KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 7, 2012

Banza Stone aja na kibao kipya cha taarab


MWIMBAJI na mtunzi mahiri wa nyimbo za muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ ameingia studio kurekodi kibao chake cha pili cha taarab.
Banza, ambaye kwa sasa ni mwanamuziki wa bendi ya Extra Bongo, alitarajiwa kuingia studio jana kurekodi wimbo huo chini ya usimamizi wa Thabiti Abdul.
Kibao hicho cha Banza kinajulikana kwa jina la Play Boy na kinatarajiwa kuanza kusikika hewani hivi karibuni.
Huo utakuwa wimbo wa pili kwa Banza baada ya kung’ara katika wimbo wake wa kwanza wa ‘Kuzaliwa mjini’, ambao pia ulitungwa na Thabit, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kikundi cha Mashauzi Classic.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Thabiti alisema ni kweli ameamua kumtungia Banza wimbo mwingine wa taarab baada ya kupata hamasa kutoka kwa mashabiki wa muziki huo.
“Mashabiki wengi walikuwa wanataka Banza aendelee kuimba nyimbo za taarab. Wamekuwa wakinilaumu kwa kumweka kimya kwa muda mrefu,”alisema Thabiti.
“Nami nimeona ni kweli, kwa vile wimbo wa Kuzaliwa mjini ulipokelewa vyema na mashabiki, ni vyema aendelee kuimba taarab,”aliongeza.
Mbali na kusumbuliwa na mashabiki, Thabiti alisema Banza mwenyewe naye amekuwa akimpigia simu mara kadhaa akimuomba amtungie wimbo mwingine wa taarab.
“Banza mwenyewe alikuwa akinisumbua, anasema nilipomtungia wimbo wake wa kwanza, nilikuwa kama nimembeeb, hivyo anataka aendelee kuimba taarab,”alisema Thabiti.
Kwa mujibu wa Thabiti, wimbo wa Kuzaliwa mjini, aliutunga miaka sita iliyopita, lakini hadi sasa bado unawavutia mashabiki wengi kutokana na maudhui ya wimbo na mipigo ya ala.
Banza amewahi kupigia bendi mbalimbali za muziki wa dansi nchini, lakini iliyomweka kwenye chati ya juu kimuziki ni Twanga Pepeta International.
Baadaye alijiunga na bendi ya TOT Plus, ambayo aliiongoza kwa miaka takriban mitano kabla ya kuanzisha bendi yake binafsi ya Bambino Sound.
Mtunzi huyo mahiri wa nyimbo za muziki wa dansi pia aliwahi kuimbia bendi ya Twanga Chipolopolo na Rufita Jazz kabla ya kujiunga na Extra Bongo, inayoongozwa na Ally Choki.
Ndani ya bendi hiyo, Banza amekuwa akitamba na kibao chake kinachojulikana kwa jina la Falsafa ya Maisha. Pia amekuwa akiimba nyimbo alizowahi kutamba nazo katika bendi mbalimbali.
Hivi karibuni, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Ramadhani H-Baba aliamua kumshirikisha Banza kurekodi wimbo wake mpya wa Sina Raha. Kibao hicho kimo kwenye albamu mpya ya msanii huyo inayojulikana kwa jina la Shika hapa, acha hapa.

Kipingu apigiwa debe TFF


BAADHI ya watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wajumbe wa mkutano kuu wa shirikisho hilo wameamua kumpigia debe Idd Kipingu ili awanie nafasi ya urais wa taasisi hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wiki kadhaa umebaini kuwa, Kipingu anapigiwa debe kuchukua nafasi ya rais wa sasa wa shirikisho hilo, Leodeger Tenga kutokana na uwezo wake kiungozi.
Kipingu aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) na pia mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Kwa mujibu wa uchunguzi, Kipingu anapigiwa debe kuchukua nafasi hiyo iwapo makamu wa kwanza wa rais wa zamani wa TFF, Crescentius Magori atakataa kugombea wadhifa huo.
Baadhi ya watendaji wa TFF wamemwelezea Kipingu kuwa ni kiongozi mwadilifu na ndiye pekee mwenye sifa za kumrithi Tenga katika wadhifa huo.
Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka 2013 baada ya uongozi wa sasa chini ya Tenga kumaliza muda wake Desemba mwaka huu.
Tayari Tenga ameshatangaza kuwa hatawania tena nafasi hiyo katika uchaguzi huo, lakini ataendelea kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Wadau wengine wa soka waliotajwa kuizengea nafasi hiyo ni pamoja na katibu mkuu wa zamani wa Yanga, Jamal Malinzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa wa TFF, Athumani Nyamlani.
Inadaiwa kuwa, tayari Nyamlani na Malinzi wameshaanza kufanya kampeni za kuwania wadhifa huo kwa kutembelea katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura.
Juhudi za kumtafuta Kipingu ili aeleze iwapo anakubaliana na maombi ya wadau kumtaka agombee wadhifa huo, hazikuweza kufanikiwa kwa vile siku nzima ya jana hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.

