KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, April 29, 2016

MBEYA CITY KUWAKOSA BOBAN, FELIX KESHO


Kocha mkuu wa Mbeya City fc Kinnah Phiri ametangaza orodha ya nyota 18 watakao kuwa sehemu ya mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo  uliopangwa  kuchezwa jumamosi hii  Manungu Complex , Turiani, Morogoro.

Akizungunza na Mbeya City Fc muda mfupi  baada ya kumalizika kwa mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Sokoine jijini hapa, Kocha Phiri alisema kuwa hana tatizo na nafasi  ya 10 iliyopo timu yake hivi sasa kwenye msimamo wa ligi kwa sababu anaamini ushindi kwenye michezo miwili ijayo utakifanya kikosi chake kusogea mpaka nafasi ya 8.

“Msimamo wa ligi unaonyesha tuko kwenye nafasi ya 10, hili siyo tatizo sana kwa sababu kushinda mechi mbili zijazo kutatuingiza kwenye timu nane bora, hili ndiyo lengo letu, tunayo  michezo minne mbele nina uhakika kwamba kila mchezaji anafahamu kuwa tunatakiwa kuongeza pointi zaidi ili tumelize ligi tukiwa sehemu ya timu nane za juu” alisema.

Akiendelea zaidi Kocha  Phiri alisema kuwa kwenye mchezo huo wa  morogoro kikosini atawakosa nyota kama Raphael Daud anayeguza majereha ya mguu pia mlinzi Haruna Shamte  aliyekwenye zuio la kucheza kufuatia kadi za njano, huku pia akiwakosa Haruna Moshi Boban na nahodha Temi Felix ambaye  kwa muda mrefu amekuwa nje ya kikosi kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Ni wazi hatutakuwa na Haruna Moshi Boban anayesumbuliwa na maralia, pia tunamkosa Temi, tunafahamu alikuwa nje ya timu  akishughulikia masuala ya kifamilia amerudi kambini juzi hivyo kwa vyovyote hawezikuwa sehemu ya mchezo huo, Rahael Daud ni mgonjwa na Haruna Shamte ana  zuio la kadi za njano, kutokuwepo kwao hakuondoi dhamira yetu ya kushinda mchezo kwa sababu tumekuwa namaandalizi mazuri na muhimu kwa wachezaji wetu wengine ambao sasa wako tayari” …  alimaliza Kocha Phiri na kutaja baadhi ya nyota wakaosafiri tayari kwa kuivaa Mtibwa Sugar jumamosi hii.

Miongoni mwa nyota  ambao kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi  aliwataja  ni pamoja  na Juma Kaseja, Haningtony Kalyesubhula,John Jerome, John Kabanda,Yusuph Abdalah,Deo Julius, Tumba Lui,Hassan Mwasapili,Kenny  Ally, Hamidu Mohamed, na Meshack Samwel  na kusema  kikosi  chake  kinataraji kuanza  safari jioni ya leo moja kwa moja  kuelekea  wilayani Turiani.

YANGA YATINGA FAINALI KOMBE LA TFF, COASTAL UNION YATOZWA FAINI, MWAMUZI AFUNGIWA
Coastal Union imepoteza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga baada ya washabiki wake kuwa chanzo cha Mwamuzi kuvunja mchezo huo uliofanyika Aprili 24, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Aprili 27, 2016) jijini Dar es Salaam kwa kuzingatia Kanuni ya 28(2) ya Kombe la Shirikisho. Wakati mechi hiyo inavunjwa, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1.

Pia Coastal Union imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kuzingatia Kanuni ya 42(26) ya Ligi Kuu kutokana na vitendo vya vurugu za washabiki wake wakati wa mechi hiyo. Pia TFF haitasita kufungiwa uwanja huo iwapo vitendo hivyo vya vurugu za washabiki havitakoma.

Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah Kambuzi amefungiwa mwaka mmoja wakati Mwamuzi Msaidizi namba mbili Charles Simon ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi. Adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.

Mchezaji Adeyum Ahmed wa Coastal Union anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi kutokana na kitendo chake cha kumpiga kichwa Mwamuzi wa Akiba baada ya kutolewa nje. Hata hivyo, Ahmed hakufanikiwa kutimiza azma hiyo baada ya Mwamuzi huyo kumkwepa.

Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kutokana na kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho.

Vilevile malalamiko ya Coastal Union kutaka mechi hiyo irudiwe yametupwa baada ya Kamati ya Mashindano kubaini kuwa hayana msingi wowote.

MWILI WA PAPA WEMBA WAWASILI KINSHASA-DRC


Wednesday, April 27, 2016

UCHAGUZI YANGA KUFANYIKA KWA KUFUATA KATIBA ILIYOSAJILIWA NA SERIKALIKwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1968 na kama ilivyorekebishwa mwaka 1971, Msajili wa vilabu na vyama vya michezo ndiye mwenye mamlaka ya kusajili katiba za vilabu na za vyama vya michezo.

Kwa kuzingatia nguvu za mamlaka haya hivyo uchaguzi ujao wa yanga pamoja na chaguzi zote za vyama wanachama wa TFF zitafanyika kwa kusimamia kwenye Katiba halali iliyosajiliwa na kutambuliwa na Msajili wa vilabu na vyama vya michezo.

KAMATI YA NIDHAMU TFF KUKUTANA JUMAPILI


Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kinatarajiwa kufanyika Jumapili, Mei Mosi 2016 jijini Dar es salaam.

Kamati hiyo ya Nidhamu itapitia mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa.  Wafuatao kesi zao sitasikilizwa katika kikao hicho:

(i)  John Bocco – Azam FC

(ii) Shomari Kapombe – Azam FC

(iii) Aishi Manula – Azam FC

(iv) Amissi Tambwe – Yanga SC

(v) Donald Ngoma  - Yanga SC

(vi) Paulo Jinga – JKT Rwamkoma FC

(vii) Kipre Tchetche – Azam FC

(viii) Abel Katunda – Transit Camp

(ix) Zephlyn Laurian – JKT Rwamkoma FC

(x) Idrisa Mohamed – JKT Rwamkoma

(xi) DR. Mganaga Kitambi (Daktari) – Coastal Union

(xii)  Herry Chibakasa – Friends Rangers

(xiii) Ismail Nkulo – Polisi Dodoma

(xiv) Said Juma – Polisi Dodoma

(xv)  Idd Selaman – Polisi Dodoma

(xvi) Edward Amos – Polisi Dodoma

(xvii) Stewart Hall (Kocha)– Azam FC

ALFRED LUCAS OFISA HABARI MPYA TFF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Alfred Lucas kuwa Afisa Habari na Mawasiliano mpya wa shirikisho kuanzaia leo Aprili 27, 2016.

Alfred anachukua nafasi ya Baraka Kizuguto aliyehamishiwa katika Kurugenzi ya Mashindano kuwa Afisa Mashindano na Meneja wa Mifumo pepe ya Usajili (TMS).

Alfred ana uzoefu kutoka vyombo mbalimbali alivyovitumikia kama mwandishi wa habari na mhariri.

Kadhalika Alfred kitaaluma amesomea uandishi wa habari, uhusiano wa kimataifa na diplomasia pamoja na lugha.

Mawasiliano ya Afisa Habari,

Alfred Lucas:

Namba ya simu: 0769 088111

Tuesday, April 26, 2016

TAIFA STARS KUJIPIMA NGUVU NA HARAMBEE STARS


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na timu ya Taifa Kenya (Harambee Stars) Mei 29, 2016 jijini Nairobi.

Mchezo huo wa kirafiki utachezwa jijini Nairobi Mei, 29 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote mbili kujaindaa na michezo ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mapema mwezi Juni, 2016.

TFF kwa kushirkiana na FKF zimekubaliana kuwepo kwa mchezo huo wa kirafiki, utakotumika kama sehemu za maandalizi kwa timu zote kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu kwa AFCON 2017 mwezi Juni.

Kikosi cha Taifa Stars kianchonolewa na kocha mkuu, Charles Boniface Mkwasa kinatarajiwa kuingia kambini mwezi Mei, mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Vodacom (VPL) kujiandaa na mchezo huo wa kirafiki kabla ya kuwakabili Misri katika uwanja wa Taifa jijini Dra es salaam Juni 04, 2016.

Stars inajianda na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017 nchini Gabon dhdi ya Misri utakaochezwa Juni 04, mwaka huu.

Monday, April 25, 2016

UCHAGUZI MKUU YANGA SASA JUNI 5Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo imetangaza Juni 05, 2016 kuwa siku ya Uchaguzi Mkuu wa viongozi ndani ya klabu ya Young Africans SC ya jijini Dar es salaam.

Akiongea na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Wakili Aloyce Komba amesema mchakato mzima wa uchaguzi wa klabu ya Young Africans utakuwa ndani ya siku 33, ambapo mchakato unatarajiwa kuanza rasmi Mei 03, 2016.

Komba amesema jukumu lao Kamati ya Uchaguzi TFF  ni kusimamia na kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo unafanyika katika hali ya demokrasia.

Ifuatayo ni kalenda ya mchakato wa Uchaguzi katika klabu ya Young Africans SC:

Mei 03, 2016 Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, atatangaza mchakato wa kulabu ya Young Africans, nafasi zinazogombewa na kubandika kwenye mbao za matangazo.

Mei 04-9, 2016 – Kuanza kuchukua fomu za kugombea na mwisho wa kurudisha fomu kwa wagombea.

Mei 10, 2016 Kamati ya Uchaguzi TFF itakaa kikao cha mchujo wa awali  wa wagombea na kuandika barua za kuwajulisha wagombea juu ya mchujo wa awali.

Mei 11, 2016 Kamati ya Uchaguzi TFF itachapisha na kubandika kwenye mbao za matangazo orodha ya awali ya wagombea.

Mei 12-13, 2016 Kipindi cha kupokea na kuweka pingamizi kwa wagombea wote.

Mei 14-15, 2016 Kamagi ya Uchaguzi TFF itapitia pingamizi zote na kufanya usajili wa wagombea.

Mei 16, 2016 Kamati ya Uchaguzi TFF itatangaza na kubandika kwenye mbao za matangazo matokeo ya awali ya usahili.

Mei 17, 2016 Sekretarieti kuwasilisha masuala ya kimaadili kwenye Kamati ya Maadili ya TFF.

Mei 18-19, 2016 Kamati ya Maadili TFF itapokea, kusikiliza na kutolea maamuzi ya kamati ya maadili.

Mei 20, 2016 Kamati ya Maadili ya TFF itatangaza maamuzi ya kamati.

Mei 21-22, 2016 Kipindi cha kukata Rufaa kwa maamuzi ya masuala ya Kimaadili kwenye kamati ya Rufaa ya Maadili TFF.

Mei 23, 2016 Kamati ya Maadili tff itasikiliza rufaa za kimaadili.

Mei 24, 2016 Kamati ya Rufaa ya Maadili itatoa maamuzi ya Rufaa.

Mei 25-26, 2016 Kipindi cha kukata Rufaa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi kwenye kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TFF.

Mei 27-28, 2016 Rufaa kusikilizwa na kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.

Mei 29, 2016 Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TFF kutangaza maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Mei 30, 2016 Kamati ya Uchaguzi TFF kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa na kubandikwa kwenye mbao za matangazo.

Mei 31 – Juni 04, Kipindi cha kampeni kwa wagombea.

Juni 05, 2016 siku ya Uchaguzi Mkuu wa klabu ya Young Africans.

Wakati huo huo Kamati ya Rufaa ya TFF Jumamosi, itasikiliza pia rufaa ya klabu ya Geita Gold pamoja na rufaa ya kocha msaidizi wa Toto Africans Choke Abeid,

RIPOTI ZA WAAMUZI, KAMISAA ZAIBEBA YANGA DHIDI YA COASTAL UNIONRIPOTI za waamuzi na Kamisaa wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup kati ya wenyeji, Coastal Union na Yanga na Dar e Salaam zimetua TFF.
Na habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS SPORTS – ONLINE imezipata zinasema ripoti hizo zimeipeleka Yanga fainali baada ya mchezo kuvunjika dakika ya 110 jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mchezo huo ulivunjika wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-1 kufuatia mshika kibendera namba mbili, Charles Simon kupasuliwa juu ya jicho la kushoto kwa jiwe lililotupwa na shabiki.

Ripoti zote, ya marefa na kamisaa zinaonyesha mashabiki waliofanya fujo ni wa Coastal, maana yake Coastal ndiyo wanapoteza mchezo na Yanga inakwenda fainali,”kimesema chanzo.
Coastal Union ilitangulia kwa bao la kiungo Mcameroon, Youssouf Sabo kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma, mabao yote kipindi cha pili.
Mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao la pili mwanzoni tu mwa dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
Baada ya bao hilo, mchezo ukasimama dakika ya 105 kufuatia mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Coastal kuanza kutupa chupa na mawe uwanjani na kumjeruhi mshika kibendera namba mbili, Charles Simon juu ya jicho la kushoto.
Refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga akapuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huo dakika ya 110, huku mashabiki wakiendelea kuushambulia uwanja kwa mawe na chupa.
Kamisaa wa mechi, Osuri Kosuri kutoka Simiyu alisema kuwa wamelazikika kuvunja mchezo kufuatia vurugu zilizotokea uwanjani.
Kosuri alisema kuwa Usalama ulikuwa mdogo uwanjani hapo na askari walishindwa kuhimili vurugu.
Iwapo Yanga itapewa ushindi, itamenyana na Azam FC katika fainali mwezi ujao. Azam leo imeitoa Mwadui FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 2-2 baada ya dakika 120 Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

AZAM YATINGA FAINALI KOMBE LA TFFAZAM FC imetinga Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuwafunga wenyeji Mwadui FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Shujaa wa Azam FC alikuwa ni beki Aggrey Morris, aliyefunga penalti ya tano na kuamsha shangwe kwa wachezaji wenzake.
Wengine waliofunga penalti za Azam FC ni Nahodha John Bocco, Himid Mao, Allan Wanga na Waziri Salum wakati tatu za Mwadui zilifungwa na Malika Ndeule, Iddi Moby na Jabir Aziz.  Aliyekosa upande wa Mwadui ni Kevin Sabato.
Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Azam FC ikitangulia kwa bao la Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya tatu kabla ya Mwadui kusawazisha kupitia kwa dakika ya 82.
Katika dakika 30 za nyongeza Azam walitangulia tena kwa bao la Mcha dakika ya 97, kabla ya Jabir Aziz kuisawazishia Mwadui dakika 120.

IMETOLEWA KUTOKAA BLOGU YA BINZUBEIRY

PAPA WEMBA AFARIKI DUNIA AKIWA STEJINI
Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba, ambaye wengi tulimfahamu kama Papa Wemba alizaliwa June 14, 1949, katika kijiji cha Lubefu Wilaya ya Sankuru huko Congo amefariki leo mapema baada ya kuanguka katikati ya show kwa kilichoelezwa ni kama kupata kifafa wakati akifanya onyesho katika tamasha la Femua katika jiji la Abidjan Ivory Coast. 

Papa Wemba alikuwa mmoja ya wanamuziki wa kwanza kujiunga na bendi maarufu ya Zaiko mara baada ya kutengenezwa mwaka 1969, wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Jules Presley Shungu Wembadio, bendi hii ilikuja kutambulika kama chuo cha wanamuziki wakubwa wa Kongo, na iliweza kupoporomosha vibao kama “Chouchouna” (Papa Wemba), “Eluzam” na ” Mbeya Mbeya” (Evoloko Lay Lay), “BP ya Munu” (Efonge Gina), “Mwana Wabi” na “Mizou” (Bimi Ombale) na wimbo “Zania” (Mavuela Somo). 

Mwaka 1974 Shungu Wembadio , wakiwa na Evoloko Lay Lay, Mavuela Somo and Bozi Boziana wakaiacha Zaiko na kuanzisha kundi waliloliita Isifi Lokole. 

Julai 1975, Shungu Wembadio ndipo alipojipa jina la Papa Wemba, kundi la Isifi liliishi mwaka mmoja na kuwa na wimbo mmoja tu uliouza sana “Amazone” utunzi wa Papa Wemba. Novemba 1975, Papa Wemba, Mavuela Somo na Bozi Boziana wakaihama Isifi na kuanzisha kundi la Yoka Lokole, ambalo nalo halikumaliza mwaka. 

Kundi lilikufa pia kwa sababu Papa Wemba aliwekwa ndani kwa kudaiwa kuwa na mahusiano ya kingono na binti wa Jenerali wa jeshi. Baada ya mkasa huo ndipo Papa Wemba akaanzisha kundi la Viva la Musica, hiyo ilikuwa Februari 1977. Bendi ikaja na vibao kama “Mere Superieure,” “Mabele Mokonzi”, “Bokulaka,” “Princesse ya Sinza”. 

