KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 14, 2013

MBAGA, MSAIDIZI WAKE WAIBEBA AZAM KWA BAO LA MKONO, CHIPUKIZI WA SIMBA USIPIME



MWAMUZI Oden Mbaga leo alionekana dhahiri kuibeba Azam baada ya kuruhusu bao lake la kusawazisha lililofungwa na Humphrey Mieno baada ya kuushika mpira kwa mkono kwa makusudi.

Mieno alifunga bao hilo katika kipindi cha pili baada ya mpira wa krosi uliopigwa na Khamis Mcha kutoka pembeni kidogo ya uwanja.

Awali, mwamuzi msaidizi namba mbili alinyoosha kibendera hewani kuashiria kwamba kuna mashambi yalitendeka, lakini baada ya kumuona Mbaga akielekea kati, aliamua kukishusha mara moja na kuungana naye.

Kipa Abbel Dhaira wa Simba hakuwa amefanya jitihada yoyote ya kuokoa mpira uliopigwa na Mieno kwa sababu aliushika mpira kwa mkono mbele yake na pia alimuona mwamuzi msaidizi akinyoosha kibendera hewani.

Kutokana na utata huo, wachezaji wa Simba walimzonga Mbaga na msaidizi wake, wakilalamikia bao hilo, lakini hakuna aliyebadili msimamo.

Baadhi ya mashabiki waliohudhuria pambano hilo, wamekielezea kitendo hicho cha Mbaga kuwa ni cha fedheha kwa mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), anayetakiwa kuchezesha mechi za michuano ya kimataifa.

Katika pambano hilo, Simba ambayo ilichezesha wachezaji wengi chipukizi, ilionyesha kiwango cha juu na kuwafanya mashabiki wake wawashangilie kwa furaha kubwa. Pia mashabiki wa Yanga leo walikuwa wakiishangilia Simba ili iifunge Azam.

Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 36 wakati Azam ni ya pili ikiwa na pointi 47.

Mshambuliaji Ramadhani Singano aliibuka shujaa wa Simba baada ya kuifungia mabao yote mawili dakika ya 10 na 14 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mrisho Ngasa.

Azam ilipata bao lake la kwanza kwa njia ya penalti kupitia kwa Kipre Tchetche baada ya beki wa pembeni, Miraji Juma kumkwatua ndani ya eneo la hatari kabla ya Mieno kufunga bao la utata.

Simba: Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Haroun Chanongo/Edward Christopher, Abdallah Seseme, William Lucian/Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Singano na Mrisho Ngassa/Fliex Sunzu.

Azam :Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Luckson Kakolaki/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk, Salum Abubakar, John Bocco/Abdi Kassim, Humphrey Mieno/Jabir Aziz na Kipre Tchetche

YANGA YAMTENDEA HAKI MANJI, LEO NI SIMBA NA AZAM



YANGA jana iliendelea kuchanua katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibugiza JKT Oljoro mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo mnono wa Yanga umekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji kukilalamikia kikosi chake kwa kuibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 katika mechi zake zilizopita za ligi hiyo.

Katika kikao chake na wachezaji, Manji alisema anataka kuiona timu yake ikitoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao na kuahidi kuwazawadia sh. milioni 100 iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 52 baada ya kucheza mechi 22, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 46. Azam inatarajiwa kushuka dimbani leo kwenye uwanja huo kumenyana na mabingwa watetezi, Simba.

Katika mechi hiyo, Yanga ilijipatia mabao yake yote matatu kupitia kwa Nadir Haroub 'Cannavaro, Simon Msuva na Hamisi Kiiza.

Cannavaro alifunga bao la kwanza baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la JKT Oljoro, kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima.

Msuva aliongeza bao la pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa David Luhende, akawatoka mabeki kadhaa wa Oljoro kabla ya kufumua shuti kali lililotinga moja kwa moja wavuni.

Bao la tatu lilifungwa na Kiiza baada ya kupokea pasi kutoka kwa Niyonzima na kumpiga chenga kipa wa Oljoro kabla ya kuutumbukiza mpira wavuni.

Saturday, April 13, 2013

AMRI IBRAHIM, MKONGWE WA SOKA ANAYEWASIKITIKIA VIONGOZI WA SASA WA MCHEZO HUO




WIKI iliyopita, mwanasoka mkongwe nchini, Amri Ibrahim alielezea mambo mbalimbali yanayomkera katika uendeshaji wa mchezo huo hivi sasa hapa nchini na kupendekeza hatua mbalimbali zinazofaa kuchukuliwa na kuinua kiwango cha soka. Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, mkongwe huyo anaelezea historia yake na matukio mbalimbali anayoyakumbuka.


Amri alisema kama klabu inaye mfadhili, anapaswa kuheshimu nafasi za viongozi na makocha, vivyo hivyo vongozi, ambao alisema nao wanapaswa kuheshimu nafasi za wafadhili na makocha.

Aliipongeza TFF kwa hatua, ambazo imekuwa ikichukua kukomesha vitendo vya vurugu kwenye viwanja vya soka kwa kuwaadhibu wachezaji, waamuzi na viongozi wanaohusika kuchochea vitendo hivyo.

"Nidhamu ni muhimu sana katika soka, na ilikuwa imeshuka sana katika miaka ya nyuma. Mashabiki walifikia hatua ya kuweka mikojo kwenye chupa za maji na kuwarushi waamuzi na wachezaji uwanjani. Huu ulikuwa uhuni," alisema kiungo huyo wa zamani wa Pamba na Simba.

Aliitaka TFF kuweka wazi programu zake za kuendesha soka nchini ili wadau wa mchezo huo waweze kuzisoma, kuzielewa na kuchangia mawazo yao. Alisema ni vyema programu hizo ziwe zikisambazwa katika vyama vya soka vya wilaya ya mikoa yote nchini.

Amri alizaliwa 1959 kijiji cha Gungu kilichopo Kigoma Mjini. Alisoma elimu ya msingi mkoani Kigoma na katika mikoa ya Mwanza na Mara.

Alianza kucheza soka tangu alipokuwa mdogo kwa kutumia chandimu. Alichezea timu za mitaani na za shule alizosoma kabla ya kujiunga na Gungu Heroes na baadaye Lake Stars.

Alianza kupata umaarufu kisoka 1973 alipokuwa akichezea Lake Stars katika michuano ya kuwania ubingwa wa wilaya na mkoa. Timu hiyo ilifanikiwa kucheza fainali ya ubingwa wa Taifa na kufungwa mabao 2-0 na Simba.

Amri alijiunga na Pamba ya Shinyanga 1975 na kuichezea kwa muda mfupi kabla ya kuhamishiwa Pamba ya Mwanza. Aliichezea Pamba ya Mwanza kwa mara ya kwanza ilipomenyana na Luo Union ya Kenya katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Nyamagana na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mechi hiyo, Amri aliingizwa uwanjani kipindi cha pili na kutoa pasi kwa Ibrahim Posi, aliyefunga bao hilo na pekee na la ushindi kwa kichwa.

Wakati Amri alipojiunga na Pamba ya Mwanza, kikosi cha timu hiyo kilikuwa kinaundwa na baadhi ya wachezaji waliokuwa nyota wakati huo kama vile Joram Mwakatika, Tabu Mwakatika, Titus Bandawe, Khalid Bitebo, Hamisi Bilali, James Ng'ong'a na Makinga Shabani.

Mechi ya pili ya kimataifa kwa Amri kuichezea Pamba ilikuwa dhidi ya Galacia ya Brazil. Mechi hiyo pia ilichezwa kwenye uwanja wa Nyamagana na Pamba ilichapwa mabao 2-1.

Amri amemwelezea mwenyekiti wa zamani wa Pamba, marehemu Shabani Mwakayugwa kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa kuinua maendeleo ya soka mkoani Mwanza kutokana na kuzialika timu mbalimbali za kigeni kucheza na Pamba.

Amri alihamishiwa mkoa wa Mara kikazi 1976, ambako alijiunga na Mara Stars. Timu hiyo ilikuwa ikiongozwa na Suleiman Kigera.

Mwaka uliofuata, alirejeshwa Mwanza na kuitwa katika timu ya Taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikijiandaa kwenda Malawi kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika.

Hata hivyo, Amri hakuweza kusafiri na timu hiyo kwenda Malawi kutokana na kuumia mguu. Alisikitika kwa kupoteza nafasi hiyo, ambayo alisema kwa kawaida huwa ni ndoto ya kila mwanasoka katika maisha yake.

Baada ya kuzidi kung'ara katika kikosi cha Pamba, hatimaye Amri alinaswa na klabu ya Simba 1980. Binafsi anakiri kwamba, alikuwa na mapenzi na klabu hiyo tangu akiwa mdogo, hivyo ilipomuhitaji, hakujiuliza mara mbili.

"Viongozi wa Simba waliniona nina uwezo, maana wakati huo nilikuwa natisha katika namba zote mbili za kiungo na ushambuliaji. Nilikuwa na uwezo wa kucheza namba sita, nane, saba hadi 11,"alisema Amri, ambaye kwa kawaida ni mcheshi.

Mechi ya kwanza kuichezea Simba ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Russia. Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilichapwa mabao 3-2.

Wakati alipojiunga na Simba, kikosi cha timu hiyo kilikuwa kikiundwa na wachezaji tishio kama vile marehemu Jumanne Hassan 'Masimenti', marehemu Adam Sabu, Thuweni Ally, marehemu Athumani Mambosasa, George Kulagwa, Rahim Rumelezi, Nico Njohole, Abbas Kuka.

Amri alikuwa mmoja wa wachezaji walioiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Bra 1984. Alisema katika kipindi cha miaka saba alichoichezea Simba, mwaka huo pekee ndio ambao hakukuwepo migogoro ya uongozi.

"Niliichezea Simba katika kipindi ambacho ilikuwa ikikabiliwa na migogoro mingi. Mgogoro wa kwanza mkubwa ulizuka 1980 wakati huo, mwenyekiti alikuwa, marehemu Alfred Sanga. Baadaye akaingia David Ngonya. Mgogoro mkubwa zaidi ulizuka 1985 na kusababisha timu isambaratike,"alisema.

Anaikumba zaidi mechi ya ligi kati ya Simba na Yana iliyochezwa 1985 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Kinachomfanya aikumbuke mechi hiyo ni wachezaji wa timu zote mbili kucheza kwa kukamiana.

Kwa mujibu wa Amri, katika mechi hiyo, kipa Hamisi Kinye wa Yanga aliwachezea rafu mbaya washambuliaji Zamoyoni Mogella na Zuberi Magowa wa Simba na kuwasababishia maumivu makubwa.

Amri aliwahi kuwa kocha wa timu ya daraja la tatu ya Rhino ya Morogoro, ambayo aliiwezesha kufuzu kucheza ligi daraja la pili ngazi ya kanda.

Hata hivyo, aliamua kuacha kuifundisha timu hiyo kwa kile alichodai kuwa, kukatishwa tamaa na mfumo mpya wa ligi uliotangazwa na TFF, ambapo ligi za soka zitaanza kuchezwa katika ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa.

"Nilikata tamaa. Niliiwezesha Rhino kupanda hadi daraja la pili ngazi ya taifa, lakini baada ya kutangazwa kwa mfumo huo, nimeona jitihada zangu ni sawa na kazi ya bure,"alisema.

"Unajua klabu zetu nyingi ni za mitaani, hazina vyanzo vya uhakika vya mapato, zinategemea michango ya wanachama, sasa sisi tulishalipa ada ya kucheza ligi daraja la pili, leo hii TFF inasema ligi zote zimefutwa. Nani angeturejeshea fedha zetu za ada ya ligi." alihoji.

Monday, April 8, 2013

AZAM, BARRACK ZAINGIZA MIL 44

MECHI ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Barrack Young Controllers II ya Liberia iliyochezwa jana (Aprili 6 mwaka huu) imeingiza sh. 44,229,000.

Fedha hizo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka suluhu zimetokana na watazamaji 17,128 waliokata tiketi.

Viingilio vilikuwa sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A. Kiingilio cha sh. 2,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 15,212.

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za tiketi sh. 5,575,500, asilimia 15 ya uwanja sh. 5,798,025, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 3,865,350 na asilimia 75 iliyokwenda kwa klabu ya Azam ni sh. 28,990,500.

Mechi iliyopita ya raundi ya awali ya mashindano hayo kati ya Azam na El Nasir ya Sudan Kusini iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 16 mwaka huu iliingiza sh. 34,046,000 kwa viingilio hivyo hivyo huku ikishuhudiwa na watazamaji 13,431.

MECHI SITA LIGI KUU KUONYESHWA LIVE SUPERSPORT




Kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini kitaonesha moja kwa moja mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom katika Super Week kati ya Aprili 11 na Mei 18 mwaka huu.

Mechi hizo ni kati Azam na African Lyon itakayochezwa Aprili 11 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Yanga na Oljoro JKT ambayo sasa itachezwa Aprili 13 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam na Simba itakayochezwa Aprili 14 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na mechi kati ya Coastal Union na JKT Ruvu itakayochezwa Aprili 16 mwaka huu badala ya Aprili 10 mwaka huu.

Mechi nyingine ya Super Week itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga itakayofanyika Aprili 17 mwaka huu badala ya Aprili 13 mwaka huu.

Pia mechi nyingine itakayooneshwa live na SuperSport ni kati ya Yanga na Simba itakayofanyika Mei 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na mechi za Super Week, mechi kati ya Mtibwa Sugar na Oljoro JKT iliyokuwa ichezwe Aprili 13 mwaka huu sasa itachezwa Aprili 17 mwaka huu Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

TFF YAMKALIA KOONI NSA JOB


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtaka mshambuliaji Nsa Job wa Coastal Union kuwasilisha maelezo yake juu ya madai kuwa alipewa rushwa ya sh. milioni mbili ili asiifunge moja ya timu vigogo vya soka nchini.

Job alikaririwa Aprili 3 mwaka huu na kituo cha redio cha Clouds FM katika kipindi cha Amplifier kuwa alipewa kiasi hicho cha fedha na kiongozi wa timu husika ili asiifunge katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom, lakini alipokea fedha hizo na kuifunga timu hiyo.

Baadaye kiongozi huyo alikuwa akimtaka arejeshe fedha hizo. Pia TFF imekiandikia kituo hicho cha redio kutaka nakala ya kipindi hicho ili pamoja na maelezo ya mshambuliaji huyo vipelekwe katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

TFF itachukua hatua kali dhidi ya Job iwapo hatawasilisha maelezo yake kuhusiana na suala hilo, na imetaka wadau kutoa ushirikiano ili iweze kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye mpira wa miguu.

ASHINDA TUZO YA DSTV


Masoud Said (38), mkazi wa Mbeya akifurahia kitita cha Tshs 10,000,000 alizozawadiwa na DStv kwenye campaign ya DStv Rewards.

Kila wiki, DStv wamekuwa wakitoa Tshs 5,000,000 kwenye droo maalum kwa wateja wake wanaofanya malipo kabla ya akaunti zao kukatika.
Kushoto ni Meneja wa Fedha wa kampuni ya MultiChoice Tanzania, Francis Senguji na Meneja Masoko wa kampuni hiyo Furaha Samalu.

Thursday, April 4, 2013

AMRI IBRAHIM, MKONGWE WA SOKA ANAYEWASIKITIKIA VIONGOZI WA MCHEZO HUO

UTAKAPOKUTANA na Amri Ibrahim njiani, siyo rahisi kuamini kwamba ndiye yule kiungo na mshambuliaji aliyeng'ara katika timu za Pamba ya Mwanza, timu ya mkoa huo, Mwanza Heroes na Simba.

Kwa sasa ni mtu mzima. Umri wake ni miaka 57. Mwili wake ni mwembamba na wakati mwingine anapotembea, anaonekana kama vile anapepesuka. Uvaaji wake ni wa kawaida. Anapenda zaidi kuvaa nguo za michezo.

Kinachofurahisha ni kwamba, Amri ni mcheshi kwa mtu yeyote anayeonyesha dalili za kumfahamu. Si mtu wa kujikweza na kupenda kujionyesha, hata kama hoja inayozungumzwa na kujadiliwa mbele yake anaifahamu au inamuhusu.

Kumtafuta Amri katika mji wa Morogoro haikuwa kazi ngumu. Anapatikana zaidi kwenye ofisi za Chama cha Soka cha mkoa wa Morogoro (MRFA). Hapo ndipo kilipo kijiwe cha wanasoka wa zamani wa timu za mji huo uliozungukwa na milima mingi ya mawe.

Siku nilipokutana naye na kumweleza madhumuni ya safari yangu katika mji wa Morogoro, hakuonekana kushtuka. Tukakubaliana tukutane siku inayofuata kwenye mgahawa mmoja uliopo nje ya Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro.

Nilichoweza kugundua ni kwamba, bado Amri anaendelea kujihusisha na mchezo wa soka, akiwa kocha. Awali, alipendelea zaidi kuwafundisha vijana wadogo wa mkoa huo, lakini baadaye aliamua kuifundisha timu ya Rhino FC ya Lindi kabla ya kujiuzulu baada ya timu hiyo kuvurunda katika michuano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara msimu huu.

Kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa zamani, Amri hafurahishwi na mwenendo wa soka ulivyo hivi sasa hapa nchini. Kwa mtazamo wake, soka ya Tanzania ni sawa na mtoto aliyesimama dede. Yaani anaweza kuinuka na kusimama, lakini hawezi kutembea.

"Miaka ya nyuma, kiwango chetu cha soka kilikuwa kikubwa. Timu yetu ya taifa (Taifa Stars), ilifuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 1980 na tulitoa wachezaji wawili katika timu ya Afrika miaka ya 1970. Pia tulizitambia timu kutoka Ghana, Nigeria na Congo," alisema Amri.

Alizitaja baadhi ya sababu za kushuka kwa kiwango cha soka nchini kuwa ni pamoja na klabu na vyama vya michezo kuongozwa na watu, ambao hawana taaluma ya michezo. Aliwaita watu hao kuwa ni wavamizi wa uongozi wa michezo.

"Mtu asiye na taaluma ya michezo, asiruhusiwe kugombea uongozi. Hawa wanaharibu michezo na wanachangia migogoro. Yule anayeujua vyema mchezo wa soka, ndiye anayepaswa kupewa uongozi na yule anayeupenda mchezo huo, abaki kuwa mpenzi," alisema mwanasoka huyo mkongwe.

"Kama mtu hawezi kutongoza mwanamke yeye mwenyewe, anamtuma mwenzake kumtongozea, hayo si mapenzi. Kwa hiyo, kama huna kauli nzuri kwa wachezaji ya kuwashawishi wacheze vizuri, huwezi kufanya hivyo,"aliongeza.

Amri aliishutumu tabia ya baadhi ya viongozi wa klabu za soka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutowashirikisha wanasoka wa zamani katika kutoa mchango wa mawazo yanayoweza kusaidia kuinua kiwango cha mchezo huo nchini.

Alisema iwapo wanasoka wa zamani, hasa waliowahi kuichezea Taifa Stars watakutanishwa mara kwa mara na kuombwa kuchangia mawazo juu ya kuinua kiwango cha mchezo huo, upo uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa kiini cha matatizo yaliyopo sasa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kiungo huyo wa zamani wa Pamba na Simba alilitaja tatizo lingine linalochangia kudidimia kwa maendeleo ya mchezo huo kuwa ni kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwaandaa vijana kucheza soka tangu wakiwa wadogo.

Hata hivyo, aliipongeza TFF kwa kuanzisha michuano ya Copa Coca Cola, inayozishirikisha timu za mikoa za vijana wa umri wa chini ya miaka 17 na ile ya Kombe la Uhai, ambayo inazishirikisha timu za vijana wa chini ya umri wa miaka 20.

Aliitaja sababu nyingine ya kudidimia kwa maendeleo ya soka nchini kuwa ni kuzuka kwa migogoro ya mara kwa mara katika klabu kongwe, hasa Simba na Yanga. Alisema chanzo kikubwa cha migogoro hiyo ni ulaji wa pesa kwa vile wanachama wengi wanaopata nafasi ya kuziongoza, wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

"Nadhani wakati umefika kwa serikali kutengeneza sera, iende Bungeni ili iidhinishwe na kuifanya soka ya Tanzania iwe ya kulipwa. Sera hiyo ikipitishwa, nina hakika Simba na Yanga zitakoma. Kama serikali inaweza kutunga sheria kuhusu mambo mengine, sioni kwa nini isitunge sheria ya kuigeuza soka yetu kuwa ya kulipwa,"alisema.

Amri pia aliilaumu tabia ya makocha wenye taaluma ya kufundisha soka kuwadharau wanasoka wa zamani, waliojitolea kutoa mafunzo kwa vijana kwa lengo la kuwaendeleza.

"Kuna tabia kwa baadhi ya makocha waliosomea fani hiyo, kuwadharau wale, ambao hawakusoma, lakini wanasahau kwamba, ndio waliovumbua vipaji vya vijana na kuwaendeleza,"alisema.

"Hawa wenzetu waliosomea ukocha wa soka, wanasubiri kuitwa kufundisha timu za Simba, Yanga na Taifa Stars, hawataki kuja chini. Huku ndiko kugumu. Wanawadharau wale wanaojitolea kufundisha vijana wakati wao wanashindwa kutumia taaluma yao kufanya hivyo. Kisingizio chao siku zote ni kwamba wanazo kazi nyingi. Lakini wanapoitwa kuzifundisha Simba na Yanga, wanapata muda wa kufanyakazi hiyo,"alisema.

Amri alisema Tanzania inayo hazina ya makocha wazuri wenye uwezo wa kufundisha soka, lakini wanakosa nyenzo na pia wamekuwa wakidharauliwa, badala yake makocha wa kigeni ndio wamekuwa wakiaminiwa zaidi na kuthaminiwa.

"Wanachokosa makocha wetu wa kizalendo ni nyenzo.Leo hii akija kocha wa kigeni na kusema anataka mipira 30 na jozi 30 za raba na jozi 30 za viatu vya kuchezea soka, ataletewa mara moja. Lakini kocha mzalendo akiomba apatiwe vifaa hivyo, ataonekana kama vile chizi,"alisema kocha huyo.

"Lakini akija kocha wa nje na kutaka alipwe mshahara wa shilingi milioni tatu kwa mwezi, atapatiwa mara moja. Kocha mzalendo akiomba alipwe mshahara wa shilingi laki tatu kwa mwezi, atanyimwa na kama kulipwa, atalipwa kwa mafungu,"alisema.

Amri alisema kazi ya kufundisha soka ni ngumu, hivyo makocha wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa ili waweze kutimiza vyema majukumu yao.

Mwanasoka huyo mkongwe pia alitoa ushauri wa kuwepo na utaratibu wa pande muhimu katika uongozi wa klabu, kuheshimu nafasi za wenzao.

Itaendelea Alhamisi ijayo

WOLPER AMTUNGIA FILAMU KANUMBA


MSANII nyota wa filamu nchini, Jacqueline Wolper ameandaa filamu maalumu kwa ajili ya kumuenzi marehemu Steven Kanumba.

Wolper alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Jumapili kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Wolper hakuwa tayari kutaja jina la filamu hiyo. Alisema litajulikana siku ya uzinduzi, lakini alisisitiza ni maalumu kwa ajili ya kumuenzi Kanumba.

"Kanumba ni kila kitu kwetu katika tasnia ya filamu, ndio maana tunamkumbuka na tutazidi kumuenzi,"alisema Wolper.

Kwa mujibu wa Wolper, siku hiyo pia utafanyika uzinduzi wa filamu ya mwisho ya marehemu Kanumba, inayojulikana kwa jina la Love & Power.

Kanumba aliandaa filamu hiyo siku chache kabla ya kifo chake kilichotokea Aprili 7 mwaka jana, nyumbani kwake, Sinza, Dar es Salaam.

Maudhui ya filamu hiyo hayana tofauti na mazingira ya kifo chake, ambacho kilipokelewa kwa simanzi kubwa na mashabiki wa fani hiyo nchini.

Wakati huo huo, mdogo wa marehemu Kanumba, Seth Bosco amesema wameandaa misa ya kumuombea ndugu yao itakayofanyika Jumapili kwenye kanisa la Kimara, Dar es Salaam.

Bosco alisema juzi kuwa, baada ya misa hiyo kukamilika, mambo yote yatahamia kwenye viwanja vya Leaders, ambako utafanyika uzinduzi wa filamu ya mwisho ya marehemu Kanumba.

"Itakuwa ni siku, ambayo tutatimiza mwaka mmoja baada ya mpendwa wetu Kanumba kufariki dunia,"alisema.

NURU THE LIGHT, SHOMBESHOMBE WA KIBONGO ANAYETAMBA KIMUZIKI

WAKATI aliporekodi kibao chake cha kwanza kinachojulikana kwa jina la Walimwengu, mwanadada Nuru Mohamed, maarufu kwa jina la Nuru the Light, hakuwa akijulikana sana miongoni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini.

Ni kwa sababu hakuwa akiishi hapa nchini, japokuwa alikuwa akifika Dar es Salaam mara kwa mara kwa ajili ya kuwatembelea ndugu zake. Nuru alizaliwa na kukulia nchini Sweden, ambako ndiko wazazi wake wanakoishi.

Kilichomfanya Nuru ajitose kwenye fani ya muziki ni baada ya kuvutiwa na mwanamuziki wa kitanzania aliyekuwa akiishi Sweden wakati huo, marehemu Mtoto wa Dandu.

Mbali na kuvutiwa na mwanamuziki huyo, Nuru pia alishangaa kuona kuwa, wakati alipofika Tanzania kwa mara ya kwanza, msanii pekee wa kike aliyekuwa akitamba wakati huo alikuwa Judith Wambura 'Lady JayDee'.

"Nikawa najiuliza kwa nini hakuna wanamuziki wa kike wenye vipaji kama Lady JayDee? Nilichogundua ni kwamba wasichama wa Kitanzania hatujiamini, tuna woga wa kufanya vitu ndio sababu tunachukiana bila sababu,"alisema.

"Ukiona mwenzako amefanikiwa katika sekta fulani, unatishika. Badala ya kujitahidi ufike pale alipo, unajaribu kumjenga chuki ili arudi nyuma," aliongeza msanii huyo mwenye haiba yenye mvuto.

Nuru alisema baada ya kurudi Sweden, alimtafuta prodyuza, ambaye licha ya kutofahamu lugha ya kiswahili, aliweza kutengeneza naye wimbo wa Walimwengu, ambao anakiri kwamba ndio uliomtoa kimuziki.