Njama zasukwa kumng'oa Papic




BAADHI ya viongozi wa klabu ya Yanga kwa kushirikiana na tawi moja la klabu hiyo la mjini Dar es Salaam wamepanga mipango ya kumng’oa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, mipango hiyo ilianza kusukwa mwanzoni mwa wiki hii, ikiwa ni siku chache baada ya Yanga kutolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuanza keshokutwa, saa chache kabla ya mechi kati ya Yanga na Azam, inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viongozi hao wa Yanga wamepanga kuwashirikisha wanachama wa tawi hilo katika mpango huo kwa kuingia uwanjani na bango lenye maandishi ya kumtaka kocha huyo ajiuzulu.
Mpango huo wa viongozi wa Yanga umelenga kuonyesha hasira zao kwa Papic, ambaye anadaiwa kuwa hataki kupokea ushauri kutoka kwao katika masuala mengi ya msingi, hasa upangaji wa timu.
Viongozi hao pia wamekerwa na kitendo cha Papic kuondoka kambini mjini Cairo, Misri akiwa na wachezaji wawili na kutokomea mahali kusikojulikana.
Yanga ilikwenda Misri kupambana na Zamalek katika mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika, ambapo ilichapwa bao 1-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa Yanga kusuka mipango ya kumng’oa Papic. Waliwahi kufanya mipango hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, lakini utekelezaji wake ulikwama kwa vile hawakuwa na pesa za kumlipa kwa ajili ya kukatisha mkataba wake.
Sababu zingine za viongozi hao kutaka kumng’oa kocha huyo ni kutokuelewana kwake na baadhi ya wachezaji, ambao amekuwa hawapi nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Wachezaji, ambao kocha huyo amekuwa haelewani na hivyo kutowapanga katika mechi muhimu ni Rashid Gumbo, Godfrey Taita, Chacha Marwa, Geofrey Bonny na Jerryson Tegete na hivyo kusababisha kuzuka kwa makundi mawili ya wachezaji.
Kuna habari kuwa, iwapo Papic atakubali kujiuzulu kutokana na shinikizo hilo la viongozi na wachezaji, huenda nafasi yake ikachukuliwa na Charles Kilinda, ambaye kwa sasa ni kocha wa JKT Ruvu.

Simba yaitimulia vumbi Yanga


SIMBA imeendelea kujichimbia kileleni na kuwaacha kwa tofauti ya pointi tatu wapinzani wao Yanga wanaofukuzana nao katika msimamo wa ligi kuu, baada ya kuifumua Kagera Sugar mabao 3-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, vinara hao wa ligi wakiwa na pointi 40 kibindoni na Yanga pointi 37, walishinda kutokana na Kagera kushindwa kuonyesha upinzani kabisa huku ukosaji mabao ukitawala kwa pande zote.

Baada ya dakika 20 za kosa kosa, Simba walisahihisha makosa kwa kiungo mshambuliaji Patrick Mafisango kufunga bao la kwanza dakika 26 kutokana na kupiga shuti kali ambalo kipa wa Kagera Andrew Ntalla, alishindwa kuliona.

Mafisango alifunga goli hilo kutokana na pasi maridadi ya Juma Nyoso aliyewahi mpira wa adhabu na kumpasia kiungo huyo.

Baada ya bao hilo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na Kagera hawakucheza kwa kasi kama Simba na walipoteza muda mwingi wakati wa kurusha mipira.

Walinzi Nassoro Masoud 'Cholo' na Amir Maftah walipandisha vyema mashambulizi kwa upande wa Simba iliyowapa wakati mgumu Kagera ambao walikuwa wanawategemea Shija Mkina anayecheza kwa wakata miwa hao kwa mkopo kutoka Msimbazi na Paulo Ngwai.

Katika dakika za mwanzo, wachezaji walikuwa wanateleza kutokana mvua iliyonyesha kabla ya kuanza mchezo huku Simba wakinusurika kufungwa dakika 10 na Mkina, ambaye alipiga mkwaju uliodakwa kwa umakini na kipa Juma Kaseja.

Mkina alipata nafasi hiyo kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Muganyizi Martin ya kuwachambua mabeki wa Simba na kutoa 'pande' hilo, huku shambulizi hilo likijibiwa na Emmanuel Okwi aliyewalamba chenga walinzi wa Kagera na kuachia shuti ambalo lilitoka nje na kuwa kona butu.

Yona Ndabila naye, alimchachafya Amir Maftah na kupata mwanya wa kupiga shuti ambalo lilitoka nje sentimita chache na lango la Simba. Said Dilunga pia shuti lake lilishindwa kulenga lango la Simba dakika tatu kabla mapumziko.

Kipindi cha pili Simba walionekana wana uchu wa kuendeleza ushindi kutoka na kuwashambulia Kagera, ambapo 50 kama Felix Sunzu angekuwa makini angeipatia timu hiyo bao kutokana na mpira wake wa kichwa kutoka nje licha ya kuwazidi kete vizuri mabeki kwa kuwahi mpira wa juu.

Dakika 54 Katende alijibu mapigo kwa kumpa pasi Ndabila, lakini naye alifuata nyayo za Sunzu kwa kukosa bao na Felix Themi alisawazisha makosa ya wachezaji hao ya kukosa ufundi wa kulenga milango kwa kufunga bao la kusawazisha kwa wageni hao.

Themi aliyeingia badala ya Mkina alifunga bao hilo dakika 57 kwa shuti kali lililomshinda Kaseja aliyeanza kupangua krosi ya Katende na kumkuta mfungaji.

Kagera baada ya kusawazisha bao hilo waliridhika na kuanza kujiangusha na kusababisha mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha kumuonya kwa mdomo kipa Ntalla kwa kupoteza muda. Mwamuzi Swai aliwapa Simba penalti kutokana na beki David Charles kumuangusha Shomari Kapombe katika kisanduku cha hatari na 'tuta' hilo lilifungwa na Mafisango dakika 90, huku uzembe ukiendelea kuwagharimu Kagera kwa Sunday Frank kunyang'anywa mpira na Sunzu aliyepiga krosi iliyomkuta Okwi aliyepiga chenga mabeki na kufunga bao la tatu dakika za majeruhi.

Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Amir Maftah, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.

Kagera: Andrew Ntalla, Muganyizi Martin, David Charles, Freeman Nesta, Sunday Frank, George Kavila, Shija Mkina/Felix Themi, Daud Jumanne,Said Dilunga/Mike Katende, Yona Ndabila na Paulo Ngwai.

Saturday, March 3, 2012

Simba yazindua vipindi maalumu vya TV






































































Hivi ndivyo ilivyokuwa siku klabu ya Simba ilipozindua vipindi maalumu vya kwenye televisheni, ambavyo vitakuwa vikionyeshwa mara moja kwa wiki kupitia luninga ya clouds. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Cleopatra uliopo kwenye jengo la Quality Plazza, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam. Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Kassim Majaliwa.



Friday, March 2, 2012

Mashujaa yaibomoa tena Twanga Pepeta



BENDI ya muziki wa dansi ya Mashujaa Musica imezidi kuibomoa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ baada ya kumyakua mnenguaji wake mahiri,Lilian Tungaraza maarufu kama ‘Intanet’.
Meneja wa Mashujaa Band Maximilian Luhanga alisema kwamba wamweamua kuwachukua wanamuziki hao ili kuimarisha bendi yao katika idara hizo na tayari wameshasaini mkataba wa kuitumikia bendi hiyo kwa miaka miwili ambao onyesho la utambulisho linatarajiwa kufanyika jumatano ijayo katika ukumbi wa Nyumbani Lounge.
Hii ni mara ya pili kwa Mashujaa kuibomoa Twanga Pepeta ambapo mapema mwaka huu ilimyakua mmmoja ya waimbaji mahiri, Charlz Gabriel ‘Chaz Baba’. Kwa hisani ya http://mamapipiro.blogspot.com/

KIYOVU YAWASILI DAR



TIMU ya soka ya Kiyovu kutoka Rwanda imewasili nchini kwa ajili ya pambano lake la marudiano la michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba linalotarajiwa kuchezwa kesho kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kiyovu iliwasili nchini jana ikiwa na kikosi cha wachezaji na viongozi 25.

