kadhalika Kamati ya Utendaji ya CAF, imemteua Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Chilla Tenga kuwania nafasi ya uwakilishi katika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Katika nafasi hiyo kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Tenga atachuana na Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa Ghana.

Wengine waliopitishwa kuwania nafasi ya uwakilishi katika Kamati ya Utendaji ya FIFA kutoka nchi za Afrika ni Tarek Bouchamaoui wa Tunisia ambaye anaingia kwenye kundi la nchi zinazozungumza lugha za Kiarabu, Kireno na Kihispaniola.

Kwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa wamo Constant Omari Selemani wa DR Congo na Augustin Sidy Diallo wa Cote d’Ivoire wakati nafasi nyingine za wazi ihuhusisha mwanamke mmoja, wamo Almamy Kabele Camara (Guinea), Chabur Goc (South Sudan), Danny Jordaan (Afrika Kusini), Hani Abo Rida (Misri) na Lydia Nsekera (Burundi).

MALINZI AMPONGEZA MKURUGENZI MPYA IDARA YA MICHEZO


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Malinzi amempongeza Bw. Yusuph Singo Omari kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Tanzania.

Mapema wiki hii, Yusuph Singo Omari, aliteuliwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye kushika wadhifa huo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Leonard Thadeo aliyehamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Kabla ya uteuzi huo uliofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 kifungu namba 6, kifungu (1) (b) kikisomwa pamoja na kifungu namba 8 cha sheria hiyo, Bw. Yusuph Singo Omari alikuwa Mkufunzi Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Ardhi katika masuala ya Michezo.

Katika pongezi zake, Rais Malinzi amepokea wito wa Waziri Nape Nnauye kumpa ushirikiano wa kutosha kwa Yusuph Singo Omari atakapokuwa anatekeleza majukumu yake.

“Sisi wa TFF tunakupongeza kwa nafasi hiyo, tunachukua nafasi hii kukuahidi kukupa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yako mapya. Hii ni kuitikia wito wa Waziri Nape ambaye aliomba wanafamilia yote ya michezo kukupa ushirikiano,” alisema Malinzi alipozungumza na mtandao wa www.tff.or.tz.

Rais Malinzi alisema kwamba program za TFF kwa sasa kwa timu zake zote za taifa, hazina budi kuungwa mkono na Serikali ili kufanikisha na kiungo mkubwa katika eneo hilo ni Bw. Yusuph Singo Omari ambaye ndiye mkuu wa Idara ya Maendeleo ya michezo – mpira wa miguu ukiwa ni miongoni mwa michezo hiyo.

LIGI KUU YA TANZANIA BARA KUENDELEA TENA LEO



LIGI Kuu ya Tanzania Bara inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja ambapo Mbao itakuwa mwenyeji wa African Lyon ya Mwanza katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kadhalika Jumatatu Januari 16, 2017 kutakuwa na mchezo mmoja tu ambako Tanzania Prisons itakuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mechi nyingine itakuwa Jumanne Januari 17, 2017 – ambako Majimaji itawaalika mabingwa watetezi wa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Young Africans ya Dar es Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Kadhalika mechi nyingine ziliopangiwa tarehe na muda ni kati ya Mtibwa Sugar itakayocheza na Simba, Jumatano Januari 18, 2017 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.

Mchezo huu wa Azam na Mbeya City utaanza saa 1.00 usiku wakati michezo yote tajwa hapo juu itaanza saa 10.00 jioni lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi nyingi kupitia Kituo cha Televisheni cha Azam - Wadhamini wenza wa ligi hiyo.

Ligi hiyo ambayo pia inabarikiwa na Benki ya Diamond Trust (DTB), Mdhamini Mkuu ni Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom iliyokuza ubora wa huduma zake hapa nchini katika mawasiliano ya kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi wa maneno na intaneti yenye kasi.

AZAM YALETA KOCHA MPYA KUTOKA ROMANIA




KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, mchana huu imemtangaza, Aristica Cioaba, kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho.

Cioaba, 45, anakuja Azam FC kurithi mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.

Kocha huyo atasaidiana na makocha wazawa, Idd Nassor Cheche na Kocha wa Makipa Idd Abubakar, walioiongoza timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo saa 10.15 jioni ya leo itasaka fainali kwa kukipiga na Taifa ya Jang’ombe.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba, tayari wamefanikiwa kumpata kocha huyo na wameingia naye mkataba wa muda wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezwa.

Alisema Cioaba ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika na ataiongoza Azam FC kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa mwa msimu, ambapo baada ya kuisha watakaa tena mezani kufanya tathimini ya mafanikio yake na wapi wanaweza kuendelea kutokana na kazi iliyofanyika.

“Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC inapenda wadau wote wa mpira na wapenzi na mashabiki wa Azam kwamba klabu imempata mwalimu, ambaye ndiye ataiongoza klabu kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa msimu.

“Kwa hiyo kwa mashabiki wetu maana yake ni kwamba tukiingia kwenye mechi inayofuata ya ligi, kocha atakuwa ameanza kazi na Cheche (Idd Nassor) atakuwa msaidizi wake na benchi lake zima alilokuwa nalo hivi sasa litaendelea,” alisema.

Kawemba aliongeza kuwa hivi sasa kocha huyo atakuwa na kikosi visiwani Zanzibar kufuatilia mwenendo wa timu ulivyo na ataendelea kutoa ushauri panapohitajika na ataanza rasmi kukaa kwenye benchi mpaka pale vibali vyake vya kufanya kazi nchini vitakapokamilika.

“Taratibu hizo zitakwenda kwa mujibu wa sheria za nchi, ambapo tutaziheshimu na kuona ya kwamba tutazifanya kwa haraka zaidi ili mwalimu aweze kupata kibali cha kufanya kazi hapa nchini, kwa hayo machache tunawaomba mashabiki wetu wawe watulivu wampe sapoti kocha na wadau wote wa mpira waone ya kwamba tumefanya jambo la kheri,” alisema.

Kauli ya kwanza ya Cioaba

Kwa upande wake Cioaba, alisema kuwa anafuraha kubwa leo hii kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo huku akiahidi kazi nzuri na kuifanya timu hiyo kuwa bora.

“Najua Azam FC hapa Tanzania ni moja ya timu kubwa yenye historia huko nyuma, napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuja kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri.

“Kuhusu wakati ujao, nina furaha sana kuhusu uongozi walipoongea na mimi wakati tunaweka mipango ya timu ya hapo baadaye na hili ni jambo zuri kwa kocha, kitaaluma nawaahidi mashabiki na watu wote wanaoipenda Azam FC, niko hapa kuwapa mambo mazuri katika kazi yangu kwenye klabu,” alisema.

Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana, ambapo anafahamiana kwa ukaribu na nyota wawili wa Azam FC, Yakubu Mohammed na Yahaya Mohammed, waliosajiliwa kutoka timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo.

Mbali na kufundisha soka nchini Ghana pia amewahi kufanya kazi kwenye miamba ya Morocco, Raja Casablanca, Al Masry ya Misri na katika nchi za Romania, Kuwait, Oman na Jordan.

AZAM YAIFUNGA SIMBA 1-0 NA KUTWAA KOMBE LA MAPINDUZI





Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kombe la Mapinduzi 2017, Nahodha wa Timu ya Azam John Bocco, baada ya timu hiyo kuibuka bingwa wa kombea hilo, kufuatia kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Mjini Unguja, jana usiku

Mshambuliaji wa Azam Joseph Mahundi akiumiliki mpira, dhidi ya mchezaji wa Simba Besela Bakungu timu hizo zilipomenyana jana usiku katika mchezo wa fainali ya Mapinduzi Cup 2017,  kwenye Uwanja wa Aamaan mjini Zanzibar. Azam ilibuka kidedea baada ya kuifunga Simba 1-0.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na wachezaji wa Simba

Dk. Shein akisalimiana na wachezaji wa Azam

Dk. Shein akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Azam

Dk. Shein akiwa katika picha ya pamoja na waamuzi waliochezesha mechi ya fainali
Dk. Shein akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Simba


 

Sunday, January 8, 2017

IDDI CHECHE AIONGOZA AZAM KUIPIGA YANGA MABAO 4-0




AZAM imemaliza kileleni mwa Kundi B Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Yanga mabao 4-0 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
 

Matokeo hayo yanazifanya timu zote zimalize na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na sare moja, lakini Azam wanakuwa juu ya Yanga kwa wastani wa mabao.
 

Sasa Azam itacheza na mshindi wa pili wa Kundi B katika Nusu Fainali, wakati Yanga itacheza na mshindi wa kwanza wa kundi hilo.

Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na nahodha wake, John Raphael Bocco, maarufu kama Adebayor kwa jina la utani akifananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Manchester City, Tottenham Hotspur za England na Togo, Emmanuel Adebayor.
 

Bocco alifunga bao hilo dakika ya pili tu kwa shuti kali baada ya kuukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya shuti kali pia la kiungo Joseph Maundi.  
 

Baada ya bao hilo, Yanga walijaribu kufunguka kwa kuongeza mashambulizi, lakini leo safu ya ulinzi ya Azam ilikuwa madhubuti mno.
 

Iliweza kuokoa mipira yote ya kutokea pembeni ya Yanga na hivyo kumnyima mwanya kabisa mshambuliaji hatari wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe.
 

Katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, Yanga haikuwa na shambulizi la kutisha langoni mwa Azam, zaidi ya krosi na kona za kawaida mno, ambazo ziliokolewa kwa urahisi.
 

Lakini Bocco angeweza kufunga mabao matatu kama angetumia nafasi nyingine mbili nzuri na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alikosa bao la wazi pia baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga hadi kwenye sita na kupiga pembeni.  
 

Kipindi cha pili nyota ya Azam iliendelea kung’ara na kufanikiwa kuvuna mabao matatu zaidi.

Mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed alifunga bao la pili dakika ya 54 kwa kichwa akimzidi maarifa beki Andrew Vincent ‘Dante’ baada ya krosi ya Sure Boy.


Mahundi akafunga bao zuri zaidi kwenye mchezo huo dakika ya 80 kwa shuti la umbali wa mita zaidi ya 20 kuipatia Azam bao la tatu baada ya pasi ya Sure Boy.


Winga Mghana, Enock Atta Agyei aliyetokea benchi kipindi cha pili, akaifungia Azam bao la nne dakika ya 85 akimchambua vizuri kipa Dida baada ya pasi ya Samuel Afful aliyeingia kipindi cha pili pia.


Kwa ujumla leo Yanga ilicheza ovyo mno na Azam ingeweza kupata ushindi wa kihistoria kama ingetumia nafasi zaidi ilizotengeneza. 

Thursday, January 5, 2017

YANGA YAZIDI KUTAKATA KOMBE LA MAPINDUZI


YANGA jana iliendelea kung'ara katika michuano ya soka ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Zimanimoto ya Zanzibar mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Yanga na uliiwezesha kuongoza kundi B ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Azam. Timu hizo mbili zinatofautiana kwa mabao ya kufunga.

Mshambuliaji Simon Msuva aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao yote mawili na kuiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza robo fainali.

Alifunga bao la kwanza dakika ya 11 baada ya kumvisha kanzu kipa Mwinyi Hamisi wa Zimamoto. Awali, alipokea pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Msuva aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 21 baada ya kuwatoka mabeki wa Zimamoto na kumpiga chenga kipa Hamisi wa Zimamoto.


Wednesday, January 4, 2017

SIMBA YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI


SIMBA jana ilikuwa timu ya kwanza kupata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa KVZ bao 1-0.

Katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Simba ilijipatia bao hilo la pekee kipindi cha kwanza kupitia kwa Muzamil Yassin.

Muzamil alifunga bao hilo dakika ya 43 baada ya washambuliaji wa Simba kufanikiwa kutegua mtego  wa kuotea uliotegwa na mabeki wa KVZ.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa inazo pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikiwa inaongoza kundi hilo.

Pambano hilo lilitawaliwa na ufundi mkubwa huku KVZ ikifanikiwa kuwabana washambuliaji wa Simba kwa kutumia mtego wa kuotea.

Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Simba. Katika mechi yake ya kwanza, iliichapa Taifa Jang'ombe mabao 2-1.

Katika mechi ya awali ya kundi hilo iliyochezwa jioni, Jang'ombe Boys iliwalaza mabingwa watetezi URA ya Uganda mabao 2-1.
 
Michuano hiyo inaendelea tena leo kwa mechi za Kundi B, kati ya Zimamoto na Yanga kuanzia saa 10:00 jioni na Jamhuri dhidi ya Azam kuanzia saa 2:30 usiku.

RAUNDI YA PILI LIGI YA SOKA YA WANAWAKE KUENDELEA LEO


Duru la Pili la Ligi Kuu soka ya Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajiwa kuanza kesho Jumatano Januari 4, 2017 kwa michezo minne itakayofanyika kwenye viwanja mbalimbali.

Kwa mujibu wa ratiba, katika kundi ‘A’ pekee litakuwa na mchezo mmoja wakati kundi ‘B’ litakuwa na michezo mitatu kwa siku ya kesho Jumatano.

Mchezo pekee wa kesho wa kundi ‘A’ utakuwa kati ya Mburahati Queens ya Kinondoni, Dar es Salaam na Viva Queens ya Mtwara – mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume jijini katika mzunguko wa sita wa ligi hiyo.

Michezo mingine mitatu itakuwa ni ya Kundi B ambako Mejengo FC itacheza na Marsh Academy ya Mwanza kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati Panama ya Iringa inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Sisterz ya Kigoma kwenye Uwanja wa Samora huku Victoria Queens ikiikaribisha Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.

Kabla ya michezo ya juma lijalo, upande wa Kundi A michezo yake miwili ya mzunguko wa sita itafanyika Alhamisi Januari 5, mwaka huu ambako Evergreen ya Temeke, Dar es Salaam itacheza na Fair Play ya Tanga kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mlandizi ya Pwani inatarajiwa kuikaribisha JKT Queens ya Dar es Salaam, katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mabatini.

Tuesday, January 3, 2017

YANGA YAVUNA KAPU LA MAGOLI KWA JAMHURI KOMBE LA MAPINDUZI


YANGA jana ilianza michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kishindo baada ya kuicharaza Jamhuri ya Pemba mabao 6-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inaongoza kundi B kwa tofauti ya mabao ya kufunga kati yake na Azam, ambayo mapema jioni, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zimanimoto.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande mmoja, Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0. Wafungaji wa mabao hayo walikuwa Simon Msuva na Donaldo Ngoma, waliofunga mawili kila mmoja.

Bao la tano la Yanga lilifungwa na Thabani Kamusoko kabla ya Juma Mahadhi kuhitimisha karamu ya magoli kwa kufunga bao la sita.

TFF YAVUNJA MKATABA WA MKWASA KUINOA TAIFA STARS, YAKABIDHI MIKOBA KWA MAYANGA


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuvunja rasmi mkataba wa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, amesema leo kuwa, mkataba huo ulivunjwa rasmi jana, baada ya kufanyika kwa kikao kati ya uongozi wa shirikisho hilo na kocha huyo.

Kwa mujibu wa Lucas, mkataba wa Mkwasa ulitarajiwa kumalizika Machi, mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kocha huyo, Lucas alisema anachofahamu ni kwamba alishalipwa madai yake yote ya mishahara na kwamba, kilichobaki ni malipo ya miezi mitatu.

Akizungumzia uamuzi huo wa TFF, Boniface alithibitisha kufanyika kwa mazungumzo kati yake na shirikisho hilo kuhusu kukatisha mkataba wake.

Alisema katika mazungumzo hayo, TFF imekubali kumlipa mishahara yake iliyobaki ya miezi mitatu kwa awamu mbili tofauti.

Boniface alisema awamu ya kwanza atalipwa mwishoni mwa mwezi huu na awamu ya pili atalipwa mwezi ujao.

Kocha huyo alisema pia kuwa, alikubaliana na TFF kuhusu kupunguzwa kwa malipo ya mshahara wake wa kila mwezi kutokana na shirikisho hilo kutokuwa na uwezo kifedha.

"Katika mazungumzo yangu na TFF, waliniomba kupunguza kiwango cha malipo ya mshahara wangu wa kila mwezi kwa vile hawana uwezo kifedha. Nami kwa sababu ya kutambua ukweli huo na pia uzalendo wangu kwa taifa, nilikubaliana nao kuhusu uamuzi huo,"alisema.

Awali, Mkwasa alitakiwa kulipwa zaidi ya sh. milioni 30,kwa mwezi, kama alivyokuwa akilipwa kocha wa zamani. Hata hivyo, Mkwasa hakuwa tayari kuweka wazi kuhusu kiwango kilichopunguzwa.

Wakati huo huo, TFF  imemteua Salum Mayanga kuwa kocha wa muda  (Interim coach), wa Taifa Stars.

Mayanga anachukua nafasi ya Mkwasa, ambaye mkataba wake unafikia mwisho Machi, mwaka huu.

Kati ya majukumu yake yatakuwa ni kuandaa kikosi cha timu ya Taifa kwa ajili ya hatua ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019, ambazo mechi za awali zitanza mapema mwaka huu.

Pia, Mayanga atakuwa na jukumu la kuandaa kikosi cha wachezaji wa ndani kwa ajili ya hatua ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani (CHAN).

TFF inamshukuru Mkwasa kwa utumishi katika nafasi hiyo ulioanza Julai, 2015 na kumtakia mafanikio katika mipango yake inayofuata.

Monday, January 2, 2017

SIMBA YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI


TIMU kongwe ya soka ya Simba, juzi ilianza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Taifa Jang'ombe bao 2-1 katika mechi ya kundi A iliyochezwa usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mechi  hiyo iliyokuwa kali na ya kusisimua, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0. Mabao hayo yalifungwa na Muzamil Yassin na Juma Luizio.

Iliwachukua Simba dakika 27 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Muzamil baada ya kuuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi uwanjani, kufuatia shuti la Method Mwanjali.

Luizio aliiongezea Simba bao la pili dakika chache baadaye kwa shuti kali baada ya kuwatoka mabeki wa Taifa Jang'ombe.

Taifa ilipata bao la kujifariji dakika ya 76 baada ya beki Novaty Lufunga wa Simba kujifunga, alipokuwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Hassan Bakari.

Katika mchezo wa awali, URA ya Uganda iliibuka na ushindi  wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ.

Kwa matokeo hayo, Simba inalingana kwa pointi na URA na Taifa, ambayo katika mechi ya ufunguzi iliichapa Jang'ombe Boys bao 1-0.