KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 21, 2011

Cannavaro: Nakwenda El-Merreikh


BEKI mahiri wa timu ya soka ya Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amethibitisha kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya El Merreikh ya Sudan.
Akizungumza na Burudani wiki hii, akiwa nyumbani kwake mjini hapa kwa ajili ya mapumziko, Cannavaro alisema amefurahi kupata nafasi hiyo kwa vile ni fursa nzuri ya kuonyesha uwezo wake.
Cannavaro alisema pia kuwa, kupata kwake nafasi hiyo pia kutasaidia kuitangaza Zanzibar kisoka na hivyo kutoa nafasi kwa wachezaji wengine wa visiwa hivyo kuitwa nje.
Beki huyo, ambaye pia huichezea timu ya Zanzibar na ile ya Taifa, Taifa Stars alisema, anatarajia kuondoka nchini Desemba mwaka huu kwenda Sudan kwa ajili ya kuanza kuitumikia El- Merreikh.
Kwa mujibu wa Cannavaro, tayari ameshaingia mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili na amepata baraka zote kutoka kwa uongozi wa Yanga.
“Kwa kweli nimefarijika sana kupata nafasi hii na ninaamini nitatumia uwezo wangu wote kuitangaza Zanzibar na Tanzania kisoka ili wachezaji wengine nao waweze kupata nafasi hiyo,”alisema.
Cannavaro ameushukuru uongozi wa Yanga kwa kumkubalia kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu hiyo ya Sudan na kuongeza kuwa, anaamini hatoacha pengo katika klabu hiyo.
Uongozi wa El-Merreikh ulivutiwa na kiwango cha beki huyo wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, iliyomalizika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika michuano hiyo iliyodumu kwa wiki mbili, Yanga ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali. Katika mechi za robo na nusu fainali, ilizitoa Red Sea ya Eritrea na St George ya Ethiopia kwa njia ya penalti.

No comments:

Post a Comment