KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 3, 2011

AGBANI DAREGO: Nitafunga ndoa nitakapompata mwanaume anayenifaa




LAGOS, Nigeria
KWA kawaida, Agbani Darego hahitaji utambulisho wa aina yoyote kwani tayari jina lake lipo kwenye kitabu cha kumbukumbu cha Guiness, kufuatia kuwa mwanamke wa kwanza wa kiafrika kushinda taji la mrembo wa dunia.
Agbani (29) alishinda taji hilo miaka kumi iliyopita katika jiji la Sun City, lililopo nchini Afrika Kusini baada ya kuwabwaga washiriki wengine 92 kutoka katika nchi mbalimbali duniani.
Mrembo huyo, ambaye wiki iliyopita aliteuliwa kuwa balozi wa bidhaa za Arik, alisema wiki iliyopita kuwa, hana wazo la kuolewa kwa sasa na kwamba atafanya hivyo pale atakapompata mwanaume atakayemfaa.
“Unauliza lini nitafunga ndoa? (Anafikiri kwa muda). Nadhani ni pale utakapofika wakati mwanaume atakaponiomba nifunge naye ndoa na kuamini kwamba ndiye atakayenifaa,”alisema mrembo huyo.
Hata hivyo, mrembo huyo hakuwa tayari kuweka wazi iwapo anaye rafiki wa kiume kwa madai kuwa, hayo ni mambo yanayohusu maisha yake binafsi.
Alidokeza kuwa, anapenda kuwa na mwanaume mwenye uwezo wa kumfanya awe na furaha, bila kujali iwapo ana mvuto au la. Alisema kwake, mwonekano wa mwanaume haupi uzito.
Agbani alisema hadi sasa bado anaona fahari kubwa kwa kufanikiwa kutwaa taji la mrembo wa dunia akiwa na umri mdogo na siku zote amekuwa akimshukuru Mungu kwa mafanikio hayo.
Kwa mujibu wa mrembo huyo, kwa sasa fani hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa kama zilivyo sekta nyingine na kuongeza kuwa, anafurahi kwa vile yeye ni sehemu ya maendeleo hayo.
Mrembo huyo alikataa kuweka wazi kuhusu mkataba kati yake na Arik, lakini alisema anaona fahari kubwa kuwa balozi wa kinywaji hicho.
Alisema jukumu lake la kwanza baada ya kuteuliwa kuwa balozi wa Arik ni kupiga picha za kutangaza bidhaa hizo na kwamba mambo mengine yatafuata baadaye.
Agbani alisema amefanikiwa kuwa mwanamitindo baada ya kushinda taji la dunia na kusisitiza kuwa, anaifuahia kazi hiyo kwa sababu imemwezesha kupata mafanikio makubwa kimaisha.
Licha ya kazi yake hiyo kumfanya awe akisafiri mara kwa mara katika sehemu mbalimbali duniani, Agbani alisema hilo halimzuii kutekeleza majukumu yake mengine.
Agbani alisema anaona fahari kuzaliwa akiwa mwanamke kwa sababu ana uwezo wa kupata chochote anachokitaka, ikiwa ni pamoja na kurudi shule kusoma huku akiendelea kufanyakazi.
Mwanadada huyo wa Kinigeria hakuwa tayari kueleza iwapo kuna siku yoyote aliyowahi kupatwa na jambo lililomkatisha tamaa. Pia hakuwa tayari kueleza ni mambo gani yanayomfanya awe na furaha.
Lakini alidokeza kuwa, anapendelea zaidi kusoma vitabu na magazeti, kusikiliza muziki, hasa nyimbo za Dr. Sid, Tu Face na D’banj. Alisema anafurahia mafanikio ya wanamuziki hao wa Kinigeria.
Agbani alisema kwa sasa, hafikirii kuwa mwigizaji wa filamu kwa vile kazi hiyo inahitaji kuwa na kipaji zaidi. Alisema anafurahia kazi inayofanywa na waigizaji wa nchi hiyo, lakini haelewi iwapo anao uwezo huo.
“Lakini ninachoweza kusema kamwe usiseme hapana, siku moja naweza kujikuta nami nikijitosa kwenye fani hiyo,”alisema.
Agbani alisema ameweza kuufanya mwili wake uendelee kuwa ulivyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 kutokana na kula mlo maalumu na pia kufanya mazoezi.
Alisema amekuwa akifanya mazoezi hayo chini ya mkufunzi maalumu nchini Marekani na pia ni mpenzi sana wa kucheza mchezo wa Yoga.
Mrembo huyo alisema kamwe katika maisha yake hatarajii kupiga picha za uchi ili apate pesa na kusisitiza kuwa, mwili wake hauuzwi. Amewataka wanawake wenzake wajiamini na kujaribu kufanya kila kitu bila kukata tamaa.

No comments:

Post a Comment