'
Wednesday, October 7, 2015
SAMATTA ATOA YA MOYONI
NA MWANDISHI WETU
MBWANA SAMATA, ametoboa siri kwamba kuna wakati anashindwa kufunga mabao kutokana na aina ya mfumo wa uchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Samata, mshambuliaji wa kimataifa wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alisema hayo juzi jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu ni kwa nini amekuwa akishindwa kuifungia mabao Taifa Stars, kama anavyokuwa anapokuwa akiichezea TP Mazembe.
Samata alisema sababu nyingine inayomfanya ashindwe kucheza vizuri anapovaa jezi ya Taifa Stars, ni wachezaji wenzake kukosa uzoefu wa michuano ya kimataifa.
"Hivyo ni vyema wachezaji wazawa watoke nje ya nchi na kucheza mpira wa kulipwa kwani huko kuna mambo mengi ya kujifunza ambayo yatawafanya wawe bora zaidi wanapokuwa uwanjani," alisema Samata.
Alisema mfumo na aina ya uchezaji wa wachezaji alionao Taifa Stars ni tofauti na ule wa TP Mazembe, ambako amekuwa akishirikiana na wachezaji nyota kutoka nchi mbalimbali za kiafrika.
"Sina maana kwamba wachezaji wa Tanzania wabaya, hapana.
Nadhani labda ni mbinu na uzoefu mdogo wa mechi za kimataifa, hilo nalo ni tatizo," alisema Samata.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Simba, aliifungia TP Mazembe mabao mawili kati ya matatu, wakati timu hiyo ilipoifunga El Merreikh ya Sudan mabao 3-0 katika mechi ya nusu fainali ya klabu bingwa Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment