KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

MAMA LULU: Acheni kumuhukumu mwanangu

Mama mzazi wa msanii Elizabeth Michael 'Lulu', anayedaiwa
kusababisha kifo cha msanii Steven Kanumba, Lucresia Kalugila
amewaomba wanaharakati wamsaidie binti yake ili haki itendeke.
Mama huyo alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika
kipindi cha Wanawake Live kilichorushwa hewani na kituo cha
televisheni cha East Africa.
Ameitaka jamii iache kumtupia lawama Lulu kutokana na kifo hicho
cha Kanumba, badala yake wasubiri vyombo vya dola vifanye kazi
yake.
"Kutokana na uzito wa tukio hili, nawaomba wanaharakati
wanawake waniunge mkono ili wanisaidie katika suala hili kwa
kuhakikisha haki inatendeka kwa mtoto wangu,"alisema.
Lucresia alisema binafsi amesikitishwa na kifo cha Kanumba kwa
vile hakutegemea iwapo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na
binti yake. Alisema wote wawili alikuwa akiwaona kama watoto
wake wa kuwazaa.
"Siku zote Kanumba alikuwa akiniita mama, sikuwa na imani
kwamba angeweza kuwa na uhusiano na Lulu, lakini kwa vile
limeshatokea, tuache sheria ichukue mkondo wake,"alisema.
Aliongeza kuwa, si busara kwa baadhi ya watu kwenda kwa mama
mzazi wa marehemu Kanumba kuzungumza maneno ya uongo
dhidi ya binti yake bila kuwa na uhakika wa kile anachokisema.
"Siku ya tukio walikuwepo Kanumba na Lulu, iweje watu wengine
waanze kuzusha maneno wasiyokuwa na uhakika nayo. Tuache
vyombo vya dola vifanyekazi na kutupa majibu,"alisema.
Mama huyo pia alivitaka vyombo vya habari kuripoti habari za
uhakika kwani si kweli kwamba mtoto wake alitaka kwenda
makaburini kwa ajili ya kuuaga mwili wa Kanumba.
"Lulu yupo kituoni chini ya ulinzi wa polisi, iweje leo atake kwenda
msibani kumuaga Kanumba?" Alihoji mama huyo.
Lucresia alisema yupo pamoja na Mama Kanumba kwa vile msiba
huo ni wa wote hivyo amemtaka awe na moyo wa subira na
ustahamilivu kwa vile ukweli utajulikana.
"Mzazi mwenzangu kuwa na subira, tupo pamoja, Kanumba ni
mtoto wetu sote na mimi nina machungu na kifo chake,"alisema.

MAMA KANUMBA: Nipo tayari kumsamehe Lulu

Mama mzazi wa msanii Steven Kanumba, Flora Mutegoa amesema
yupo tayari kumsamehe msanii Elizabeth Michael 'Lulu',
anayetuhumiwa kumuua Kanumba iwapo vyombo vya sheria
vitamuona hana hatia hiyo.
Flora pia alikanusha madai kuwa, marehemu Kanumba
alikorofishana na baba yake ndiyo sababu hakuweza kushiriki
katika mazishi ya mtoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu
Kanumba, Sinza mjini Dar es Salaam, Flora alisema taarifa hizo
hazina ukweli wowote.
"Marehemu Kanumba na baba yake walikuwa na uhusiano mzuri
isipokuwa watu waliipokea tofauti filamu aliyoitoa, ambayo ilikuwa
ikielezea maisha yake. Hata mimi sijui baba yake aliipokea
vipi,"alisema.
Bi Flora aliishukuru serikali na wananchi waliojitokeza katika
mazishi ya mwanaye na kuongeza kuwa, hakutarajia iwapo
angezikwa na watu wengi kiasi kile.
Aliongeza kuwa, Kanumba na baba yake hawakutofautiana kama
inavyodaiwa na baadhi ya watu, isipokuwa anachojua ni kwamba
mtoto wake aliamua kuwa mbali na mzee ili kujitafutia maisha
yake.
Alisema Mzee Charles Kanumba alishindwa kuhudhuria mazishi ya
mwanaye kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya miguu,
ambayo yamempata uzeeni.
"Kwa kweli sina cha kusema zaidi ya kutoa shukurani zangu za
dhati kwa serikali na watu wote wakiwemo wasanii wenzake, hivi
sasa tunaendelea na mambo ya kifamilia,"alisema.
Alipoulizwa ameupokeaje msiba wa mtoto wake, Bi Flora alisema
kifo chake hakina tofauti na vifo vingine na kusisitiza kuwa, kila
binadamu lazima afe.
"Kama familia, tupo tayari kupokea taarifa zozote, ambazo
tutapewa na vyombo husika, daktari aliyeuchunguza mwili wake
pamoja na polisi, ambao bado wanaendelea na uchunguzi. Kwa
sasa siwezi kusema mengi, naiachia serikali ifanyekazi
yake,"alisema.
Mama Kanumba pia alikanusha madai kuwa, kijana wake ameacha
mtoto. Alisema anachofahamu ni kwamba, mwanaye alikutwa na
mauti akiwa hajaoa na wala hakuwahi kupata mtoto.
Alisema marehemu Kanumba ni mtoto pekee aliyezaa na baba
yake, lakini anao watoto wengine wawili aliozaa na mwanaume
mwingine.

PAPIC ASUSA KWENDA MWANZA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amegoma kusafiri na timu hiyo kwenda Mwanza baada ya kuweka mgomo bardi, kufuatia viongozi wa timu hiyo kukwepa kukutana naye.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kocha huyo amechukizwa na hatua ya viongoziwa klabu yake kugoma kukutana naye ili kuzungumzia hatma yake.
Yanga iliondoka mjini Dar es Salaam jana kwenda Mwanza, ambako Jumapili ijayo itacheza na Toto African katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha huyo kutoka Serbia anatarajiwa kumaliza mkataba wake Aprili 23 mwaka huu na taarifa zisizo rasmi zimeeleza kuwa, tayari uongozi wa Yanga umeshaanza kusaka kocha mwingine.
Hata hivyo, akizungumzia suala la kocha huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Papic hakwenda Mwanza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya tumbo, homa na mapafu.
Sendeu alisema Papic alianza kuugua siku tatu zilizopita na madaktari wamemshauri asisafiri safari ya masafa marefu kwa vile bado hajapona sawasawa.
Kwa mujibu wa Sendeu, kikosi cha Yanga kimekwenda huko kikiwa chini ya Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro.
Sendeu alisema Yanga inatarajiwa kucheza mechi moja ya kirafiki itakayochezwa Kahama mkoani Shinyanga dhidi ya timu ya Ambassador kabla ya kuondoka kesho kwenda Mwanza. Katika msafara huo, mshambuliaji Hamizi Kiiza aliachwa kutokana na kuchelewa kuungana na wenzake, lakini anatarajiwa kuondoka leo na kwenda moja kwa moja Mwanza.

Monday, April 9, 2012

MUHIMBILI YATOA RIPOTI KIFO CHA KANUMBA

Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamethibitisha kuwa, msanii nyota wa filamu
nchini, Steven Kanumba, amefariki kwa tatizo la mtikisiko wa ubongo unaojulikana
kitaalamu kama 'brain concussion'.'

Brain concussion' ni hali ya ubongo kushindwa kufanyakazi kwa muda kutokana na
mtu kuumizwa kichwa au kushikwa na kiwewe kikali.

Kwa mujibu wa magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti toleo la leo, taarifa za ndani zilizopatikana juzi kutoka kwa jopo la madaktari bingwa watano walioufanyia uchunguzi mwili wa Kanumba,zinaeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa.

Mmoja wa madaktari hao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye hakutaka kutajwa
gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia
uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.

"Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia muda wa saa nne asubuhi
hadi saa saba kasoro za mchana na tukagundua kuwa, marehemu alifariki kutokana
na mtikisiko wa ubongo, kwa kitaalamu brain concussion,"alisema.

Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo alizungumza kwa ufupi kuwa,
waligundua kwamba ubongo ulikuwa umevimba na kushuka mpaka karibu na uti wa
mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji na ndiyo maana msanii huyo alikufa
pale pale.

Daktari wa awali alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo, ambao husababisha
kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure).

"Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya
nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka,"alisema daktari huyo.

Aliongeza kuwa, mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wa Kanumba.

Alisema:" Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndio maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji."

Aliongeza:" Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huwezo kutokwa na mapovu mdomoni na hukoropma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki."

Daktari huyo alisema, sehemu ya maono na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa mkemia mkuu ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.

MAMA SALMA KIKWETE ATOA POLE KWA MAMA KANUMBA

MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha msanii nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba nyumbani kwa msanii huyo Sinza, Dar es Salaam.


MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete akikumbatiana na mama mzazi wa msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba alipokwenda kumpa pole mama wa msanii huyo nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.

MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete akiwa na mama mzazi wa msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba alipokwenda nyumbani kwa msanii huyo kumpa pole.

RATIBA YA MAZISHI YA KANUMBA

Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa
jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa
leo makaburi ya Kinondoni, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu,
mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya
wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda
wote wa Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi
ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo
kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye
shughuli nzima.
RATIBAMwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka
Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa
Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa
ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote
kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga
kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima
mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.
Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa
na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa
atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed
Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00
kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.Saa 6:00 mchana, ratiba ya
kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati
wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni,
msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea
makaburini.Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya
marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu
yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.Utulivu, unyenyekevu na
ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga
mpendwa wetu Kanumba.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee
kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua.
Jina lake lihimidiwe.
K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

KANUMBA KUZIKWA KESHO

Mazishi ya msanii nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba yamepangwa kufanyika kesho kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya msanii huyo, Jacob Steven JB alisema jana kuwa, mwili wa marehemu Kanumba utaagwa kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni kuanzia saa nne mbalimbali.
JB alisema shughuli ya kuuaga mwili wa msanii huyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wasanii, mashabiki na ndugu wa marehemu.
Kwa mujibu wa JB, mazishi yamepangwa kufanyika saa 10 jioni kwenye makaburi ya Kinondoni.
JB alisema shughuli ya kuuaga mwili wa Kanumba itakwenda sambamba na misa mbalimbali za kumuombea dua.

MAMA MZAZI WAANUMBA MSIBANI

Mama mzazi wa msanii Steven Kanumba, Florence Mtegoe (aliyeshika tamaa) akiwa nyumbani kwa msanii huyo pamoja na waombolezaji wengine.

PINDA AMUOMBOLEZA KANUMBA

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda akitia saini kwenye kitabu cha maombolezo ya kifo cha msanii Steven Kanumba nyumbani kwake Sinza mjini Dar es Salaam.

KIKWETE ATIA SAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO

RAIS Jakata Kikwete akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha msanii Steven Kanumba, nyumbani kwake, Sinza mjini Dar es Salaam juzi.

