KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 22, 2016

SERENGETI BOYS YANUSA FAINALI ZA AFRIKA ZA UNDER 17


TIMU ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys, imefanikiwa kupenya hatua ya mwisho ya mtoano kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Amajimbos ya Afrika Kusini mabao 2-0.
 

Fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana, zimepangwa kufanyika mwakani Madagascar, Mchezo huo ulipigwa jana katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
 

Bao la kwanza la Serengeti Boys katika mchezo huo, lilifungwa na Mohamed Abdalah dakika ya 34 akiunganisha krosi iliyochongwa na Hassan Juma huku bao la pili likiwekwa kimiani dakika ya 84 na Husein Makame.
 

Katika mchezo wa awali uliochezwa Afrika Kusini, kwenye Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Mabao yote katika mchezo wa awali, yalipatikana kipindi cha pili kwa mikwaju ya penati kwa kila upande. 


Afrika Kusini ndio walioanza kupata penati dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.
 

Katika mchezo wa jana, Serengeti Boys ilionekana kuwa na kiu ya kupata ushindi wa mapema baada ya kulisakama lango la Amajimbos mara kwa mara.
 

Kikosi cha Serengeti Boys, kilipata pigo dakika ya 45 baada mwamuzi, Noiret Jim Bacari wa Comoro kumtoa kwa kadi nyekundu mchezaji Ali Hamis baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa Afrika Kusini.
 

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Serengeti Boys wakiwa pungufu, walijipanga zaidi kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao.
 

Timu hizo ziliendelea kushambuiliana kwa zamu huku Amajimboz wakifika langoni mwa Serengeti kwa kushtukiza, lakini mpaka dakika ya mwisho, vijana wa Tanzania waliibuka washindi katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment