KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 27, 2015

BUSUNGU, MAGULI WAONGEZWA TAIFA STARS

 KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amewaongeza kikosini washambuliaji Malimi Busungu wa Yanga SC na Elias Maguri katika kikosi kitakachomenyana na Algeria katikati ya mwezi ujao.
Taifa Stars itamenyana na Algeria katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2018 Urusi, baada ya kuitoa Malawi katika hatua ya kwanza.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Mkwasa ametaja wachezaji 28 ambao watakwenda kambini Oman Novemba 2, mwaka huu.
Mkwasa amewataja wachezaji hao kuwa ni makipa; Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam FC), Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan (Yanga SC), Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka (Simba SC) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba SC) na Salum Telela (Yanga SC).
Washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Free State Stars, A. Kusini), Farid Mussa, John Bocco (Azam FC), Simon Msuva, Malimi Busungu (Yanga SC), Elias Maguri (Ruvu Shooting) na Ibrahim Hajib (Simba SC).
Mkwasa amesema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 1 katika hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kabla ya safari ya Muscat, Oman kwa kambi ya siku 10.
Amesema wakiwa Oman, pamoja na mazoezi, watacheza mchezo mmoja au miwili ya kujipima na wenyeji wao, iwapo watakuwa tayari kabla ya kurejea Dar es Salaam Novemba 11 tayari kwa mchezo wa kwanza na Algeria Novemba 14, Uwanja wa Taifa.
Amesema kikosi kitaondoka Dar es Salaam kwenda Algiers Novemba 16, tayari kwa mchezo wa marudiano Novemba 17.

No comments:

Post a Comment