KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 11, 2011

SUNZU, KAGO, OKWI NI MOTO

EMMANUEL Okwi

VICTOR Costa


HARUNA Moshi


Boban, Costa wana soka la Ulaya

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Victors ya Uganda, Joseph Mutiaba amekichambua kikosi cha Simba kwa kusema, baadhi ya wachezaji wake ni tishio na wengine wanahitaji kunolewa zaidi.
Mutiaba alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa mara baada ya Simba kupambana na Victors na kuchapwa bao 1-0.
Pambano hilo lilikuwa sehemu ya tamasha la ‘Simba Day’, lililofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Kocha huyo alisema katika pambano hilo, Simba ilionyesha kiwango kizuri, lakini baadhi ya wachezaji wake walionekana kuwa na mapungufu kadhaa.
Mutiaba alisema mshambuliaji Emmanuel Okwi ni winga machachari, ana kasi na mwepesi wa kupiga chenga, lakini anahitajika kufanya mazoezi zaidi ili kujiweka fiti.
Alisema kisoka, Okwi ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda zaidi wa kuelewana na washambuliaji wenzake ili waweze kupanga mashambulizi ya uhakika na kufunga mabao kirahisi.
Kocha huyo alisema, katika pambano hilo, Okwi alitoa pasi nyingi, lakini zilishindwa kufanyiwa kazi na wachezaji wenzake kutokana na kuzidiwa kasi na mipira.
Kwa upande wa Gervas Kago, kocha huyo alisema ni mchezaji mwenye nguvu na stamina na uwezo wa kumiliki mpira, lakini anahitaji msaada wa karibu kutoka kwa mawinga wenzake.
Mutiaba alisema, mchezaji huyo kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati alikuwa akishindwa kufanya maamuzi sahihi na ya haraka kutokana na kukosa msaada kutoka kwa wenzake na hivyo kupiga mipira mbele bila malengo.
Alimwelezea mshambuliaji Felix Sunzu kutoka Zambia kuwa, ni mchezaji mzuri, lakini mashabiki wa Simba wamekosa uvumilivu na kumpa muda wa kutosha kuisoma soka ya Tanzania.
Alisema Sunzu hana tofauti na mshambuliaji Fernando Torres, aliyesajiliwa kwa dau kubwa la pesa na Chelsea, akitokea Liverpool, lakini ameshindwa kuonyesha cheche zake kutokana na mashabiki kutompa muda wa kuzoea mchezo wa timu yake mpya.
“Kilichojidhihirisha kwa Torres ni kupatwa na kiwewe kila anapokuwa uwanjani kutokana na hofu ya jinsi ya kuwakonga nyoyo mashabiki wa Chelsea, hali ambayo pia imejitokeza kwa Sunzu,”alisema.
Mutiaba amewataka mashabiki wa Simba kumpa muda Sunzu wa kuizoea soka ya Tanzania na pia wasimruhusu kujawa na hofu moyoni kila anapokuwa uwanjani kwani wakifanya hivyo, watamfanya ashindwe kabisa kucheza soka.
Alimwelezea kiungo mpya Patrick Mafisango kutoka Rwanda kuwa, ana kazi nzito ya kumudu soka ya Tanzania kwa vile ni mchezaji pekee mpya aliyesajiliwa na Simba katika safu hiyo na hivyo kukosa ushirikiano wa kutosha.
Hata hivyo, Mutiaba alisema Mafisango ni mchezaji mwenye mipango na uwezo binafsi hivyo iwapo atapewa muda wa kutosha, anaweza kutoa msaada mkubwa kwa Simba.
“Kama mlivyoona, katika mchezo huu, amekuwa akizunguuka huku na kule akitafuta nani wa kupokezana naye mipira na kutoa pasi fupi fupi, lakini nadhani wenzake hawajauzoea mchezo huo,”alisema.
Akiwazungumzia beki Victor Costa na mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, kocha huyo alisema, wana uwezo wa juu kisoka, lakini wanapaswa kucheza kwa ushirikiano zaidi na wenzao wageni.
Mbali na kuwasifu wachezaji hao kimchezo, kocha huyo alisema, kutokana na soka waliyoionyesha, wanapaswa kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.

No comments:

Post a Comment