KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 21, 2011

MWASITI: Udhalilishaji kwa wasanii wa kike ukomeshwe


MCHEZA filamu na mpambaji maarufu wa waigizaji nchini, Mwasiti Mohamed amesema, baadhi ya watayarishaji wa sinema wa kiume wamekuwa na tabia ya kuwadhalilisha wasanii wa kike.
Mwasiti, maarufu kwa jina la Shishi amesema, watayarishaji hao wamekuwa wakitumia udhaifu wa wasanii wa kike kuwalazimisha kufanyanao mapenzi ili wawapatie nafasi kwenye filamu zao.
“Sio siri, udhalilishaji kwa wasanii wa kike ni mkubwa kwa sababu baadhi ya watayarishaji wa filamu wamekuwa wakiutumia umaarufu wao kuwalazimisha wasanii hao kufanyanao mapenzi,”alisema Mwasiti alipozungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii.
Mwasiti alisema si jambo baya kwa wasanii kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini ni vyema wafikie uamuzi huo kwa hiari bila ya kuwepo kwa kishawishi chochote.
Alisema inapotokea msanii wa kiume anamtaka msanii wa kike, anapaswa kumweleza jambo hilo bayana na muhusika akubali badala ya kumlazimisha.
Akizungumzia maendeleo ya fani hiyo nchini hivi sasa, Mwasiti alisema yanaridhisha, isipokuwa kikwazo kikubwa ni uwezo mdogo wa wasanii na watayarishaji wa filamu.
Alisema utengenezaji wa filamu unahitaji gharama kubwa ya pesa, ambazo watanzania wengi hawana na ndio sababu baadhi ya filamu zinakosa mvuto na uhalisia.
“Ukitaka kuandaa filamu inayoelezea ama kuonyesha matukio halisi ya ndani ya mahabusu na jela za Tanzania, huwezi kupata nafasi hiyo kutoka serikalini,”alisema.
“Vilevile si rahisi kwa watayarishaji wa filamu kupata nafasi ya kutumia mahakama zetu kutengeneza filamu, ama kutumia matukio ya nyumba kuungua na magari kugongana kwa sababu gharama zake ni kubwa,”aliongeza,
Mwasiti alisema binafsi ameandaa filamu inayoelezea mtiririko wa matukio hayo, lakini anashindwa kuitengeneza kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha.
Alisema katika nchi zilizoendelea katika tasnia hiyo barani Afrika, zikiwemo Nigeria, Afrika Kusini, Ghana na zinginezo, utengenezaji wa filamu za aina hiyo ni rahisi kwa sababu wanao uwezo mkubwa kifedha.
“Wenzetu bajeti zao za kutengeneza filamu ni kubwa, wana uwezo wa kujenga nyumba za muda na kutumia hata magari halisi kutengeneza ajali, lakini sisi hatuwezi,”alisema.
Kwa mujibu wa Mwasiti, hata utumiaji wa silaha katika kutengeneza filamu za Kibongo ni mgumu kwa sababu si rahisi kupata silaha halisi kama vile bunduki na bastola na zinapotumika huwa ni za plastiki, hivyo kukosa uhalisia.
Alilitaja tatizo lingine linaloikumba fani hiyo kuwa ni ubinafsi wa baadhi ya watayarishaji wa filamu katika uteuzi wa washiriki, ambapo alidai kuwa, wengi hufanya upendeleo.
Alisema kwa sasa, wapo waigizaji wengi wazuri wa filamu nchini, lakini wanakosa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kutokana na uteuzi wa washiriki kutofanywa kwa umakini.
Mwasiti pia aliilaumu serikali kwa kupiga marufuku filamu ya shoga kuuzwa nchini kwa madai kuwa, inakiuka maadili ya Kitanzania. Alisema filamu hiyo ilikuwa ikielezea matukio halisi yanayotokea katika jamii za Kitanzania, hivyo ilipaswa kuachwa ili itoe funzo.
Alisema inashangaza kuona kuwa, katika baadhi ya filamu, washiriki wengi wa kike wamekuwa wakivaa mavazi nusu uchi na kukiuka maadili ya Kitanzania, lakini zimeachwa bila kuchukuliwa hatua yoyote.
“Zipo baadhi ya filamu zina kasoro nyingi. Utakuta wasanii wa kike wanavaa nusu uchi, wengine wanavaa nguo za kutokea usiku wanapoigiza majumbani na wengine wanaigiza wakiwa nyumbani, lakini aanavaa vimini. Haya yote hayapendi na yanaondoa uhalisia katika filamu,”alisema.
Mwasiti pia alilalamikia soko la filamu nchini kuwa kwa sasa ni gumu, hali inayosababisha wasanii waendelee kulipwa malipo kidogo huku wasambazaji wakifaidika zaidi kimapato.
Kwa sasa, Mwasiti amekamilisha kutengeneza filamu yake binafsi, inayojulikana kwa jina la ‘She is Mine’, akishirikiana na msanii mwenzake, Halima Yahya ‘Da Vina’. Filamu hiyo ipo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote.
Alisema filamu hiyo inaelezea juu ya matatizo mengi yanayowakumba binadamu katika maisha yao ya kila siku, sababu zake na jinsi ya kuyatatua.
Wasanii wengine walioshiriki kucheza filamu hiyo ni Halima, Ndumbago Misayo ‘Thea’ na Hashim Kambi.
Filamu zingine, ambazo Mwasiti ameshiriki kuzicheza ni Point of no return, Pretty Girl, iliyotayarishwa na Kampuni ya RJ, inayomilikiwa na Vicent Kigosi ‘Ray’ pamoja na Jirani na Safari, zilizotayarishwa na Rashid Mrutu.
Mwasiti, ambaye pia aliwahi kucheza tamthilia ya Martin, alisema anavutiwa zaidi na wasanii wanaomudu kuvaa uhusika katika filamu wanazocheza.
Mwanadada huyu aliyesomea utaalamu wa kupamba wasanii wa filamu na shughuli zingine, amewataka watayarishaji wa fani hiyo kuwatumia kwa lengo la kuzinafidhisha zaidi kazi zao na pia kuzipa uhalisia.

No comments:

Post a Comment