MTOTO WA KIBONGO AULA SENEGAL



Mchezaji Sifael Orgenes Mollel (14) amechaguliwa katika mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwenda kituo cha vipaji (centre of excellence) kilichoko Dakar, Senegal.
Mollel kutoka kituo cha Karume alichaguliwa katika mchakato wa mwaka jana uliofanywa na mng’amua vipaji vya soka (scout) kutoka Hispania kwa niaba ya Aspire Football Dreams yenye makao makuu yake Doha, Qatar.
Mpango huo wa Aspire Football Dreams kwa Tanzania una vituo 14 na mchakato wa kusaka mchezaji mmoja kila mwaka uhusisha vituo vyote hivyo ambapo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto wasiopungua 176.
Mbali ya Karume, vituo vingine ni Kigamboni, Kawe, Tandika, Makongo, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani na Tabata.
Mollel atakuwa kwenye kituo hicho cha Dakar kwa muda usiopungua miaka mitatu na anatarajiwa kuondoka nchini Machi 6 mwaka huu.
Kwa mwaka wa kwanza wazazi wake watalipwa dola za Marekani 2,500, wa pili dola 2,750 na wa tatu dola 3,000.
Mpango wa Aspire Football Dreams ambao unafadhiliwa na mtoto wa Mfalme wa Qatar una vituo viwili vya kuendeleza watoto wenye vipaji (centre of excellence) ambayo viko Doha na Dakar. Mpango huo huo pia unaendeshwa katika nchi 16 tofauti duniani. Nchi hizo ni Cameroon, Costa Rica, Gambia, Ghana, Guatemala, Ivory Coast, Kenya, Mali, Nigeria, Paraguay, Rwanda, Senegal, Tanzania, Thailand, Uganda na Vietnam.
U17 KUJINOA KWA RUVU SHOOTING
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) leo (Machi 2 mwaka huu) imeanza kambi yake ya wiki moja ambayo hufanyika kila mwezi jijini Dar es Salaam chini ya kocha Kim Poulsen.
Serengeti Boys inayofanya mazoezi Uwanja wa Karume itahitimisha kambi hiyo Machi 9 mwaka huu kwa kucheza mechi na timu ya U20 ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani ambayo iko Ligi Kuu ya Vodacom.
Baada ya Serengeti Boys kumaliza kambi Machi 9 mwaka huu, siku hiyo hiyo timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) nayo itaingia kambini chini ya Poulsen katika mpango wa timu hizo kufanya mazoezi ya wiki moja kila mwezi na kucheza mechi moja.

Thursday, March 1, 2012

MZEE YUSSUF AWAPIGA BAO THABITI NA ALLY J

Mwimbaji nyota wa muziki wa taarab nchini, Mzee Yussuf amewabwaga mahasimu wake, Thabiti Abdul na Ally J katika shindano la kumtafuta nani mkali wa kupiga kinanda katika muziki huo.

Shindano hilo liliendeshwa kwa takriban mwezi mmoja kupitia blogu hii ya liwazozito, ambapo wasomaji wake walitakiwa kupiga kura ili kumchagua nani mkali kati yao.

Mmiliki wa blogu hiyo, Rashid Zahor amesema shindano hilo lilianza mwishoni mwa Januari na kumalizika Februari 29 mwaka huu.

Jumla ya kura zilizopigwa kwa washiriki wote wanne wa shindano hilo, akiwemo Chid Boy ni 47.

Mzee ni mwimbaji na kiongozi wa kundi la Jahazi, Thabiti ni mmoja wa wakurugenzi wa kikundi cha Mashauzi Classic, Ally J ni rais wa kundi la Five Stars Modern Taarab wakati Chid Boy ni mpiga kinanda wa Jahazi.

Mzee aliongoza kwa kupata kura 23, ambazo ni sawa na asilimia 48 ya kura zilizopigwa.

Thabiti alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 14, ambazo ni sawa na asilimia 29 ya kura zilizopigwa.

Ally J alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura saba, ambazo ni sawa na asilimia 14 ya kura zilizopigwa wakati Chid Boy alishika mkia kwa kupata kura tatu, ambazo ni sawa na asilimia sita.

Nachukua fursa hii kuwashukuru wale wote walioshiriki kupiga kura kwa ajili ya kumchagua nani mkali wa kupiga kinanda. Blogu yenu hii itaendelea kuwaandalia mashindano ya wasanii mbalimbali kwa lengo la kubaini ubora wao kupitia kwenye kazi zao.

KHADIJA YUSSUF ANAPOMTUZA MZEE YUSSUF



KIONGOZI wa kundi la taarab la Jahazi, Mzee Yussuf (kulia) akitunzwa pesa na dada yake, Khadija Yussuf wakati alipokuwa akiimba wimbo wake mpya wa Mpenzi Chokolate katika onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.

Odama sasa kutengeneza filamu zake mwenyewe


BAADA ya kung’ara kwa muda mrefu katika fani ya uigizaji filamu, mwanadada Jenifer Kyaka ‘Odama’ sasa ameamua kuwa mtayarishaji wa fani hiyo.
Odama alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ameanzisha kampuni yake ya J. Production kwa ajili ya kazi hiyo.
Mwanadada huyo alisema amefikia uamuzi wa kuanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kutimiza ndoto yake ya kuwa mjasiliamali.
Odama alisema kampuni hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kurekodi filamu atakazokuwa akizitayarisha yeye mwenyewe.
Hata hivyo, Odama alisema kampuni hiyo pia itakuwa ikitoa huduma ya kupiga picha za filamu kwa ajili ya watayarishaji wengine.
“Kwa sasa hali ya ushindani ni kubwa sana kwa hiyo kama hauna kampuni kwa ajili ya utayarishaji wa filamu zako, utasumbuka na hata kuharibu kazi yako, “alisema.
“Unapotumia kampuni ya nje, unakutana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa kazi zako, lakini pia unakosa usimamizi wa kazi hiyo,” aliongeza mwanadada huyo mwenye umbo na sura jamali.
“Unaweza kupoteza muda mwingi kwani unapompatia kazi mtendaji hata kama ana kazi nyingi hasemi, hali ambayo inaweza kuharibu ratiba yako kwa kucheleweshewa kazi na hata kuharibiwa,”alisema Odama.
Mwanadada huyo aliwalalamikia wahariri wa filamu, ambao sio waaminifu kwa madai kuwa ndio chanzo kikubwa cha filamu nyingi kuchelewa kuingia sokoni ama kuharibika.
Odama ni mmoja wa wasanii waliopo kwenye tasnia ya filamu kwa miaka mingi, akiwa amecheza filamu zaidi ya 36 kati ya hizo, tisa akiwa ameshiriki kama mtayarishaji.
Baadhi ya filamu zilizompatia umaarufu mkubwa ni pamoja na All about love, Odama, Shumileta na Rude.
Alisema filamu ya Rude ameitengeneza kupitia kampuni yake ya J Production na tayari imeshakamilika. Alisema filamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote.
“Ni filamu nzuri sana kuanzia uigizaji, hadithi yake na hata wasanii walioigiza wako juu katika tasnia ya filamu. Wapenzi wa filamu zangu wajiandae kupokea kazi ya ukweli,” anasema Odama.
Washiriki wengine waliocheza filamu ya Rude ni Stanley Msungu ‘Chotara la Kihehe, Ruth Suka ‘Mainda’ na wengineo.

D'Banj kwa mademu!


LAGOS, Nigeria
MWANAMUZIKI nyota wa Nigeria, Dapo Daniel Oyebanjo ameelezwa kuwa ndiye anayeongoza kwa kuwa na wapenzi wengi nchini humo.
Dapo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la D’Banj anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wacheza filamu wengi wa Kinigeria.
Baadhi ya waigizaji wanaotajwa kumzimia mwanamuziki huyo ni pamoja na Genevieve Nnaji, ambaye amekuwa akikanusha madai hayo.
Genevieve alikaririwa hivi karibuni akidai kuwa, hana uhusiano wa kimapenzi na D’Banj na kwamba urafiki wao ni kama wa kaka na dada.
Mbali na Genevieve, mwanamuziki huyo pia alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu tajiri wa kike nchini humo, Ini Edo.
Waigizaji wengine wa kike, ambao wamewahi kuwa na uhusiano wa kike na D’Banj ni pamoja na Nadia Buari, Ruky Sanda, Mercy Johnson, Empress Njamah, Abiola Bashorun na mtangazaji wa channel O, Nonhle Thema.
Mzaliwa huyo wa Jimbo la Ogun pia amedaiwa kuwa na uhusiano na Amina Abubakar, binti wa makamu wa rais wa zamani wa Nigeria, Alhaji Atiku Abubakar na Jennifer Obayuwama, ambaye ni binti wa Polo Boss

