KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, October 30, 2015

TAIFA STARS KWENDA ALGERIA KWA FASTJET




Timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inatarajiwa kusafiri na ndege binafsi ya kukodi ya shirika la Fastjet kuelekea nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Novemba 17 mjini Algiers.

Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege la Fasjet kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Jimmy Kibati amesema kampuni yao imefikia makubaliano na TFF ya kuwa msafirishaji rasmi wa timu ya Taifa kwa ajili ya mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi 2018 dhidi ya Algeria.

Jimmy amesema katika safari hiyo, Fastjet itatoa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 156 walioketi, sambamba na wafanyakazi wa ndege, ambapo wao wametoa punguzo la asilimia 35 katika gharama nzima ya safari ya kuelekea Algeria.

Aidha Jimmy ameongeza kuwa safari hiyo itakua ya masaa 7 ambapo ndege itaitoka Dar es salaam na kutua Djamena – Chad kuongeza mafuta kabla ya kuendelea tena na safari mpaka nchini Algeria.

Naye katibu wa kamati ya Taifa Stars, Teddy Mapunda aliwashukuru Fastjet kwa kukubali kuwa wasafirishaji rasmi wa TaifA Stars kwa mechi dhidi ya Algeria, huku akisema gharama za safari za mtu mmoja kusafiri ni dolla 800 kwenda na kurudi.

Teddy amewaomba watanzania, wapenzi, washabiki wa mpira wa miguu wanaotaka kusafiri kufika ofisi za TFF zilizopo Karume kwa ajili ya kujiandiksha na kuelekea taratibu nzima za safari.

CAF YAIJIA JUU ZANZIBAR


Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) leo hii limeamuru Kamati ya muda inayoongoza Chama cha Mpira Zanzibar (ZFA) iondoe mahakamani mashatka yote dhidi ya uongozi halali wa ZFA.

Katika barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu wa ZFA na nakala yake kuletwa TFF, CAF imesisitiza kuwa kwa mujibu wa katiba za CAF na FIFA ni marufuku masuala ya mpira kupelekwa mahakamani, ZFA ni mwanachama mshiriki wa CAF (Associate Member).

CAF inaigiza kamati ya muda ya ZFA hadi tarehe 07 Novemba, 2015 iwe imetekeleza maagizo na kuhakikisha uongozi halali uliochaguliwa na ZFA unarejea katika shughuli zake uongozi ZFA.

Jambo hili lisipotekelezwa CAF imesema itaifungia Zanzibar uanachama wake. Kikanuni na kikatiba kufungiwa uanachama maana yake ni Mwanachama husika kusitishwa ushiriki katika shughuli zote zinazosimamiwa na FIFA, CAF na wanachama wake wote.

Shughuli hizo ni pamoja na kushiriki mashindano ya kimataifa, kozi mbalimbali na misaada ya kifedha, vifaa, ufundi nk.

TFF inatoa wito kwa mara nyingine kwa pande zinazokinzana kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao kwa faida ya mpira wa Zanzibar, Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

TFF YAMPONGEZA DK MAGUFULI




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za pongezi Dk. John Pombe Magufuli kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika salamu zake, Malinzi amesema TFF ina imani na ahadi za mikakati yake ya kuongeza uwekezaji wa serikali katika maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limetuma salamu za pongezi kwa viongozi wa mpira wa miguu nchini waliochaguliwa kuwa wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Viongozi waliochaguliwa katika nafasi ya Ubunge ni John Kadutu – mbunge wa Ulyankulu – Tabora, (mjumbe wa mkutano mkuu kutoka Mwanza) na Alex Gashaza – mbunge wa Ngara (Makamu mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Kagera)

Aidha waliochaguliwa Udiwani katika maeneo yao ni Khalid Abdallah (Mjumbe wa kamati ya Utendaji – TFF),  Yusuph Kitumbo- (Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tabora), Omari Gindi- (Mwnyekiti wa Chama cha mpira wa Miguu mkoa wa Kigoma), Bathromeo Kimaro - (Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Singida) na Omar Kinyeto (Mjumbe wa mkutano mkuu mkoa wa Singida),  Golden Sanga (Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Ruvuma), Pachal Kihanga (Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa mkoa Morogoro), Yusuf Manji (Mwenyekiti wa klabu ya Yanga SC) ambao wote ni wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF.

TFF inawaomba kutumikia halmashauri zao kwa mafanikio na kutilia mkazo kuhifadhi maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo mbalimbali hususani mpira wa miguu mashuleni.

Thursday, October 29, 2015

SIMBA YAJITUTUMUA, YANGA YABANWA


TIMU kongwe ya soka ya Simba jana iliwapoza machungu mashabiki wake baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja waTaifa, Dar es Salaam.

Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo kiduchu, mabingwa watetezi Yanga walibanwa mbavu na Mwadui ya Shinyanga kwa kulazimishwa sareya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ushindi wa Simba umewapa ahueni kubwa mashabiki wake baada ya kupoteza mechi iliyopita kwa kuchapwa bao 1-0 na Prisons mjini Mbeya.

Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza dakika ya saba.

Kiiza, ambaye alikosa mechi mbili zilizopita, alifunga bao hilo kwa kuunganisha wavuni kwa shuti kali mpira wa krosi uliopigwa kutoka wingi ya kulia na beki Hassan Ramadhani.

Coastal Union nusura isawazishe dakika ya 23 wakati Ismal Mohamed alipoingia na mpira na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Vincent Angban wa Simba.

Kiiza angeweza kuiongezea bao Simba dakika ya 44 baada ya kupewa jukumu la kupiga mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo la hatari la Coastal Union, lakini shuti lake lilitoka nje.

Wakati huo huo, mshambuliaji Bakari Kigodeko jana aliipokonya Yanga tonge mdomoni baada ya kuifungia Mwadui bao la kusawazisha.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata mabao kupitia kwa Donald Ngoma, aliyefunga yote mawili.

Bao la kwanza la Mwadui lilifungwa na Paul Nonga kabla ya Kigodeko kusawazisha.


Tuesday, October 27, 2015

SIMBA KUIVAA COASTAL UNION KESHO, YANGA KUKIPIGA NA MWADUI LIGI KUU



Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea kesho kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali, ikiwa inaingia katika raundi ya tisa huku kila timu ikisaka ushindi wa pointi tatu muhimu.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba SC watawakaribisha Coastal Union kutoka jijini Tanga, mchezo utakaonza majira ya saa 10:30 jioni, huku Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Stand United uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wachimba Almasi wa Mwadui FC watawakaribisha Yanga SC katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto African watakua wenyeji wa maafande wa Mgambo Shooting katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Wakata miwa wa Turiani, Mtibwa Sugar watakua wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, huku watoza ushuru wa jiji la Mbeya katika uwanja wa Sokoine Mbeya City watakua wenyeji wa Majimaji kutoka mkoani Ruvuma.

Ligi hiyo itaendelea siku ya Alhamis kwa michezo miwili kuchezwa, Tanzania Prisons watakua wenyeji wa African Sports katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, JKT Ruvu watakua wenyeji wa Azam FC katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

TWIGA STARS KUJIPIMA NGUVU NA MALAWI


Timu ya Taifa Tanzania ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars) inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Wanawake ya Malawi Novemba 7, 2015 jijini Dar es salaam.

Mchezo huo wa kirafiki ni sehmu ya kujipima kwa Twiga Stars inayonolewa na kocha Rogasian Kaijage, ambayo ilishiriki Fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) mwezi Agosti – Septemba nchini Congo – Brazzavile.

Awali, Twiga Stars ilikuWa icheze mchezo huo nchini Malawi Oktoba 24, kabla ya chama cha soka nchini humo (FAM) kuahirisha mchezo huo, na sasa mchezo huo utacheza nchini Tanzania Novemba 07, 2015.

