KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 11, 2014

LOGA ATUPIWA VIRAGO SIMBA, AMWITA AVEVA MBABAISHAJI



SIKU moja baada ya Simba kumtimua, kocha wa zamani wa timu hiyo, Zdravko Logarusic, ameibuka na kudai kuwa viongozi wa klabu hiyo ni wababaishaji.

Logarusic, raia wa Croatia alisema Simba imemfanyia mchezo mchafu kwa kumfukuza katika mazingira ya kutatanisha.

Kauli ya 'Loga' imekuja muda mfupi baada ya Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, kutangaza juzi Dar es Salaam kumtimua kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Logarusic, alisema alifahamu Simba itamfukuza kazi muda si mrefu kwa kuwa haikuwa ikimuhitaji.

Logarusic alisema alianza kutofautiana na uongozi, baada ya kukataa kufuata baadhi ya mambo ambayo walitaka afanye kinyume na utaratibu wake wa kazi.

Kocha huyo alisema baada ya msuguano huo, aliamua kufuata walichokuwa wakitaka na hatua ilichangia kutimiza malengo.

Alisema amekuwa na msuguano wa chini kwa chini na uongozi tangu ulipoingia madarakani naalitarajia asingeweza kufanya nao kazi.

Alisema amefukuzwa kazi kihuni bila kufuata utaratibu na waliamua kumpa mkataba mbovu usiokuwa na tija kwa upande wake ili wamdhulumu haki zake.

"Mwezi mmoja uliopita walinipa mkataba uliosema yeyote atakayevunja atamlipa mwenzake mshahara wa mwezi mmoja lakini mkataba huo nilijua siwezi kuutumikia," alisema Logarusic.

Alisema licha ya kufukuzwa hana hofu kwa kuwa anaamini ni kocha bora ambaye anayejua vyema misingi ya kazi yake, hivyo atapata kibarua kingine na maisha yataendelea.

Logarusic alisema anasubiri alipwe haki yake na kupata tiketi ili aondoke nchini kwenda kutafuta kibarua sehemu nyingine.

Hata hivyo alisema huenda akarejea nchini Kenya kuinoa Gor Mahia ambayo imemuita kwa mazungumzo ya kupewa kazi. Kochwa Gor Mahia Bobby Williamson ameteuliwa kuinoa timu ya taifa 'Harambee Stars'.

Awali, Aveva alisema kocha huyo amekuwa akionywa mara kwa mara lakini amekuwa mkaidi na kushindwa kujirekebisha jambo ambalo uongozi umeshindwa kuivumilia.

Kocha huyo alitwaa mikoba ya Abdallah 'King' Kibadeni, aliyetimuliwa muda mfupi kabla ya ligi hiyo kumalizika msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment