KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 11, 2011

Sudan Kusini yaomba kucheza Chalenji


SUDAN Kusini imewasilisha maombi ya kutaka kujiunga na Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema kwa njia ya simu juzi kutoka Nairobi kuwa, Sudan Kusini iliwasilisha maombi hayo mapema mwezi uliopita.
Hata hivyo, Musonye alisema nchini hiyo haiwezi kupata uanachama wa CECAFA hadi itakapopata baraka za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) na lile la Afrika (CAF).
Musonye alisema, kabla ya kuwasilisha maombi hayo, Sudan Kusini ilikuwa imeonyesha nia ya kutaka kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini Tanzania.
“Wanapaswa kusubiri kabla ya kuruhusiwa kushiriki katika michuano inayoandaliwa na CECAFA,”alisema Musonge.
Kwa mujibu wa Musonye, nchi hiyo inapaswa kwanza kupata uanachama wa FIFA na CAF ndipo iruhusiwe kushiriki katika michuano inayoandaliwa na baraza hilo.
“Tunafurahia kuwa na nchi nyingine mpya ndani ya ukanda huu wa Afrika, lakini ushiriki wake kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, utategemea baraka za CAF na FIFA,”alisema.
“Tumesaliwa na miezi minne kabla ya michuano hiyo kuanza na sidhani kama kwa wakati huo Sudan Kusini itakuwa tayari imeshapata baraka za vyama hivyo,”alisema.
Kwa kawaida, huchukua muda mrefu kabla ya nchi mpya kukubaliwa kuwa mwanachama wa CAF na FIFA. Zanzibar imekuwa ikiruhusiwa kushiriki michuano ya CECAFA, lakini bado haijaruhusiwa kushiriki kwenye mashindano ya FIFA kama taifa huru.
Kwa sasa, CECAFA inaundwa na nchi wanachama 11. Nchi hizo ni Sudan Kaskazini, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Zanzibar, Somalia, Djibouti, Eritrea, Ethiopia na Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment