KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 15, 2014

PHIRI AMWAGA WINO SIMBA MWAKA MMOJA, KIKOSI CHAPELEKWA MAFICHONI ZANZIBAR


KOCHA Mkuu mpya wa Simba, Patrick Phiri kutoka Zambia (kulia) akibadilishana hati za mkataba wake na Rais wa Simba, Evance Aveva katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Regency mjini Dar es Salaam jana. Phiri ametia saini mkataba wa kuifundisha Simba kwa mwaka mmoja. (Picha kwa hisani ya Blogu ya BINZUBEIRY)

KIKOSI cha Simba kinaondoka mjini Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, kikosi hicho kitakwenda Zanzibar kikiwa chini ya kocha wake mpya, Patrick Phiri na kitarejea Dar es Salaam siku chache kabla ya kuanza kwa ligi.

Ratiba ya ligi kuu inaonyesha kuwa, michuano hiyo imepangwa kuanza Septemba 20 mwaka huu, ikitanguliwa na mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kati ya mabingwa Azam na washindi wa pili, Yanga.

Mmoja wa viongozi wa kamati ya utendaji ya Simba, alisema jana kuwa tayari klabu hiyo imeshakamilisha usajili wa wachezaji wake, wakiwemo watano kutoka nje ya nchi.

Phiri amerejea nchini kurithi mikoba ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Zdravko Logarusic, ambaye mkataba wake ulivunjwa wiki iliyopita kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Hadi sasa mkataba wa Phiri umefanywa kuwa siri, lakini kuna habari kuwa kocha huyo atakuwa akilipwa zaidi ya dola 5,000 za Marekani kwa mwezi, kiwango ambacho alikuwa akilipwa kwa mara ya mwisho alipokuwa akiifundisha timu hiyo miaka minne iliyopita.

Phiri aliwahi kufanyakazi kwa awamu tatu tofauti kuanzia 2004 hadi 2010, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kutwaa mataji mawili ya ligi kuu na Kombe la Tusker. Kocha huyo ndiye aliyeiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2009/2010 bila kupoteza mechi.

No comments:

Post a Comment