Omotola akana kuwa mja mzito


LAGOS, Nigeria
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye mwigizaji machachari wa Nigeria, Omotola Jalade amekanusha madai kuwa ana uja uzito.
Omotola aliueleza mtandao wa nigeriafilms wiki hii kuwa, taarifa hizo ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
Mwanamama huyo mwenye watoto wanne ameamua kueleza ukweli wa mambo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti hivi karibuni kuwa, ni mja mzito.
Vyombo hivyo vya habari vilidai kuwa, Omotola amekuwa haonekani hadharani mara kwa mara kwa vile hataki ijulikane kwamba ana uja uzito.
“Hizi ni taarifa za kushangaza sana na sijui wamezipata wapi,”alisema mwanamama huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.
“Tulianza na tatizo la umeme na sasa linaishia kwenye tuhuma za uja uzito. Ndio tatizo la umaarufu,” aliongeza mama huyo, aliyecheza filamu zaidi ya 80.
Baadaye, mwanamama huyo aliandika kupitia mtandao wa tweeter:“Kile watu wanachokiandika, ndicho watu wanachokisoma.”
Omotola, ambaye pia ni mwanamuziki nyota nchini Nigeria, alitimiza umri wa miaka 34, ilipofika Februari 7 mwaka huu na amezaa watoto wanne na mumewe, ambaye ni rubani wa ndege, Matthew Ekeinde.
Mbali na kuwa mwigizaji na mwanamuziki, Omotola pia anamiliki taasisi, ambayo inajihusisha na kuwasaidia watoto yatima na wenye matatizo.

EMEM: Sijavunja ndoa ya Monalisa


LAGOS, Nigeria
MTAYARISHAJI maarufu wa filamu katika Nollywood, Emem Isong amekanusha madai kuwa, amechangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa ya mcheza filamu nyota wa nchi hiyo, Monalisa Chinda.
Akihojiwa na mtandao wa nigeriafilms wiki hii, Emem alisema licha ya taarifa hizo kumsikitisha, pia zimemfadhaisha kwa sababu hazina ukweli wowote.
“Nilijisikia vibaya sana na kushangaa kwa nini walizusha maneno hayo?” Alisema Emem.
“Kwani mimi ni Mungu? Nawezaje kuvunja ndoa ya mtu mwingine? Ni jambo la kawaida kutokea katika maisha ya binadamu,”aliongeza mwanamama huyo.
Emem alisema Monalisa ni rafiki yake wa muda mrefu na walikuwa na kawaida ya kutembeleana mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Emem, kila Monalisa alipokuwa na tatizo, alipenda kwenda kupumzisha akili nyumbani kwake na haoni iwapo kwa kufanya hivyo, alishiriki kuiparaganyisha ndoa yake.
Alisema hadi sasa haelewi ni kwa nini watu wamemzushia maneno hayo, lakini alisisitiza kuwa, Mungu ndiye anayeujua ukweli wa jambo hilo.
Emem amejitokeza kuwa mtayarishaji maarufu wa filamu nchini Nigeria na filamu zake nyingi zimejizolea umaarufu mkubwa. Emen ni mkali katika kuandika maelezo ya filamu na amekuwa akiifanyakazi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Siwezi kuacha uigizaji filamu-Ini Edo



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu tajiri wa kike nchini Nigeria, Ini Edo amesema kamwe hawezi kuachana na fani hiyo licha ya kufunga ndoa hivi karibuni.
Ini alisema mjini hapa wiki hii kuwa, licha ya kuishi mbali na mumewe, ndoa yao inakwenda vizuri na kila mmoja anaheshimu kazi ya mwenzake.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo jamali, alifunga ndoa mwaka jana na mfanyabiashara, Philip Ehiagwina wa Nigeria, ambaye anaishi Marekani.
“Nimeweza kuimiliki ndoa yangu,” alisema Ini. ‘Inategemea jinsi unavyoweka vipaumbele vyako na kuepuka vitu visivyokuwa na maana. Unapaswa kufahamu ni wakati gani unapaswa kuwepo mahali fulani na ni wakati gani hupaswi kuwepo mahali hapo.’
‘Ninachoweza kukifanya ni kuweka sawa maisha yangu ya kawaida na yale ya kikazi. Mume wangu anaishi Marekani, lakini tunakutana mara kwa mara. Aliondoka Nigeria Januari mwaka huu na mimi nitakwenda Marekani hivi karibuni, ‘ aliongeza.
‘Sifikirii iwapo nitaacha uigizaji. Naweza kujitosa katika kazi zingine, ambazo zinahusiana na filamu,’ alisisitiza mwanadada huyo.
Alipoulizwa kuhusu kashfa mbalimbali ambazo zimekuwa zikimuandama, Ini alisema mumewe anamfahamu vyema kuliko mtu mwingine yeyote.
‘Baadhi ya wakati wanapozungumza mambo kuhusu mimi, huwa tunakuwa pamoja. Hunitazama na kuniuliza kama mimi ni mtu yule yule, ambaye watu wanamzungumzia. Anaelewa nini ninachoweza kukifanya, ‘ alisema.
Ini alisema kamwe hajutii kuwa mwigizaji kwa vile fani hiyo imemwezesha kunufaika kimaisha. Alisema kwake, anajihisi amejaliwa kuwa na kipaji cha kazi hiyo.
‘Napenga uigizaji, licha ya mitazamo finyu kuhusu mimi. Sifikirii iwapo ningependa kufanya kitu kingine. Lakini baadhi ya wakati, ninakerwa na vitu vinavyoandikwa kuhusu mimi, hasa vikiwa vya uongo. Nimewahi kuchukua hatua za kisheria huko nyuma. Hiyo ndiyo njia pekee ya kupigania haki zetu,’ alisema.
Mwanadada huyo alisema anapenda kuendelea kuwa mwigizaji kwa kipindi kirefu kijacho na kuongeza kuwa, hata kama hatoigiza, ataendelea kuwa katika biashara hiyo.
Ini alianza kung’ara katika fani ya uigizaji mwaka 2000 na tangu wakati huo hadi sasa,ameshacheza filamu zaidi ya 50. Ni mwigizaji mwenye kipaji, akili na mzuri wa sura na umbo.
Hivi karibuni, Ini ambaye anayo shahada ya sanaa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Calabar, alizindua filamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la I’ll take my chances.

Uhuru SC yajifua kwa Kombe la NSSF



WACHEZAJI wa timu ya soka ya Uhuru wakiwa mazoezini kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la NSSF inayotarajiwa kuanza Machi 10 mwaka huu.

Basena atumia mawakili kuibana Simba


KOCHA wa zamani wa Simba, Moses Basena ameamua kuweka mawakili wawili kwa ajili ya kudai haki zake kwa klabu hiyo baada ya kuvunja mkataba kati yao.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Uganda juzi, Basena alisema amefikia uamuzi huo baada ya kugundua kuwa, uongozi wa Simba unakwepa kumlipa haki zake.
Basena alisema tayari ameshawasiliana na mawakili hao na kuongeza kuwa, wanaweza kufungua kesi ya madai dhidi ya Simba wakati wowote.
Uamuzi wa Simba kufungua kesi hiyo umekuja baada ya Simba kuvunja mkataba wake wa miaka miwili na kumwajiri kocha mpya, Milovan Cirkovic kutoka Serbia.
Awali, kocha huyo kutoka Uganda aliwasilisha malalamiko yake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kabla ya kuyapeleka kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Uongozi wa Simba ulikaririwa hivi karibuni ukidai kuwa, umemtaka kocha huyo awasilishe vyeti vyake kabla ya kumlipa madai yake.
Alipouilizwa jana kuhusu suala hilo, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema hana taarifa yoyote juu ya jambo hilo.