BUSUNGU, MAGULI WAONGEZWA TAIFA STARS

 KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amewaongeza kikosini washambuliaji Malimi Busungu wa Yanga SC na Elias Maguri katika kikosi kitakachomenyana na Algeria katikati ya mwezi ujao.
Taifa Stars itamenyana na Algeria katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 Urusi, baada ya kuitoa Malawi katika hatua ya kwanza.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Mkwasa ametaja wachezaji 28 ambao watakwenda kambini Oman Novemba 2, mwaka huu.
Mkwasa amewataja wachezaji hao kuwa ni makipa; Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam FC), Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan (Yanga SC), Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka (Simba SC) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba SC) na Salum Telela (Yanga SC).
Washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Free State Stars, A. Kusini), Farid Mussa, John Bocco (Azam FC), Simon Msuva, Malimi Busungu (Yanga SC), Elias Maguri (Ruvu Shooting) na Ibrahim Hajib (Simba SC).
Mkwasa amesema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 1 katika hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kabla ya safari ya Muscat, Oman kwa kambi ya siku 10.
Amesema wakiwa Oman, pamoja na mazoezi, watacheza mchezo mmoja au miwili ya kujipima na wenyeji wao, iwapo watakuwa tayari kabla ya kurejea Dar es Salaam Novemba 11 tayari kwa mchezo wa kwanza na Algeria Novemba 14, Uwanja wa Taifa.
Amesema kikosi kitaondoka Dar es Salaam kwenda Algiers Novemba 16, tayari kwa mchezo wa marudiano Novemba 17.

Thursday, October 22, 2015

AZAM YAIBANJUA NDANDA 1-0


BAO pekee la beki Shomary Salum Kapombe limeipa ushindi wa bao 1-0 Azam FC dhidi ya wenyeji, Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda, Sijaona, Mtwara.
Kapombe alifunga bao hilo dakika ya 79 kwa kichwa akimalizia krosi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC ifikishe poniti 19, sawa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga SC wanaoendeleza kuongoza ligi hiyo kwa wastani wa mabao.
Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Serge Wawa Pascal, Said Mourad, Frank Domayo, Himid Mao, Ame Ali ‘Zungu’/Khamis Mcha, Kipre Tchetche/Jean Mugiraneza na Ramadhani Singano ‘Messi’/John Bocco.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo, Mwadui FC wameibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Mabao ya Mwadui leo yamefungwa na Jerry Tegete dakika ya saba na 32 na Jamal Mnyate dakika ya 75, wakati bao pekee la Mgambo limefungwa na Abuu Daudi dakika ya 64.
JKT Ruvu imetoka sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Mbeya City imeshinda 1-0 dhidi ya African Sports ya Tanga bao pekee la Geoffrey Mlawa dakika ya 15 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

YANGA YAIGAGADUA TOTO AFRICAN



YANGA SC imejiweka vizuri katika kiti cha usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 4-1 Toto Africans ya Mwanza jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 19 baada ya mechi saba, ikiwazidi kwa pointi tatu Azam FC ambao kesho wanacheza mechi ya saba dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na beki wa kulia, Juma Abdul dakika ya tisa kwa shuti kali umbali wa zaidi ya mita 20 akimaizia kona ya Haruna Niyonzima.
Hata hivyo, Yanga SC wangeweza kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa wanaongoza kwa mabao zaidi kama wangetumia vizuri nafasi zote walizotengeneza, ikiwemo penalti ambayo alikosa Mzimbabwe Donald Ngoma.
Ngoma alikosa penalti hiyo dakika ya 45 ikipanguliwa na kipa wa Toto, Mussa Mohammed baada ya yeye mwenyewe kumnawisha mpira beki Carlos Protas na refa Ahmada Simba wa Kagera akaamuru pigo hilo.
Katika kipindi cha kwanza, Toto walifanya shambulizi moja tu la maana, Miraji Athumani ‘Madenge’ akishindwa kumalizia vizuri pasi ya Edward Christopher dakika ya 42 kwa kumpa nafasi kipa wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ kupangua.
Kipindi cha pili, Yanga SC walianza na mabadiliko Juma Abdul akimpisha Simon Msuva ambaye alikwenda kufunga bao la pili dakika ya 49.
Toto Africans ilipata bao lake dakika ya 62 kupitia kwa Miraj Athumani ‘Madenge’ kwa kichwa akimalizia mpira ulioparazwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Bernad Evarigetus.
Mrundi Amissi Tambwe aliipatia Yanga SC bao la tatu dakika ya 81 akimalizia krosi ya Simon Msuva ambaye alifunga bao la nne dakika ya 90 akimalizia pasi ya Mbrazil Andrey Coutinho.
Beki wa Toto, Hassan Khatib alionyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 90 na ushei kwa utovu wa nidhamu na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Simon Msuva dk46, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan/Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Godfrey Mwashiuya/Andrey Coutinho. 
Toto Africans; Mussa Mohammed, Hassan Khatib, Robert Magadula/Miraj Makka, Hamisi Kasanga, Carlos Protas, Salimn Hoza/William Kimanzi, Japhet Vedastus/Jaffar Mohammed, Abdallah Seseme, Evarigetus Bernad, Edward Christopher na Miraji Athumani.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

SIMBA YAKALISHWA KITAKO NA PRISONS


BAO pekee la Mohammed Mkopi dakika ya 62 limeipa Prisons FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC  jana kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hicho kinakuwa kipigo cha pili kwa Simba SC inayofundishwa na Muingereza Dylan Kerr katika Ligi Kuu msimu huu, baada ya awali kufungwa 2-0 na mahasimu, Yanga SC.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika nne kipindi cha kwanza, baada ya Nahodha wa Prisons, kudai mchezaji wa Simba SC, Pape Ndaw, ana kitu mfano wa hirizi kiunoni.
Suala hilo lilifika kwa mwamuzi na mchezaji huyo kupelekwa katika chumba maalum na kukaguliwa na msimamizi wa mechi hiyo, Joseph Mapunda.
Hata hivyo, zilitokea vurugu za hapa na pale kwa kila upande ukiona unaonewa, ingawa Ndaw alirejea uwanjani kuendelea na mchezo baada ya ukaguzi huo.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Elias Maguri amefunga mabao mawili dakika za 47 na 60 timu yake, Stand United ikishinda 3-0 dhidi ya Majimaji ya Songea Uwanja wa Kambarage Shinyanga, bao lingine likifungwa na Pastory Athanas dakika ya 66.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi,  Simon Sserunkuma/Mwinyi Kazimoto, Awadh Juma/Said Ndemla, Pape Ndaw, Joseph Kimwaga na Peter Mwalyazi/Ibrahim Hajib.
Prisons; Aron Kalambo, Laurian Mpalile/Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Lambart Sabiyanka, Juma Seif ‘Kijiko’/Ally Milanzi, Mohammed Mkopi, Jeremiah Juma na Benjamin Asukile.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

KAMATI YA STARS YAANZA KUKUSANYA MICHANGO



Katibu wa Kamati ya Taifa Stars, Teddy Mapunda leo amefanya makutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, ambapo ametumia nafasi hiyo kutangaza namba za simu za uchangiaji kwa Watanzania kwa ajili ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Akiongea na waandishi wa habari, Teddy amesema watanzania wanaweza kuichangia Taifa Stars kiasi chochote cha fedha kuanzia shilingi mia moja (TZS 100) kwenda namba 0654-888868 (Tigo Pesa) na 0789-530668 (Airtel Money) ambazo zitatumika kwa ajili ya motisha kwa wachezaji, uhamasishaji/masoko na maboresho ya kambi za ndani na nje ya nchi.

Aidha Teddy amesema Kamati ya Taifa Stars inaandaa utaratibu kwa ajili ya washabiki watakaotaka kusafiri kuelekea nchini Algeria katika mchezo wa marudiano, waweze kuchangia gharama za usafiri ili waweze kwenda kuipa sapoti Stars katika mchezo wa marudaiano Novemba 17, 2015.

“KamatI inaendelea na mchakato wa kukamilisha suala la kambi ya Taifa Stars, na mpaka sasa tunasubiri majibu kutoka katika vyama vya soka vya vya nchi tunazotaka kuweka kambi ambazo ni Afrika Kusini, Dubai na Oman kabla ya kutangaza rasmi kambi itakapokuwa” Alisema Teddy.

Kamati inawaomba watanzania, wadau, washabiki na wapenzi wa mpira miguu nchini kuichangia timu ya Taifa kupitia namba zilizotolewa na pia kujitokeza kwa wingi kuujaza uwanja wa Taifa siku ya mchezo wa tarehe 14 Novemba, 2015.

Tuesday, October 20, 2015

KIIZA MCHEZAJI BORA WA MWEZI



Mshambuliaji wa timu ya Simba, Hamisi Kiiza ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Septemba.

Kwa kuibuka mchezaji bora, Kiiza atazawadiwa sh. milioni moja kutoka kwa mdhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.

Kiiza ambaye ameisadia Simba kufanya vizuri kwenye mwezi huo, ikiwemo kufunga mabao matatu (hat trick) kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar aliwashinda washambuliaji wa timu za Stand United (Elias Maguli) na Yanga (Amisi Tambwe).

Ndani ya mwezi Septemba ambapo zilichezwa raundi tano, Kiiza amefunga jumla ya mabao matano.

LIGI KUU BARA KUPIGWA LEO; YANGA NA TOTO; SIMBA NA PRISONS



Ligi kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku timu 8 zikisaka kupata pointi tatu muhimu.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Young Africans watawakaribisha Toto Africans, mchezo utakaonza majira ya saa 10:30 jioni, mjini Shinyanga Stand United watakua wenyeji wa Majimaji katika uwanja wa Kambarage mjini humo.

Tanzania Prisons watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.

Alhamis ligi hiyo itanendelea kwa michezo minne pia kucheza katika viwanja mbalimbali, JKT Ruvu wataikaribisha Mtibwa Sugar uwanaj wa Karume jijini Dar es salaam, Mwadui FC watacheza dhidi ya Mgambo Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.

Jijini Mbeya, Mbeya City watawakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine, huku Ndanda FC wakiwa wenyeji wa waoka mikate wa bakhresa Azam FC katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

RAUNDI YA 11 LIGI KUU BARA KUCHEZWA NOVEMBA 7 NA 8



Mechi za raundi ya 11 za Ligi Kuu ya Vodacom zilizokuwa zichezwe Novemba 7 na 8 mwaka huu sasa zitafanyika Desemba 12 na 13 kupisha maandalizi ya Taifa Stars ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.

Taifa Stars inatarajia kuingia kambini mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi ya kwanza dhidi ya Algeria ambayo itafanyika Novemba 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana nchini Algeria, Novemba 17 mwaka huu.

Mechi hizo za Vodacom zitakazochezwa Desemba 12 ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga (Tanga), Kagera Sugar na Ndanda (Tabora), Stand United na Mwadui (Shinyanga), Mbeya City na Mtibwa Sugar (Mbeya), Azam na Simba (Dar es Salaam) na Majimaji na Toto Africans (Songea). Mechi za Desemba 13 ni kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons (Dar es Salaam), na Coastal Union na African Sports (Tanga).

Pia mechi tatu za raundi ya sita ambazo hazikuchezwa Oktoba 4 mwaka huu kupisha mechi ya Taifa Stars na Malawi sasa zitafanyika Desemba 16 mwaka huu. Mechi hizo ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam), na African Sports na Yanga (Tanga), mchezo kati ya Ndanda na Simba (Mtwara utapangiwa tarehe ya kuchezwa.

Nayo mechi namba 59 kati ya JKT Ruvu na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Oktoba 21 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam imesogezwa mbele kwa siku moja hadi Oktoba 22 mwaka huu ili kuipa nafasi ya mapumziko JKT Ruvu ambayo jana (Oktoba 18 mwaka huu) ilicheza mechi yake ya raundi saba mkoani Shinyanga

SDL KUENDELEA NOVEMBA 14



Ligi Daraja la kwanza nchini (SDL) sasa itaanza Novemba 14 badala ya Oktoba 31 ili kutoa fursa kwa bodi ya Ligi kukamilisha maandalizi mengine ikiwemo viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo ya ligi hiyo.

Makundi ya SDL ni kama ifuatavyo; Kundi A ni Abajalo FC (Tabora), Singida United (Singida), Mvuvuma FC (Kigoma), Milambo FC (Tabora), Green Warriors (Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam) wakati kundi B ni Bulyanhulu FC (Shinyanga), JKT Rwamkoma (Mara), Pamba FC (Mwanza), AFC Arusha, Madini FC (Arusha) na Alliance Schools (Mwanza).

Kundi C ni Kariakoo (Lindi), Mshikamano FC (Dar es Salaam), Cosmopolitan (Dar es Salaam), Abajalo FC (Dar es Salaam), Changanyikeni Rangers (Dar es Salaam) na Villa Squad (Dar es Salaam). Kundi D ni African Wanderers (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Town Small Boys (Ruvuma), Wenda FC (Mbeya), Coca-Cola Kwanza FC (Mbeya) na Sabasaba United (Morogoro).

Monday, October 19, 2015

KAMATI MPYA YA TAIFA STARS YAZINDULIWA




Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa Stars iliyoteuliwa hivi karibuni na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bwana Farough Baghozah leo hii amekutana na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam na kuitambulisha rasmi kamati hiyo.

Katika kamati hiyo ya Taifa ya Stars wapo Michael Wambura – Makamu Mwenyekiti, Bi Teddy Mapunda – Katibu, Wakili Imani Madega – Mweka Hazina, na wajumbe wengine ni Juma Pinto, Isaac Chanji, Salum Abdalla na Moses Katabaro.

Pia Mwenyekiti amechukua fursa hiyo kutangaza kamati ndogondogo na wajumbe wake kama ifuatavyo:
 
1. Maandalizi ya timu, zikiwemo huduma kwa timu ya Taifa stars
Mwenyekiti – Imani Madega
Wajumbe – Msafiri Mgoyi,Teddy Mapunda.

2. Uhamasishaji wa mchezo (Michezo ijayo) na Masoko
Mwenyekiti – Juma Pinto
Wajumbe – Baraka Kizuguto, Mlamu Ng’ambi, Charles Hamka, Hashim  Lundenga, Maulid Kitenge, Shaffih Dauda, Salehe Ally, Peter Simon,  Edo Kumwembe na Mahmoud Zubeiry.

3. Kamati ya Fedha

Mwenyekiti – Farough BaghozahWajumbe – Teddy Mapunda, Michael Wambura, Imani Madega,          Juma Pinto, Isaac Chanji, Moses Katabaro na Edgar Masoud.

4. Mikakati ya ushindi – itakuwa na kamati ndogondogo na zitakuwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti Farough Baghozah, Teddy Mapunda, Mohamed Nassoro, Philemon Ntahilaja, Isaac Kasanga, Cresencius Magori.

Pia kamati imetangaza kauli mbiu ya ushindi inayosema “NCHI YETU, TIMU YETU, TAIFA LETU, USHINDI WETU” itakayoanza kutumika kuanzia leo hii.  Pia Kamati imemteua Bi Teddy Mapunda kuwa msemaji mkuu wa kamati hiyo.

Timu inatarajia kuweka kambi Nje ya Nchi kwa takribani siku 12 ili kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria Novemba 14 Dar es salaam, na Novemba 17 nchini Algeria.

Aidha Mwenyekiti alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania wote warudishe imani kwa timu yao, wajitokeze kwa wingi kwenye mechi ijayo tarehe 14 November dhidi ya Algeria hapa nyumbani.  

Pia akatoa wito kwa Watanzania Wote kuchangia timu kwa hali na mali (Madawa, Maji, vifaa vya michezo na kadhalika)…aliongeza ‘Mwenyekiti wa Kamati Bwana Farough Baghouzah.

Saturday, October 17, 2015

SIMBA YAIFYATUA MBEYA CITY



BAO pekee la beki Mganda, Juuko Murushid dakika ya tatu, limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini hapa jioni ya leo.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 15 baada ya kucheza mechi sita na kuendelea kuwa nafasi ya tatu, nyuma Yanga na Azam zenye pointi moja zaidi kila moja.
Simba SC ilicheza vizuri leo na kama washambuliaji wake wangekuwa makini, wangeweza kuvuna mabao zaidi.
Mshambuliaji Haruna Moshi aliichezea kwa mara ya kwanza leo Mbeya City tangu asajiliwe msimu huu na alidumu uwanjani kwa dakika 60 tu kabla ya kumpisha Hamad Kibopile.
Kipa wa zamani wa timu ya vijana ya Chelsea ya England, Vincent Angban raia wa Ivory Coast leo aliidakia Simba SC kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu na kulinda vyema lango la Wekundu la Msimbazi.
Hii inakuwa mara ya kwanza Simba SC kuifunga Mbeya City tangu ipande Ligi Kuu, msimu wa kwanza wakitoa sare mechi zote na msimu uliopita Wekundu wa Msimbazi wakifungwa mechi zote.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Yanga SC na Azam FC zimetoka sare ya 1-1, Majimaji FC imeifunga 1-0 African Sports, Ndanda FC imetoka sare ya 0-0 na Toto Africans, Stand United imeifunga 3-0 Prisons, Coastal Union imefungwa 1-0 na Mtibwa Sugar.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoonyeshwa moja kwa moja na Azam TV, itaendelea kesho kwa michezo miwili, Mgambo Shooting na Kagera Sugar uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Mwadui FC na JKT Ruvu Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Juma Kaseja, Hassan Mwasapile, John Kabanda, Haruna Shamte, Yohana Morris, Christan Sembuli/Abdallaha Seif dk46, Rafael Khalifa, Steven Banda, Haruna Moshi 'Boban'/Hamad Kibopile dk60, Themi Felix na Joseph Mahundi.
Simba SC; Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Jonas Mkude/Awadh Juma dk60, Justice Majabvi, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto/Joseph Kimwaga dk80, Mussa Hassan Mgosi na Abdi Banda/Peter Mwalyanzi dk60.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

YANGA, AZAM ZASHINDWA KUTAMBIANA



AZAM FC na Yanga SC zimetoshana nguvu, baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC iendelee kuongoza ligi kwa wastani wa mabao, ikiwa ina pointi 16 sawa na Azam FC baada ya kila timu kucheza mechi sita.
Mchezo huo uliochezeshwa refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Zimbabawe, Donald Ngoma dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kipre Tchetche akishangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kusawazisha

Ngoma alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya Malimi Busungu, ambaye naye alipokea mpira mrefu wa beki wa kulia, Juma Abdul, Yanga SC ikitoka kushambuliwa.
Yanga SC ilistahili kumaliza kipindi hicho wakiwa wako mbele, kwani waliwazidi wapinzani wao katika kumiliki mpira.
Lakini katika utengenezaji wa nafasi timu zote zililingana, Yanga SC wakipoteza nafasi mbili za wazi kama Azam FC.
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alidaka shuti la Busungu dakika ya sita na dakika ya 33, Kelvin Yondan alimhadaa vizuri beki wa Azam FC, Serge Wawa Pascal, lakini Manula akaokoa.
Mshambuliaji Mkenya wa Azam FC, alijaribu kuunganisha kwa kichwa ha mkizi krosi ya John Bocco, lakini mpira ukaenda nje dakika ya 19 na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliingia vizuri kwenye eneo kla hatari la Yanga SC, lakini Mwinyi Hajji Mngwali akatokea na kuokoa. 
Kipindi cha pili, Azam FC walibadilika na kuanza kucheza kwa kujiamini na mambo yalikuwa mazuri zaidi upande wao, baada ya mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche kuingia kuchukua nafasi ya Allan Wanga.
Na ni Kipre Tchetche huyo huyo aliyekwenda kuisawazishia bao Azam FC dakika ya 82 akimchambua vizuri ‘Tanzania One’, Ally Mustafa ‘Barthez’ baada ya kupokea pasi ya Farid Mussa.
Yanga SC walihamishia kambi kwenye lango la Azam FC kusaka bao la ushindi na wakafanikiwa kupata penalti dakika ya 88, lakini mkwaju wa Mzimbabwe Thabani Kamusoko ukapanguliwa na kipa Aishi Manula.
Hata hivyo, penalti hiyo ilionekana kuwa ya utata, kwani Simon Msuva alimtoka beki, David Mwantika akamchambua kipa Aishi Manula lakini mpira ukaenda juu kidogo ya lango la Azam FC na kutuama kwenye nyavu za juu.
Katika mastaajabu ya wengi, Refa Kambuzi akaamuru mkwaju wa penalti, ambao wachezaji wa Azam FC walipingana naye kwa dakika zaidi ya moja, kabla ya kukubali kwa shingo upande na Aishi akainusuru timu yake kuzama.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Cannavaro, Mbuyu Twite/Said Juma ‘Makapu’ dk78, Salum Telela/Deus Kaseke dk89, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu/Simon Msuva dk56.
Azam FC; Aishi Manula, Aggrey Morris, David Mwantika, Serge Wawa Pascal, Shomary Kapombe, Farid Mussa Shah Malik, Kipre Balou/Frank Domayo dk69, Himidi Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk57, Allan Wanga/Kipre Tchetche dk63 na John Bocco.

MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA LEO
Okotba 17, 2015
Yanga SC 1-1 Azam FC
Majimaji FC 1-0 African Sports
Mbeya City 0-1 Simba SC
Ndanda FC 0-0 Toto Africans
Stand United 3-0 Prisons
Coastal Union 0-1 Mtibwa Sugar

Thursday, October 15, 2015

KUZIONA YANGA, AZAM BUKU TANO


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom siku ya Jumamosi kati ya Yanga SC dhidi ya Azam utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, kiingilio vha chini kikiwa ni shilingi elfu tano (5,000) kwa viti vyenye rangi ya bluu, Kijani na Machungwa.

Tiketi za mchezo huo zitauzwa siku ya mchezo Jumamosi katika eneo la Uwanaj wa Taifa jijini Dar es salaam, ambapo kingilio cha juu kitakua ni Shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa VIP A, na Shilingi Elfu Ishirini (20,000) kwa VIP B & C.

Mwamuzi wa mchezo huo atakua Abdallah Kambuzi kutoka mkoani Shinyanga, akisaidiwa na Makame Mdogo (Shinyanga), Robert Luhemeja (Mara), mwamuzi wa akiba Frank Komba (Dsm) huku Kamisaa wa mchezo akiwa Joseph Mapunda kutoka mkoa wa Ruvuma.

Michezo mingine ya Ligi Kuu ya Vodacom siku ya Jumamosi ni Majimaji FC dhidi ya African Sports katika uwanja wa Majimaji mjini Songea, Ndanda FC wakiwakaribisha Toto African katika dimba la Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mbeya City FC watawakaribisha Simba SC kwenye dimba la uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Stand United wakiwakaribisha Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyaga, Jijini Tanga Coastal Union watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa michezo miwili, Maafande wa Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Kagera Sugar uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku wachimba Almasi wa Mwadui FC wakiwakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Mwadui Complex.

Ligi Daraja la Kwanza chini (FDL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo 12 kuchezwa katika viwanja mbalimbali kutoka katika makundi yote matatu ya A, B, na C.

Ijumaaa African Lyon watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, ukiwa ni mchezo wa kundi A.

Jumamosi Kundi A, Mjii Mkuu (CDA) watakua wenyeji wa Kiluvya Uinted katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, KMC wakiwakaribisha Polisi Dar kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Kundi B, Kimondo FC watawakaribisha Polisi Morogoro uwanja wa Vwawa – Mbozi, Burkinafaso dhidi ya Kurugenzi uwanja wa Jamhuri Morogoro, Njombe Mji dhidi ya JKT Mlale uwanja Amani Njombe.

Kundi C, Mbao FC dhidi ya Panone FC uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Rhino Rangers dhidi ya Polisi Mara uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, Geita Gold Vs Polisi Tabora uwanja wa Nyankumbu Geita na JKT Kanembwa Vs JKT Oljoro uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili kuchezwa, Ashanti United watawakaribsiha Friends Rangers uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, huku Ruvu Shooting wakiwa wenyeji wa Lipuli FC katika uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.

TFF YAUNDA KAMATI YA TAIFA STARS



Katika kuimarisha maandalizi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) kuelekea katika mashindano mbalimbali ikiwemo mechi mbili za ugenini na nyumbani dhidi ya Algeria, Rais wa TFF Jamal Malinzi ameunda kamati maalum itakayoitwa “Kamati ya Taifa Stars” ambayo majukumu yake yatakua:

(i) Kuimarisha huduma kwa wachezaji,

(ii) Uhamasishaji na Masoko,

(iii) Kuhamasisha wachezaji,

(iv) Kuandaa na kusimamia mkakati wa Ushindi.

