KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

CHRISS: Kava za filamu wizi mtupu



MTUNZI, mtayarishaji na mwongozaji maarufu wa filamu na tamthilia nchini, Chrissant Mhengga amesema, utengenezaji wa kava nyingi za filamu umelenga kuwaibia mashabiki wa tasnia hiyo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mhengga alisema, kava nyingi zinazotengenezwa hapa nchini kwa ajili ya filamu, haziendani na maudhui ya filamu hizo.
Akitoa mfano, Mhengga alisema mara nyingi kava za filamu zinakuwa na urembo mwingi kwa ajili ya kuvutia wateja, lakini vikorombwezo vinavyowekwa havimo ndani ya filamu husika.
“Utakuta kwenye picha ya kava, muhusika ama wahusika wakuu wanaonekana wamevaa mavazi ya gharama, lakini ndani ya filamu hakuna sehemu yoyote wanayoonekana wakiwa wamevaa mavazi hayo,”alisema.
“Na wakati mwingine unaweza kuona picha ya kava ikionyesha macho ya mmoja wa wahusika yanawaka moto, lakini ukitazama filamu yenyewe, huwezi kukutana na tukio hilo,”aliongeza.
Mhengga alilaumu tabia ya baadhi ya watayarishaji wa filamu nchini, kutoa zaidi ya filamu kumi kwa mwaka na kuongeza kuwa, huo ni udanganyifu kwa mashabiki wa fani hiyo.
Alisema kuharakisha kutoa filamu kwa sababu ya pesa, kumechangia kuifanya tasnia hiyo ionekane kuwa ya kulipua kutokana na filamu nyingi kukosa ubora unaotakiwa.
Mhengga pia alilaumu tabia ya kuzipa filamu za kibongo majina ya Kiingereza kwa madai kuwa, kufanya hivyo ni kuishusha thamani lugha ya Kiswahili, ambayo alisema ina utajiri mkubwa wa misemo na nahau zenye mvuto.
“ Huu ni upungufu mkubwa katika filamu zetu kwa sababu lugha ya Kiswahili ina hazina ya maneno mengi na yenye ladha nzuri. Sasa kama wanazipa filamu majina ya kiingereza, kwa nini waweke tafsiri yake kwa Kiswahili kwenye mabano?” Alihoji.
Muongozaji huyo wa filamu pia aliwatupia lawama watayarishaji wengi wa filamu nchini kwa kupendelea zaidi hadithi za mapenzi, ambazo alisema sio utamaduni wa kiafrika.
Alisema filamu za mapenzi hazihusiani na maisha halisi ya Kitanzania kwa sababu huo ni utamaduni wa kizungu na kwamba zipo hadithi nyingi na nzuri zinazohusu mila na utamaduni wa kiafrika, ambazo zinafaa kutengenezewa filamu.
Mhengga alisema uzuri wa filamu unategemea zaidi uzito wa hadithi na mwongozo wake na kwamba, jamii ya Tanzania bado inahitaji zaidi kuelimishwa kuliko kuburudishwa.
Alisema ni kweli kwamba maendeleo ya fani ya filamu hivi sasa ni makubwa, lakini filamu nyingi hazina mvuto na mafunzo kwa jamii kutokana na kukosekana utaalamu katika kuziandaa.
“Kuna dada mmoja mtayarishaji wa filamu kule Kenya, alipohojiwa alisema, alitumia miezi minane kuandika mwongozo wa filamu yake, lakini akatumia wiki moja katika kupiga picha. Hii inaonyesha kuwa, hadithi na mwongozo ni mambo muhimu na ya kuzingatiwa sana katika utengenezaji wa filamu,”alisema.
Mtaalamu huyo wa mambo ya filamu alisema, filamu nyingi za kibongo zimeandaliwa kama tamthilia kwa vile ndani ya filamu moja, zinaweza kupatikana filamu zingine tatu au nne.
Mhengga, ambaye ni mwasisi wa kundi la sanaa la Kaole na mwalimu wa wasanii wengi maarufu nchini alisema, ni kweli kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa wakilipwa fedha nyingi hivi sasa kutokana na fani hiyo, lakini bado kiwango wanachokipata ni kidogo.
Alisema iwapo kungekuwepo na usimamizi mzuri katika mauzo ya filamu na kazi hiyo ingekuwa ikifanyika kwa utaalamu wa hali ya juu, wasanii wangeweza kupata fedha nyingi zaidi na hivyo kunufaika na vipaji vyao.
“Hata kama utamlipa msanii shilingi milioni 10 kwa filamu moja, kutokana na maisha wanayoishi, bado pesa hizo haziwezi kutosheleza mahitaji yao kwa sababu wanapenda sana kutanua na kujionyesha,”alisema.
Mhengga ametoa mwito kwa wasanii wa maigizo, kupenda kujifunza zaidi kuhusu fani hiyo kwa kusoma mambo yanayohusu filamu kupitia kwenye mitandao na pia kuomba ushauri kutoka kwa waliowazidi utaalamu.
Kwa sasa, Mhengga yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha filamu yake mpya ya ‘Hazina ya marehemu’ kabla ya kuibuka na filamu nyingine, itakayojulikana kwa jina la ‘Ndoa ya hayawani’.
Alisema ameamua kuziita filamu zake kwa majina ya Kiswahili ili mashabiki waweze kujua ndani yake kuna nini badala ya kuzipa majina ya Kiingereza, ambayo majina na maudhui yake huwa tofauti.

No comments:

Post a Comment