Jabu, Ulimboka wapigwa chini Msimbazi


UONGOZI wa klabu ya Simba umeamua kuwaondoa kambini wachezaji wake wawili, Juma Jabu na Ulimboka Mwakingwe.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wachezaji hao wameondolewa kambini kutokana na kuwa majeruhi.
Kamwaga alisema Jabu anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu wakati Ulimboka bado anaendelea kutibiwa nyonga.
Ofisa huyo wa Simba alisema wachezaji wengine wanaendelea na mazoezi kwenye kambi yao iliyopo Mbamba Beach nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Kiyovu ya Rwanda.
Simba inatarajiwa kurudiana na Kiyovu mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya awali iliyopigwa wiki mbili zilizopita mjini Kigali, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Ili ifuzu kusonga mbele, Simba inahitaji ushindi wa idadi yoyote ya mabao.
Katika hatua nyingine, Kamwaga amesema kikosi cha Kiyovu kinatarajiwa kutua nchini leo jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo imepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Wanyama iliyopo Sinza.
Kamwaga alisema Kiyovu inakuja nchini ikiwa na kikosi cha watu 25 wakiwemo wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.
Alisema Simba haina wasiwasi na Kiyovu na kusisitiza kuwa, wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kusonga mbele.
Wakati huo huo, uzinduzi wa kipindi cha Simba, ambacho kitakuwa kinarushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds umepangwa kufanyika kesho.
Uzinduzi huo utafanyika kwenye ukumbi wa Cleopatra uliopo kwenye jengo la Quality Plaza lililopo barabara ya Nyerere mjini Dar es Salaam.

Wapiganaji 10 kuiongoza Yanga Misri


VIONGOZI 10 ‘wapiganaji’ wa klabu ya Yanga wanatarajiwa kuiongoza timu hiyo kwenda Misri kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, msafara wa Yanga utakuwa na wachezaji na viongozi wasiopungua 40 na utaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri.
Sendeu alisema kamati ya utendaji ya Yanga imeamua viongozi 10 waandamane na timu hiyo kwenda Misri kwa ajili ya kuwatoa hofu wachezaji na pia kukabiliana na vitendo vyovyote vya hujuma.
Alisema msafara wa timu hiyo utaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa.
Aliwataja viongozi wengine watakaofuatana na timu hiyo kuwa ni Mwenyekiti, Lloyd Nchunga na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa. Wengine ni wajumbe wa kamati ya utendaji Ally Mayay, Mussa Katabalo, Tito Solo, Theonest Rutashobora, Seif Ahmed, Kibwana Matokeo na Abdalla Bin Kleb.
Hata hivyo, Sendeu hakuwa tayari kutaja kikosi cha wachezaji kinachotarajiwa kwenda Misri, lakini alisema wachezaji sita wataachwa kutokana na sababu mbalimbali.
Aliwataja wachezaji watakaoachwa kuwa ni Yaw Berko, Salum Telela, Mohamed Mbegu, Godfrey Bonny.
Wachezaji wanaotarajiwa kuwemo kwenye msafara huo ni makipa Shaaban Kado na Saidi Mwalami. Mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Godfrey Taita, Nadir Haroub, Athumani Iddi, Chacha Marwa.
Viungo na washambuliaji ni Seif Kijiko, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Hamizi Kiiza, Davis Mwape, Kenneth Asamoah, Shamte Ally, Kigi Makasi, Jerry Tegete na Pius Kisambale.
Yanga na Zamalek zinatarajiwa kurudiana keshokutwa katika mechi itakayopigwa kwenye uwanja wa jeshi mjini Cairo. Mechi hiyo haitakuwa na watazamaji na kila timu imeruhusiwa kuingia na watu wasiozidi 40.
Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Ili ifuzu kusonga mbele, Yanga italazimika kuishinda Zamalek ama kutoka nayo sare ya idadi kubwa ya mabao, ambayo yataiwezesha kunufaika na mabao mengi ya ugenini.

BONANZA LA TASWA MACHI 24


BONANZA la waandishi wa habari linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), limepangwa kufanyika Machi 24 mwaka huu kwenye ufukwe wa Msasani, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa Jamii na Sheria wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Steve Kilindo aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, kampuni yake imepanga kutumia sh. milioni 62.5 kudhamini bonanza hilo.
Kilindo alisema wamepanga kutumia kiasi hicho cha pesa ili kuhakikisha kuwa, bonanza hilo linafanyika kwa kiwango na ubora wa hali ya juu.
Alisema waandishi wa habari ni wadau wakubwa wa kampuni yake hivyo lengo lao kubwa ni kuona bonanza hilo linafana kwa vyakula, vinywaji, burudani na michezo mbalimbali.
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru TBL kwa kudhamini bonanza hilo kwa mwaka wa tano mfululizo na kuongeza kuwa, limekuwa likitoa fursa nzuri kwa wadau wa habari kukutana na kufahamiana.
Pinto alisema bonanza hilo linatarajiwa kuwakutanisha waandishi wa habari 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, ambao watashindano katika michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, riadha na mbio za kwenye magunia.