KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 3, 2011

MONALISA, ARINZE, OMOTOLA WANENA

OMOTOLA JALADE

SEGUN Arinze

MONALISA Chinda
LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Monalisa Chinda amesema hajutii kuachana na mumewe kwa sababu anayamudu na kuyafurahia maisha anayoishi hivi sasa.
Monalisa alisema mjini hapa wiki hii kuwa, ameshayazoea maisha hayo kwa sababu siku zote amekuwa akijipa moyo kwamba hakuna, ambalo hawezi kulifanya.
“Ni kwa sababu nimeshazoea. Kama utajiambia moyoni kwamba hili ni gumu, siwezi kulifanya, itakuwa hivyo. Kwa sasa mimi ni kama mwanaume, mwanamke na mama. Sina mwanaume wa kunisaidia,”alisema.
“Ni kweli najihisi kukosa kitu fulani, lakini sijali. Ndiye ninayepaswa kuhakikisha nyumba ipo katika hali nzuri, kuwasha jenereta na kupeleka gari kwa fundi. Hizi ni kazi za wanaume, lakini sina wa kuzifanya,”aliongeza.
“Sitaki kumtegemea mtu yeyote kwa sababu nikifanya hivyo, nitaonekana dhaifu. Niliweza kuzifanya kwa kupenda nilipoolewa, hivyo sioni tofauti. Sipendi watu wanifanyie mambo yangu,” alisema mwigizaji huyo.
Monalisa alisema ameamua kuanzisha safu maalumu kwenye gazeti moja la kila wiki la nchi hiyo kwa lengo la kuelezea uzoefu wake katika maisha ya ndoa.
Alisema tangu akiwa mdogo, alipenda kuandika matukio yake ya kila siku kwenye kitabu cha kumbukumbu na alikuwa akifanya hivyo hata baada ya kuolewa.
Mwigizaji huyo alisema, baada ya matatizo kuanza kutokea katika ndoa yake, mtu wa kwanza kumwendea alikuwa mama yake mzazi, ambaye alimuomba ushauri juu ya nini la kufanya.
Kwa mujibu wa Monalisa, mama yake alimshauri kufanya kile, ambacho moyo wake utamwelekeza kukifanya.
Katika hatua nyingine, mmoja wa waigizaji wenye mvuto nchini Nigeria, Segun Arinze amesema, hakujitosa kwenye fani hiyo kwa bahati ama upendeleo, bali alikuwa akiipenda tangu alipokuwa mdogo.
Arinze alisema wiki hii mjini hapa kuwa, baba yake hakuwa akipenda awe mwigizaji kwa vile alipendelea zaidi awe mwanasheria, lakini baadaye alikubaliana na uamuzi wake.
Alisema baba yake alilazimika kuukubali uamuzi wake huo baada ya kufurahishwa na filamu aliyocheza na kuonyeshwa kwenye TV ya nchi hiyo.
“Baba alipoiona, alikuja akaniamsha ili nami niione. Alipokwenda kazini asubuhi, watu wengi walimweleza kwamba waliniona kwenye TV. Lakini bibi yangu hakuvutiwa na kazi hiyo. Alitaka niwe mwanasheria. Alidai kuwa, kazi hiyo hailipi na ya kihuni,”alisema.
Arinze, ambaye alianza uigizaji mwaka 1984 alisema, hali ilikuwa tofauti kwa mama yake mzazi, ambaye siku zote alikuwa akimuunga mkono.
Kwa mujibu wa Arinze, bibi yake alibadili msimamo siku alipomtembelea nyumbani kwake Suleja, ambako umati mkubwa ulikuwa ukimfuata kwa nyuma huku ukipaza mayowe kwa kusema Black Arrow.
“Ninaposema kundi la watu, namaanisha zaidi ya watu alfu nne. Bibi alichanganyikiwa. Hakuyaamini macho yake na aliona fahari juu yangu na kazi niliyoichagua,”alisema.
Mbali na uigizaji, Arinze ambaye ana shahada ya sanaa, pia ni mwanamuziki, mtayarishaji na mwongozaji wa filamu.
Wakati huo huo, nyota wa uigizaji nchini Nigeria, Omotola Jalade amesema kuolewa na mume, ambaye hajihusishi na fani hiyo, kumekuwa na faida kubwa kwake.
Omotola aliueleza mtandao wa GSC wiki hii kuwa, iwapo angeolewa na mwigizaji mwenzake, ama mtu yeyote anayejihusisha na fani hiyo, huenda ndoa yake isingedumu hadi sasa.
“Mume wangu hajihusishi na fani yangu, hivyo simuoni mara kwa mara na pia mimi sihusiani na fani yake, hivyo hanioni mara kwa mara. Kwa jumla, hatuonani mara kwa mara,”alisema.
“Nadhani hiyo inatupa nafasi, kitu ambacho ni muhimu katika ndoa. Anayo nafasi, nami ninayo nafasi. Usisahau kwamba, ndoa ni muungano wa watu wawili tofauti,”aliongeza.
“Nilikuwa na maisha yangu kabla ya kukutana naye, kama ilivyo kwake yeye, hivyo tunahitaji kuelewana, kuheshimu uhuru wa kila mmoja wetu na mambo yetu binafsi,” alisema mwanamama huyo mwenye watoto wanne.
“Nadhani moja ya sababu zinazofanya ndoa nyingi kuwa kwenye matatizo ni wanandoa kutoelewa kwamba wao ni watu tofauti na wapo kwenye muungano wa maisha,”alisema.
“Sababu kubwa ya sisi kuwa pamoja ni kujaribu kuyafanya maisha yetu yawe mepesi siyo magumu. Ninachomaanisha ni kwamba, sipaswi kukufuatilia muda wote nawe hupaswi kufanya hivyo,” aliendelea kulonga mwanamama huyo.

No comments:

Post a Comment