KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 20, 2016

AZAM YATUPWA NJE KOMBE LA SHIRIKISHO



WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho, Azam wametupwa nje baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Esperance ya Tunisia.

Kipigo hicho ilichokipata Azam jana, katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili, iliyochezwa mjini Tunis, kimeifanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-2.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Azam ilishinda mabao 2-1 na hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Licha ya kucheza ugenini, Azam iliweza kuwabana vyema wapinzani wao hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika, ambapo timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Katika kipindi hicho, kipa Aisha Manula wa Azam alilazimika kufanyakazi ya ziada mara kwa mara, kuokoa mashuti ya washambuliaji wa Esperance, waliokuwa na uchu mkubwa wa kufunga mabao.

Mambo yalibadilika dakika za mwanzo za kipindi cha pili baada ya mshambuliaji ASaad Bguir kuifungia Esperance bao la kuongoza kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 20.

Mpira huo wa adhabu ulitokana na kosa la beki wa kati wa Azam, David Mwantika, kumchezea rafu Ben Youssef wa Esperance, nje kidogo ya eneo la hatari.

Esperance ilifanikiwa kuongeza bao la pili lililofungwa na Haithem Jouini dakika ya 63 kabla ya kuongeza la tatu dakika ya 80 kupitia kwa Ben Youssef.

Katika mechi hiyo, Azam iliwakosa wachezaji wake nyota, Shomari Kapombe, ambaye ni mgonjwa, Kipre Tchetche, ambaye ni majeruhi, Serge Wawa, ambaye pia ni majeruhi na Jean Baptiste Mugiraneza, anayetumikia adhabu ya kadi.

No comments:

Post a Comment