Viva la Musica ilitoa wanamuziki wakali ambao waliendelea kufanya makubwa kama vile katika muziki wa Kongo. Wakali kama Fafa de Molokai, Debs Debaba, King Kester Emeneya, Koffi Olomide, Djuna Djanana, Dindo Yogo, Maray-Maray, Lidjo Kwempa, Reddy Amissi, Stino Mubi ni kati ya wanamuziki waliowahi kupitia Viva La Musica. 

Koffi Olomide alipewa jina hilo na Papa wemba baada ya kutunga wimbo mmoja na Papa akafurahi na kumsifu na toka siku hiyo, Antoine Agbepa Koffi akajulikana kama Koffi Olomide .

Papa Wemba pia alijulikana kama muigizaji baada ya kucheza filamu ya La Vie est Belle na pia akaonekana tena kwenye filamu iliyoitwa Kinshasa Kids

Februari 18, 2003 Papa Wemba alikamatwa kwa kosa la kusaidia kuingiza wahamiaji haramu Ufaransa na akafungwa  kwa miezi mitatu na nusu. 


Mwenyewe alisema aliokoka wakati yuko jela na kuongelea hayo katika wimbo wake “Numéro d’écrou”, ambapo anasema Mungu alimtembelea gerezani. 

Mwaka jana, Papa Wemba alifanya onyesho Bagamoyo kwenye tamasha la Karibu Music Festival. Mungu amlaze pema Papa Wemba.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA JOHN KITIME

Friday, April 22, 2016

SERENGETI BOYS KUFUNGUA DIMBA NA WAMAREKANI


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini India (AIFF) limetoa ratiba ya michuano ya vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) itakayoanza kutimua vumbi Mei 15 -25 katika mji wa Goa nchini India kwa Serengeti Boys kufungua dimba na Marekani.

Michuano ya AIFF inashirikisha timu tano za vijana wenye umri chini ya miaka 17 kutoka nchi za Korea Kusini, Marekani, Malysia, Tanzania na wenyeji India.

Mashindano hayo yatafanyika katika uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa kuanzia Mei 15, ambapo Tanzania itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Marekani, huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utchezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.

Kikosi cha Serengeti Boys kianatarajiwa kuingia kambini mwishoni mwa mwezi Aprili, 2016 kujiandaa na michuano hiyo ya vijana na kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 mwakani nchini Madagascar.

YANGA SASA KUKIPIGA NA WAANGOLA KOMBE LA SHIRIKISHO


MECHI ZA MCHUJO WA KUWANIA KUCHEZA HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO
Yanga SC (Tanzania) Vs Sagrada Esperanca (Angola)
MO Bejaia (Algeria) Vs Esperance (Tunisia)
Stade Malien (Mali) Vs FUS Rabat (Morocco)
Etoile Du Sahel (Tunisia) Vs CF Mounana (Gabon)
TP Mazembe (DRC) Vs Stade Gabesien (Tunisia)
Ahli Tripoli (Libya) Vs Misr Makassa (Misri)
El Merreikh (Sudan) Vs Kawkab (Morocco)
Mamelodi Sundowns (Africa Kusini) Vs Medeama (Ghana)
(Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Mei 6 na 8 na marudiano kati ya Mei 17 na 18, 2016)

Thursday, April 21, 2016

YANGA YATUPWA NJE MICHUANO YA KLABU BINGWA AFRIKA


MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana walitolewa katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Al Ahly ya Misri.

Katika mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa mjini Cairo, Yanga ilikuwa ikihitaji ushindi ama sare ya zaidi ya mabao mawili ili iweze kusonga mbele.

Kutokana na kipigo hicho, Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam.

Mshambuliaji Abdalla Said ndiye aliyeisukuma Yanga nje ya mashindano hayo baada ya kuifungia Al Ahly bao la pili katika muda wa nyongeza.

Said alifunga bao hilo kwa kichwa kikali baada ya kupokea krosi kutoka kwa Walid Soliman. Kipa Dida wa Yanga alijaribu kuchupa kuokoa mpira huo, lakini aliishia kudaka hewa.

Al Ahly ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 52 kupitia kwa kiungo wake, Hossam Ghay, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa kona ya Ahmed Fathi.

Yanga ilisawazisha bao hilo dakika ya 57 kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma, akimalizia krosi ya Juma Abdul.

Wednesday, April 20, 2016

HASSAN KESSY BYE BYE SIMBA


UONGOZI wa Simba leo umetangaza kumsimamisha beki wao Hassan Kessy ambaye atakosa mechi tano sawa na muda wa kumalizika kwa mkataba wake ambapo yeye ametamka kwamba bado anajihesabia ni mchezaji wao na kama wamevunja mkataba basi wamlipe chake.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara ilieleza kuwa mechi tano alizopigwa marufuku beki huyo ni sawa na mwezi mmoja uliobaki kwenye mkataba wake hivyo tayari mchezaji huyo muda wake wa kukaa Simba utakuwa umekwisha.

Kessy amesimamishwa kwa kosa la kumchezea faulo mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher na hivyo kupewa kadi nyekundu na kuisababishia timu yake kucheza ikiwa pungufu ambapo Simba ilifungwa bao 1-0, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kessy amepata taarifa hizo mara tu baada ya viongozi wake kutangaza na kusikitika kwamba yeye alifanyiwa kitendo kibaya na kipa wao Vincent Angban, lakini hajachukuliwa hatua yoyote ila yeye aliyefanya kosa la kimchezo la bahati mbaya ameadhibiwa.

''Nimesikia taarifa hiyo na tayari  nimewasiliana na meneja wangu  (Athuman Tippo) ila bado najihesabia nipo kwenye mkataba na Simba, kama wao wamevunja mkataba wangu basi wanastahili kunilipa stahiki zangu, hizi ni changamoto japokuwa mimi nimefanyiwa jambo baya na wamekaa kimya.

