KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, April 8, 2016

KANU ATEMBELEA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE




Aliyekuwa mchezaji nguli wa timu ya taifa ya Nigeria au Super Eagles, Nwankwo Kanu ambaye pia kwa sasa ni balozi wa makampuni ya StarTimes barani Afrika leo ametembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya  Muhimbili (MNH) kwa lengo la kujua ni jinsi gani taasisi hiyo inafanya kazi pamoja na kuwajulia hali wagonjwa wa moyo waliolazwa katika Taasisi hiyo. pia

Akizungumza  baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo Kanu ameelezea kuguswa na tatizo la ugonjwa wa moyo hasa kwa watoto wadogo ambao amewatembelea na kuahidi kubadilishana uzoefu kuhusu huduma za matibabu zinazotolewa na wataalamu wa tasisi hiyo.

“Tatizo la moyo ni kubwa sana kwa sasa na limekuwa likiongezeka kwa kasi lakini cha kusikitisha ni kuwa sio kila mtu anaweza kumudu gharama za matibabu yake. Hivyo basi kuna umuhimu mkubwa sana kwa serikali na wadau wengine kuanzisha vituo maalumu kama hivi ili kuwasaidia wasiojiweza.” Alisema Kanu

Katika mazungumzo yake mchezaji huyo wa nyota wa zamani ambaye aliwahi kuwika na vilabu kama vile vya Arsenal, Ajax na Inter Milan, amesema kuwa pamoja na kuja kwa shughuli mbalimbali kama balozi wa kampuni ya StarTimes lakini pia ana nia ya kushirikiana na watalaamu wa Taasisi hiyo ya Moyo. Alielezea kuwa lengo ni kuwasaidia matibabu watoto wenye matatizo ya Moyo ambao wazazi wao hawana uwezo na kwamba watazungumzia suala hilo.

“Nimefarijika sana kuona serikali ya watu wa Tanzania inachukua hatua stahiki katika kuwasaidia wananchi wake. Pia ningependa kuchukua fursa hii kuwataka watanzania hasa wanamichezo kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwani ukijua tatizo mapema ni rahisi kupata matibabu na kupona. Tumeona mifano michache ya wachezaji maarufu mbalimbali barani Afrika na kwingineko duniani wakifariki au kunusurika kufa wakiwa katika ya mchezo kutokana na kutoweka wazi mustakabali wa afya zao.” Alihitimisha balozi huyo wa StarTimes barani Afrika

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Godwin Godfrey amelezea kuwa tangu Julai mwaka jana mpaka sasa tasisi hiyo kwa kushirikiana na wataalam kutoka nje ya nchi wamewafanyia upasuaji watoto zaidi ya 200.

Nwankwo Kanu mbali na kujizolea umaarufu na heshima kubwa katika medani za soka barani Afrika na Ulaya yeye pia alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka 1996 na ndipo alipoamua kufungua taasisi yake ya moyo inayoitwa “The Kanu Heart Foundation.”

Taasisi yake hiyo iliyoko nchini Nigeria ambako ndiko alipozaliwa aliianzisha kwa madhumuni makubwa ya kusaidia wenye matatizo kama yake na ameahidi taasisi hiyo kushirikiana na taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika masuala mbalimbali.

No comments:

Post a Comment