KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 21, 2011

Twanga Pepeta, Msondo kumchangia Gurumo


BENDI ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International imeandaa onyesho la pamoja kati yake na Msondo Ngoma kwa ajili ya kumchangia kiongozi wake, Muhidin Gurumo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET), inayomiliki Twanga Pepeta, Asha Baraka alisema juzi kuwa, onyesho hilo litafanyika keshokutwa kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, Dar es Salaam.
Asha alisema lengo la onyesho hilo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya Gurumo, ambaye hali ya afya yake si nzuri, kufuatia kuugua na kulazwa mara mbili kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kiongozi huyo wa Twanga Pepeta alisema wameamua kuandaa onyesho hilo kutokana na kutambua na kuthamini mchango wa Gurumo katika kuendeleza muziki wa dansi nchini.
“Tumeamua kwamba, mapato yote yatakayopatikana katika onyesho hilo yatakwenda kwa Mzee Gurumo kwa ajili ya kugharamia matibabu yake,”alisema.
Kwa mujibu wa Asha, wakati wa onyesho hilo, mshindi wa taji la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011, Mary Khamis ataonyesha umahiri wake wa kucheza miondoko ya bendi hiyo.
Mbali na kumchangia Gurumo, Asha alisema bendi yake pia italitumia onyesho hilo kutangaza albamu yake mpya, inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu.
Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na Kauli, Kiapo cha mapenzi, Umenivika umaskini, Mtoto wa mwisho, Dunia daraja na Penzi na shemeji.
Asha amewataka mashabiki wa muziki wa jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kumuenzi mwanamuziki huyo mkongwe.

No comments:

Post a Comment