KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 6, 2016

SERENGETI BOYS YAIPIGA TENA MISRI


TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys jana iliibuka tena na ushindi dhidi ya vijana wenzao wa umri huo kutoka Misri.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Dar es Salaam, Serengeti Boys iliichapa Misri mabao 3-2.

Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Serengeti Boys dhidi ya Misri. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Serengeti
Boys iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Timu zote mbili zimetumia mechi hizo kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo, zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Madagascar.

Misri ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 22 lililofungwa na Ahmed Saad kabla ya Serengeti Boys kusawazisha dakika ya 28 kwa bao lililofungwa na Ibrahim Abdalla.

Serengeti Boys iliyoonyesha kandanda ya kiwango cha juu, iliongeza bao la pili dakika ya 36 lililofungwa na Selemani. Timu hizo zilikwenda mapumziko Serengeti Boys ikiwa mbele kwa mabao 2-1.

Timu zote mbili ziliongeza kasi ya mashambulizi katika kipindi cha pili kabla ya Serengeti Boys kupata bao la tatu lililofungwa na Abdalla.

Bao hilo halikuikatisha tamaa Misri, ambayo ilifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 75 kupitia kwa Diaa Wahed.

No comments:

Post a Comment