 Kamati hii itaongozwa na Mwenyekiti Farough Baghouzah, Teddy Mapunda (Katibu), Wajumbe ni Juma Pinto, Michael Wambura, Iman Madega, Salum Abdallah na Isaac Chanji.

Aidha Kamati hiyo imepewa jukumu la kuwashirikisha wadau mbalimbali wa mpira wa miguu katika kutekeleza majukumu hayo.

Wadau wa mpira wa miguu ambao kamati itashirikiana nao ili wajumuike na kusaidia majukumu mbalimbali katika kamati hiyo wanaombwa waitikie wito huo.

Tuesday, October 13, 2015

YANGA, AZAM KUVAANA WIKIENDI HII, SIMBA NA MBEYA CITY



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, ikiwa katika mzunguko wa saba timu 14 zitapambana kusaka pointi 3 muhimu.

Young Africans watawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi, huku timu zote zikiwa na pointi 15 kileleni zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa.

Kabla ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam, kutakua na mchezo wa utangulizi wa kuombea amani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, 2015.

Mchezo huo utawakutanisha viongozi wa dini watakocheza dhidi ya mabalozi wanaofanya kazi nchini, mechi hiyo itaanza saa 8:25 mchana na kumalizika saa 9:15 alasiri.

Majimaji FC ya mkoani Ruvuma watakua wenyeji wa African Sports kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea, huku Ndanda FC wakiwakaribisha Toto African kutoka jijini Mwanza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Jijini Mbeya, watoza ushuru wa jijini hilo Mbeya City FC watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine, Chama la wana Stand United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Coastal Union wagosi wa kaya wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa michezo miwili kuchezwa, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakwani, huku Mwadui FC wakicheza na maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Mwadui Complex.

Taarifa zote za TFF, Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja wa Kwanza (FDL) ikiwemo ratiba, matokeo na msimamo, wafungaji zinapatikana kwenye tovuti ya TFF, www.tff.or.tz

STARS, ALGERIA KUKIPIGA NOVEMBA 14



Mchezo wa hatua ya pili kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Algeria (The Fox Desert) utafanyika tarehe 14 Novemba, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager itacheza mchezo huo dhidi ya Mbweha wa Jangwani siku ya Jumamosi Novemba 14, na mchezo wa marudiano kuchezwa siku tatu baadae Algeria 17 Novemba, 2015.

Kikosi cha Stars chini ya Kocha Mkuu Charles Mkwasa kimefanikiwa kusonga hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Malawi (The Flames) kwa jumla ya mabao 2-1, nyumbani ikishinda 2-0, na kufungwa 1 – 0 jijini Blantyre.

Sunday, October 11, 2015

TAIFA STARS YACHAPWA 1-0 NA MALAWI, LAKINI YASONGA MBELE


Na Princess Asia, BLANTYRE
TANZANIA imetimiza ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya kufungwa 1-0 na Malawi mchana wa leo Uwanja wa Kamuzu mjini hapa.
Tanzania inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya Jumatano kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilifungwa na John Banda dakika ya 42 aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Chiukepo Msowoya

Taifa Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu, mshambuliaji Mbwana Samatta alikaribia kufunga, baada ya kumtoka beki Limbikani Mnzava, lakini kipa Simplex Nthala akaokoa.
Malawi wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya shuti kali la Banda kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
Barthez akafanya kazi nzuri tena dakika ya 10 baada ya kuokoa michomo miwili mfululizo ya Malawi.
Stars ilizinduka dakika ya 35 baada ya Thomas Ulimwengu kumtoka vizuri beki wa Malawi Yamikani Fodya baada ya pasi ndefu ya Samatta, lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko, akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo la Malawi, lakini bado mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa Tanzania.
Dakika ya 58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliokoa hatari langoni mwake na dakika ya 62 Malawi walifanya mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni mwa Stars, ikiwemo kupata kona mbili.      
Dakika ya 72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.
Malawi walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Wachezaji wa Tanzania walitumia dakika nne za majeruhi kujiangusha kupoteza muda na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wote walionyeshwa kadi za njano kwa sababu hiyo.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo Novemba.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Said Ndemla/John Bocco dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Mrisho Ngassa dk75.
Malawi; Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Miracle Gabeya/Robin Ngalande dk76, Yamkani Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri, Chimango Kayira, Micium Mhone, Chiukepo Msowoya, John Banda na Shumaker Kuwali. 
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

Saturday, October 10, 2015

TAIFA STARS YATUA SALAMA MALAWI


Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinachodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premieum Lager kimewasili salama katika mji wa Blantyre nchini Malawi jioni ya leo tayari kwa mchezo wa marudiano siku dhidi ya wenyji siku ya jumapili.

Stars inayonolewa na makocha wazawa Charles Boniface Mkwasa na Hemedi Morocco iliondoka leo kwa usafiri wa shirika la ndege la Fastjet na kuwasili jiji la Lilongwe saa 4 asubuhi kabla ya kuanza safari ya bus kuelekea Blantayre iliyochukua takribani masaa 3.

Wachezaji wote wapo katika hali nzuri kuelekea katika mchezo wa marudiano dhidi ya Malawi siku ya Jumapili ambapo Stars itashuka dimbani kusaka matokeo mazuri yatakayoiwezesha kufuzu kwa hatua ya pili, katika mchezo wa awali  uliochezwa jijini Dar es salaam, Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2- 0.

Stars inatarajiwa kufanya mazoezi kesho jioni katika uwanja wa Kamuzu Banda uliopo Blantyre, uwanja ambao utatumika kwa mchezo wa siku ya Jumapili.

Kuelekea mchezo huo wa marudiano, Kocha wa Stars Charles Mwasa amesema vijana wake wote wapo katika hali nzuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo.

Katika hatua nyingine mabus mawili yenye washabiki wa Stars Supporter yako njiani kuelekea nchini Malawi kwa ajili ya kuipa sapoti timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mchezo huo wa Jumapili.

TWALIB AMWAGA MIPIRA 100 YA UFUKWENI



Kocha wa timu ya Taifa ya Oman ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer), Twalib Hilal jana ametoa msaada wa mipira 10 kwa ajii ya mchezo wa soka la ufukweni ambao umeanza kuwa maarufu nchni.

Twalib ambaye ni kocha na Mkufunzi wa FIFA wa soka la ufukweni alikabidhi mipira hiyo kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya mchezo huo.

Kesho Jumamos tarehe 10 Oktoba, 2015 kocha Twalib atakutana na makocha, waamuzi wa mchezo wa ufukweni waliopo jijii Dar es salaam ili kubadilishana uzoefu saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume.

STAR TV YATOA MILIONI 450 KUONYESHA LIVE LIGI DARAJA LA KWANZA



Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) leo limeingia mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya shilingi milioni mia nne hamsini (450,000,000), na kituo cha luninga cha Star Tv kurusha matangazo ya Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL)

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa kusaini mkataba huo, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliishukuru kampuni ya Sahara Media Group kwa kuamua kuwekeza katika mpira wa miguu nchini kwa kuamua kuonyesha ligi daraja la kwanza.

Malinzi ameviomba vilabu vya FDL kutumia udhamini huo kama chachu ya mafanikio na kufanya vizuri katika ligi hiyo itakayotoa timu tatu za kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (FDL) msimu ujao.

Aidha Malinzi amewaomba wamiliki wa viwanja vinavyotumika kwa michezo ya FDL kuviweka katika hali nzuri ya matunzo ili mechi zinazochezwa katika viwanja hivyo ziweze kuwa nzuri kiufundi na muonekano wa kwenye Luninga.

Jumla ya udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza kwa sasa ni shilingi bilioni moja na milioni mia tatu hamsini (1,350,000,000) ikiwa ni udhamini wa milioni mia tisa (900,000,000) kutoka StarTimes  mdhamini mkuu wa FDL na milioni mia nne hamsini (450,000,000) kutoka StarTv.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Sahara Media Group, Samwel Nyala ameishukuru TFF kwa kuwapa nafasi hiyo ya haki za matangazo kampuni yake kwa michezo ya Ligi Daraja la kwanza nchini (FDL).

Katika kuhakikisha michezo hiyo inaonekana kwa wingi zaidi, Nyala alisema watafungua mkondo (Channel) ya Star Sports Plus itakayokua itakayokuwa inaonyesha michezo tu ikiwemo ligi daraja la kwanza (FDL).

Akiongea kwa niaba ya vilabu ya ligi daraja la kwnza nchini (FDL), Asha Kigundula - Afisa habari wa klabu ya Friends Rangers ya jijini Dar es salaam, ameishukuru TFF kwa kuweza kuwapatia udhamini kwenye ligi, jambo ambalo litawapelekea kujiandaa na kufanya vizuri katika ligi msimu huu.

Wednesday, October 7, 2015

TAIFA STARS YAWAADHIBU WAMALAWI, SAMATTA NA ULIMWENGU WATUPIA MAWILI NYAVUNI



TIMU ya Taifa (Taifa Stars),jana iliwapa raha baada ya kuichapa kwa mabao 2-0 timu ya Taifa ya Malawi katika Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam,mchezo huo wa kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia,zitakazo fanyika mwaka 2018 nchini Russia.

Stars ilianza mchezo huo kwa kasi ambapo dakika ya pili,Shomari Kapombe alipanda na mpira na kupiga mpira wa krosi iliyomkuta Mrosho Ngasa lakini alishindwa kufunga baada ya kuzongwa na walinzi wa Malawi.

Mbwana Samata alipachika bao la kuongoza dakika ya 18 baada ya kupewa pasi nzuri na Thomas Ulimwengu ambapo walionekana kuisumbua sana ngome ya timu ya Malawi katika mchezo huo.

Kasi ya Stars ilizidi kuwa kubwa ambapo dakika ya 22 ya mchezo huo,Ulimwengu alifunga bao la pili baada ya kupokea mpira wa krosi kutoka kwa Haji Mwinyi.

Malawi nao walifanya shambulizi dakika ya 37, baada ya kipa Ali Mustapha 'Barthez'kudaka shuti kali lililofumuliwa na  John Banda.

Taifa Stars nao walifanya shambulizi la nguvu dakika ya 43 baada ya Farid Musa kupanda na mpira na kisha kupiga krosi iliyomkuta Ulimwengu ambaye alikosa bao.

Dakika ya 55 Ulimwengu alipanda na mpira na kumpa pasi safi Mrisho Ngasa ambapo alikosa bao kwa kichwa baada ya  kupiga nje ya lango la Malawi.

Stanley Sanudi anapewa kadi ya njano dakika ya 72 na mwamuzi wa mchezo huo,Hagi Yabarow Wiish baada ya kumfanyia madhambi Farid Musa wa Taifa Stars.

Malawi walikosa bao dakika ya 80Isaac Kaliati kupiga shuti kali ambalo liliokolewa na kipa Ali Mustapha 'Barthez'.

Taifa Stars iliwakilishwa na Ali Mustapha,Shomari Kapombe,Haji Mwinyi,Nadir Haroub,Kelvin Yondan,Himid Mao,Thomas Ulimwengu/Ibrahimu Ajibu,Said Ndemla,Mbwana Samata,Mrisho Ngasa/Salum Telela  na Farid Musa/Saimon Msuva.

Malawi:Simplex Nthala,Stanley Sanudi,Mivale Gabeya,Yamkani  Fadya,Limbikani Mzava,Gerald Phiri/Isaac Kaliati, Chimango  Kayira,Micium Mhone/Mamase Chiyasa,Chawangiwa Kawanda,John Banda/ na Robin Ngalande/Gabadinho Mhango.

HAKUNA DHAMBI MKWASA KUPEWA MKATABA TAIFA STARS-YANGA



NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumpa Charles Boniface Mkwasa, mkataba wa miaka miwili wa kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars siyo dhambi.

Yanga imesema hawana pingamizi lolote kwa TFF, kumpatia kocha huyo msaidizi wa mabingwa hao wa soka nchini, mkataba wa kudumu wa kuinoa Taifa Stars, kwa vile amekwenda kuitumikia nchi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, alisema uamuzi huo wa TFF ni sahihi kwa vile Mkwasa anavyo vigezo vyote muhimu vya kuwa kocha wa timu ya taifa.

Alisema Yanga inaona fahari kubwa kwa Mkwasa kupata mkataba wa kudumu wa kuinoa Taifa Stars ili aweze kuelekeza nguvu zake kwenye kikosi hicho.

"Sisi hatuna pingamizi. Unajua mara nyingi amekuwa hatulii,mara yupo Yanga, mara anakwenda Taifa Stars. Sasa amepata kazi ya kudumu, hakuna dhambi yoyote," alisema Muro.

Kauli hiyo ya Muro, imekuja siku chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza rasmi kumpa mkataba huoMkwasa, ambao umeanza rasmi Oktoba Mosi, mwaka huu, na utamalizika Machi 31,2017.

Awali, kocha huyo alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo kwa muda mfupi wa miezi mitatu kabla ya TFF kuukubali uwezo wake na kuamua kumpa mkataba wa kudumu.

SAMATTA ATOA YA MOYONI



NA MWANDISHI WETU

MBWANA SAMATA, ametoboa siri kwamba kuna wakati  anashindwa kufunga mabao kutokana na aina ya mfumo wa uchezaji  wa timu ya taifa, Taifa Stars.

Samata, mshambuliaji wa kimataifa wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alisema hayo juzi jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu ni kwa nini amekuwa akishindwa kuifungia mabao Taifa Stars, kama anavyokuwa anapokuwa akiichezea TP Mazembe.

Samata alisema sababu nyingine inayomfanya ashindwe kucheza vizuri anapovaa jezi ya Taifa Stars, ni wachezaji wenzake kukosa uzoefu wa michuano ya kimataifa.

"Hivyo ni vyema wachezaji wazawa watoke nje ya nchi na kucheza mpira wa kulipwa kwani huko kuna mambo mengi ya kujifunza ambayo yatawafanya wawe bora zaidi wanapokuwa uwanjani," alisema Samata.

Alisema mfumo na aina ya uchezaji wa wachezaji alionao Taifa Stars ni tofauti na ule wa TP Mazembe, ambako amekuwa akishirikiana na wachezaji nyota kutoka nchi mbalimbali  za kiafrika.

"Sina maana kwamba wachezaji wa Tanzania wabaya, hapana.
Nadhani labda ni mbinu na uzoefu mdogo wa mechi za kimataifa, hilo nalo ni tatizo," alisema Samata.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Simba, aliifungia TP Mazembe mabao mawili kati ya matatu, wakati timu hiyo ilipoifunga El Merreikh ya Sudan mabao 3-0 katika mechi ya nusu fainali ya klabu bingwa Afrika.

MKWASA APEWA MKATABA WA KUDUMU TAIFA STARS



Charles Boniface Mkwasa amepewa mkataba wa kudumu kukinoa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu na kumalizika  Machi 31, 2017.

TFF Imefikia makubaliano hayo na kocha Mkwasa baada ya kurudhika na utendaji wake katika kukinoa kikosi cha timu ya Taifa, ambapo mpaka sasa ameweza kuingoza Stars katika sare ya michezo miwili dhidi ya Uganda na Nigeria.

Kufuatia kusaini mkataba huo, Mkwasa atapatiwa huduma na marupurupu yote aliyokuwa akipewa kocha aliyeondoka.

Naye kocha Mkwassa ameeleza kufurahishwa na makubaliano haya na ameahidi kufanya kila jitihada kuhakikisha kiwango cha Timu ya Taifa kinapanda.

Aidha Kocha Mkwassa ametoa wito kwa wadau wa mpira kumpa ushirikiano katika majukumu yake mapya.

TAIFA STARS WAAHIDI USHINDI DHIDI YA WAMALAWI LEO


Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, Charles Mkwasa amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa leo dhidi ya Malawi kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018.

Mkwasa amesema kikosi chake kipo kaika hali nzuri baada ya kufanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi ambapo wachezaji wote wapo katika hali nzuri wakiwemo wachezaji wawili Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kutoka klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.

“Tunatambua umuhimu wa mchezo wa kesho, wachezaji wana ari na morali ya hali ya juu, kikubwa tunawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kuja kutu sapoti katika mchezo huo wa kesho” Alisema Mkwasa.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Malawi (The Flames), Ramadhan Nsanzurwimo amesema wanaiheshimu Tanzania, wanatambua kesho kutakua na mchezo mzuri, na wao kama Malawi wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Jumatano kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Malawi (The Flames) kuwa ni shilingi elfu tano (5,000) katika mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Viingilio vilivyotangazwa leo ni kiingilio cha juu kabisa kwa mchezo huo shilingi elfu kumi (10,000) kwa viti vya VIP B & C, huku viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani ikiwa ni shilingi elfu tano (5,000).

Stars inayonolewa na kocha mzawa Charles Boniface Mkwasa imeendelea kujifua katika viwanja vya Gymkhana na uwanja Taifa jioni kujiandaa mchezo huo wa Jumatano dhidi ya Malawi, huku wachezaji wakiwa wenye ari na morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mechi hiyo.

Wachezaji 22 wapo kambini akiwemo mshambuliaji Mrisho Ngasa anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini aliyeripoti jana mchana kambini, huku wachezaji wawili Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wakitarajiwa kujiunga na wenzao leo wakitokea Lubumbashi – Congo DR.

Wakati huo huo timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) imewasili nchini jana saa 4 asubuhi na kufikia katika hoteli ya De Mag iliyopo Mwanayamala, ambapo kikosi hicho leo kimefanya mazoezi asubuhi katika uwanja wa Boko Veterani.

Waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Somalia, kamisaa na mtathimin waamuzi wa wanatarajiwa kuwasili leo nchini na kufikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.

Mwamuzi wa kati ni Hagi Yabarow Wiish (Somalia), akisaidiwa na Hamza Hagi Abdi (Somalia), Salah Omar Abubakar (Somalia), mwamuzi wa akiba Bashir Olad Arab (Somalia), mtathimini wa waamuzi Sam Essam Islam (Misri) na kamisaa wa mchezo ni Muzambi Gladmore (Zimbabwe).

Saturday, October 3, 2015

KILIMANJARO STARS KUCHEZA KOMBE LA CHALENJI



Timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imedhibitisha kushiriki michuano ya timu za Taifa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Chalenjji) itakayofanyika nchini Ethiopia kuanzia Novemba 21 – 06 Disemba, 2015.

Michuano ya CECAFA Chalenji ndio michuano mikongwe zaidi barani Afrika ambapo jumla ya nchi 12 wanachama hushirki michuano hiyo iliyofanyika mara ya mwisho mwaka juzi nchini Kenya na wenyeji kutwaa Ubingwa huo.

Nchi wanachama wa CECAFA ni Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somali, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.

MALINZI ATUMA PONGEZI MSUMBIJI NA CAMEROON



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za pongezi kwa Alberto Simago Junior wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Msumbiji (FMF) na Sidiki Tombi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Cameroon (FECAFOOT) kufuatia kuchaguliwa kuwa marais wa mashiriksho ya mpira miguu.

Katika salam zake kwenda FMF na FECAFOOT, Malinzi amesema kuchaguliwa kwao kuogoza mashirikisho hayo kumetokana na imani ya wanafamilia wa mpira miguu.

Kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF na familia ya mpira wa miguu nchini, anawapa pongezi kwa kucgahuliwa kwao.

TFF inaahidi kushirikiana na uongozi mpya wa FMF na FECFOOT katika maendeleo ya mpira wa miguu Afrika na Dunia kote.

TAIFA STARS YAANZA KUITAFUTIA DOZI MALAWI



Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kimeanza mazoezi leo mchana katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo dhdi ya Malawi utakaocheza Jumatano Oktoba 7, 2015 kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Stars inayonolewa na kocha mkuu mzawa Charles Mkwasa, akisaidiwa na Hemed Morroco, Peter Manyika na mshauri wa Ufundi Abdallah Kibadeni wameingia kambini jana katika hoteli ya Urban Rose iliyopo Kisutu jijini Dar es salaam.

Wachezaji wote wameripoti kambini isipokuwa wachezaji wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mrisho Ngasa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaotarajiwa kuungana na wenzao mwishoni mwa wiki baada ya kumaliza michezo inayowakabili wikiendi hii.

Wachezaji waliopo kambini ni magolikipa All Mustafa, Aishi Manula, Said Mohamed, walinzi Juma Abdul, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro”.

Wengine ni viungo Himid Mao, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Said Ndemla, Salum Telela, Deus Kaseke, Saimon Msuva, Farid Musa, washambuliaji John Bocco, Rashid Mandawa na Ibrahim Hajibu.

LEO NI MGAMBO SHOOTING NA COASTAL UNION



Mzunguko wa raundi ya sita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) unatarajiwa kuendelea kesho Jumamosi na Jumapili kwa timu 10 kucheza kusaka alama 3 muhimu.

Jijini Tanga Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani, Majimaji FC watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Jumapili Stand United chama la wana watawakaribisha watoza ushuru wa jiji la Mbeya (Mbeya City) katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na Toto Africa watakua wenyeji wa JKT Ruvu jijini Mwanza uwanja wa CCM Kirumba.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUENDELEA LEO



Ligi Daraja la Kwanza nchini (StarTimes First League) inaendelea wikiendi hii kwa makundi yote matatu kucheza, michezo 11 itachezwa mwishoni mwa wiki siku za Jumamos na Jumapili katika viwanja mbalimbali nchini.

Jumamosi Kundi A, Ashanti United watakua wenyeji wa Mji Mkuu (CDA) katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, KMC watawakaribisha Polisi Dodoma katika uwanja wa Mabatini – Mlandizi.

Kundi B, Lipuli FC watawakaribisha Polisi Morogoro katika uwanja wa Wambi mkoani Iringa, Kimondo FC watakuwa wenyeji wa JKT Mlale kwenye uwanja wa CCM Vwava – Mbozi, huku Burkinafaso ya Morogoro ikiwakaribisha Njombe Mji katika uwanja wa Jamhuri.

Kundi C, JKT Kanembwa watakuwa wenyeji wa Panone FC katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, JKT Oljoro watawakaribisha Polisi Moro uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Geita Gold watacheza na Rhino Rangers uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita na Polisi Tabora watawakaribsiha Mbao FC mjini Tabora uwanja wa Ali Hassa Mwinyi.

Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili ya Kundi A, Friends Rangers watacheza dhidi ya African Lyon uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, na Polisi Dar watakua wenyeji wa Kiluvya FC katika uwanja wa Mabatini Mlandizi.

Thursday, October 1, 2015

TFF YATIA SAINI MKATABA NA BIMA YA AFYA


Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amesaini mkataba wa mwaka mmoja na mfuko wa huduma ya afya (NHIF) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na viongozi wa benchi la ufundi.

Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika katika hoteli ya Protea Courtyard iliyopo Upanga jijini Dar es salaam ambapo katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF Rehani Athumani walisaini kwa niaba ya pande hizo mbili.

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa uwekaji sahihi mkataba huo, Mwesigwa amesema anaishukuru NHIF kwa kudhamini kutoa huduma ya afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi kwa vilabu vyote 16 vinavyoshiriki Ligi kuu ya Vodacom.

Aidha Mwesigwa ameviomba vilabu vya Ligi Kuu nchini kutoa ushirikiano na watoa huduma ya afya kwa wachezaji na viongozi kutoka NHIF pindi watakapokuwa wanafika kwenye vilabu vyao kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,  Rehani Athumani akiongea kwa niaba ya mfuko huo amesema wako tayari kufanya kazi na kutoa huduma ya afya kwa ngazi zote ikiwemo kwa timu za madaraja ya chini pia.

TFF na NHIF zimeingia mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini wa huduma ya afya kwa wachezaji kwa ligi kuu na viongozi wa benchi la ufundi, mkataba ambao unaeza kuongezwa kila unapomalizika.

TFF kwa kupitia bodi ya ligi inavitaka vilabu vyote vya Ligi Kuu vitoe ushirikiano kwa wafanyakazi wa NHIF katika kurahisiha shughuli za usajili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na nyaraka sahihi zikiwemo picha za wahusika katika muda sahihi.

MALINZI AFUNGA KOZI YA WAAMUZI CHIPUKIZI



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi leo amefunga kozi ya waamuzi chipukizi wasiokuwa na beji za FIFA katika hoteli ya Holiday, ambapo jumla ya waamuzi 30 kutoka nchi 28 barani Afrika walihudhuria.

Akiongea wakati wa kufunga kozi hiyo Malinzi alitoa wito kwa wahitimu wajikite kwenye maadili kwa kuzingatia mafunzo waliyopata ili katika kipindi kifupi wote wapate beji za FIFA na waonekane kweye mashindano makubwa kama fainali za AFCON na mashindano ya Kombe la Dunia.

Kabla ya Hotuba ya Mgeni rasmi mwakilishi wa CAF Eddy aliishukuru TFF kwa maandalizi mazuri na usimamizi bora kwa kipindi chore cha kozi hii, na kuahidi kuleta kozi nyingine kubwa hapa nchini.

Naye mwakilishi wa FIFA Carlos Hendrique alitoa shukurani zake za dhati kwa TFF kwa kuwa tayari wakati wote kushirikiana na FIFA hali ambayo imefanyika TFF iaminike na itegemewe na FIFA kweye program mbalimbali

Kozi hiyo ya waamuzi imefanyika kwa mara ya kwanza hapa barani Afrika.

FIFA iliiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa kozi hii kwa nchi zinazo zungumza kiingereza. Kwa upande wa nchi zinazo zungumza kifaransa kozi ya aina hii imefanyika nchini Morocco

Washiriki 30 kutoka nchi 28 barani Afrika wamehudhuria kozi hii ilivyokuwa itafundishwa na Wakufunzi wa Sita kutoka CAF na FIFA.

SIMBA HAKUNA KULALA



TIMU ya Simba, jana iliweza kuichapa Stand United bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee la Simba lilifungwa na mshambuliaji Joseph Kamwaga dakika 57 muda mfupi baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Said Ndemla. Alipokea pande safi kutoka kwa Simon Ssenkuruma.

Timu hizo, zilianza mchezo kwa kasi huku kila upande ukionekana kuwa na molari ya kuibuka na ushindi katika mpambano huo.

Dakika ya 18, Jacob Masawe aliwatoka walinzi wa Simba na kupiga shuti kali ambalo lilidakwa na kipa wa Simba, Peter Manyika.

Simba nao walijibu mapigo dakika ya 23, baada ya Jonas Mkude kupiga shuti ambalo lilidakwa na kipa wa Stand United, Frank Muwonge.

Dakika ya 24 ya mchezo mabeki wa Simba walifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la beki Nassoro Masoud 'Cholo' ambaye alipanda na kupiga shuti ambalo lilikuwa linaelekea wavuni, lakini Hassan Isihaka aliokoa.

Ssenkuruma alipokea krosi safi kutoka kwa Mohamed Hussein, dakika ya 30 ambapo alipiga shuti lililotoka nje ya lango la Stand United. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Stand walimiliki vizuri mpira kuliko Simba.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila upande ukisaka ushindi ambapo dakika ya 48,Peter Mwalyanzi alikosa bao baada ya kupiga shuti ambalo liliokolewa na kipa Frank Muwonge wa Stand.

Dakika ya 49, Juuko alioneshwa kadi ya njano na mwamuzi Ahmada Simba kutoka mkoa wa Kagera   baada ya kushika mpira huku Seleman Selembe wa Stand naye alipewa kadi ya njano,dakika ya 55 kwa kumchezea madhambi Juuko .

Hata hivyo,dakika ya 56, Erick Kayombo alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Hassan Ramadhan .

Dakika ya 72,nusura Elias Maguli afunge bao la kusawazisha baada ya kipa Peter Manyika kukaa vibaya kwenye lango lake na beki Hassan Isihaka aliokoa mpira huo kabla ya kuingia wavuni.

Mohamed Hussein alipewa kadi ya njano baada ya kuchelewesha kurusha mpira,Maguli katika dakika ya 78,alipiga shtu likagomba mwamba  katika mlingoti na kuwa kona ambayo haikuzaa bao kufuatia pande safi la Pastory Athanas.


Simba iliwakilishwa na Peter Manyika,Hassan Ramadhan'Kessy', Mohamed Hussein, Murshid Juuko,Hassan Isihaka, Jonas Mkude,Justice Majabvi,Said Ndemla/Joseph Kimwaga, Peter Mwalyanzi, Simon Ssenkuruma/Awadh Juma na Boniface Mganga/Abdi Banda.

Stand United: Frank Muwonnge, Nassoro Said, Abuu Ubwa, Philip Imetusela, Rajab Zahir, Hassan Dilunga, Jacob Masawe, Ericky Kayombo/Elias Maguli, Vitaris Mayanga/Hassan Banda, Seleman Selembe/Haruna Chanongo na Pastory Athanas.

Matokeo mengine,timu ya Mgambo JKT,iliweza kuifunga bao 1-0 timu ya African Sports ya Tanga katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani,Tanga.

Majimaji imeweza kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya Ndanda FC ya Mtwara katika uwanja wa Majimaji,Songea.

Azam FC nayo imeendelea kukusanya pointi 15 baada ya kuifunga Coastal Union kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Azam Complex.

Timu ya Mwadui imetoka sare na timu ya Prisons  bila ya kufungana  katika uwanja wa Sokoine,Mbeya na  JKT Ruvu imetoka suluhu ya bila kufungana na Kagera Sugar huko mkoani Tabora.

YANGA MBELE KWA MBELE, YAITUNGUA MTIBWA 2-0



NA AMINA ATHUMANI, MOROGORO

TIMU ya Yanga imezidi kujikita kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuvunja mwiko kwa kuilaza Mtibwa Sugar bao 1-0.

Yanga imefikisha pointi 15, baada ya kushinda mechi zote tano tangu kuanza ligi hiyo Septemba 12,  mwaka huu. Timu hizo zilipepetana jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mshambuliaji mpya, Malimi Busungu, alitimiza azma yake ya kuifunga Mtibwa, baada ya kufunga bao hilo dakika ya 52 kwa shuti lililompita kipa Said Mohammed.

Busungu aliyejiunga na Yanga kutoka Mgambo JKT, juzi alitoa ahadi ya kufunga bao katika mchezo huo baada ya kuwaziba mdomo Simba Jumamosi iliyopita.

Mchezo ulianza kwa timu hizo kucheza kwa tahadhari, lakini dakika ya 13 Mtibwa ilibisha hodi langoni mwa Yanga baada ya Vincent Barnabas, kufumua shuti ambalo liliokolewa na kipa Ali Mustapha 'Barthez'.

Yanga ilijibu shambulizi baada ya beki wa kushoto Haji Mwinyi, kupanda mbele kusaidia mashambulizi dakika ya 26 kupiga mkwaju uliopanguliwa na kipa Mohammed.

Dakika 30 kipindi cha kwanza timu hizo zilicheza mpira wa kukamiana uliochezwa katikati bila washambuliaji kuleta madhara langoni mwa wapinzani.

Dakika ya 38 beki, Salum Mbonde wa Mtibwa, alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi, Erick Onoka wa Arusha kwa mchezo mbaya.

Yanga ilianza ligi kwa kuinyuka Coastal Union mabao 2-0, ilishinda 3-1 dhidi ya Prisons, iliifunga JKT Ruvu 4-1, iliinyuka Simba 2-0.

Mtibwa:  Said Mohammed, Rodgers Fred, Issa Rashid, Andrew Vincent, Salum Mbonde, Shabani Nditi, Vincent Barnabas/Ali Shomari, Mzamiru Yassin, Selemani Rajabu, Mohammed Ibrahim na Shizya Kichuya.

Yanga: Ali Mustapha, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Thabani Kamusoko, Salum Telela, Malimi Busungu, Said Juma, Amiss Tambwe na Donald Ngoma.