KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, August 19, 2016

MALINZI AMPONGEZA RAIS MPYA WA SOKA BOTSWANA, AOMBOLEZA KIFO CHA HAVELANGE



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za pongezi Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Botswana Maclean Letshwiti aliyechaguliwa kushika wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Maclean Letshwiti ambaye ni nguli katika masuala ya biashara, alimshinda Tebogo Sebego kwa kura 32 kwa 28.

Katika barua yake ya pongezi kwenda kwa Letshwiti, Rais Malinzi amemtakia kila la kheri Rais huyo mpya wa BFA aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Mochudi Centre Chiefs maarufu kwa jina la Magosi.

Katika barua hiyo, Malinzi amesema: “Nakuandikia barua hii kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF na kwa niaba yangu mwenyewe, kukupongeza wewe baada ya kushinda nafasi ya urais katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Bostwana.”

“Mheshimiwa Rais, uchaguzi wenu ni ushahidi tosha wa kazi nzuri iliyowapa imani katika klabu uliyoiongoza na shirikisho la mpira wa miguu hapo Bostwana.,” amesema Malinzi katika taarifa yake na kuahidi ushirikiano wa kutosha kwa Rais Letshwiti.

Kadhalika, Rais Malinzi aliwapongeza Segolame Ramotlhwa na Marslow Motlogelwa waliochaguliwa kuwa Makamu Rais wa Kwanza na Makamu Rais wa Pili kwa kufuatana.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kutokana na kifo cha Rais wa zamani wa FIFA, Joao Havelange aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Katika salamu hizo, Rais Malinzi amesema amepokea taarifa za kifo cha Joao Havelange kwa masikitiko makubwa akimkumbuka zaidi pale aliongeza washiriki wa kombe la dunia kutoka timu 16 hadi 32, ambapo mashindano 6 yalifanyika chini ya utawala wake.

Joao Havelange, raia wa Brazil alikuwa mtangulizi wa Sepp Blatter katika shirikisho la mpira wa miguu duniani kuanzia mwaka 1974 hadi 1998. Blatter alijiuzulu nafasi ya Urais wa FIFA Aprili, 2013 kutokana na ripoti ya uchunguzi wa madai ya kupokea rushwa.

Joao Havelange aligua kwa muda mrefu na kulazwa hospitali tangu mwaka 1999 alipokumbwa na ugonjwa wa mapafu.

Alikuwa mmoja wa wanakamati wa Olimpiki (IOC), kuanzia mwaka 1963 hadi 2011 alipojiuzulu kwa sababu ya kudhoofu kwa afya yake. Havelange aliiwakilisha Brazil katika mashindano ya Olympic ya Kuogelea mwaka 1936, mwaka ambao aliidhinishwa kuwa mwanasheria kabla ya kuchaguliwa na IOC.

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Joao  Havelange mahala pema peponi. Bwana alitoa, Bwana alitoa, jina la Bwana lihimidiwe.

No comments:

Post a Comment