KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, August 19, 2014

OKWI BYE BYE YANGA, KIKOSI CHATUA PEMBA



KLABU ya Yanga imeondoka mjini Dar es Salaam jana kwenda Pemba kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Yanga imekwenda Pemba bila ya mshambuliaji wake nyota, Emmanuel Okwi kutoka Uganda, ambaye ameshindwa kuripoti kambini kwa wakati uliopangwa.

Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema jana kuwa, kikosi hicho kimekwenda Pemba kikiwa na msafara wa watu 35.

Njovu alisema kwa sasa wameamua kuachana na Okwi na kwamba hawatakuwa na muda tena wa kumjadili mshambuliaji huyo.

Kiongozi huyo wa Yanga alisema, klabu yake imeamua kuelekeza nguvu zaidi katika ligi kuu, inayotarajiwa kuanza Septemba 20 mwaka huu.

Alisema benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Marcio Maximo, litaendelea kutoa mafunzo kwa wachezaji waliokwenda Pemba.

"Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia suala la Okwi, muda ukifika, tutaweka bayana, tumeamua kujikita zaidi kwenye mazoezi,"alisema Njovu.

Awali, Maximo alikaririwa akisema kuwa, atatoa kipaumbele kwa wachezaji waliofanya mazoezi ya pamoja kwa takriban miezi miwili na kwamba mchezaji, ambaye hayupo, hatakuwa na chake.

Okwi ndiye mchezaji pekee,ambaye hajaripoti kambini hadi sasa tangu alipokwenda kuichezea Uganda katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Yanga inatakiwa kukata jina la mchezaji mmoja wa kigeni kati ya sita ilionao kama sheria za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinavyotaka.

Wachezaji wa kimataifa waliopo Yanga ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima (Rwanda), Hamisi Kiiza (Uganda), Genilson Santos 'Jaja' na Andrey Coutinho (Brazil).

Kwa mujibu wa Njovu, Yanga inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki, moja dhidi ya Chipukizi ya Pemba na nyingine dhidi ya timu kutoka nje ya nchi.

Njovu alisema kikosi cha Yanga kitakuwa kikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gombani ulioko Pemba, ambao umewekewa nyasi za bandia.

Yanga inatarajia kukata utepe wa ligi kuu kwa kumenyana na mabingwa watetezi, Azam katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, itakayopigwa Septemba 13 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment