KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 3, 2011

JACKLINE WOLPER: Sipendi kufuatwafuatwa


TASNIA ya filamu nchini imezidi kushika kasi kiasi cha baadhi ya wasanii kuanza kufaidika kimaisha na kupata umaarufu maradufu.
Miongoni mwa wasanii hao, kuna walioanza mbali na kuteseka kuitangaza sanaa hiyo hadi kuja kupendwa na wengi na sasa imekuwa lulu nchini.
Wasanii kama Steven Kanumba, Vicent Kigosi ‘Ray’, Jacob Steven ‘JB’, Yvonne Charly ‘Monalisa’, Lucy Komba na wengineo wametoka mbali na jahazi la filamu hadi kupanda chati na kuvutia kizazi kipya.
Moja ya wasanii wa kizazi hicho ni Jackline Wolper, ambaye karibu miaka minne, amekuwa mwigizaji nyota wa filamu kutokana na kazi zake kukubalika ipasavyo.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika mapema wiki hii kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam, mwigizaji huyo ameeleza mambo mbalimbali kuhusu maisha yake ya uchezaji filamu na alivyofika alipo sasa.
Jackline katika moja ya mambo ya msingi, kwanza kabisa anasema licha ya kujikita kwenye uigizaji filamu kwa miaka michache, amekuwa staa anayekabiliwa na migogoro mingi, ambayo anadai haipendi kwa vile si tabia yake.
Amesema anapenda kuelewana, kucheka na kila mtu na hata kubadilishana mawazo, lakini anajuta kwa jinsi umaarufu unavyomuingiza katika bifu na watu mbalimbali.
“Ndiyo inatokea hivyo na wakati mwingine magazeti huwa yanaandika tu, lakini sitaki ugomvi na mtu yeyote napenda kuelewana na wenzangu,” anasema Jackline.
Akielezea tukio la kudaiwa alivamia jukwaa na kumtolea lugha chafu Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba mwezi uliopita, Jackline anasema hakuwa na lengo hilo na kilichoandikwa kimepotoshwa.
“Nilikwenda jukwaani kutaka anipe nafasi nizungumze kutolea ufafanuzi wa kitu alichokuwa anasema na sikutaka kumfanyia vurugu kabisa,” anasema Jackline.
Mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club mwezi uliopita, uliitishwa na Mwakifwamba kuzungumzia wasanii wa filamu kukosa nidhamu kwa kuvaa nguo zisizofaa kwa maadili na wingi wa kashfa zao za ngono kuchapishwa katika magazeti ya udaku.
Jackline anadaiwa alifura kwa hasira baada ya matamshi ya rais huyo wa TAFF kuonyesha kama yalikuwa yamemlenga yeye na baadhi ya kampani yake.
Akielezea dhana ya kuanzishwa Club ya Bongo Movie, ambayo yeye ni katibu wa umoja huo, anasema imelenga kuwashirikisha wasanii katika kusaidiana kwa hali na mali.
Jackline anakanusha kwamba walianzisha umoja huo kwa ajili ya kutaka kuua shirikisho la filamu nchini.
“Hiyo si maana yake bali tumeanzisha umoja wa kusaidiana kwa shida na raha na kuendeleza sanaa ya filamu nchini,” anafafanua Jackline.
Msanii huyo ametoa changamoto kwa wasanii wenzake wa filamu, wasiendekeze bifu kwa vile hazijengi na badala yake wakaze buti ili kuendeleza sanaa hiyo kwa vile sasa imekuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Amesema kwa sababu hiyo, wawekezaji wazalendo nao wawekeze katika filamu kuliko kuwaachia Watanzania wenye asili ya Kiasia pekee.
Jackline anadai kuwa, kujitokeza kwa Waasia wengi kuwekeza mitaji yao katika filamu, kuna maanisha kuwa ina faida, ambapo amewataka wazawa kuingiza mitaji yao ili kuongeza ushindani wa malipo kwa wasanii na kuondoa unyanyasaji uliokithiri.
“Kampuni zinazojihusisha na masuala ya kutengeneza filamu na kusambaza ni chache na karibu zote zinashikwa na waasia, tunataka na watanzania wengine waweke mitaji yao ili tulipwe vizuri na kutuinua wasanii wa filamu,” anasema.
Jackline amesema kuwa ana furaha baada ya kuingia mkataba wa kufanya kazi za filamu na Kampuni ya Papa-Z Entertainment kwa vile, inamlipa vizuri na ushindani uliopo umesaidia wasanii wengine kupata maslahi bora.
Amesema kuwepo kampuni chache kulisabisha baadhi yao wawe wanyonge kutokana na kunyanyasika katika usambazaji wa kazi, ambapo sasa kila inapoongezeka kampuni nyingine ya usambazaji, inakuwa nafuu kwao.
“Sasa mimi nina jeuri ya kuishi mjini kutokana na kampuni ya Papa-Z ambao wananilipa vizuri na ninashirikiana nao katika kazi nyingi,” anaeleza Jackline, ambaye pia ana kampuni inayoitwa Line Wolper Production, ambayo inasimamia kazi zake.
Akizungumzia manufaa aliyopata katika maisha yake tangu awe msanii wa filamu, anasema ukiacha ustaa, amenufaika kwa vingi ambavyo amedai ni siri yake.
Jackline amesema pamoja na unyonyaji wanaofanyiwa katika filamu, anamshukuru Mungu kwa alichopata maishani mwake, ambapo amekiri wasanii wenye majina makubwa angalau wanaambulia kitu kuliko chipukizi.
“Kwa sisi ambao tayari tuna majina makubwa kidogo alhamdulilah, lakini kwa chipukizi ndiko kuna kilio kikubwa sana kama cha hakimiliki kwani imekuwa vigumu kudhibiti na nadhani hili tatizo halitakwisha vizazi na vizazi,” anasema msanii huyo.
Jackline aliibuka katika filamu mwaka 2007 baada ya kushawishiwa na msanii Lucy Komba ajikite kwenye fani hiyo.
Anasema aliungwa mkono na kuelekezwa vitu vingi na msanii huyo mzoefu na alicheza filamu nyingi za ‘Ama zako ama zangu’, ‘Kipenzi changu’, ‘Red Valentine’ na ‘Family Tears’, ambazo ziliteka soko na kumfanya ajulikane.
Baadaye alitunga filamu zake mbili ya ‘Wekeend’ na ‘My Princess’, ambazo zilifanya vizuri sokoni na akapata moyo wa kuwa mwigizaji rasmi.
Filamu nyingine alizoigiza ni ‘Utumwa wa mapenzi’ na ‘All About Love’ iliyotungwa na Jennifer Kiaka ‘Odama’, ambayo anasema aliipenda kutokana na kuvaa vyema uhusika kwa kuwa aliigiza kama mtoto.
Jackline pia anasema katika filamu iliyomsisimua sana tangu awe msanii ni ‘Last Minutes’ ya Leah Richard a.k.a Lamata, ambayo alicheza na Bajomba.
“Naipenda na huwa nairudia kuitazama kwa sababu inaelimisha, kuna siku wakati natoka super market (dukani) kuna mtu mmoja alilia baada ya kukutana na mimi mlangoni alisema niliigiza maisha yake lakini, bahati nilikuwa pamoja na mtunzi (Lamata) alimuelewesha hakumtungia mtu kisa kile,” anasema msanii huyo.
Jackline amesema kuwa kwanza anajipenda mwenyewe halafu Irene Uwoya kutokana na kufanana naye kiasi cha kudiriki kumuita pacha wake, ambaye anadai vitu anavyofanya katika filamu na maisha yake kwa ujumla anavikubali.
Nje ya nchi anampenda msanii nyota wa filamu wa Marekani, Halle Berry kwa alivyo mtulivu katika uigizaji na msafi.
Msanii huyo amesema mwakani anatarajia kwenda Malyasia kusomea masuala ya biashara na masoko kwa vile matarajio yake ya baadaye kujikita katika fani hiyo.
Jackline Wolper alizaliwa Moshi Mjini mwaka 1988 na alisoma kwenye shule tatu tofauti, lakini aliishia kidato cha tano katika shule ya Masai mwaka 2007 na baada ya hapo hakuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu ambazo hakutaka kuzitaja.
Baadaye alijiunga na chuo cha USA Contact na kuhitimu stashahada ya masoko na biashara. Wazazi wa msanii huyo wanaishi Kibaha, Pwani na ni wafanyabiashara.

No comments:

Post a Comment