KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 11, 2011

K-SHER: Nilijitoa Tip Top kuheshimu ndoa yangu



Asema hawezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja

Alitaka kuasili mtoto albino ili kumsaidia, lakini mama yake aligoma


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khadija Shaaban ‘K-Sher’ amesema, aliamua kujitoa katika kundi la Tip Top Connection kwa lengo la kuheshimu ndoa yake.
K-Sher amesema, asingeweza kuendelea kuwemo kwenye kundi hilo kwa vile asingeweza kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.
Msanii huyo mwenye sauti maridhawa, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa na kituo cha Radio France International.
K-Sher alisema si kweli kwamba aliondoka kwenye kundi hilo baada ya kutimuliwa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini.
“Wakati nilipokuwa Tip Top Connection, nilikuwa peke yangu, sikuwa nimeolewa. Lakini kwa sasa mimi ni mama na mke wa mtu, napaswa kupanga mambo yangu mwenyewe,”alisema msanii huyo, ambaye mwanaye anajulikana kwa jina la Jam K.
“Nisingeweza kumudu kuendelea na muziki nikiwa Top Top Connection na wakati huo huo kuihudumia familia yangu kwa wakati mmoja, ndio sababu nimeamua kupiga muziki kwa kujitegemea ili niweze kupanga mambo yangu mwenyewe,”alisema.
K-Sher alisema madai kwamba aliondoka Tip Top Connection kwa kutimuliwa, hayana ukweli wowote na kusisitiza kuwa, yalitolewa na mmoja wa viongozi wa kundi hilo kwa lengo la kumpaka matope.
Alisema wakati alipoamua kuachana na kundi hilo, alitoa taarifa kwa uongozi, lakini kiongozi mmoja hakuufurahia uamuzi wake huo kwa vile yeye ndiye aliyekuwa chachu.
“Kiongozi huyo hakufurahia kuona nimeondoka Tip Top halafu nimekaa kimya. Alishangaa. Akaanza kunipakazia kwenye vyombo vya habari,”alisema.
“Kinachoshangaza, licha ya kiongozi huyo kunipakazia, akasema wananiruhusu nirudi. Sasa inakuwaje mtu aliyetimuliwa kundini kwa makosa ya utovu wa nidhamu anarejeshwa?” Alihoji.
“Na ni kwa nini nionekane mtovu wa nidhamu kwenye kundi? Mimi naheshimika na watu wote ndio sababu najuana na watu wengi,”alisisitiza msanii huyo, ambaye amewahi kuimba na wasanii mbalimbali nyota wa muziki huo.
Msanii huyo alisema, hafikirii iwapo kuondoka kwake Tip Top Connection kumeacha pengo, kwa vile wapo wasanii wengi wa kike wenye vipaji wanaoweza kuchukua nafasi yake.
K-Sher alikiri kuwa, yeye ni mmoja wa wasanii wachache wa muziki huo, ambao hawajawahi kukumbwa na kashfa ya aina yoyote na hiyo ni kutokana na kujiheshimu kwake mbele ya jamii.
Alisema malezi aliyoyapata kutoka kwa wazazi wake tangu akiwa mdogo yalifuata maadili ya kiislamu na ni watu wanaoheshimika, hivyo anapaswa kulinda heshima yao.
Mwanamama huyo alisema, licha ya kufanyakazi peke yake hivi sasa, ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwa vile anajuana na watu wengi hivyo anasikiliza na kuheshimu ushauri wao kwake.
Kwa sasa, K-Sher ameingia mkataba wa kufanyakazi katika Programu ya Wanamuziki Hai, ambayo lengo lake ni kutoa elimu kwa jamii inayokabiliwa na matatizo mbalimbali ya maisha. Kwa kuanzia, elimu hiyo imekuwa ikitolewa katika mkoa wa Shinyanga na Mererani mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa K-Sher, anaifurahia programu hiyo kwa vile imemwezesha kutembelea katika vijiji mbalimbali, kukutana na watu wengi na kujifunza mazingira tofauti ya maisha ya watu.
“Huko nyuma sikuwa nikifikiria maisha ya watu wengine, lakini sasa nimeweza kujifunza hilo na kubaini kuwa, asilimia kubwa ya watanzania, hasa wanaoishi vijijini, wanaishi maisha ya dhiki sana,”alisema.
Msanii huyo mwenye sauti maridhawa, inayofanana na ile ya ndege mnana wa porini alikiri kuwa, kuna wakati alitaka kuasili mtoto wa kike, ambaye ni albino, lakini mzazi wa mtoto huyo hakuwa tayari kumkubalia.
Alisema uamuzi wake huo, ulilenga kumsaidia mtoto huyo kwa vile alimpenda sana, hakufurahishwa na maisha ya wazazi wake na pia alitaka amwezesha kukabiliana na kadhina wanazopata watu wa jamii ya aina yake.
Alipoulizwa iwapo ni jambo linalowezekana kwa nchi za Afrika kuungana na kuwa kitu kimoja, K-Sher alisema hilo haliwezekani kutokana na tofauti ya maisha na mitazamo.
“Hilo ni jambo gumu hata kwa wasanii kwa sababu kila mtu anatoka katika mazingira tofauti, wapo wasomi na wasiosoma, wapo wanaoelewa na wasioelewa, wapo wanaoweka mbele na wasiopenda pese, hivyo ni vigumu,”alisema.
“Ingekuwa sote tuna mtazamo mmoja, jambo hilo lingewezekana,”alisisitiza.
K-Sher ni msemaji wa Umoja wa Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya nchini, ambao lengo lake ni kuwaunganisha wasanii wa muziki huo katika kushughulikia matatizo yao.
Aliyataja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha sheria ya hakimiliki inafuatwa na kuheshimiwa na pia usambazaji wa kazi zao unafanyika kwa njia ya halali.
Aliwataja wanamuziki wa kimataifa wanaomvutia, na ambao angependa siku moja afanye nao kazi kuwa ni P-Square, Fali Ipupa, Kofi Olomide, Salif Keita na Yvonne Chakachaka.

No comments:

Post a Comment