''Mkataba wangu umebaki wa mwezi mmoja kwa maana unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Daima nitaendelea kumshukuru na kumuomba Mungu kwa kila hatua ninayopitia, hivyo haya yote yanayotokea namwachia yeye,'' alisema Kessy.

Simba imebakiza mechi tano ambazo  ni ile ya Azam, Mwadui, Majimaji, Mtibwa Sugar na JKT Ruvu.

AZAM YATUPWA NJE KOMBE LA SHIRIKISHOWAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho, Azam wametupwa nje baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Esperance ya Tunisia.

Kipigo hicho ilichokipata Azam jana, katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili, iliyochezwa mjini Tunis, kimeifanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-2.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Azam ilishinda mabao 2-1 na hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Licha ya kucheza ugenini, Azam iliweza kuwabana vyema wapinzani wao hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika, ambapo timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Katika kipindi hicho, kipa Aisha Manula wa Azam alilazimika kufanyakazi ya ziada mara kwa mara, kuokoa mashuti ya washambuliaji wa Esperance, waliokuwa na uchu mkubwa wa kufunga mabao.

Mambo yalibadilika dakika za mwanzo za kipindi cha pili baada ya mshambuliaji ASaad Bguir kuifungia Esperance bao la kuongoza kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 20.

Mpira huo wa adhabu ulitokana na kosa la beki wa kati wa Azam, David Mwantika, kumchezea rafu Ben Youssef wa Esperance, nje kidogo ya eneo la hatari.

Esperance ilifanikiwa kuongeza bao la pili lililofungwa na Haithem Jouini dakika ya 63 kabla ya kuongeza la tatu dakika ya 80 kupitia kwa Ben Youssef.

Katika mechi hiyo, Azam iliwakosa wachezaji wake nyota, Shomari Kapombe, ambaye ni mgonjwa, Kipre Tchetche, ambaye ni majeruhi, Serge Wawa, ambaye pia ni majeruhi na Jean Baptiste Mugiraneza, anayetumikia adhabu ya kadi.

Tuesday, April 19, 2016

TFF YAZITAKIA HERI YANGA NA AZAM


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezitakia kila la kheri timu za Azam FC na Yanga SC katika michezo yao ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).

TFF imezitaka Azam FC na Yanga kupambana katika michezo yao ugenini ili kupata matokeo mazuri yatakayozifanya ziweze kusonga mbele katika hatua inayofuata, ikiwa kwa sasa ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Azam FC inayoshirki michuano ya Kombe la Shirkisho barani Afrika (CAF CC), leo saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki inashuka dimba la Olymique 07 November, Rades jijini Tunis kuwakabili wenyeji Esperance ST katika mchezo wa marudiano.

Kesho Jumatano, Yanga SC watakuwa ugenini kuwakabili wenyeji Al Ahly SC katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya mabingwa barani Afrika (CAF CL), mchezo utakaochezwa saa 12:30 jioni katika uwanja wa Borg El Arab kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

SERENGETI BOYS KUKIPIGA NA MAREKANI, KOREA KUSINI


Timu ya taifa ya Tanzania vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ inatarajiwa kushiriki mashindano maalumu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini India, yatakayozishirikisha nchi za Marekani, Malasyia na Korea Kusini na wenyeji mapema mwezi Mei, 2016.

Chama cha Soka nchini India (AIFF) kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.

Jumla ya nchi tano zitashiriki mashindano hayo yatakayofanyika katika mji wa Goa, kuanzia Mei 15-25, 2016 ambapo michezo itachezwa kwa mfumo wa ligi kwa kila timu kucheza michezo minne, kabla ya mchezo wa mwisho wa fainali wa kumpata Bingwa wa mashiandano hayo.

Serengeti Boys, ambayo imeshacheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa mpaka sasa, mmoja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya vijana wa Misri (The Pharaohs), inatarajiwa kuingia kambini mwishoni mwa mwezi Aprili, 2016, katika hosteli za TFF, zilizoko Karume, kujiandaa kwa safari ya kuelekea nchini India kushiriki michuano hiyo.

Kikosi cha Serengeti Boys kinachonolewa na kocha Bakari Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa, chini ya mshauri wa ufundi wa timu za vijana Kim Poulsen, kinatarajiwa kuwa kambini kwa muda wa wiki mbili kabla ya safari kuelekea Goa, India kushiriki mashindano hayo.

Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys, kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Vijana barani Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 – 2 Julai, 2016.

Monday, April 18, 2016

SIMBA CHALI KWA TOTO AFRICAN

SI rahisi kuamini, lakini hivyo ndivyo ilivyotokea. Timu kongwe ya soka ya Simba jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 na Toto African ya Mwanza katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara,iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipigo hicho kilipeleka majonzi makubwa kwa mashabiki wa Simba, ambao mara baada ya mchezo huo kumalizika, waliwafanyia vurugu viongozi na wachezaji wa klabu hiyo.

Mashabiki hao walisikika wakisema kuwa, wamechoshwa kuiona timu hiyo ikipokea vipigo mfululizo na hivyo kupoteza kabisa matumaini ya kutwaa ubingwa.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Simba. Wiki iliyopita, timu hiyo kongwe pia ilichapwa bao 1-0 na Coastal Union katika mechi ya Kombe la TFF.

Bao pekee na la ushindi la Toto African, lilifungwa na kiungo Waziri Junior dakika ya 20 kwa shuti la umbali wa mita 20 lililotinga moja kwa moja wavuni.

Katika mchezo wa leo, Simba ilicheza pungufu baada ya beki wake wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu Edward Christopher wa Toto.

Mapema dakika ya 31, Kocha wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea maneno machafu refa Ahmed Simba wa Kagera.

Kwa matokeo hayo, Simba bado inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza 25, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 55 baada ya kucheza mechi 24. Yanga inaongoza kwa kuwa na pointi 59.

KICHUYA WA MTIBWA MCHEZAJI BORA WA MWEZI MACHI


Mshambuliaji Shiza Ramadhan Kichuya wa timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Machi kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu wa 2015/2016.

Kichuya alionyesha kiwango cha juu katika mwezi huo uliokuwa na raundi nne, hivyo kuisaidia timu yake kushinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza.

Katika mechi hizo ambazo zote Kichuya alicheza, alifanikiwa kufunga mabao mawili kati ya matano yaliyofungwa na timu yake. Alifunga dhidi ya Coastal Union kwa ushindi wa mabao 3-0, na JKT Ruvu Stars ambapo Mtibwa Sugar ilishinda mabao 2-1.

Uwezo aliouonyesha kwa mwezi huo ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amwite kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake kwa ajili ya mechi dhidi ya Chad iliyofanyika Machi 23, 2016 jijini N'Djamena.

Washindani wa karibu wa Kichuya walikuwa washambuliaji Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar, na Abdulrahman Mussa wa JKT Ruvu Stars ambao pia waling'ara kwa upande wa timu zao kwa mwezi huo.

Kichuya ambaye huu ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu, kwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora kwa Machi atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.

Wachezaji bora wa miezi mitatu iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Yanga (Januari 2016) na mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016).

TFF YALAANI VURUGU ZA SIMBAShirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limelaani kitendo cha baadhi ya mashabiki wa mpira wa miguu kufanya vurugu mara baada ya mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Toto Africans uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

TFF imesikitishwa na kitendo hicho cha mashabiki wa klabu ya Simba SC, na kusema inalaani kitendo hicho ambacho sio cha kiuana michezo, huku ikiwataka wanachama, washabiki kuheshimu viongozi wa klabu zao waliopo madarakani na kama kuna masuala ya kujadili wakayajadili katika vilabu vyao.

Mashabiki wa klabu ya Simba walifanya vurugu kwa kurusha mawe, wakilenga kuwadhuru viongozi wa klabu hiyo pamoja na wachezaji, magari waliyokuwa nayo baada ya timu yao kupoteza mchezo dhidi ya Toto Africans kwa bao 1- 0.

Jeshi la Polisi baada ya kuwasishi mashabiki kuondoka eneo la uwanja punde tu mchezo ulipomalizika, mashabiki hao walikaidi na kuendelea kurusha mawe hali iliyopelekea jeshi kutumia mabomu ya machozi kuwatanya katika eneo hilo.
 

Kufutia kitendo hicho, Jeshi la Polisi lilihakikisha bus la timu ya Simba SC na viongozi wake wanaondoka salama uwanjani baada ya kuwatawanya mashabiki hao, kwa kupitia mlango wa karakana ya wachina waliojenga uwanja huo.

Aidha TFF imeviomba vyombo vya Usalama na Ulinzi kuwachukulia hatua kali mashabiki waliohusika na kitendo hicho, kwani kufanya vurugu ni kosa la jinai na wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

TFF YATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA MASALU NGOFILO


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetuma salamu za rambirambi kwa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mwanza (MZFA), kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti mstaafu wa MZFA na makamu mwenyekiti wa FAT Silvanus Makalu Ngofilo aliyefariki dunia juzi jijini Mwanza.

Katika salamu zake, TFF imewapa pole familia ya marehemu Ngofilo ndugu, jamaa, marafiki, wadau wa mpira wa miguu kanda ya Ziwa na kusema Shirikisho liko pamoja nao katika kipindi hiki cha maomblezo.

Mazishi ya Silvanus Makalu Ngofilo yatafanyika kesho Jumapili kijijini kwao Mwamanyili, Wilayani ya Busega mkoa wa Shinyanga ambapo TFF itawakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Vedasto Lufano.

Marehemu Ngofilo wakati wa uhai wake aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa FAT wakati wa Muhidin Ndolanga na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FAT, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mwanza (MZFA) 1984-1994, ambapo baada ya kustaafu alipewa wenyekiti wa heshima na MZFA.

MALINZI AMPONGEZA RAVIA KWA KUCHAGULIWA KUWA RAIS ZFA


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Ravia Idarous Faina wa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) katika uchaguzi ulifanyika jana katika ukumbi wa Uwanja wa Gombani, Pemba.

Katika salamu zake, Malinzi amesema anampongeza Ravia kwa kuchaguliwa kwake, na hiyo imeonyesha imani kubwa kwa waliomchagua kuongoza ZFA katika kipindi kingine.

Malinzi amewapongeza vingozi wote wapya waliochaguliwa katika uchaguzi huo, na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika shughuli zote za maendeleo ya mpira wa miguu.

Uchaguzi wa kupata viongozi wa ZFA ulifanyika jana Gombani kisiwani Pemba, ambapo Ravia aliibuka mshindi na kutetea nafasi yake, nafasi ya makamu wa rais Ugunja kienda kwa Mzee Zam Ali, na makamu wa Pemba ikichukuliwa na Ali Mohamed Ali.

SIMBA KUSHIRIKI KOMBE LA NILE BASIN


Klabu ya Simba SC ya jijini Dar es salaam imethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Nile Basin Club Championship, inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) itakayoanza kutumia vumbi Mei 22, 2016 nchini Sudan.

Mashindano ya vilabu Kombe la Nile Basin huandailiwa na CECAFA kwa kushirikisha vilabu vilivyoshika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi kwa nchi wanachama wa CECAFA.

Bingwa michuano ya kombe hilo atajinyakulia zawadi ya dola za kimarekani U$30,000, mshindi wa pili dola U$20,000, huku mshindi wa tatu akipata kitita cha dola za kimarekani U$10,000.

Nile Basin inashirikisha vilabu kutoka katika nchi wanachama wa CECAFA ambazo ni Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Zanzibar.

Vitoria University kutoka Uganda ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo baada ya kuifunga AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika mwaka 2014.

Sunday, April 17, 2016

YANGA YAKIPASHA MOTO KIPORO CHA MTIBWA, YAICHAPA BAO 1-0 LIGI KUU


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana walirejea kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilijipatia bao hilo la pekee dakika ya 59 kupitia kwa Simon Msuva.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 57 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.

Hata hivyo, Simba inaweza kurejea tena kileleni mwa ligi hiyo leo iwapo itaifunga Toto African katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Thursday, April 14, 2016

MISS TABATA 2016 KUANZA MAZOEZI JUMANNE DAR WEST PARK

 
Na Mwandishi Wetu

MAANDALIZI ya kumsaka mrembo wa kitongoji cha Tabata mwaka huu ‘Miss Tabata 2016’ yanatarajiwa kufanyika kuanzia Jumanne Aprili 19 kwenye Ukumbi wa Da West Park, Tabata jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa shindano hilo Joseph Kapinga alisema jana kuwa warembo wote waliojiandikisha wanatakiwa kufika mazoezini na bado fomu za kushiriki shindano hilo zinaendelea kutolewa.

Kapinga alisema kwamba Keen Arts ambayo ni kampuni tanzu ya Bob Entertainment ndiyo imepewa kibali cha kuendesha shindano hilo na waratibu wa taifa Lino Agency iliyoko chini ya mkurugenzi wake Hashim Lundenga.

Mratibu huyo alisema uzinduzi rasmi wa shindano hilo utafanyika mwishoni mwa mwezi huu.

“Baada ya uzinduzi washiriki watatembelea hifadhi ya Mikumi na Dar es Salaam Zoo ikiwa ni njia mojawapo ya kutangaza utalii wa ndani,” Kapinga alisema.

Aliwataka warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo kujitokeza na kusema fomu hizo pia zinapatikana kwenye ukumbi wa Da West Park na ofisi za Miss Tanzania zilizoko Mikocheni.

Miss Tabata ni miongoni mwa vituo vitatu vilizoko kanda ya Ilala huku vingine vikiwa ni Ukonga na Dar City Centre.

Washiriki watano kutoka kila kituo watashiriki kwenye shindano la Miss Ilala na hatimaye Miss Tanzania baadaye mwaka huu.

Ambasia Mallya ndiye mrembo anayeshikilia taji la kitongoji hicho ambacho kimetoa wawakilishi waliofanya vizuri katika ngazi ya taifa.

Wadhamini ambao wameshathibitisha kudhamini shindano hilo ni pamoja na CXC Africa, Fredito Entertainment, Saluti5 na Bob Entertainment.

NAPE, MAKONDA WAWAONGOZA MAMIA YA MASHABIKI WA MUZIKI KUMZIKA NDANDA KOSOVO


YANGA, AZAM ZAIBUKA NA USHINDI LIGI KUUNa Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya nyumbani baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Shukrani kwake, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima aliyefunga bao la ushindi mwishoni kipindi cha pili, baada ya kubanwa kiasi cha kutosha na Mwadui.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 56 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukaa nafasi ya pili nyuma ya Simba SC yenye pointi 57 za mechi 24.
Hadi mapumziko, timu timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Yanga walitangulia kupata bao kupitia kwa Simon Msuva aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Issoufou Boubacar.
Mwadui walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji Kelvin Sabati aliyeukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ baada ya shuti lake mwenyewe.
Bao hilo lilitokana na makosa ya kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Kamusoko aliyepiga mpira ukanaswa na kiungo wa Mwadui, Razack Khalfan nje kidogo ya boksi akampasia Sabati aliyefunga.
Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosakosa za pande zote mbili.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko wakiwapumzisha Pato Ngonyani na Issoufou Boubacar na kuwaingiza Vincent Bossou na Godfrey Mwashiuya.
Refa Selemani Kinugani alimtoa kwa kadi nyekundu, Iddi Mobby dakika ya 70 kwa kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Kamusoko.
Yanga ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 86 likifungwa na kiungo Haruna Niyonzima kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kichwa ya mshambuliaji Donald Ngoma kufuatia krosi ya beki Oscar Joshua.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeshinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Shukrani kwake, Nahodha John Raphael Bocco aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 62 kwa penalti baada ya mshambuliaji Kipre Herman Tchetche kuchezewa rafu kwenye boksi.
AzamFC sasa inafikisha pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, ikiendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

Wednesday, April 13, 2016

NUSU FAINALI KOMBE LA FA YAZIKUTANISHA YANGA NA COASTAL UNION


Droo ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imefanyika usiku huu moja kwa moja (live) kupitia kituo cha luninga cha AzamTwo, huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata nafasi ya kucheza nyumbani.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, imewashuhudia vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Young Africans wakipata nafasi ya kucheza michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.

Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku wagosi wa Kaya Coastal Union wakicheza dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga siku hiyo hiyo.

Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya kombe hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).

Wakati huo huo wadhamini wa michuano hiyo Azamtv kupitia kituo chake cha michezo cha Azam Sports, leo wameweza kulionyesha hadharani kwa mara ya kwanza kombe la ubingwa na kukikabidhi kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine.

YANGA, MWADUI KAZI IPO LEO


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano, kwa michezo miwili ya viporo kuchezwa katika viwanja vya Manungu Turiani mkoani Morogoro na uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Young Africans wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, watakua wenyeji wa Mwadui FC inayokamata nafasi ya sita katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar walio katika nafsi ya nne ya msimamo wa ligi kuu watawakaribisha Azam FC walio juu yao nafasi ya tatu, mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Manungu Turiani mkoani Morogoro.

TFF YAWASHUKURU WADAU WA SOKA NCHINI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewapongeza viongozi, mashabiki, wachezaji wa vilabu na timu za Taifa kwa kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ya kimataifa iliyochezwa mpaka sasa.

Katika kipindi cha mwezi mmoja, Tanzania imeshiriki katika michuano mbalimbali ya kirafiki, mashindano ngazi za vilabu, timu za taifa ikiwemo ya Wanawake (Twiga Stars), Vijana (Serengeti Boys) na Taifa Stars.

Katika michezo kumi iliyochezwa mfululizo mpaka sasa, timu za  Tanzania hazijapoteza mchezo hata mmoja mpaka sasa, ikiwa ni kwa vilabu pamoja na timu za taifa za Wanawake, Vijana na Taifa Stars.

Twiga Stars ilitoka sare ya bao 1- 1 dhidi ya Zimbabwe mchezo uliochezwa Harare, Yanga ikaifunga APR mjini Kigali 2-1, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es salaa, wakati Azam FC ilifunga Bidvest 3-0 Johanesburg na kuendeleza tena ushindi wa 4-3 Azam Complex Chamazi.

Taifa Stars ikiwa mjini N’Djamena ilibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chad katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2017, Serenegti Boys ikiifunga The Pharaohs kutoka Misri katika michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa (2-1), (3-1) michezo iliyochezwa Uwanja wa Taifa na Azam Complex Chamazi.

Mchezo wa tisa wa kimataifa, Yanga SC ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), huku Azam FC ikiibuk na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esperance ya Tunisia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).

TFF inawaomba wachezaji, viongozi, wadau na Mashabiki kuendelea kupigana kusaka ushindi katika michezo inayofuata na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania nje ya nchi.

Monday, April 11, 2016

KANU AAHIDI KUSAIDIA KUINUA SOKA YA TANZANIA


Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

BALOZI wa Star Times barani Afrika, Nwankwo Kanu, ameahidi kusaidia kuinua kiwango cha soka nchini kwa kutoa mafunzo kwa vijana.

Kanu, alisema hayo mwishoni mwa wiki, baada ya kupokea zawadi ya jezi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, yenye jina lake kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa.

Mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, alisema amekuja nchini kwa mwaliko wa Star Times, lakini amepanga kuja tena kwa shughuli zake binafsi za kimichezo.

Kanu, ambaye aliwahi kung'ara kisoka alipokuwa klabu za Ajax Amsterdam ya Uholanzi, Inter Milan ya Italia, Arsenal, West Bromwich na Portsmouth za England, alisema amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata wakati wa ziara yake hapa nchini.

Kutokana na mapokezi hayo, Kanu alisema anaamini mchango wake katika soka ya Tanzania unahitajika.

“Mustakabali wa mpira wa miguu wa Tanzania utakuwa mkubwa kama Watanzania watapenda kufuatilia masuala ya mpira wa miguu kupitia ligi tofauti tofauti. Kadri unavyoangalia michezo mbalimbali ya kimataifa, ndivyo unavyozidi kujifunza,” alisema Kanu.

Kwa upande wake, Mwesigwa aliishukuru Star Times Tanzania kwa kuthamini soka kwa kumleta nchini mchezaji nguli wa kimataifa wa Nigeria, Kanu.

Mwesiga, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya chakula cha jioni, kilichoandaliwa na Kampuni ya StarTimes, kwa lengo la kumkaribisha Kanu.

“Kupitia StarTimes, tutaboresha mpira wetu kwa kuangalia ligi mbalimbali za mataifa ya Ujerumani, Italia na Ufaransa,” alisema Mwesigwa.

Kanu, alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka 1996 na ndipo alipoamua kufungua taasisi yake ya moyo inayoitwa 'The Kanu Heart Foundation.'

Taasisi hiyo iliyoko nchini Nigeria, ambako ndiko alikozaliwa, aliianzisha kwa madhumuni ya kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya moyo na ameahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika masuala mbalimbali ya kitabibu.

Wakati huo huo, Kanu ametembelea na kushiriki kutoa mafunzo kwa watoto wa kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park cha jijini Dar es Salaam.

Akiwa kwenye kituo hicho, Kanu alielezea kufurahishwa kwake kuona watoto hao watoto wameandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya michezo mbalimbali, kwa kuwa sio wengi  wanaopata fursa hiyo.

“Wakati mimi ninaanza kucheza mpira, hakukuwa na kituo kizuri kama hiki wala jezi, viatu na walimu wazuri mlio nao sasa. Hii ni fursa ya kipekee kwenu nyinyi kuweza kuonyesha juhudi za kujifunza ili mje kuwa kama mimi siku za mbeleni.

"Leo mimi nimekuwa maarufu ni kwa sababu nilikuwa na nidhamu, bidii, dhamira na kuwasikiliza walimu wangu walipokuwa wananifundisha. Hatimaye leo hii nina mafanikio makubwa, ninaishi maisha mazuri, wazazi wangu pia wanaishi mahali pazuri, wanasafiri na kupata wanachokitaka kwa sababu tu ya mimi kufanikiwa,"Kanu aliwaambia watoto hao.

Aliwataka watoto wa kituo hicho kuonyesha bidii, utii na dhamira ya dhati kwa kila wanachokifanya.

"Ningependa kuwashauri wadogo zangu kuwa popote utakapokwenda duniani kwenye mchezo wa soka, viwanja na mipira inayotumika ni hii hii wala hakuna tofauti yoyote.

"Hivyo sioni kama kuna kitu cha kuwazuia na nyinyi msifanikiwe. Kama nilivyowaambia awali, bidii, nidhamu, dhamira na utii kwa walimu wenu ndio msingi wa mafanikio ya mwanasoka yeyote yule duniani. Nawatakia kila la kheri na siku nyingine nikija Tanzania naahidi kuwatembelea tena,” aliwasisitizia vijana hao.