Saturday, April 7, 2012

Kanumba alikuwa mtu wa watu,



KUTOKANA na kifo cha msanii Steven Kanumba, mitandao mbalimbali jana ilifurika wasomaji na wachangiaji wakitaka kujua na kujuzana mambo mbalimbali kuhusu msanii huyo, huku wengine wakifuatilia michango aliyowahi kuitoa enzi za uhai wake.
Ifuatayo ni michango yake michache katika mtandao wa twitter, ambao alipenda kuutumia kuwasiliana na watu mbalimbali wakiwemo wabunge, wanasiasa na watu wa kawaida.
Katika ukurasa wake, mtandao huo unaonyesha kuwa juzi, 'alichati' na mashabiki wake fulani, lakini mwishoni aliishia kuvituhumu vyama vyao (vya wasanii) kwa kutomsaidia mwenzao aitwaye Kajala Masanja, ambaye yupo mahabusu.
Kanumba alisema: "Wakati msanii mwenzetu Kajala yuko jela, eti TAFF na Bongo Movie hawamtambui Kajala wala hawawezi kusaidia lolote, hii roho mbaya inatoka wapi? "
Pia siku tatu zilizopita (kabla ya jana), Kanumba aliandika katika ukurasa huo akiwatuhumu mashabiki wanaopenda kumpingia simu usiku na mwisho wa siku wanakuwa hawana cha kusema zaidi ya kutaka tu kumsalimia.
Kanumba alisema: "Sometym mashabiki mnaboa sana, m2 unapiga cm ucku wa manane ukiulizwa shida? oh nilikuwa nataka kukusalimia? mchana mnakua wp? kdg mara unaringa"
Aidha siku 13 kabla ya jana, aliwatumia ujumbe mashabiki wake kupitia ukurasa huo akiwaonya dhidi ya mtu aliyekuwa akitumia jina lake katika mtandao wa Facebook akitaka atumiwe fedha, ambapo Kanumba aliandika akisema:"TAFADHALI MASHABIKI WANGU WOTE FACEBOOK KUNA MTU ANATUMIA JINA LANGU LA STEVEN KANUMBA KUOMBA PESA,PLZ MSITUME NI MWIZI".
Katika kuonyesha mapenzi yake kwa Kajala, siku 18 zilizopita, Kanumba aliandika katika mtandao huo akiwaomba mashabiki wake wamuombee msanii huyo ambaye yupo mahabusu, alisema: "Everybody plz pray for Kajala, prison is not a gud place to be."
Aidha katika blogu yake ya kanumbathegreat juzi Kanumba aliweka picha ya ndege wakiwa juu ya mbuzi na kuandika maneno yafuatayo:
Look at this pic careful. Mmoja ya vitu tulivyotofautishwa na wanyama na ndege ni akili ya kujua mema na mabaya, tizama hao ndege na huyo mbuzi hawana akili kabisa, lakini wanapendana ndio maana unaona wako pamoja, ila binadamu aliyepewa akili ana roho mbaya sana. Katika mafundisho ya YESU KRISTO alisema neno kuu nawapeni PENDANENI. Hata uwe na uwezo wa kuhamisha milima kama huna upendo ni bure, mpende jirani yako kama unavojipenda, upendo haujivuni, hauhesabu mabaya, hautakabari, hauhusudu.....nk
WAKORINTHO 13, Mungu ana akili sana kutuumba kwa mwili huu wa nyama, laiti kama angetuumba kwa vioo au sightmirror ili uweze kuona mwenzako anakuwazia nini?anakufanyia nini?anapanga nini juu yako? ungekuta ni heri ukaishi msituni na wanyama wakali kuliko kukaa na binadamu. Katika tafiti zangu nimegundua kuna dawa mbalimbali mfano ya kichwa, homa nk, lakini dawa ya chuki na roho mbaya hakuna. Kama hiki kingekuwa kipindi kama kile cha zamani za Sodoma na Gomora au cha Nuhu, ambacho Mungu alikuwa akiadhibu hapo hapo, watu wengi sana wangeumbuka hasa wale wanaojifanya wasafi usoni, lakini rohoni ni tofauti. Mungu atusaidie sana hasa sisi vijana tujue kusimama katika ukweli na uwazi, tuubebe upendo wa dhati toka rohoni huku mdomoni tukitamka amani ya kweli impendezayo Mungu ili watoto wetu waje watuenzi kwa mazuri na dunia ijivunie uwepo wetu.
Wakati wa uzinduzi wa duka la mitindo ya mavazi uliofanyika hivi karibuni, Kanumba aliandika maneno yafuatayo kupitia kwenye blogu yake: TULIOSAPOTI MPAKA KITUO HIKI KUFIKIA HAPA KILIPO SOMA MAJINA HAPO JUU JINA LANGU LIPO HAPO. KUSEMA UKWELI INAPOKUJA MAMBO YA KUSAIDIA JAMII, NAJITAIDI KUTOA NINACHOKUA NACHO MAANA HAPA HUKUMBUKA MANENO YA MWANDISHI ALBERT PINE: "What we do for ourselves dies with us. What we do for others and the world remains and is immortal."
Siku chache zilizopita, Kanumba alionekana kukerwa na taarifa zilizoripotiwa na gazeti moja la udaku zikimkariri kusema maneno, ambayo hakuyasema. Aliandika hivi kwenye blogu yake:TAFADHALI SANA SIJASEMA MANENO HAYO WALA SIJAHOJIWA LOLOTE KUHUSU HUO MTAFUTANO,SASA HIYO NUKUU IMETOKA WAPI??VIJANA WENZANGU EBU TUJIFUNZE KUSIMAMA KTK UKWELI MAANA HATA MUNGU HAPENDEZWI NA UONGO.
MASHABIKI WAMLILIAKatika ukurasa wake facebook, mashabiki na rafiki zake walifurika kutuma salamu zao na hizi ni chache kati ya nyingi zilizoko katika ukurasa huo.
Peris Mamadi Ratemo: "Its hard to take it!May ur soul rest in peace!We av every reason to celebrate u!"
Jane Kati: "REST IN PEACE KANUMBA"
Gayle Gabriel: rest in peace Kanumba Steve, every year I celebrate my daughter's birthday, I will remember u because u share birthday with my daughter"
Fatma Binti Mrisho Watuta: "Hata nimekosa la kusema.. ila kwa Mola tunatoka na marejeo ni kwake pia"
Kudra Makunzo: "R.I.P Kanumba Steve, Tanzanians love u, but God loves u more"
Ezekiel Simon Munge: "R.I.P The great one Steve Kanumba!"
Mary Maganga: "Gone too soon! R.I.P Kanumba,you'll be missed by many."
Joyce Joseph Mollel: "Gone to soon...! RIP Steve Kanumba!"
Johnson Mkubwa Super: Kanumba tunaku miss tungekua na uwezo ungeludi tunakupenda ila mungu amekupenda zaidi yetu sawa uende salama tunajisikia vibaya huku nchini Canada" Nigaze Perfect: "We are and for alway miss you Kanumba, rest in peace my friend."
Sophie Kessy: "R.I.P Stevin Kanumba Nyota ya filamu iliyozimika ghafla tutakukumbuka daima we will miss you Kanumba."
Malikia Hapi Kichuna: "R.I.P ua gone 2 soon"
Katika ukurasa huo, nyota huyo alikuwa na marafiki aliowasajili 3,693 huku kukiwa na picha 619 zinazoonyesha mambo na matukio mbalimbali yanayomhusu.

KIFO CHA KANUMBA NI PIGO KUBWA-WASANII

VICENT KIGOSI RAY

WILLIAM MTITU

SANDRA

STEVE NYERERE


MONALISA

CLOUD

IRENE UWOYA

WASANII mbalimbali wa fani ya filamu nchini wameelezea hisia zao kutokana na kifo cha msanii mwenzao, Steven Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Baadhi ya wasanii hao wamesema kifo cha Kanumba kimeacha pigo kubwa katika tasnia ya filamu nchini na kwamba si rahisi pengo lake kuzibika. Zifuatazo ni kauli zilizotolewa na baadhi ya wasanii.
VICENT KIGOSI ‘RAY’

Kanumba alikuwa mtu aliyependa kupambana ili kutimiza ndoto na tulianza kupendana tangu tukiwa hatuna pesa (wakipanda daladala) hadi tulipoachana na usafiri huo wa umma kwa kuanza kutumia magari binafsi.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha Kanumba, nilifika nyumbani kwake na kujitahidi kutaka kujua kilichomsibu rafiki yangu kwa kumshika na kumtikisa bila mafanikio.
Nilipofika nilianza kumuita, nikamshika mkono na kumtikisa tikisa, lakini hakuna nilichofanikiwa. Kanumba alikuwa amefariki dunia.
Mimi na Kanumba tulikuwa na mashindano. Yeye akifanya hiki, mimi nafanya kile, lakini hivyo ndivyo ilivyo maana hata tulipoanza na filamu ya Johari, tulikuwa watu wa kawaida sana.
Kimsingi Kanumba hakupenda tu aonekane yeye, lakini alitaka na wengine wafahamike na zaidi alijitahidi sana kuitangaza Tanzania duniani.
Ingekuwa vipi hata bendera ya nchi ingepepea nusu mlingoti kwa sababu ya Kanumba maana ameitangaza sana nchi yetu huko nje, kiasi kwamba hakuna wasikomjua-kaenda Uingereza, Nigeria, Kongo, Uganda, Marekani na sehemu nyingi tu akitangaza sanaa hii na jina la Tanzania.
Urafiki wetu ulifika mahali tukawa kama ndugu, lakini zaidi ulikuwa wa (urafiki) wa kimashindano zaidi mathalan, yeye alipomleta Ramsey Noah (nyota wa filamu wa Nigeria), mimi nilikuwa nafikiria kumleta nyota mmoja wa Ghana. Pia viwanja vyetu tumenunua jirani jirani huko Mbezi Mpiji na tulipanga kuanza kujenga pamoja.
STEVE NYERERE

Kanumba alikuwa tegemeo langu kubwa katika sanaa na ni yeye pamoja na Ray (Vincet Kigosi) walinipa wazo la kucheza filamu, nikaamua kuanza na Mr. President. Hata juzi, mimi na Ray tulikuwa naye pale Club Maisha, ambapo yeye alikuwa juu anakunywa bia zake na sisi tulikuwa chini na Twanga Pepeta ilikuwa inatumbuiza pale.
Kama asingekuwa Kanumba, mimi nisingekuwa na maisha niliyo nayo, hata gari nililonalo nisingelipata maana ni yeye na Ray ndio walionisaidia kufika hapa nilipo.
ISSA MUSSA 'CLOUD’

Naweza kumueleza Kanumba kwamba alikuwa msanii mbunifu, aliyependa kujituma na kila unakokwenda, ilikuwa lazima kumkuta. Hakuchagua sana maishani mwake, iwe kwenye 'fasheni shoo', muziki au kokote, lazima utaikuta sura yake. Hali hiyo inaonyesha alikuwa mtu wa aina gani.
Sisi wasanii wa filamu tumepata pigo, lakini sio letu pia la Watanzania na Waafrika kwa ujumla. Kwa upande wa wasanii, pigo hili linatukumbukusha wenzetu wa Bongo Fleva walivyompoteza Mtoto wa Dandu (James Ndandu). Sina zaidi ila tunapaswa kumuombea Kanumba maana safari yake ameimaliza na alichotuachia ndicho tunachopaswa kuiga.
WILLIAM MTITU

Nilipata taarifa kama saa sita hivi (usiku), nikaenda pale (nyumbani kwa Kanumba) nikamkuta Ray na wasanii wengi, lakini Kanumba alikuwa amelala macho yake yako juu.
Nilisikitika sana na bado nasikitika kwa hakika siamini mpaka sasa. Kumbuka Kanumba ni msanii mkubwa, kafanya kazi nyingi nzuri hata tulipofika Muhimbili tulikuwa watu wengi wamefika pale.
(Baadhi ya) manesi na madaktari walishindwa kufanya kazi wakaja pale mochwari kushuhudia, wasanii wa muziki na watu wengine wengi tu. Tukio lilikuwa la kusikitisha sana, Kanumba alikuwa amevaa pensi yake, amechana nywele. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba Kanumba hajaacha familia.
IVON SHERRY ‘MONALISA’

Kanumba alikuwa mmoja wa rafiki zangu wa karibu. Nimeumia sana. Nitaadhirika. Tulishaanza kufanya kazi za nje za kimataifa na tulitakiwa tukafanye filamu Ghana mwaka huu.
MOHAMED FRANK

Wakati tunaanza Kaole Sanaa Group mwaka 2002-2003, Kanumba alikuwa rafiki yangu wa karibu alipofanikiwa, hakuwasahau wasanii wenzake.
Nilipopata taarifa ya kifo chake sikuamini. Nilimwambia Dino, mbona siku ya wajinga imeshapita. Sikuamini kwa sababu siku moja niliwahi kupokea ujumbe ukisema Tino amefariki wakati si kweli. Dino akanisisitizia kwamba Kanumba amefariki. Ilinibidi nifunge safari moja huo huo hadi nyumbani kwake Sinza.
Kanumba atabaki kuwa Kanumba. Kifo chake ni pigo kubwa. Hakuna msanii anayeweza kuziba pengo lake. Tunapaswa kumshukuru Mungu. Siku zake za kuishi hapa duniani zimefikia mwisho.
Ameondoka akiwa kijana mdogo sana. Umri wake ni miaka 28. Ni juzi juzi tu alitengeneza filamu inayoitwa Ndoa yangu. Sijui alitaka kueleza nini katika filamu hiyo. Ni kama drama, lakini ndio ukweli wenyewe.
SANDRA

Kanumba alikuwa rafiki yangu sana. Tulipokuwa Kaole, alizoea sana kunitania. Siku moja aliniambia ‘Dada Sandra, nampenda sana yule mwanamke (msanii mwenzao), lakini naogopa kumwambia kwa sababu sina pesa.’ Alikuwa mtu wa utani sana.
ADAM SWEBE

Tumempoteza mtu aliyefanya mambo makubwa na ambayo hayawezi kusahaulika katika tasnia ya filamu. Na bado alikuwa na ndoto ya kufanya mambo mengi zaidi. Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya filamu.
THEA

Huu ni msiba mkubwa na umetushua. Najiuliza kwa nini Kanumba.
IRENE UWOYA

Siwezi kumsahau Kanumba katika maisha yangu. Amenisaidia sana katika fani ya filamu. Kifo chake ni pigo kubwa sana kwangu na watanzania wote. Tumempoteza mtu muhimu.
UGONE MPHEHO

Ulikuwa mtu mbele ya watu, Ukajivika tabasamu cheko na bashasha,Ulikuwa wa mwanzo na jemadari, Kuona mbele na safari kuongoza,Ulikuwa wa mwisho kununa, Ulipokisimangwa kwa kero na ujuvi,Wewe ulishika panga, ukaingia mwituni na njia kutupasulia!Eh jiti kuu la mwituni, ndege wema na wabaya watamiapo,Eh mzizi ulotambaa, ukagusa nyika na bahari kwa pamoja,Eh mbuyu wa thamani, dawa poa na sumu kali zote zipo,Eh wimbo wa pozeo, jua la kuchea na na mwezi wa kuchwea.Nikwambe nini jabali, ulobeba tasnia,Nikusifuje kwa hili, mbinguni wakasikia,Leo dunia hulali, Pepo yakutazamia,













BURIANI STEVEN KANUMBA


NI pigo kubwa na zito. Si kwa familia ya marehemu Steven Kanumba pekee, bali hata kwa wasanii wa fani ya filamu nchini pamoja na mashabiki wa fani hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ni vigumu kuelezea namna kila mtu anayemfahamu Kanumba alivyopokea na kuguswa na taarifa za kifo chake. Wapo walioamini, lakini wengine waliona kama ni ndoto. Wengine walidhani taarifa hizo ni za uzushi.
Kwa wengine, taarifa za kifo cha Kanumba zilionekana kama vile ni za utani. Hawakuamini. Wapo waliopiga simu huku na kule kutaka uthibitisho na wengine walifunga safari hadi nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Taarifa za kifo cha Kanumba zilianza kusambaa saa tisa usiku wa kuakia jana. Kila aliyepata taarifa hizo naye alimtaarifu mwenzake. Baada ya saa chache, asilimia kubwa ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakawa wamepata taarifa hizo, hasa baada ya kuanza kutangazwa na vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Kanumba (28) alifariki dunia nyumbani kwake Sinza baada ya kudondoka na kujibamiza sakafuni akiwa chumbani kwake. Tukio hilo lilitokea baada ya kuzozana na mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, kulijitokeza hali ya kutokuelewana kati ya Kanumba na Lulu na kusababisha wagombane. Inasemekana Lulu alimsukuma Kanumba na kugonga kichwa chake chini.
Habari ambazo hazijathibitishwa zimeeleza kuwa, Kanumba alikuwa akioga ili watoke matembezini ndipo alipomsikia Lulu akiongea kwa simu na mtu mwingine na alipotoka kumuuliza, ndipo mzozo kati yao ukaanza.
Mdogo wa Kanumba, ambaye alikuwepo nyumbani usiku huo, Seti alithibitisha kutokea kwa majibizano kati ya kaka yake na Lulu na kuongeza kuwa, binti huyo ndiye aliyempa taarifa za Kanumba kuanguka chumbani kwake.
Seti alisema baada ya kuingia chumbani kwa Kanumba, alimkuta amedondoka sakafuni huku povu likimtoka mdomoni na baadaye wakabaini kwamba alishakata roho. Lulu, ambaye alitoweka nyumbani hapo kutokana na kuchanganyikiwa, anashikiliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Hivyo ndivyo mauti yalivyomkuta Kanumba. Ametangulia kule ambako binadamu wote lazima watafika, lakini kila mmoja kwa siku na muda wake.
Ni kweli kwamba mauti huugeuza mwili wa binadamu ukawa vumbi, lakini yale mema aliyoyafanya hapa duniani yatabaki kuwa kumbukumbu kwa miaka mingi ijayo.
Wasanii wengi wa filamu wameelezea kuguswa mno na kifo cha Kanumba kwa sababu alikuwa mfano wa kuigwa kwao kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata kiusanii katika kipindi kifupi cha maisha yake.
Kwa mashabiki wa filamu za kibongo, Kanumba alikuwa ni namba moja na kwa kiasi kikubwa aliweza kuweka viwango kwani alikuwa anafaa kwa kila kona kuanzia kuigiza mpaka kuvaa.
Kanumba alikuwa akiishi maisha tofauti na wasanii wenzake hivyo kuwavutia watu wa rika zote. Amemaliza kipindi chake cha miaka 28 akiwa ameacha kumbukumbu ambayo itaishi kwa muda mrefu.
Kanumbaa alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Bugoyi na baadaye sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza kidato cha nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita. Ni wakati huo akiwa Jitegemee, Kanumba alianza shughuli za sanaa katika kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam. Alishiriki kucheza tamthilia nyingi za kundi hilo zilizokuwa zikirushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV kama vileTufani, Gharika, Baragumu na Sikitiko Langu.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti, alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima. Baadhi ya filamu alizotunga na kuzicheza na kumpatia umaarufu mkubwa ni pamoja na Haviliki, Dangerous Desire, She is My Sister, Dar 2 Lagos, Cross my Sin, Village Pastor, Family Tears, Johari, Riziki, Deception, The Shock, Uncle JJ, Off Side, More than Pain, Young Billionaire, This is it, Moses, Devil Kingdoma, Because of you na Big Daddy.
Marehemu Kanumba pia aliwahi kushirikiana na baadhi ya wasanii maarufu wa Nigeria kucheza filamu zake. Miongoni mwa wasanii hao ni Ramsey Nouah, Mercy Johnson, Emmanuel France na Nkiru Silvanus.
Enzi za uhai wake, Kanumba aliwahi kushinda tuzo nyingi za filamu ikiwa ni pamoja na mwigizaji bora mwaka 2006 na 2007 na msanii bora wa mwaka 2007 na 2008.
Kanumba hakuwa tu mwigizaji na mtayarishaji maarufu wa filamu. Hivi karibuni aliteuliwa kuwa balozi wa Oxfam Grow kwa Tanzania.
Baadhi ya watu, ambao Kanumba alikuwa akiwataja mara kwa mara na kuwashukuru kutokana na mafanikio aliyoyapata ni pamoja na Chrissant Mhengga, Sharifa Kalala, Mtitu, Sanura Hussein, Vicent Kigosi na wasanii wa kundi la Kaole.
Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake, upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi. Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasnia ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa kupitia sanaa hii. Wanigeria kwa sasa wanaijua Tanzania kupitia filamu. Vivyo hivyo kwa nchi ya Ghana, ambako Kanumba alikwenda kucheza filamu mwaka jana akiwa na Monalisa.
Nchi nyingi za Afrika zinaijua Tanzania hivi sasa kupitia fani ya filamu na hii ni kutokana na kazi nzuri ya Kanumba. Mwenyewe aliwahi kukaririwa akisema kuwa ndoto yake ni kucheza filamu za Hollywood, ambako aliwahi kutembelea mwaka jana.
Buriani Kanumba. Kifo chako kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yako mahali pema.


Thursday, April 5, 2012

KASEJA: Hatutishiki na vitimbi vyao




NAHODHA wa Simba, Juma Kaseja, amesema vitimbi wanavyofanyiwa na wenyeji
havitawafanya wapunguze ari ya kushinda pambano lao dhidi ya Setif kesho.
Akizungumza na tovuti ya Simba, Kaseja alisema wametazama kwa makini matukio
mbalimbali yanayofanywa na wenyeji wao na wamebaini yako mambo ambayo lengo
lake ni kuwaondoa mchezoni.
“Hebu fikiria, watu wanataka kutusafirisha kwa basi kwa masaa sita wakati wanajua
kanuni ni masaa mawili tu. Halafu, badala ya kutusafirisha hadi mji wa Setif
tulipocheza, wao wametupeleka kwanza mji mwingine na halafu wakatusafirisha kwa
basi kuja Setif. Hizi ni mbinu zao lakini tunazijua,” alisema.
Kaseja alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba walioitoa Zamalek ya Misri katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika miaka kumi iliyopita na anasema hakuna cha
ajabu iwapo timu yake itaitoa Setif.
“Katika uzoefu wangu wa soka, timu pekee ya kiarabu ambayo ilitutendea vema
ilikuwa ni Harass Al Hadoud ya Misri miaka miwili iliyopita. Lakini hawa walikuwa wema
kwa sababu walikuwa wametufunga katika mechi ya kwanza na hivyo hawakuwa na
wasiwasi.
“Ukiona Waarabu wanakufanyia vitimbi ujue wana wasiwasi na wewe. Kama hawana
hofu, watakupa kila unachohitaji. Nashukuru kwamba tuna wachezaji wazoefu wa
kutosha wanaoweza kupambana na lolote,” alisema.

Wakati huo huo, Simba kesho inashuka kwenye Uwanja wa Mei 8, 1945, jijini Setif, Algeria; uwanja ambao una historia ya kipekee nchini humu.
Tarehe 8, Mei mwaka 1945, majeshi ya Ufaransa iliyokuwa ikiikalia kimabavu Algeria
yaliua wananchi kati ya 6,000 hadi 45,000 wa Setif katika mapambano yaliyofanyika
mjini humo.
Uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 30,000 ulibadilishwa jina wakati huo na
kupewa jina hilo la tarehe –kwa kifaransa Stade Mai 8 1945, kwa heshima ya watu
waliopoteza maisha siku hiyo.
Mauaji hayo ndiyo yaliyosababisha timu ya Setif kubadili rangi ya jezi zake kutoka
nyeupe na kijani na kuwa nyeusi na kijani –nyeusi ikiwa na maana ya kuomboleza
maelfu hayo ya watu waliouawa siku hiyo.

MILOVAN: Hali ya hewa haiwezi kutuathiri





KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema hali ya hewa ya mji wa Setif
ambayo ni baridi kali inaweza kuwa faida kwa timu yake na si hasara.
Akizungumza na tovuti ya Simba, Milovan alisema hali ya hewa ya baridi huwafanya
wachezaji wasichoke mapema tofauti na joto ambalo huchosha.
Kuna baridi za aina mbili. Kuna baridi inayotokana na hali ya hewa ya mahali na kuna
baridi inayotokana na eneo kuwa kwenye miinuko (altitude). Zote ni baridi lakini zina
tofauti.
“Ile ya miinuko huwafanya wachezaji washindwe kupumua vizuri na huwa na athari
mbaya sana. Tuliliona hili kwenye mechi ya Kiyovu lakini hapa Setif hakuna miinuko
sana kama Rwanda na hivyo wachezaji wanaweza kucheza vizuri,” alisema.
Alisema jambo la muhimu kwa timu yake ni kutoathiriwa na sauti za washangiliaji wa
Setif wala kughadhabika kirahisi wanapochokozwa na wapinzani wao.
“Mechi yetu na Setif ni ngumu sana. Kila timu ina nafasi ya kufanya vizuri ingawa sisi
tuna faida kutokana na ushindi tulioupata nyumbani. Ni jukumu letu kuhakikisha
tunaulinda ushindi wetu,” alisema.

TFF yalaani mauaji ya bosi wa FA Somalia

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amepokea kwa masikitiko taarifa za shambulizi la kigaidi lililofanywa jana asubuhi (Aprili 4 mwaka huu) jijini Mogadishu, Somalia na kupoteza maisha ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Somalia (SFF), Said Mohamed Nur.
Kwa niaba ya TFF na wadau wa mpira wa miguu Tanzania anatuma salamu za rambirambi kwa Makamu Mwenyekiti wa SFF, Ali Said Ghuled kutokana na kifo hicho cha ghafla cha shambulizi la bomu cha Nur ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Amesema Nur alishiriki kikamilifu katika kujenga maisha ya wananchi wa Somalia kwa kupitia mpira wa miguu, hivyo analaani kwa nguvu vitendo vya kigaidi ambavyo pia vimepoteza maisha ya watu wengine katika tukio hilo.

Kwa kipindi chote cha maisha yake, Nur ameutumikia mpira wa miguu katika ngazi tofauti nchini kwake na ukanda huu wa CECAFA, hivyo kifo chake ni pigo kwa Tanzania, na daima itaendelea kukumbuka mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu.

Rais Tenga amesema TFF iko pamoja na familia ya Marehemu katika kuomboleza msiba huu mzito na kuwataka wawe na uvumilivu na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa kwao.

Kwa mechi zote za TFF zitakazochezwa katika kipindi cha siku 7 zijazo kutakuwa na dakika moja ya kusimama kimya kwa ajili ya kuomboleza msiba huo. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amina.

Wachezaji Yanga wapunguziwa adhabu



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesikitishwa na
vitendo vilivyofanywa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo namba 132 wa
Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yao na Azam uliofanyika Machi 10 mwaka huu.


Vilevile imesikitishwa na uongozi wa klabu ya Yanga kushindwa kuvikemea hadharani
vitendo hivyo vilivyofanywa na wachezaji wake.

Kamati hiyo ilikutana jana (Aprili 4 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Kamishna
mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana kujadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Yanga
kupinga uamuzi uliofanywa na Kamati ya Ligi ya TFF dhidi ya wachezaji hao.

Mbele ya Kamati hiyo, Yanga ilikuwa na rufani mbili. Rufani ya kwanza ya Machi 11
mwaka huu iliomba matokeo ya mchezo huo yafutwe, ikiwemo kadi walizooneshwa
wachezaji wao na mwamuzi aadhibiwe kwa kushindwa kumudu mchezo huo.

Wakati ikifanya mawasilisho (submissions) mbele ya Kamati, Yanga iliamua kuondoa
rufani hiyo kwa vile katika ya pili iliyokatwa Machi 14 mwaka huu ikipinga adhabu
zilizotolewa ina kifungu (j) kilichodai Kamati ya Ligi ya TFF ilikosea kutotoa uamuzi
wowote kwa refa aliyedaiwa kutoa maneno ya kashfa na kejeli kwa wachezaji wao.

Baada ya kusikiliza submissions za pande zote mbili (walalamikaji- Yanga) ambao
walikiri hatia ya vitendo hivyo na kuomba wachezaji wake wapunguziwe adhabu, na
(walalamikiwa- TFF), Kamati imetoa uamuzi ufuatao;

Mchezaji Nurdin Bakari amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu za ligi na faini ya
sh. milioni moja. Omega Seme amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu na faini ya
sh. milioni moja.

Nadir Haroub atatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ambayo haikatiwi rufani.

Lakini Kamati ya Nidhamu imeondoa adhabu ya mechi nyingine tatu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa vile hizo atazitumikia kwa pamoja, lakini adhabu ya faini ya sh. 500,000 inabaki, hivyo atalipa jumla ya sh. milioni moja.

Stephano Mwasika ambaye alifungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja,
adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za msimu wa ligi
2011/2012, lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili.

Kwa upande wa Jerryson Tegete aliyefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000,
adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za ligi msimu huu
(2011/2012), lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili. Adhabu ya Yanga kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake inabaki kama ilivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).

Vilevile adhabu ya faini ya sh. 500,000 kutokana na timu hiyo kupata kadi tano na kuendelea kwenye mechi moja inabaki kama ilivyo vile kanuni ya 25(1) haikatiwi rufani. Kamati imesema adhabu zimeanza kutumika tangu zilipotolewa na Kamati ya Ligi, hivyo kwa ambapo tayari wameshatumikia mechi kadhaa zinahesabika.

Kwa watakaoshindwa kulipa faini wataendelea kuwa nje ya uwanja mpaka fedha hizo zitakapolipwa.

Mwenyekiti Tibaigana amewataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji wao, na makosa hayo yakijirudia adhabu kali zaidi zitatolewa. Pia Kamati ya Nidhamu ya TFF haikujadili suala la Yanga kunyang’anywa pointi tatu katika mchezo kati yake na Coastal Union kwa vile hakukuwa na rufani hiyo mbele yake.

KABURU: Lazima tuishinde ES Setif

KIKOSI cha timu ya soka ya Simba kiliondoka nchini Jumatatu iliyopita kwenda Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya huko inayotarajiwa kuchezwa kesho mjini Setif. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, ATHANAS KAZIGE, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ anaelezea mikakati na matumaini yao katika mechi hiyo.
SWALI: Kikosi chenu kimeshaondoka nchini kwenda Algeria kwa ajili ya mechi yenu ya marudiano dhidi ya ES Setif, itakayochezwa Ijumaa. Mmejipanga vipi kuhakikisha kuwa mnashinda mechi hiyo?
JIBU: Tumejipanga vizuri. Kwanza kabisa viongozi tumefanya kazi yetu ya utawala kwa umakini mkubwa na kila kitu kuhusu Simba kwenda Algeria kimekwenda vizuri.
Unajua safari ni hatua, hivyo tumejipanga kwenda katika vita ya marudiano, ambayo tuna hakika itakuwa ngumu kwetu kwa vile wapinzani wetu hawatakuwa tayari kufungwa nyumbani kwao tena mbele ya mashabiki wao.
Pamoja na ukweli huo, sisi kama viongozi tulishawasiliana na ubalozi wa Tanzania uliopo Algeria kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri na tayari baadhi ya viongozi wetu wa kamati ya ufundi walishatangulia huko.
SWALI: Nimemsikia mwenyekiti wenu Ismail Aden Rage akisema kwamba, wapo baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Algeria, ambao wameahidi kuwashangilia kwa nguvu zote wakati wa mechi hiyo. Je, taarifa hizo ni za kweli?
JIBU: Habari hizo ni za kweli. Wapo watanzania wengi kule Algeria, ambao wameahidi kutuunga mkono. Kwa maana hiyo, Simba itakwenda Algeria ikiwa haina wasiwasi wa kukosa kuungwa mkono.
Kule Algeria wapo wanafunzi wengi kutoka hapa nchini, ambao wamekwenda huko kusoma katika vyuo mbalimbali. Watanzania hao ndio waliotuahidi kutuunga mkono katika mechi hiyo.
SWALI: Mmepanga kusimama kwa muda Misri kwa ajili ya kujipanga kabla ya kwenda Algeria. Lengo lenu ni lipi hasa ?
JBU: Tumeamua kusimama Misri kwa muda kwa ajili ya kufanya mazoezi angalau kwa siku moja na kisha siku inayofuata, tutaondoka kwenda Algeria. Sababu hasa ya kusimama kwa muda Misri ni kutaka kuzoea hali ya hewa ya huko, ambayo inafanana na ile ya Algeria.
Nina hakika wachezaji wetu wataweza kuizoea hali hiyo ya hewa haraka ili waweze kukabiliana vyema na wapinzani wenu. Tumefanya hivyo kwa sababu tulipata tabu sana tulipokwenda Rwanda kucheza na Kiyovu katika mechi ya raundi ya kwanza.
SWALI: Kuna wakati Rage alitoa ahadi ya kuwashonea suti wachezaji wote wa Simba. Je, ameshatimiza ahadi hiyo kabla ya timu kuondoka kwenda Algeria?
JIBU: Ni kweli, tayari wachezaji wetu wote pamoja na viongozi wa benchi la ufundi wameshapata suti hizo na walizivaa siku walipoondoka kwenda Algeria.
Lengo la uongozi kuwanunulia suti wachezaji ni kuipa timu heshima yetu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Klabu zetu zinapaswa kubadilika hivi sasa kwa kwenda na wakati. Tunapaswa kuwavalisha wachezaji wetu nguo za heshima ili waonekane kuwa na thamani mbele ya watu.
Tumepanga kuendelea kufanya mambo makubwa zaidi katika mechi zetu zijazo na hilo litaonekana hapo baadaye. Tunataka wachezaji wetu waweze kujitambua kwamba wapo kwenye klabu kubwa, ambayo inahitaji kuheshimiwa, si kimchezo tu, bali hata kwa mavazi.
SWALI: Kuna ahadi yoyote mliyotoa kwa wachezaji wenu ili kuwahamasisha waweze kushinda mechi hiyo?
JIBU: Ahadi ya zawadi ipo, lakini hiyo ni siri ya klabu, hatuwezi kuitangaza kwa vile ni mambo ya ndani ya klabu yetu ya Simba.
SWALI: Nini maoni yako kuhusu mwenendo wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambayo kwa sasa inaelekea ukingoni?
JIBU: Ligi ya msimu huu ni ngumu ndio sababu hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa kuibuka na ubingwa. Ushindani bado ni mkubwa kwa timu tatu za kwanza na yoyote itakayoshinda mechi zilizosalia, inaweza kutwaa ubingwa.
Pengine jambo la msingi ningependa kuwaomba waamuzi wa ligi hiyo waheshimu na kuzingatia sheria 17 za soka ili washindi waweze kupatikana kutokana na uwezo wao uwanjani badala ya kubebwa.
SWALI: Unauelezeaje ushindani uliopo kati yenu, Yanga na Azam katika kuwania ubingwa?
JIBU: Kwa maoni yangu, naweza kusema kwamba mchuano ni mkali na tunaendelea kupambana ili kuhakikisha tunaivua ubingwa Yanga. Hilo linawezekana kwa vile ndani ya kikosi chetu kuna ushirikiano mkubwa kati ya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.

Wednesday, April 4, 2012

Kiongozi T-Motto akiti Mzee Yussuf ni kiboko

MKURUGENZI wa kundi la muziki wa taarab la Tanzania Motto,Amini Salmini Amour amekiri kuwa, kundi la Jahazi kwa sasa liko juu na kazi zake zinapendwa na mashabiki wengi.
Amini amesema pia kuwa, nyota ya kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yussuf 'Mfalme' inaendelea kung'ara katika medani ya muziki wa taarab na anamuheshimu.
Kiongozi huyo wa Tanzania Motto alisema hayo wiki hii mjini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Burudani kuhusu maendeleo ya taarab nchini.
“Jahazi ni kundi lililoleta mabadiliko makubwa katika muziki wa taarab hapa nchini na Yussuf ni muimbaji hodari, mbunifu na mwenye kuona mbali, hakuna kundi au mwimbaji anayeweza kumfikia kwa sasa,”alisema.
Amini alisema binafsi anakiri kwamba Yussuf yupo juu kimuziki na kundi lake litaendelea kutamba kwa muda mrefu bila kuwa na mpinzani.
Akizungumzia kundi lake la Tanzania Motto, Amini alisema limeanza kujipanga upya baada ya kuanza kwa kusuasua mwishoni mwa mwaka jana.

Waamuzi wanne wafungiwa Z'bar

Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
WAAMUZI wanne wa soka wamefungiwa kuchezesha mechi za michuano mbalimbali ya ligi za Zanzibar kwa muda wa mwaka mmoja kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni pamoja na Ramadhani Ibada Kibo na Mgaza Kinduli wanaotambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA). Wengine ni Remtullah Ali na Mohammed Kassim.
Adhabu hizo zilitangazwa juzi na Ofisa Habari wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Munir alisema ZFA imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, waamuzi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
“Baada ya kuziadhibu klabu pamoja na wachezaji, tumebaini kuwa baadhi ya waamuzi nao wamekuwa chanzo cha vurugu michezoni, hivyo tumechukua uamuzi wa kuwasimamisha,”alisema.
Ofisa huyo alisema wameamua kutoa adhabu kali kwa waamuzi hao ili liwe fundisho kwa wengine, wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Alisema ZFA imetoa onyo kwa waamuzi wengine wanaochezesha ligi mbalimbali, kuheshimu sheria 17 za mchezo huo, vinginevyo nao watakumbwa na fagio la chuma.
“ZFA imechoshwa na vitendo vya vurugu vinavyotokea katika mechi mbalimbali za ligi, hivyo inatoa onyo kwa waamuzi wazingatie sheria 17 za soka,”alisema.