Katika wimbo huo, Nuru amezungumzia matatizo mbalimbali yaliyowahi kumkuta katika maisha yake, kila alipokuwa akija nchini kuwatembelea ndugu zake, ambapo watu wengi walikuwa wakimfikiria kwamba ni binti wa kitajiri.

Baada ya muda si mrefu, Nuru aliibuka na kibao kingine kinachokwenda kwa jina la Msela, ambacho kilizua gumzo kwa mashabiki kutokana na maudhui yake.

"Nilipotoa wimbo huu, mashabiki wengi hawakunielewa. Wakawa wanajiuliza, iweje msichana huyu mrembo anawapenda wasela. Kwangu neno msela ni tofauti na inavyoeleweka kwa watu wengine. Msela ni mtu anayependa kuchapakazi hata kama amevaa suti,"alisema Nuru.

"Usimuhukumu mtu kwa mwonekano wake, lazima umchunguze ili upate ukweli," alisisitiza mwanadada huyo, ambaye kwa kawaida ni mcheshi na mzungumzaji mno, akiwa anapenda kujichanganya na watu wa aina tofauti.

Licha ya kuajiriwa nchini Sweden na pia kujihusisha na biashara, Nuru alisema hafanyi muziki kwa ajili ya kujifurahisha kwa vile ni fani anayoipenda na kuvutiwa nayo.

Nuru anavutiwa zaidi na wasanii Juma Kassim 'Nature' na Joseph Haule 'Profesa Jay', ambao amewaelezea kuwa wana vipaji vya asili na kuimba nyimbo zenye mvuto.

"Navutiwa na Nature kutokana na staili ya maisha yake. Wakati mwingine huwa anaimba vitu nisivyovielewa, lakini navipenda,"alisema.

"Navutiwa na Profesa Jay kwa sababu ni msanii asiyekuwa na maringo wala kujikweza. Yupo kama alivyo. Kwa msanii wa aina yake, angekuwa na maringo mno,"aliongeza.

Kwa upande wa wasanii wa kike, Nuru alisema anapenda kufanya kolabo na Grace Matata na Nakaaya Sumari kwa vile wana vitu, ambavyo havifanani, lakini vikichanganywa pamoja vinakuwa bomba.

Mbali na kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nuru pia ni prodyuza. Ndiye aliyetengeneza vibao vyake vya Walimwengu na Msela.

Ili kwenda na wakati kimuziki, Nuru alisema utaratibu wake ni kurekodi CD na Audio za nyimbo zake kwa pamoja. Alisema lengo ni kuwawezesha mashabiki wake kupata burudani ya nyimbo zake kwa wakati mmoja.

"Sipendi kutoa kitu kimoja kimoja, mtu mwingine akisikia wimbo kwenye CD, hawezi kuelewa mpaka aone video yake. Kuna wengine hawajui kiswahili, lakini akiona video, anaelewa,"alisema.

Nuru hajaolewa na kwa mujibu wa maelezo yake, hahitaji rafiki wa kiume kwa wakati huu. Alisema anachotaka ni kutimiza malengo aliyojiwekea.

Msanii huyo hafurahishwi na maonyesho ya baadhi ya wasanii wa Tanzania waliyowahi kuyafanya katika nchi za Ulaya. Alisema maonyesho mengi aliyowahi kuyashuhudia Sweden, yaliyowahusisha Naseeb Abdul 'Diamond' na Jay More yalikuwa feki.

"Nafurahi kuona wasanii wa Tanzania wanapata nafasi ya kufanya maonyesho Ulaya, lakini mengi yanakuwa hayana hadhi kwa sababu wanapelekwa katika kumbi ndogo mno na mashabiki wanaohudhuria wanakuwa wachache,"alisema.

Nuru alisema moja ya malengo yake katika siku zijazo ni kupigania haki za wasanii wa Tanzania, hasa katika suala la usambazaji wa kazi zao, ambao ameuelezea kuwa kwa sasa ni duni.

Alisema amejifunza mengi kutokana na vifo vya wasanii Steven Kanumba na Sharo Milionea, ambao familia zao hazinufaiki lolote kutokana na kazi zao.

Nuru alisema binafsi amekuwa akisajili nyimbo zake katika chama cha hakimiliki cha Sweden, hivyo hata kama atafariki, familia yake itaweza kunufaika kutokana na kazi zake.

Ametoa mwito kwa wasanii kuungana na kuacha kujengeana chuki bila sababu za msingi. "Hii habari ya mimi napiga hip hop, mimi napiga bongo fleva, haiwezi kutufikisha popote. Usimcheke mwenzako, tuwe na utaratibu wa kusaidiana,"alisema.

Amemfagilia Adam Juma kwa kuwa mshauri wake mzuri kimuziki baada ya kumuona amekata tamaa kutokana na maprodyuza wengi kumtongoza na kumtaka kimapenzi. Adam ni mtaalamu wa kutengeneza video za muziki.

"Hivi sasa nina msimamo. Prodyuza akinitongoza, namtukana papo hapo na sifanyi naye kazi,"alisema Nuru, ambaye ni mtoto pekee wa kike katika familia yake, akiwa na kaka zake watatu.

TFF YAZINDUA MPANGO WA MAENDELEO 2013-2016

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo.

Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.

Rais Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA.

Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.

“Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini tumeongeza mashindano ya aina mbalimbali kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo katika mpango wa sasa ni kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,” amesema.

Rais Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na watu kujitolea ambapo ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika wote kuwa na mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana kazi ya kufanya katika mpango huo.

“Naomba washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya kusoma, toa maoni yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.

Amesema maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo unahitaji ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa mpira wa miguu Tanzania bado ni wa kujitolea.

Rais Tenga amesema ahadi ya TFF ni kushirikiana na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi kwa ujumla.

Amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF, Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy).

EXTRA BONGO, JAHAZI KUNOGESHA BONANZA LA TASWA


Juma Pinto Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari za michezo TASWA akitangaza bendi ya muziki itakayotumbuiza kwenye bonanza la waandishi wa habari litakalofanyika Aprili 6 Jumamosi kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es salaam, kulia ni Katibu Mkuu wa TASWA Amiri Mhando na kulia ni Doris Malulu Ofisa Uhusiano TBL
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi Modern ndiyo burudani zitakazonogesha tamasha la vyombo vya habari litakalofanyika Dar es Salaam kesho (Jumamosi).

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kutambulisha burudani hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinachoandaa bonanza hilo, Juma Pinto alisema maandalizi kuhusiana na tamasha hilo linalojulikana kama Media Day Bonanza yamekamilika.

Alisema wameichukua Extra Bongo inayoongozwa na Ally Choki na Jahazi Modern inayoongozwa na Mzee Yusuph kutokana na makundi hayo kuwa juu hivi sasa katika muziki kwa maeneo yao.

“Tunaamini watakaokuja kwenye tamasha watakuwa na furaha ya aina yake na tumejiandaa vya kutosha,” alisema Pinto na kueleza kuwa bonanza hilo litafanyika viwanja vya Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Pia Pinto alisema bendi ya Msondo Ngoma Music itapiga kwenye viwanja hivyo kuanzia saa moja usiku baada ya bendi za Extra Bongo na Jahazi kumaliza kutumbuiza Media Day na kwamba imetoa ofa kwa wanahabari watakaotaka kubaki kuendelea kupata burudani mpaka usiku wa manane.

“Msondo wana bonanza lao kila Jumamosi, sasa wamekubali kwamba wanahabari watakaotaka kubaki baada ya bonanza kumalizika jioni wabaki wajiunge na Msondo Ngoma,” alisema Pinto.

Bonanza hilo la TASWA linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema wamejipanga vya kutosha na kwamba wadau wafike kwa wingi kuhakikisha mambo yanaenda kama yalivyopangwa.

“TBL ni mdau mkubwa wa wanahabari, tumewaandalia mambo mazuri, naomba msikose,” alisema Malulu na kuongeza kuwa wanaamini wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari wanaotarajiwa kushiriki bonanza hilo watafurahi vya kutosha siku hiyo.

Naye Choki akizungumza kwenye mkutano huo, alisema vijana wake wamejipanga vya kutosha kushambulia na kuwa dhamira yao ni kuona wana habari wanafurahi vya kutosha na kuwa mambo waliyowaandalia kila mtu atafurahi kuiona Extra Bongo.

WAREMBO WAOMBWA KUJITOKEZA MISS KIGAMBONI




KAMATI ya mashindano ya urembo ya kitongoji cha Kigamboni kinawaomba warembo kutoka sehemu mbalimbali kujitokeza kuwania taji la shindano hilo litakalofanyika hivi karibuni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa shindano hilo, wa kampuni ya K& L Media Solutions, Somoe Ng’itu, alisema kuwa nafasi iko wazi kwa wasichana wote wenye sifa za kushiriki shindano hilo kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Mratibu huyo alisema kwamba lengo la kuweka wazi na kuwahamasisha warembo ni kutaka kutoa nafasi kwa wasichana wengi zaidi kujiandikisha na hatimaye kutoa ushindani kwenye kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika baadaye mwezi ujao.

“Shindano letu liko wazi na tunakaribisha warembo kutoka sehemu yoyote hapa nchini kuchuana, tunataka mwaka huu tufanye vizuri zaidi katika mashindano ya Miss Tanzania,” alisema Somoe.

Alisema kwamba kamati inaamini ushiriki mkubwa wa wasichana ndio utasaidia kutoa mshindi atakayeiwakilisha vyema Kigamboni katika mashindano yanayofuata ya Kanda ya Temeke na kwenye fainali za ngazi ya Taifa za Redd’s Miss Tanzania.

Aliongeza kuwa fomu kwa ajili ya shindano hilo zinatolewa bure na zinapatikana katika ofisi za gazeti la NIPASHE, Angella Msangi (TBC1), mgahawa wa Hadees ulioko Posta, ofisi za Miss Tanzania, na kwa barua pepe somoebaby@yahoo.com.

“Kigamboni ni eneo la kipekee na tunatarajia mwaka huu kufanya vizuri kwa kuwahusisha wadau wote kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho, tunafahamu mshindi ataiwakilisha Kigamboni na si kwamba ataenda kwenye fainali baada ya kupata ushirikiano wa wakazi wa eneo hili,” aliongeza.

Mrembo anayeshikilia taji ni Edda Sylivester ambaye mwaka jana alishika nafasi ya tatu kwenye fainali za taifa huku mshindi wa taifa ni Brigitte Alfred ambaye mwaka huu ataenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya dunia.

Tuesday, April 2, 2013

DK. MWAKYEMBE MGENI RASMI BONANZA LA TASWA



WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye bonanza la vyombo vya habari linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).


Bonanza hilo litafanyika Jumamosi wiki hii viwanja vya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja usiku likidhaminiwa na na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mwakyembe atakabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali watakaoibuka siku hiyo, pia atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.

Lengo la bonanza ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja na huwa linafanyika mara moja kwa mwaka, likiandaliwa na TASWA.

Bonanza hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki.

Tunataka bonanza la mwaka huu liwe la aina yake kuanzia mgeni rasmi, burudani, michezo na mambo mengine yawe ya kuvutia, ambapo Alhamisi Aprili 4,2013 saa tano asubuhi kutakuwa na mkutano na wanahabari mgahawa wa City Sports Lounge, Posta Dar es Salaam ambao ni maalum kutangaza makundi yatakayotumbuiza kwenye Media Day na tunatarajia makundi hayo nayo yatakuwepo kwenye mkutano huo.

Tunaomba vyombo vya habari ambavyo havijathibitisha ushiriki wao kwa njia ya maandishi vifanye hivyo kama vilivyoagizwa kwenye barua zao za mialiko, vinginevyo ushiriki wao hautathaminika.

Bonanza litaanza saa tatu asubuhi, ambapo baadhi ya michezo itakayoshindaniwa ni soka ya ufukweni, netiboli, wavu, mbio za magunia, mbio meta 100, kuruka kichura, kuvuta kamba, kucheza muziki na kuimba.

WACOMORO KUZICHEZESHA AZAM NA BARRACK



Shrikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi watakaochezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na Barrack Young Controllers II ya Liberia itakayochezwa Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi wa kati ni Adelaide Ali, mwamuzi msaidizi namba moja ni Amaldine Soulaimane wakati Ibrahim Mohame atakuwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ansudane Soulaimane.

Kamishna wa mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni atakuwa Abdelhamid Radwan kutoka Misri. Maofisa hao wa mechi hiyo watafikia kwenye hoteli ya Holiday Inn.

Wakati huo huo, Barrack Young Controllers II imewasili nchini leo (Aprili 2 mwaka huu) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.

Timu hiyo iliyofia hoteli ya Sapphire Court itafanya mazoezi leo jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake kwa ajili ya mechi hiyo huku wapinzani wao Azam wakiendelea kujinoa kwenye uwanja wao wa Azam Complex.

Monday, April 1, 2013

WAPINZANI WA AZAM KUTUA DAR KESHO




Timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia inatarajia kuwasili nchini kesho (Aprili 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam itakayochezwa Jumamosi (Aprili 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Young Controllers itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.

Msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 37 wakiwemo wachezaji 21 na utaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo Robert Alvin Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.

Wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy, Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.

Benchi la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu Robert Lartey akisaidiwa na Samuel Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel Massaquoi.

Timu hiyo inatarajia kundoka kurejea Monrovia, Aprili 8 mwaka huu kupitia Nairobi, Kenya saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir.

Sunday, March 31, 2013

NANCY SUMARI: KUJIAMINI KUMENIFIKISHA NILIPO



MREMBO wa Tanzania wa 2005, Nancy Sumari amesema kufanya kitu bila kuogopa kushindwa ndio siri ya kufanikiwa kwake katika mambo mbalimbali.

Akihojiwa katika kipindi cha Makutano kilichorushwa hewani wiki iliyopita kupitia kituo cha televisheni cha DTV, Nancy alisema katika maisha yake, haogopi kufanya kitu chochote hata kama hana uzoefu nacho.

Nancy alisema utamaduni wake huo wa kujiamini ndio uliomwezesha kushinda mataji ya Miss Dar Indian Ocean, Miss Kinondoni na hatimaye Miss Tanzania.

Mbali na kutwaa mataji hayo, Nancy pia alikuwa Mtanzania wa kwanza kuweka rekodi ya kushinda taji la Miss World Africa 2005 baada ya kufuzu kuingia hatua ya fainali.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema, kabla ya kujitosa katika mashindano ya urembo, aliwahi kufanyakazi kama muuzaji katika duka la fenicha na kulipwa mshahara wa sh. 120,000 kwa mwezi.

Alisema aliamua kufanyakazi hiyo baada ya kukwama kupata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha sheria, kutokana na chuo hicho kutoruhusu mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne kwa elimu ya Kenya, kujiunga moja kwa moja kwa masomo ya shahada.

"Nilifanyakazi hiyo kwa moyo wote hadi nilipopata nafasi ya kushiriki mashindano ya urembo baada ya waandaaji kuniona na kuvutiwa na mimi,"alisema.

Akizungumzia uamuzi wake wa kuchapisha kitabu cha Nyota Yako, Nancy alisema umetokana na kutokuta vitabu vya watoto madukani vilivyoandikwa na waandishi wa Tanzania.

"Mbali ya kuwa mimi ni mama kwa wakati huu, kila nilipokwenda kwenye maduka ya vitabu, nilikosa vitabu vya watoto vilivyoandikwa na waandishi wa Tanzania. Vingi vimeandikwa na waandishi wa nje,"alisema.

"Hivyo niliamua kuandika kitabu, ambacho watoto wa kike wa Tanzania wataweza kukisoma na kuvutiwa kufanya kile, ambacho nimekiandika kwenye kitabu hicho,"aliongeza.

Kwa mujibu wa Nancy, kitabu hicho kinapatikana katika maduka ya Scholastica lililopo Mlimani City na Novel Idea lililopo Masaki, Dar es Salaam kwa bei ya sh. 5,000.

Nancy amewataka vijana wanaochipukia kujaribu kuwa wazuri kwa sababu kila mmoja anafanya makosa, hakuna aliye sahihi kwa asilimia 100.

"Lakini ni muhimu kama binadamu, tujitahidi kufanya vitu sahihi, sawa na unapoona ua linafifia, limwagilizie maji likue na unapomwona mwenzako anahitaji msaada na unayo nafasi, usisite kumsaidia,"alisema.

Nancy kwa sasa ni Mkurugenzi wa Matukio wa Kampuni ya Frontline Management, ambayo amekuwa akiiongoza kwa kushirikiana na mrembo mwenzake, Irene Kiwia na anatarajia kumaliza masomo ya Chuo Kikuu Julai mwaka huu.

MOURINHO, ABRAMOVICH WAMALIZA TOFAUTI ZAO




LONDON, England
MMILIKI wa klabu ya Chelsea ya England, Roman Abramovich amemaliza tofauti kati yake na kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Jose Mourinho na kukubaliana kumrejesha katika klabu hiyo.

Abramovich na Mourinho walifikia makubaliano hayo Jumatatu iliyopita baada ya kufanya mazungumzo kwa faragha.

Mourinho alikuwepo nchini England kwa ajili ya kushuhudia mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Brazil na Russia iliyochezwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge. Katika mechi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Abramovich alitofautiana na Mourinho baada ya kocha huyo kushindwa kuiwezesha Chelsea kutwaa mataji aliyokuwa akiyataka baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa England, Kombe la FA na Kombe la Carling.

Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti jana kuwa, Abramovich amekuwa akimtaka Mourinho arejee England kwa mara ya pili kwa ajili ya kuinoa Chelsea.

Tayari Abramovich na Mourinho wameshafikia makubaliano hayo, lakini hakuna yeyote kati yao aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports, Mourinho alisema kwa sasa bado yeye ni kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania na kwamba lengo lake ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu huu.

Hata hivyo, Mourinho hakuona aibu kuelezea mapenzi yake kwa England na kuvifananisha vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa sawa na sukari na pilipili katika chakula chake cha kila siku.

Abramovich amekuwa na mapenzi makubwa kwa Mourinho baada ya kushindwa kumpata kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, ambaye amejiunga na Bayern Munich ya Ujerumani.

"Siwezi kupinga. Licha ya hali hii ya hewa, napenda kuwepo hapa,"alisema Mourinho, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Special One.

"Nafikiri siku moja nitarejea katika ligi kuu ya England katika klabu ya Chelsea au nyingineyo. Chelsea ipo moyoni mwangu, hivyo siku moja nitarejea. Tunayo nyumba hapa, binti yetu anakuja kusoma London hivyo kuwepo kwangu London ni kitu cha kawaida kwetu," aliongeza kocha huyo.

"Lakini kila ninapokuja hapa na watu wakiniona nakatiza mitaani ama kufanya manunuzi, wanaanza kuunganisha mambo. Sijali kwa sababu kila siku ninapopata nafasi, naeleza wazi kwamba napenda kuwepo hapa. Nilikuwa na wakati mzuri hapa na kwamba nitarejea. Huwa sipendi kusema mengi kuhusu hisia hizi kwa sababu napenda kuwepo hapa,"aliongeza.

Mbali na Chelsea, Mourinho pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Manchester United na Manchester City.

Kwa sasa, Chelsea inanolewa na kocha wa muda, Rafael Benitez, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa hawamuungi mkono kutokana na matokeo mabaya katika ligi.

"Nilikuwepo Manchester wiki tatu zilizopita na hali ya hewa ya huko ilikuwa nzuri zaidi. Nilifanya mazungumzo na Sir Alex Ferguson kwa kumtumia ujumbe japokuwa alikuwa akikabiliwa na mechi,"alisema Mourinho.

"Lakini Manchester ni utawala wa Sir Alex na ningependa kazi hiyo iwe ya kudumu kwake. Bila shaka haiwezi kuwa hivyo, lakini ningependa aendelee na kazi hiyo kwa miaka mingi zaidi," alisisitiza.

Mourinho pia aliizungumzia Manchester City na kocha wake, Roberto Mancini. Alisema kutokana na kocha huyo kuiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, hafikirii iwapo yanaweza kufanyika mabadiliko yoyote.

"Hata kwa Benitez, natumaini kila kitu kinakwenda vizuri kwake na watamaliza msimu vizuri,"alisema Mourinho, ambaye pia amewahi kuzinoa FC Porto ya Ureno na Inter Milan ya Italia.

"Mwisho wa siku, nipo Real Madrid, nakabiliwa na majukumu mazito hadi mwisho wa msimu huu. Tumefuzu kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, tumefuzu kucheza fainali ya Kombe la Mfalme, hivyo watu wanaelewa mimi ni kocha wa kulipwa na kwamba kwa sasa nafikiria kazi yangu Real Madrid," alisema kocha huyo.

Mourinho alisema anaona fahari kuwa kocha aliyeweza kutwaa mataji mawili ya ligi ya mabingwa wa Ulaya akiwa na timu tofauti na kwamba angependa kutwaa tena taji hilo msimu huu.

Kocha huyo alisema atavunjika moyo iwapo atashindwa kutwaa taji hilo msimu huu baada ya baadhi ya vigogo kama vile Manchester United na Chelsea kutolewa hatua ya awali.

Hata hivyo, alikiri kuwa timu zote nane zilizosalia katika michuano hiyo ni nzuri na yoyote inaweza kutwaa ubingwa.

Msimu huu umekuwa mbaya kwa Mourinho, kufuatia Real Madrid kuzidiwa kwa tofauti ya pointi 13 na mahasimu wao, Barcelona katika msimamo wa ligi kuu ya Hispania.

Matumaini pekee ya kocha huyo kwa sasa yamebaki katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya na Kombe la Mfalme wa Hispania, ambapo Real Madrid itacheza fainali dhidi ya Atletico Madrid.

Real Madrid imepangwa kumenyana na Galatasaray ya Uturuki katika robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.

YANGA YAWAONYA WAFANYABIASHARA



KLABU ya Yanga imewaonya wafanyabiashara wanaotengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya klabu hiyo bila idhini ya uongozi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kufanya hivyo ni makosa kisheria na kwamba wahusika watachukulia hatua.

"Kwa miaka mingi sasa, kumekuwepo na tabia kwa wafanya biashara mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi kujihusisha na utengenezaji, uingizaji na uuzaji wa bidhaa zenye nembo ya Yanga.

"Yanga inapenda kutoa angalizo kuwa tabia hiyo iliyokithiri ni ukiukwaji wa sheria na unaikosesha klabu mapato halali, ambayo ingeyapata kutokana na matumizi ya nembo yake,"alisema Mwalusako.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema, nembo ya Yanga iliyosajiliwa rasmi kwa msajili Juni 2, 2009, inamilikiwa na klabu hiyo hivyo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kuitumia bila ridhaa ya uongozi.

"Kwa mantiki hiyo, Yanga inatangaza rasmi kuwa ni marufuku kwa kampuni, mtu binafsi au kikundi chochote kutengeneza ama kuuza bidhaa zenye nembo ya Yanga bila ridhaa ya klabu.

Iwapo itatokea mtu yeyote kukiuka amri hii, uongozi utachukua hatua kali za kisheria ili kuikomesha,"alionya Mwalusako.

Kiongozi huyo wa Yanga amewashauri wafanya biashara wanaotaka kutengeneza na kuuza bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo, kuwasiliana na uongozi ili wapewe haki hiyo kisheria.

Alisema mfanya biashara atakayekubali kufikia makubaliano na uongozi, atakubaliwa kutengeneza ama kuingiza bidhaa hizo kwa malipo maalumu.

Hata hivyo, Mwalusako alionya kuwa, lazima bidhaa hizo ziwe zenye kiwango na ubora, ambao utakubaliwa na kupitishwa na uongozi wa Yanga.

Mwalusako ametoa mwito kwa wanachama na wapenzi wa Yanga kutonunua bidhaa zozote zenye nembo ya klabu hiyo iwapo muuzaji hajaruhusiwa na uongozi kufanya hivyo.

WADAU WA FILAMU WAMPONGEZA WEMA KWA KUMWOKOA KAJALA



WADAU mbalimbali wa fani ya filamu wamempongeza msanii nyota wa tasnia hiyo nchini, Wema Sepetu kwa kumwokoa msanii mwenzake, Kajala Masanja kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12.

Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, wadau hao walisema kitendo kilichofanywa na Wema kumlipia Kajala faini ya sh. milioni 13 ni cha ujasiri na mfano wa kuigwa.

Kajala, ambaye alisota rumande kwa mwaka mmoja, alinusurika kwenda jela Jumatatu iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili kati ya matatu ya kutakatisha fedha.

Mume wa msanii huyo, Faraja Chambo alihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kupatikana na hatia ya makosa yote matatu na kushindwa kulipa faini ya sh. milioni 213.

Kajala na Chambo, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Marchi 15, mwaka jana, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama ya kubadilisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala, Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

"Kwa kweli kitendo kilichofanywa na dada huyu ni ujasiri wa aina yake. Wapo wasanii wengine maarufu wa filamu, lakini wameshindwa kumsaidia mwenzao kama alivyofanya Wema,"alisema Robert Justine, mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam.

Mwanadada Lucy Tesha, mkazi wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam alisema, alichokifanya Wema, hakuna mwingine wa kumlipa fadhila zake, isipokuwa Mwenyezi Mungu.

"Wema asisubiri kulipwa wema wake hapa duniani. Atalipwa na Mungu,"alisema dada huyo.

Mkazi mwingine wa Buguruni, aliyejitambulisha kwa jina la Chambo Waziri alisema, Wema amefanya kile, ambacho si watanzania wengi wanaweza kukifanya.

"Fikiria, Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka 13, wazazi wake ni masikini, yeye na Wema ni marafiki wa kawaida tu, lakini amemsaidia utadhani ndugu yake wa kuzaliwa tumbo moja,"alisema.

Shamsa Majid, mkazi wa Ilala Boma alisema, msanii mwingine anayestahili kupongezwa ni Mahsen Awadh, maarufu kwa jina la Dk. Cheki kutokana na kuwa mstari wa mbele kusaidia wenzake.

"Kwa kweli nampa big up Cheni. Alikuwa mstari wa mbele kumsaidia Lulu (Elizabeth Michael) na juzi tumemuona akiwa mstari wa mbele kumsadia Kajala. Hawa wengine wamebaki maneno maneno tu,"alisema.