KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 4, 2014

TAIFA STARS YATUPWA NJE NA MSUMBIJI KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA


Na Boniface Wambura, MAPUTO


KOCHA wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema kwamba refa Mganda, Dennis Batte alikataa bao halali lililofungwa na John Bocco ‘Adebayor’ jana katika mchezo dhidi ya wenyeji Msumbiji, Uwanja wa Zimpeto mjini hapa.

Akizungumza baada ya mchezo huo ulioisha kwa Mambas kushinda 2-1 jana, Mholanzi huyo alilalamikia bao ambalo Taifa Stars ilifunga dakika ya 17 kupitia kwa Said Murad, lakini likakataliwa na mwamuzi Dennis Bate kutoka Uganda.

Aidha, Nooij amesema moja ya sababu za kikosi chake kupoteza mechi dhidi ya Mambas jana ni wachezaji wake kucheza kwa wasiwasi katika kipindi cha kwanza.

Taifa Stars iliruhusu bao la kwanza sekunde chache kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya makundi iliyochezwa leo (Agosti 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto hapa Maputo.

Bao hilo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3 lilifungwa kwa kichwa na mshambuliaji Josemar Machaisse.

Nooij alisema wasiwasi katika kipindi cha kwanza ndio ulioipa Msumbiji fursa ya kutawala mechi hiyo katika kipindi hicho na kukimalizia ikiwa mbele kwa bao hilo la mshambuliaji huyo wa klabu ya Bravos de Maquis ya Angola.

Alisema timu yake ilitulia kipindi cha pili baada ya kumuingiza Amri Kiemba badala ya Khamis Mcha.

Aliongeza kuwa mchezaji Elias Pelembe aliyeifungia Msumbiji bao la pili dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu nje ya eneo la hatari ndiye aliyemaliza mchezo huo.

Pia ni mchezaji huyo aliyebadili matokeo ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ambapo Msumbiji ilisawazisha dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na ambayo ilicheza vizuri kipindi cha pili ilipata bao lake dakika ya 78 na Mbwana Samata kwa shuti la pembeni akiwa nje ya eneo la hatari na kumshinda kipa Dario Khan.

Matokeo hayo yameipeleka Msumbiji katika kundi C lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Mechi za hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco zitaanza kuchezwa mwezi ujao.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Taifa Stars inarejea Dar es Salaam leo (Agosti 4 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Air Tanzania.

No comments:

Post a Comment