KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 15, 2015

NOOIJ KUTAJA KIKOSI CHA TAIFA STARS MABORESHO



Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij anatarajia kutaja kikosi cha Maboresho kitakachoingia kambini Januari 18 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu jijini Mwanza.

Nooij atataja kikosi hicho kwenye mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Januari 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume.


RAUNDI YA PILI TAIFA CUP WANAWAKE JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya pili ya mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa wikiendi hii (Januari 17 mwaka huu) kwenye miji minane tofauti nchini.

Timu tisa zilizofuzu kutoka raundi ya kwanza baada ya mechi za nyumbani na ugenini akiwemo mshindwa bora (best loser) zitaungana na Ilala, Kinondoni na Temeke kucheza raundi ya pili. Mechi za marudiano za raundi hiyo zitachezwa Januari 21 mwaka huu.

Hatua ya robo fainali itakayochezwa Januari 26 na 27 mwaka huu pamoja na nusu fainali na fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Proin Promotions itafanyikia jijini Dar es Salaam.

RAMBIRAMBI MSIBA WA STEPHEN NSOLO

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) uliotokea jana (Januari 13 mwaka huu) jijini Mwanza.

Msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Nsolo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Aliongoza SHIREFA akiwa Katibu kuanzia mwaka 1975 hadi 1994.

Kabla ya hapo alikuwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga kwa kipindi cha miaka kumi. Pia aliwahi kuwa mwamuzi wa daraja la kwanza na kamishna wa mpira wa miguu kwa muda mrefu.

TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, SHIREFA na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Januari 14 mwaka huu) katika makaburi ya Shinyanga Mjini. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

No comments:

Post a Comment