KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 20, 2015

WACHEZAJI, VIONGOZI 12 KUHUKUMIWA NA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake.

Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.

Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.

Kwa upande wake, Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.

Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.

Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

SDL KUANZA MZUNGUKO WA PILI JANUARI 31
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) sasa utaanza Januari 31 mwaka huu, badala ya Januari 24 mwaka huu kama ilivyopangwa awali ili kutoa fursa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia usajili wa dirisha dogo.

Timu zinazocheza ligi hiyo katika makundi manne tofauti ni; Milambo FC, Mji Mkuu FC (CDA), Mvuvumwa FC, Singida United, na Ujenzi Rukwa (Kundi A), Arusha FC, Bulyanhulu FC, JKT Rwamkoma FC, Mbao FC, na Pamba SC (Kundi B).

Nyingine ni Abajalo FC, Cosmopolitan, Kariakoo Lindi, Kiluvya United, Mshikamano FC, na Transit Camp (Kundi C), wakati Kundi D ni Magereza Iringa, Mji Njombe, Mkamba Rangers, Town Small Boys, Volcano FC, na Wenda FC.

No comments:

Post a Comment