KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 1, 2015

YANGA MBELE KWA MBELE, YAITUNGUA MTIBWA 2-0



NA AMINA ATHUMANI, MOROGORO

TIMU ya Yanga imezidi kujikita kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuvunja mwiko kwa kuilaza Mtibwa Sugar bao 1-0.

Yanga imefikisha pointi 15, baada ya kushinda mechi zote tano tangu kuanza ligi hiyo Septemba 12,  mwaka huu. Timu hizo zilipepetana jana kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mshambuliaji mpya, Malimi Busungu, alitimiza azma yake ya kuifunga Mtibwa, baada ya kufunga bao hilo dakika ya 52 kwa shuti lililompita kipa Said Mohammed.

Busungu aliyejiunga na Yanga kutoka Mgambo JKT, juzi alitoa ahadi ya kufunga bao katika mchezo huo baada ya kuwaziba mdomo Simba Jumamosi iliyopita.

Mchezo ulianza kwa timu hizo kucheza kwa tahadhari, lakini dakika ya 13 Mtibwa ilibisha hodi langoni mwa Yanga baada ya Vincent Barnabas, kufumua shuti ambalo liliokolewa na kipa Ali Mustapha 'Barthez'.

Yanga ilijibu shambulizi baada ya beki wa kushoto Haji Mwinyi, kupanda mbele kusaidia mashambulizi dakika ya 26 kupiga mkwaju uliopanguliwa na kipa Mohammed.

Dakika 30 kipindi cha kwanza timu hizo zilicheza mpira wa kukamiana uliochezwa katikati bila washambuliaji kuleta madhara langoni mwa wapinzani.

Dakika ya 38 beki, Salum Mbonde wa Mtibwa, alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi, Erick Onoka wa Arusha kwa mchezo mbaya.

Yanga ilianza ligi kwa kuinyuka Coastal Union mabao 2-0, ilishinda 3-1 dhidi ya Prisons, iliifunga JKT Ruvu 4-1, iliinyuka Simba 2-0.

Mtibwa:  Said Mohammed, Rodgers Fred, Issa Rashid, Andrew Vincent, Salum Mbonde, Shabani Nditi, Vincent Barnabas/Ali Shomari, Mzamiru Yassin, Selemani Rajabu, Mohammed Ibrahim na Shizya Kichuya.

Yanga: Ali Mustapha, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Thabani Kamusoko, Salum Telela, Malimi Busungu, Said Juma, Amiss Tambwe na Donald Ngoma.

No comments:

Post a Comment