KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 11, 2015

TAIFA STARS YACHAPWA 1-0 NA MALAWI, LAKINI YASONGA MBELE


Na Princess Asia, BLANTYRE
TANZANIA imetimiza ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya kufungwa 1-0 na Malawi mchana wa leo Uwanja wa Kamuzu mjini hapa.
Tanzania inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya Jumatano kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilifungwa na John Banda dakika ya 42 aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Chiukepo Msowoya

Taifa Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu, mshambuliaji Mbwana Samatta alikaribia kufunga, baada ya kumtoka beki Limbikani Mnzava, lakini kipa Simplex Nthala akaokoa.
Malawi wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya shuti kali la Banda kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
Barthez akafanya kazi nzuri tena dakika ya 10 baada ya kuokoa michomo miwili mfululizo ya Malawi.
Stars ilizinduka dakika ya 35 baada ya Thomas Ulimwengu kumtoka vizuri beki wa Malawi Yamikani Fodya baada ya pasi ndefu ya Samatta, lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko, akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo la Malawi, lakini bado mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa Tanzania.
Dakika ya 58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliokoa hatari langoni mwake na dakika ya 62 Malawi walifanya mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni mwa Stars, ikiwemo kupata kona mbili.      
Dakika ya 72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.
Malawi walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Wachezaji wa Tanzania walitumia dakika nne za majeruhi kujiangusha kupoteza muda na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wote walionyeshwa kadi za njano kwa sababu hiyo.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo Novemba.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Said Ndemla/John Bocco dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Mrisho Ngassa dk75.
Malawi; Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Miracle Gabeya/Robin Ngalande dk76, Yamkani Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri, Chimango Kayira, Micium Mhone, Chiukepo Msowoya, John Banda na Shumaker Kuwali. 
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment