KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

KOVA MGENI RASMI MISS ILALA


KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shindano la kumsaka mrembo wa kanda ya Ilala.
Mratibu wa shindano hilo, Jackson Kalikumtima alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, warembo 12 wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji hilo.
Kwa mujibu wa Kalikumtima, shindano hilo limepangwa kufanyika kesho kuanzia saa mbili usiku katika viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Dar es Salaam.
Kalikumtima alisema washindi watatu wa kwanza wa shindano hilo, wanatarajiwa kuiwakilisha kanda ya Ilala katika shindano la kumsaka Miss Tanzania 2011 litakalofanyika Septemba mwaka huu.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kamanda Kova kuhudhuria mashindano ya urembo akiwa mgeni rasmi, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo miaka michache iliyopita.
“Tunajivunia kuwa pamoja na kiongozi huyu kwa sababu ndiye mwenye dhamana ya usimamizi wa ulinzi na usalama katika Jiji la Dar es Salaam na pia warembo wanaoshiriki kwenye shindano hili walishiriki katika shughuli za kuhamasisha ulinzi anaousimamia,”alisema Kalikumtima.
Aliongeza kuwa, kuwepo kwa Kamanda Kova katika shindano hilo ni uthibitisho wa wazi wa kuwepo kwa ulinzi mkali na kuwataka watu wanaomiliki vyombo vya usafiri wasiwe na wasiwasi wa usalama wao.
Kalikumtima alisema mandhari ya uwanja huo itabadilishwa na kugeuzwa kuwa eneo la starehe na burudani na kwamba michoro ya viwanja hivyo imetengenezwa kwa kufananishwa na Taman Mini Indonesia Park iliyoko katika Jiji la Jakarta.
Alisema kiingilio cha juu katika shindano hilo kitakuwa sh. 60,000, ambapo watakaolipa fedha hizo, watapata huduma ya chakula cha jioni kwenye viwanja hivyo.
Kwa mara ya mwisho, mrembo wa Ilala, Angela Damas alishinda taji la Miss Tanzania mwaka 2002. Mwaka 2003, Ilala ilishika nafasi ya tatu kupitia mrembo wake, Nargis Mohamed wakati mwaka 2004, mrembo wake mwingine, Verdiana Kamugisha alishika nafasi ya pili.
Kalikumtima alisema shindano hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Vodacom Tanzania, Paradise City Hotel, Syscorp Group, Channel Ten, Michuzi Blogspot, Paris Pub, Papazi Entertainment, Maisha Club, TV Sibuka, Sofia Production, Fabak Fashion na Clouds FM.

No comments:

Post a Comment