KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 10, 2016

NAPE AWAPA DARASA WASAMBAZAJI WA FILAMU



Na Raymond Mushumbusi WHUSM
 

Wasambazaji wa Filamu na Muziki nchini wameashauriwa kuzingatia na kufuata Sheria za nchi katika usambazaji wa kazi hizo.
 

Ushauri huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokutana na Umoja wa Wasambazaji wa Filamu na Muziki kujadili mustakabali wa usambazaji wa kazi za Sanaa nchini.
 

“ Nia yangu  njema sina nia ya kumuumiza mtu nataka sheria na  taratibu zilizopo zifuatwe mnapotekeleza majukumu yenu ya usambazaji wa Filamu na muziki” alisema Mhe. Nape.

Mhe. Nape Moses Nnauye amewahakikishia wasambazaji hao kuwa Serikali ipo pamoja nao na watashirikiana kwa pamoja ili kuweza kutafuta namna bora ya kuboresha usambazaji wa Filamu na Muziki nchini.
 

Mhe. Nape ameongeza kuwa yuko tayari kupokea mawazo na ushauri kutoka kwa Wasambazaji wa Filamu na Muziki nchini katika kupata namna nzuri ya kutatua changamoto zilizopo na kuboresha njia za usambazaji wa kazi za Sanaa.
 

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Wasambazaji wa Filamu na Muziki nchini  Bw. Joseph Lyakurwa amempongeza Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye kwa jitihada za Serikali katika kupambana na wizi wa kazi za Sanaa nchini na kuomba kuendelea na kuwasaka na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka Sheria na taratibu katika usambazaji wa kazi za Sanaa.
 

“ Nakuomba Mhe. Waziri tukishalipa kodi zote zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo baada ya hapo mfanyabiashara atakayekamatwa amekiuka Sheria na taratibu hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake”.alisema Bw. Lyakurwa.
 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu  Bibi. Joyce Fissoo amewashauri Wasambazaji wa Filamu na Muziki kuzingatia ubora wa kazi wanazozisambaza ili kuweza  kushindana  na soko la filamu na muziki wa nje.
 

“ Nawaomba wasambazaji wa Filamu na Muziki muzingatie ubora wa kazi mnazo zisambaza kwani tunashindana na filamu za jje kwahiyo tukizingatia hilo Filamu na Muziki wetu utasonga mbele” Alisema Bibi. Joyce.
 

Baada ya kikao hicho baina ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye na Umoja wa Wasambazaji wa Filamu na Muziki nchini,kamati ya watu saba imeundwa kukaa na kujadiliana na kupata suluhisho la namna bora ya usambazaji wa kazi za Sanaa na kuwasilisha ripoti kwa Mhe. Waziri.

No comments:

Post a Comment