KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 1, 2015

SIMBA HAKUNA KULALA



TIMU ya Simba, jana iliweza kuichapa Stand United bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee la Simba lilifungwa na mshambuliaji Joseph Kamwaga dakika 57 muda mfupi baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Said Ndemla. Alipokea pande safi kutoka kwa Simon Ssenkuruma.

Timu hizo, zilianza mchezo kwa kasi huku kila upande ukionekana kuwa na molari ya kuibuka na ushindi katika mpambano huo.

Dakika ya 18, Jacob Masawe aliwatoka walinzi wa Simba na kupiga shuti kali ambalo lilidakwa na kipa wa Simba, Peter Manyika.

Simba nao walijibu mapigo dakika ya 23, baada ya Jonas Mkude kupiga shuti ambalo lilidakwa na kipa wa Stand United, Frank Muwonge.

Dakika ya 24 ya mchezo mabeki wa Simba walifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la beki Nassoro Masoud 'Cholo' ambaye alipanda na kupiga shuti ambalo lilikuwa linaelekea wavuni, lakini Hassan Isihaka aliokoa.

Ssenkuruma alipokea krosi safi kutoka kwa Mohamed Hussein, dakika ya 30 ambapo alipiga shuti lililotoka nje ya lango la Stand United. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Stand walimiliki vizuri mpira kuliko Simba.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila upande ukisaka ushindi ambapo dakika ya 48,Peter Mwalyanzi alikosa bao baada ya kupiga shuti ambalo liliokolewa na kipa Frank Muwonge wa Stand.

Dakika ya 49, Juuko alioneshwa kadi ya njano na mwamuzi Ahmada Simba kutoka mkoa wa Kagera   baada ya kushika mpira huku Seleman Selembe wa Stand naye alipewa kadi ya njano,dakika ya 55 kwa kumchezea madhambi Juuko .

Hata hivyo,dakika ya 56, Erick Kayombo alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Hassan Ramadhan .

Dakika ya 72,nusura Elias Maguli afunge bao la kusawazisha baada ya kipa Peter Manyika kukaa vibaya kwenye lango lake na beki Hassan Isihaka aliokoa mpira huo kabla ya kuingia wavuni.

Mohamed Hussein alipewa kadi ya njano baada ya kuchelewesha kurusha mpira,Maguli katika dakika ya 78,alipiga shtu likagomba mwamba  katika mlingoti na kuwa kona ambayo haikuzaa bao kufuatia pande safi la Pastory Athanas.


Simba iliwakilishwa na Peter Manyika,Hassan Ramadhan'Kessy', Mohamed Hussein, Murshid Juuko,Hassan Isihaka, Jonas Mkude,Justice Majabvi,Said Ndemla/Joseph Kimwaga, Peter Mwalyanzi, Simon Ssenkuruma/Awadh Juma na Boniface Mganga/Abdi Banda.

Stand United: Frank Muwonnge, Nassoro Said, Abuu Ubwa, Philip Imetusela, Rajab Zahir, Hassan Dilunga, Jacob Masawe, Ericky Kayombo/Elias Maguli, Vitaris Mayanga/Hassan Banda, Seleman Selembe/Haruna Chanongo na Pastory Athanas.

Matokeo mengine,timu ya Mgambo JKT,iliweza kuifunga bao 1-0 timu ya African Sports ya Tanga katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani,Tanga.

Majimaji imeweza kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya Ndanda FC ya Mtwara katika uwanja wa Majimaji,Songea.

Azam FC nayo imeendelea kukusanya pointi 15 baada ya kuifunga Coastal Union kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Azam Complex.

Timu ya Mwadui imetoka sare na timu ya Prisons  bila ya kufungana  katika uwanja wa Sokoine,Mbeya na  JKT Ruvu imetoka suluhu ya bila kufungana na Kagera Sugar huko mkoani Tabora.

No comments:

Post a Comment