KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 11, 2015

STARS MABORESHO KUKIPIGA NA RWANDA JAN 22 MWANZA


Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kitacheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mechi hiyo ni sehemu ya programu ya Kocha Mart Nooij kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya mechi za mchujo michuano ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN). Mechi za mchujo za michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Rwanda zinaanza Mei mwaka huu.

Kocha Nooij anatarajia wakati wowote kutangaza kikosi cha timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ambacho kitakusanyika Januari 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam, na siku moja baadaye kwenda jijini Mwanza.

TAIFA CUP WANAWAKE KUPIGWA JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya kwanza za mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa kesho (Januari 10 mwaka huu) kwenye miji 11 tofauti nchini.

Katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin, Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora itacheza na Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simiyu na Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha na Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro na Tanga (Uwanja wa Ushirika).

Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma na Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya na Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi na Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma na Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.

Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwaka huu, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.

Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwaka huu.

Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

No comments:

Post a Comment