'
Thursday, October 29, 2015
SIMBA YAJITUTUMUA, YANGA YABANWA
TIMU kongwe ya soka ya Simba jana iliwapoza machungu mashabiki wake baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja waTaifa, Dar es Salaam.
Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo kiduchu, mabingwa watetezi Yanga walibanwa mbavu na Mwadui ya Shinyanga kwa kulazimishwa sareya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Ushindi wa Simba umewapa ahueni kubwa mashabiki wake baada ya kupoteza mechi iliyopita kwa kuchapwa bao 1-0 na Prisons mjini Mbeya.
Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza dakika ya saba.
Kiiza, ambaye alikosa mechi mbili zilizopita, alifunga bao hilo kwa kuunganisha wavuni kwa shuti kali mpira wa krosi uliopigwa kutoka wingi ya kulia na beki Hassan Ramadhani.
Coastal Union nusura isawazishe dakika ya 23 wakati Ismal Mohamed alipoingia na mpira na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Vincent Angban wa Simba.
Kiiza angeweza kuiongezea bao Simba dakika ya 44 baada ya kupewa jukumu la kupiga mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo la hatari la Coastal Union, lakini shuti lake lilitoka nje.
Wakati huo huo, mshambuliaji Bakari Kigodeko jana aliipokonya Yanga tonge mdomoni baada ya kuifungia Mwadui bao la kusawazisha.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata mabao kupitia kwa Donald Ngoma, aliyefunga yote mawili.
Bao la kwanza la Mwadui lilifungwa na Paul Nonga kabla ya Kigodeko kusawazisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment