'
Thursday, April 14, 2016
YANGA, AZAM ZAIBUKA NA USHINDI LIGI KUU
Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya nyumbani baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Shukrani kwake, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima aliyefunga bao la ushindi mwishoni kipindi cha pili, baada ya kubanwa kiasi cha kutosha na Mwadui.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 56 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukaa nafasi ya pili nyuma ya Simba SC yenye pointi 57 za mechi 24.
Hadi mapumziko, timu timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Yanga walitangulia kupata bao kupitia kwa Simon Msuva aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Issoufou Boubacar.
Mwadui walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji Kelvin Sabati aliyeukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ baada ya shuti lake mwenyewe.
Bao hilo lilitokana na makosa ya kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Kamusoko aliyepiga mpira ukanaswa na kiungo wa Mwadui, Razack Khalfan nje kidogo ya boksi akampasia Sabati aliyefunga.
Baada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosakosa za pande zote mbili.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa mabadiliko wakiwapumzisha Pato Ngonyani na Issoufou Boubacar na kuwaingiza Vincent Bossou na Godfrey Mwashiuya.
Refa Selemani Kinugani alimtoa kwa kadi nyekundu, Iddi Mobby dakika ya 70 kwa kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Kamusoko.
Yanga ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 86 likifungwa na kiungo Haruna Niyonzima kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kichwa ya mshambuliaji Donald Ngoma kufuatia krosi ya beki Oscar Joshua.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeshinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Shukrani kwake, Nahodha John Raphael Bocco aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 62 kwa penalti baada ya mshambuliaji Kipre Herman Tchetche kuchezewa rafu kwenye boksi.
AzamFC sasa inafikisha pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, ikiendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment