KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

Sikinde yaipiga bao Msondo Ngoma


BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imewapiga bao mahasimu wao, Msondo Ngoma baada ya kumnyakua mwimbaji wao nyota, Shukuru Majaliwa.
Majaliwa, ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alitambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Sikinde katika onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Majaliwa alisema ameamua kujiunga na Sikinde kwa ridhaa yake mwenyewe na bila ya ushawishi wa mtu yeyote.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, nilikuwa nimepotea njia kwenda Msondo, lakini sasa nipo nyumbani. Kuanzia leo mimi ni mwimbaji wa Sikinde,”alisema mwanamuziki huyo, aliyeshangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki wa bendi hiyo.
Aliongeza kuwa, kabla ya kujiunga na Sikinde, aliwaeleza viongozi wa bendi hiyo sababu za kuondoka kwake Msondo na kuongeza kuwa, walimwelewa ndio maana walimkubalia ombi lake.
Majaliwa alikuwa akifanyakazi Msondo Ngoma akiwa ‘deiwaka’ kutokana na kuwa mwajiriwa wa JWTZ. Pia ni mwanamuziki wa bendi ya jeshi hilo ya Mwenge Jazz.
Kufuatia uamuzi wake huo, Majaliwa pia atakuwa akifanyakazi Sikinde akiwa ‘deiwaka’. Ajira yake jeshini haimbani kufanyakazi katika bendi za uraiani.
Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo, kiongozi mkuu wa Sikinde, Habibu Abbas ‘Jeff’ alisema, wameingia naye mkataba maalumu na kuongeza kuwa, tayari ameshaanza mazoezi na bendi hiyo tangu Jumanne iliyopita.
Jeff alisema mwimbaji huyo mwenye uwezo wa kuiga sauti ya marehemu Moshi William, anafanya mazoezi ya kuimba nyimbo mpya za bendi hiyo na pamoja na wimbo wake binafsi.
“Kusema ule ukweli, kwa muda mrefu tulikuwa tukihitaji mwanamuziki wa aina yake na sasa tumempata. Tutaamini atatusaidia sana katika kuinyayua juu zaidi bendi yetu,”alisema.
Jeff alisema kabla ya kuingia mkataba na Majaliwa, waliitisha kikao cha wanamuziki wote wa Sikinde na kuulizana iwapo atawafaa na wote kwa pamoja walimkubali.
Majaliwa anatarajiwa kuanza kuitumikia rasmi Sikinde leo katika onyesho lao la pamoja na Extra Bongo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment